Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.
Kwanza kabisa niapongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, nampongeza Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wake, Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Mavunde pamoja na Baraza zima la Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Wabunge wenzangu wa Tabora kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutatua kero ya tumbaku Mkoani Tabora. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakuombea kila la heri, Mwenyezi Mungu akuwezeshe ili umalize kero hii ya tumbaku ambayo imetukabili kwa miaka mingi sana. Tunakuamini, tunajua utaimaliza na umedhamiria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya, wameanzisha programu maalum ya kuhakikisha wanafuatilia Ilani ya Chama cha Mapinduzi itekelezeke, lakini kufuatilia ahadi zote za viongozi wakuu. Nawapongeza pia kwa kuhamia Dodoma, wamefanya kazi kubwa. Tulikuwa tunasikia toka tukiwa wadogo kwamba Serikali inaenda Dodoma, lakini imeenda Dodoma leo hii. Tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Kitengo cha Baraza la Uwezeshaji ambacho kipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Baraza la Uwezeshaji limefanya kazi kubwa ya kuwatambua, kuwabaini wajasiriamali wadogo ambao kwa Mkoa wa Tabora wameianza kazi hiyo na kuwawezesha
kuwapa mitaji ili waweze kusonga mbele na huu ndiyo uchumi wa kati ambao tunautaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri tu Serikali yangu, naishauri Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba hili Baraza la Uwezeshaji lingeungana na watu wa SIDO likaungana na Wizara ya Viwanda ili kuwawezesha hawa wajasiriamali wadogo sasa waweze kuingia kwenye viwanda vidogo
vidogo, mkiungana nadhani itakuwa vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee kuhusu bajeti. Nimesikia wenzangu wanasema kwamba kulikuwa na bajeti hewa, nimesikia jana kuna neno linaitwa bajeti hewa ambapo mimi kama Mbunge wa Tabora sikubaliani na hiki kitu cha bajeti hewa na sababu ninazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ukiniambia bajeti hewa, mimi nimeingia hapa Bungeni mwaka 2011, nilikuwa nahangaika kila siku kugombana kuhusu maji ya mradi wa Ziwa Victoria, leo hii mkandarasi yuko site toka mwaka 2016. Kwa hiyo, ukiniambia bajeti hewa, siwezi
kukuelewa. Tulikuwa tunahangaika na barabara ya lami ya Chaya – Tula ambayo inaunganisha kutoka Dar es Salaam - Tabora mpaka Urambo kwa lami, leo hii mkandarasi yuko site. Pia tulikuwa tunahangaika kwamba uwanja wetu wa ndege unatua ndege ndogo tu, leo hii mkandarasi yuko site anafanya matengeneza ya kupanua uwanja wa Tabora.
Kwa hiyo, sikubaliani kabisa na kuniambia kwamba kuna bajeti hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, punda hasifiwi kwa rangi zake, anasifiwa kwa kazi anazozifanya na mzigo anaobeba. Hii Serikali ya Hapa Kazi Tu inafanya kazi sana, Rais wangu Mheshimwia Dkt. Magufuli anafanya kazi sana. Wamwache Mheshimiwa Rais afanye kazi! Toka nikiwa mdogo nikiwa Tabora nasikia Waheshimiwa Wabunge wa Tabora wanalalamika kuhusu reli ya kisasa, lakini leo hii minara ya reli ya umeme imeanza kutengenezwa. Reli ya standard gauge inajengwa. Leo mtu ananiambia kuna bajeti hewa, sitakaa nikubali. Huu ni uongo na niwaombe Wabunge wenzangu, tuseme Serikali inapofanya mambo mazuri, tusinyamaze, tusiogope, tuseme. Nimetoka kifua mbele, nasema Serikali yangu imefanya mambo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa humu Bungeni kipindi kilichopita, kaka yangu Mheshimiwa Zitto kama yupo atasema. Tulikuwa tukisimama tukiungana kulilia ndege, wanasema nchi gani hii, inashindwa hata na Rwanda, haina hata ndege moja. Leo tuna ndege, watu wanasema kwa
nini tumenunua ndege? Wamwache Mheshimiwa Rais afanye kazi, waiache Serikali ifanye kazi. Tukifanya kazi, mnasema, tusipofanya kazi, mnasema. Tunajua binadamu hata ufanye nini, hawezi kukusifia kwa asilimia 100, tufanye kazi kama tulivyojipangia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea elimu bure.
Kuna mtu labda ana hela watoto wake hawasomi shule hizi anaona utani. Leo hii shule zimejaa, madarasa yamejaa, watoto wanasoma, hakuna ma-house girl vijijini. Yote hii ni juhudi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu na Serikali yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeona juzi, mwaka 2016 hii bajeti hewa UDSM, leo hii watoto 4,000 watakaa kwenye mabweni UDSM, yamejengwa kwa muda wa haraka sana. Leo unaniambia Serikali haijafanya chochote, sitakubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, REA, tumemwona Mheshimiwa Muhongo huko, umeme unawaka vijijini. Leo hii tunashindwa kusifia Serikali yetu. Nawaomba Wabunge wenzangu, tusiingie baridi, tutoke tuseme mema yaliyofanywa na Serikali yetu. Watu wanasema viwanda, viwanda gani? Vitajengwa lini? Viwanda hewa. Mpaka hapa ninapoongea, tunajenga viwanda 2,160 na hii issue ya viwanda tumeanza juzi mwaka 2016, Magufuli kaingia mwaka mmoja. Mimi niwaulize Wabunge wenzangu, ninyi kwenye Majimbo yenu mwaka mmoja mmefanya mangapi?
Mbona mnaisema Serikali tu! Kuna watu hapa hawajawahi kufanya chochote.
Akimwona DC ameenda kwenye mkutano wa DC, naye anakwenda kama Mbunge. Lako wewe kama Mbunge liko wapi? Tuoneshe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali yangu, nampongeze Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wake, wanafanya kazi. Hii nchi ni kubwa jamani, kazi ni ngumu. Ni rahisi sana kukosoa, lakini ukiambiwa kafanye wewe, hiki kitu ni kigumu
jamani, tuwatie moyo, tuwaombee kwa Mwenyezi Mungu waweze kutekeleza walioyaahidi. Ni faida yetu sisi wote.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajisifu Tanzania ni kisiwa cha amani, Tanzania ina amani, Tanzania ina utulivu, nani aliyetuletea utulivu? Ni Usalama wa Taifa. Leo tumo humu, tuna amani tu. Leo tukitoka tutaenda Club, tunaenda tunarudi hata saa 9.00 usiku, tuna amani. Kama kuna madoa madogo madogo, basi yatashughulikiwa, lakini tusiseme Usalama wote hawafanyi kazi. Hiki kitu nakataa na nitaendelea kukataa. Tuko hapa kwa sababu ya amani.
Tunajisifu, tuna sifa dunia nzima, kisiwa cha amani. Amani inatengenezwa, kuna watu hawalali kwa ajili ya amani hii tuliyonayo, ni lazima tuwatie moyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifuga mbwa ukiona habweki, bweka mwenyewe. Leo nimeamua kusema mwenyewe. Wenzetu hawa kama hawayaoni haya, leo nimeamua kuyasema mimi niliyeyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee kidogo kuhusu Msajili wa Vyama vya Siasa (Registrar), amekuwa akishambuliwa sana. Nasema vyama vingi ni tatizo, ni kazi kubwa. Sheria zake anazozisimamia, ndiyo maana leo tumekaa Wabunge wa CUF, wa CCM, wa CHADEMA
tunaongea kwa sababu wa usimamizi mzuri wa Registrar.
Tulishuhudia watu walitaka kupigana viti kule Ubungo kwenye mikutano yao, lakini Registrar kwa kazi yake kubwa aliyoifanya, ndiyo leo CUF kuna amani na utulivu. Ndiyo leo wameweza kukaa pale wote wakiwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata shida sana tunapokuwa tunawashambulia wataalam, tuwatie moyo kwa kazi wanazozifanya. Pale kwenye upungufu tusiache kusema; tuseme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie kusema, naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, nampongeza sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli na sisi tumwambie tupo, tutasema. Sisi ni wanasiasa, kazi yetu ni kusema. Tutasema na tunamuunga mkono kwa asilimia mia moja kwa kazi anazozifanya. CCM oyee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunisikiliza.