Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Ally Abdulla Ally Saleh

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Malindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza hakuna mwenye nia mbaya, sote ni wananchi na sote hii ni nchi yetu. Tunachofanya ni wajibu wetu kuikosoa Serikali na kuishauri Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwenye deni la Taifa. Jana wakati wa presentation ya Mheshimiwa Mama Hawa hapa, wakati ilipozungumzwa na Kambi ya Upinzani kwamba deni ni kubwa na kwamba kuna haja ya kufanya auditing ili tunapoingia katika Mpango huu ambao utagharimu Shilingi trilioni 107 tujue deni letu kabisa kabla hatujaingia huko, Mheshimiwa Mama Hawa alijaribu ku-defend akatoa vigezo vingi vya kuonesha kwamba deni hili bado ni manageable. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka kusema kwamba, wenzetu wengine pia walisema madeni yao ni manageable. Bolivia wana mafuta, walisema deni lao ni manageable, lakini baadaye wakaingia kwenye matatizo makubwa! Argentina wana uchumi mzuri na ndiyo wanaoongoza kwa uchumi wa ng‟ombe duniani, walifikiri deni lao ni manageable na waka-collapse! Hali kadhalika na Greece!
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naungana kwanza na Waziri Kivuli wa Fedha wa Kambi ya Upinzani kwamba ni vizuri Bunge hili likatoa Azimio au tukazungumza kwamba kuna haja ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kutufanyia auditing ili tujue tunasimama wapi. Katika hizo Shilingi trilioni 107 za kuendesha Mpango, maana yake pia tutakopa. Tumefika hapa kwa ajili ya mikopo ambayo hairudishwi. Kwa hiyo, ni bora wananchi wetu wajue tuna madeni kiasi gani kabla hatujasonga mbele na vipi tutaya-manage madeni hayo. Hilo ni la kwanza! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili ni kuhusiana na kipato. Tumeambiwa kwamba sasa hivi kipato chetu kwa Mtanzania ni wastani wa Dola 1,006. Kipato hiki tunaambiwa kwamba, ndicho ambacho Mtanzania anapata. Tumekuwa tukisema hapa kwamba kipato hiki hakionekani kwa Mtanzania wa kawaida, ni pesa za makaratasi zaidi; na tunaambiwa kwamba, tunaelekea kwenye kipato cha Dola 3,000, ndiyo lengo letu!
Mheshimiwa Spika, kama mwananchi, napenda tufikie huko na nchi iingie katika kipato cha kati, lakini Mpango haukueleza base kubwa zaidi; haujapanua base kubwa zaidi ya namna ya kuelekea kwenye kipato hicho kwa kuamini tu kwamba, viwanda ndiyo vitatuletea kipato, lakini ziko sehemu nyingine nchi hii hazihitaji viwanda wala Watanzania wote hawatafanya kazi kwenye viwanda. Kwa hiyo, rai yangu ilikuwa ni kupanua base.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, naambiwa katika Wilaya ya Lushoto au Mtanzania yeyote anajua kwamba wao wanaongoza kwa mazao ya kilimo, mfano mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Lushoto wanatoka Wakomoro wanakuja pale wanachukua bidhaa wana-pack kabisa wanazipeleka Comoro na pengine zinafika mpaka Ufaransa! Sasa kwa nini tuwaachie Wakomoro wafanye kazi hiyo badala ya kuimarisha wananchi wetu tukawapa fedha wakaweza kufanya vitu kama vile tuka-add value katika bidhaa zetu za kilimo ili kufikia masoko kama hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, tumeacha area moja kubwa sana katika nchi yetu; area ya uvuvi. Uvuvi wetu ni wa ndoana, wa hapa karibu karibu. Uvuvi wetu haujawa mkubwa wa kutosha. Nimesema katika Kikao kilichopita kwamba tunashindwa na nchi ndogo ya Seychelles ambayo ina watu 100,000 lakini wanaongoza kwa uvuvi wa jodari! Kwa duniani wao ni wa pili!
Mheshimiwa Spika, tuna ukanda wa bahari wa kilometa 1,400 hatujautumika vya kutosha. Jana nilisikia hapa kwamba kuna taarifa kwamba kwenye benki kuna dirisha la kilimo katika mambo ya ukopaji, napenda nione tunafungua Benki ya Uvuvi, iwe specifically located kwa sababu tuna sekta kubwa sana, uvuvi wa kutoka maziwani mpaka kwenye bahari kuu. Kwa hiyo, napenda Serikali ilizingatie hili ili tu-take fursa ambayo inaweza ikapatikana.
Mheshimiwa Spika, kingine ambacho nataka kusema, ni kuhusiana na Mtwara Corridor au sehemu ya Kusini. Kusema kweli, ingawa hapa Bungeni kwa observation yangu, mara nyingi watu wanajivutia Kikanda.
Mheshimiwa Spika, watu wanazungumzia habari ya Reli ya Kati na utaona wengi wanaozungumzia Reli ya Kati maana yake ni watu ambao wanatokea upande wa huko. Kwa fikra yangu nahisi Mtwara is the next big thing in Tanzania, really! Yaani kwa kanda ile kule! Hivi sasa kuna gesi, viwanda vinakuja na capital chemicals nyingi kutokana na LNG ambayo ukitoa gesi maana yake unapata LNG na viwanda vya aina nyingi.
Mheshimiwa Spika, pia, juzi juzi nimesoma kwamba yamegunduliwa madini ya graphite. Madini haya hivi sasa waliotangaza kugundua ni kampuni ya Marekani na mmoja katika Board Members (Stith) ni mtu ambaye alikuwa Balozi wa Tanzania…
MHE. ALLY SALEH ALLY: Anaitwa Stiff, anasema graphite iliyogunduliwa Tanzania inaweza kuwa ya pili baada ya China duniani, lakini pia inaweza kuwa ya kwanza kuliko hata China. Kwa hiyo, ina maana kuna potential kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, jana Waziri mmoja alituambia hapa kwamba kuna mpango wa kilimo cha mihogo ya tani milioni 200 kinakuja na soko lipo, lakini sioni uwekezaji unaofanana; kwa communication, unaofanana na rasilimali zilizoko Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumefungua Corridor ya Kusini kwa Uwanja wa Songwe. Tuna Uwanja wa Kilimanjaro. Kuna haja sasa hivi ya kuwa na Uwanja wa Kusini wa Kimataifa ili uelekee upande mwingine, tufungue Corridor nyingine, katika kila kona ya Tanzania tuwe tuna uwanja ambao unafanana na uwezo na hali tunayosema tunataka tuwenayo. (Makofi)
Kwa hiyo, nashauri kwamba the next big thing kuitazama ni Corridor ya Kusini, tujipange vizuri tuweze kuitumia vizuri ili tuweze kufaidika na gesi na vitu vingine ambavyo vinaambatana na mambo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kingine ninachotaka kuzungumzia ni kuhusu Shirika la Ndege la Tanzania. Actually mpaka tulipofika hapa ilikuwa ni aibu sana kwamba nchi hii tumekubali Shirika letu la National Carrier kufa na hatukuweza kulitengeneza, mpaka hivi sasa tunataka kutengeneza kwa kuwa na ndege mbili. Tunasema kwamba tunatarajia kuwa na watalii wengi kwa sababu tutakuwa na ndege mbili. Actually kuwa na ndege ni kitu kingine na kupata watalii ni kitu kingine. Unaweza kuwa na ndege, lakini kama huna routes zinazofaa na kama hujapata kununua route kwa watu wengine na kama hujaweza kuiuza nchi upya, bado utalii hauwezi kukusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na kuwa na ndege mbili, ambazo sifikiri kama itakuwa ni kitu kikubwa sana, lakini kwa maana ya kuanzia angalau tumeanza, nashauri pia, kama tunataka kufufua Shirika la ATC, mbali ya kwamba tunatakiwa tufagie ATC yote, lakini pia tutafute strategic partners ambao wanaweza kutupa routes nyingine ambazo tutaweza kuzitumia.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa humu ndani routes zetu nyingi tumeshaziuza, tumempa Fast Jet kwa routes za ndani. Sasa utashindanaje na Fast Jet wakati ameshaweza kuji-establish kwa muda wa miaka mitatu ambayo yupo hivi sasa na wewe unakuja na ndege mpya? Kwa hiyo, ni lazima tuingie na Mashirika, tuwe na strategic partners ambao wataweza kutusaidia kutufungulia njia nyingine.
Mheshimiwa Spika, pia tutafute model nzuri ya kuwa na Shirika la Ndege. Ethiopia pamoja na kwamba walikuwa katika kipindi cha Haile Selassie, vita, udikteta, lakini bado ni shirika ambalo lilikuwa haliguswi na ndiyo maana limebaki kuwa shirika la mfano kwa Afrika na linafanya kazi na limekuwa likienda vizuri. Kwa hiyo, tusione aibu kuazima management au kuchukua management ikaja kutuwekea sawa mambo ili Shirika lile liende katika hali inayoweza kufaa na ikatusaidia sote kama nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kusemea ni suala la usalama na utawala bora. Nina mifano michache sana ya nchi ambazo zimeweza kufanikiwa katika kuingia kuwa nchi za viwanda ambazo zimekuwa hazina utulivu au zimekuwa zikiendeshwa na madikteta. Nchi chache kama Singapore na Lee Kuan Yu mfumo wake wa uongozi ulikuwa ni wa kubana lakini ilifanikiwa.
Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo hatuwezi kuliachia hivi hivi. Hatuwezi kuwa na chaguzi ambazo kila mara sauti ya wananchi haisikiki, hatuwezi kuwa na chaguzi ambazo Serikali inapeleka majeshi na inalinda chama kimoja halafu tutarajie kwamba tutapiga hatua katika maendeleo. Kwa hiyo, suala hili ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho ningependa ku-cut across the board ni suala la disability, watu wanaoishi na ulemavu. Hili ni eneo ambalo Mbunge yeyote humu ndani halizungumzi kama vile siyo kesho yeye litamtokea.
Mbunge yeyote hazungumzi, kama vile hatuna asilimia 12 ya Watanzania ambao wana ulemavu wa aina moja au aina nyingine. Kwa hiyo, napenda program yote ya Serikali tusiseme tu katika UKIMWI, lakini pia katika disability, ika-cut across kote ili tuweze kutengeneza mazingira na tuweze kufanikisha ili kuona watu wenye ulemavu wanaweza kuchangia na wanaweza kupata fursa za aina nyingine yeyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho nataka kusemea juu ya kile ambacho Waziri Simbachawene alikitolea taarifa hapa juu ya mshahara wa Rais. Actually aliye-raise suala la mshahara wa Rais ni yeye mwenyewe Rais. Ame-raise mshahara wa Rais yeye mwenyewe kwa sababu pengine alitaka liwe publicity stunts kwamba yeye ni Rais ambaye anapunguza mshahara na kwamba yuko pro-people na hivi na hivi. (Makofi)
Kwa hiyo, hili suala limekuja hapa siyo kwa sababu sisi tumelianzisha, ni kwa sababu yeye alianzisha. Kama itakuwa ilikosewa, ni kwamba waliomshauri walikuwa wamwambie kumbe hawezi kubadilisha mshahara wake akiwa yeye katika madaraka, lakini wanaofuata wanakuwa na madaraka. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa lakini wakati mwingine wananchi wanajua wapi pana publicity stunts na wapi ni sifa ya kweli. Ahsante sana.