Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Rashid Ali Abdallah

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo leo hii kusimama hapa. Pia nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na kupongeza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa jinsi ilivyoelekeza Serikali kwa mwelekeo wa mwaka 2017/2018. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nitazunguka katika maeneo machache kabisa kuhusu ulinzi na usalama wa taifa, utawala bora na uchumi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote duniani inaongozwa kwa kutegemea Katiba na Sheria. Ni hatari kubwa sana kuona Katiba na Sheria za nchi zinavunjwa wakati watawala wanasaidia na kufurahia. Narejea, Katiba na Sheria zinavunjwa katika nchi hii, watawala wanasaidia lakini pia wanafurahia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri zaidi ni uchaguzi haramu wa Zanzibar wa Machi, 2015. Uchaguzi huu ulivunja Katiba ya nchi, viongozi walifurahia na wamesaidia, lakini tunasema mapambano yanaendelea, haki ya Zanzibar tutaidai na tunaendelea kuidai na itapatikana kwa hali yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitendo vya uvunjaji wa sheria kwa Msajili wa Vyama Siasa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ni Kamati ya Bunge, inapofanya kazi Kamati ya Bunge ina maana Bunge zima linafanya kazi. Taarifa za Kamati ya Katiba na Sheria inaweka wazi kwamba Msajili
wa Vyama vya Siasa amevunja Sheria za Vyama vya Siasa na kuingilia uhuru wa vyama vya siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni taarifa ya Bunge na taarifa ya Bunge inakemea kitendo hiki cha Msajili wa Vyama vya Siasa. Kauli hii ni ya Bunge, siyo Kamati ya Katiba na Sheria.
Waheshimiwa Wabunge wote lazima mwone hili lipo na limekemewa na Kamati ya Katiba na Sheria. Kwenda kinyume kwa Msajili kwa vitendo hivi, atakwenda kinyume na taarifa za Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo siikubali na Kamati ya Sheria ilimwita Msajili, ikamhoji (ukurasa wa 30 naendelea kusoma) na ikamwonya Msajili huyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba masikitiko yangu na nitaendelea kusikitika sana kuona Jeshi la Polisi linashiriki kisiasa wazi wazi na kuleta hujuma na kuvunja sheria wakati Jeshi la Polisi linalinda uvunjaji wa sheria. Nalaani sana vitendo hivi. Watu wote mnafahamu, mnajua na mnaona, halihitaji ushahidi, Serikali imenyamaza kimya. Hii nasema ni mkakati wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi limepoteza mwelekeo kwa wananchi na litaendelea kupoteza mwelekeo kwa wananchi kwa sura hii, tutakuwa hatuna imani kabisa na Jeshi la Polisi. Na mimi nilishasema, sitaki kuchangia Jeshi la Polisi, sina imani kabisa na Jeshi la Polisi.
Baadhi ya Jeshi la Polisi wanavunja sheria, Serikali ipo inayamaza kimya, wanashiriki uvunjaji wa majengo ya chama, Jeshi linalinda na linaangalia tu bila kuchukua hatua yoyote. Kitendo hiki ni kibaya sana kwa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msajili pamoja na washirika wake mlivunja Katiba ya Vyama vya Siasa na mlivunja Sheria za Usajili. Kwa kufanya hivyo, amevunja msingi mkubwa wa utawala bora na kwa misingi hiyo, amevunja demokrasia nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Msajili ajue, matokeo yake ni nini? Matokeo yake ataliingiza Taifa hili katika mgogoro mkubwa kwa Muungano wetu, lakini atahatarisha amani ya Taifa hili, la tatu, ataingiza Taifa hili katika mgogoro wa kiuchumi. Mnalifurahia lakini matokeo
yake mtayaona mbele tunakokwenda. Kwa kufanya haya, uchumi wetu utadorora, ndani na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende haraka haraka kuhusiana na masuala ya uchumi. Sekta za uzalishaji mara nyingi zinakuwa ni sekta za kiuchumi na kwa maana hiyo kuna nchi nyingi ambazo zimejikita katika maeneo mahsusi ya kiuchumi, kwa mfano, nchi ya Afrika Kusini imejikita katika biashara, madini na utalii; Algeria mafuta na uzalishaji; Nigeria mafuta na mawasiliano, Morocco utalii, viwanda vya nguo pamoja na kilimo. Tanzania kuna msururu kabisa, series!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kuna series za mambo ya kiuchumi, kuna kilimo, viwanda, maliasili, madini, gesi, usafirishaji and so on and so forth. Kilimo kinawakilishwa kwa asilimia 75 na Watanzania, kilimo kinabeba Watanzania wengi sana, lakini awamu hii inaelekea kana kwamba kilimo siyo kipaumbele chake hasa, kina viashiria hivyo. Nasema hivyo kwa sababu mwaka 2015/2016 Serikali iliyopita ilitoa pembejeo za kiasi cha shilingi bilioni 78, lakini Serikali hii hadi kufika hapa imetoa pembejeo za shilingi bilioni 10. Kutoka shilingi bilioni 78 mpaka shilingi bilioni 10, hivi kweli Serikali hii inawaambia nini wakulima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kusema kwamba kilimo kinaanza kushuka na kwa sababu hakuna mbolea ya kutosha ambayo imetolewa na Serikali, tutegemee upungufu mkubwa wa mazao katika kipindi kinachofuata. Hili litakuwa ni tatizo kubwa kweli kwa wananchi walio wengi wa
Tanzania.