Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Pia naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ameweza kunijalia afya njema ili niweze kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kuongelea suala zima la uwezeshaji wananchi kiuchumi. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 15 ameongelea suala la uwezeshaji wanawake kiuchumi na ukisoma pale ndani ameandika kuhusiana na maendeleo ya wanawake kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake wa mwaka 2007 ambao unalenga kuwawezesha wanawake kiuchumi ili waweze kukopesheka. Lakini kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 Mfuko huu wa Maendeleo ya Wanawake haukutengewa fedha zozote. Naomba niiombe Serikali itusaidie kutenga fedha kwa ajili ya kuuwezesha huu Mfuko
wa Maendeleo ya Wanawake ili wanawake waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa nina kikao na wanawake wa Mkoa wa Mwanza, kwa kweli swali zito ambalo nilikumbana nalo ni huu Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. Wanauliza Mfuko huu wa Maendeleo ya Wanawake unawasaidiaje wanawake ili waweze kujishughulisha na masuala mazima ya uchumi? Ukiangalia wanawake wengi wa Mkoa wa Mwanza wanajishughulisha na shughuli mbalimbali kama vile mama lishe hata wamachinga pia wapo ambao ni wanawake lakini kama Mfuko huu wa Wanawake usipotengewa fedha, ni jinsi gani
wanawake wataweza kujikwamua kiuchumi? Hivyo, naomba sana katika bajeti ya Waziri Mkuu basi suala hili la wanawake liweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika mataifa makubwa duniani na hata yale ya nchi jirani kama vile Zimbabwe, Malawi na Msumbiji na nchi nyingine hata Kenya tu hapo jirani, wamekuwa wakiliangalia suala zima la wanawake katika kutenga bajeti. Ukiangalia hapa Tanzania katika bajeti zote ambazo zimekuwa zikitengwa suala la mwanamke limekuwa liki-lag behind. Unakuta mwanamke anatajwa katika maeneo machache sana. Sisi wanawake tumeamua sasa kuiambia Serikali, lakini kuiomba kwa unyenyekevu mkubwa sana kwamba sasa ianze kuangalia suala zima linalowahusu wanawake. Kwa sababu wanawake ndiyo ambao wanachangia katika pato la Taifa na hivyo basi naomba wasiachwe nyuma. Hivyo basi, naendelea kuisihi Serikali yangu kuuangalia mfuko huu na kuweza kutenga fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Wizara hii ya Afya inayoshughulika na wanawake, huyu mama ambaye ndiyo ameshikilia hii Wizara, dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, tunapomuweka kuwa yeye ndiyo mshika dhamana ya wanawake hapa Tanzania halafu mfuko ule haujatengewa fedha, ina maana tunamdhoofisha huyu dada katika kuisimamia hii Wizara ya wanawake. Kwa hiyo, naendelea kusisitiza na kuiomba Serikali, kwa mwaka huu wa fedha iweze kutoa fedha na kuweka kwenye mfuko ule ili kuweza kuwasaidia wanawake kwenye VICOBA ambavyo wamevianzisha waweze kujikopesha na kuweza kujikwamua kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niongelee suala la afya. Katika hotuba ya Waziri Mkuu ukiangalia ameongelea suala zima la afya na amesisitiza kwa kusema kwamba Serikali inaendelea kujenga vituo vya afya ili kuhakikisha wanawake nchini wanapata huduma za kiafya
vizuri. Ukiangalia katika afya kuna pillars tatu, yaani zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali za Wilaya. Kule ndiko ambako zile basic needs za afya zinaanzia. Katika Mkoa wa Mwanza tunavyo vituo vya afya vya Serikali 46 tu ukiunganisha na vituo vingine vya binafsi jumla ni vituo 388.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hivi vituo 46 va Serikali ni vituo vinne tu katika mkoa wa Mwanza ndivyo ambavyo vinatoa huduma ya upasuaji. Wanawake wengi wamekuwa wakipoteza maisha wakati wa kuleta watoto hapa duniani. Ukiangalia idadi ya vifo vya akina mama Mkoa wa Mwanza ni 21% na hiyo inatokana na kukosa huduma za upasuaji katika vituo vyetu vya afya. Hivyo basi, naiomba Serikali iweze kutusaidia katika Mkoa wa Mwanza kuwezesha kutupa vituo vya afya ambavyo vinaweza vikatoa huduma za afya ili viweze kuongezeka kutoka vituo vinne tufikie hata vituo 15 kwa kuanzia ili wanawake wasiweze kuendelea kupoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Sustainable Development Goals, goal mojawapo ni
kuhakikisha huduma za mama na mtoto na za wajawazito zinapatikana kwa urahisi na kuendelea kuondoa vile vifo vya mama na mtoto. Kwa hiyo, kama tumeingia mkataba huu
wa kwenye Sustaibale Development Goals, naiomba Serikali iweze kutusaidia katika Mkoa wa Mwanza kutuboreshea vituo vyetu vya afya ili viweze kutoa huduma ya upasuaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka siku moja hapa nilipokuwa nikiuliza swali langu la nyongeza niliuliza suala la wanawake wanavyopata huduma za upasuaji lakini hawapati huduma za upasuaji kwa kupangiwa. Nilipokuwa naongea kile kitu nafahamu kwa sababu mama anapopata ujauzito kuna matatizo ambayo huwa yanaonekana kwenyescan kabla hata muda wake wa kujifungua haujafika. Kwa hiyo, kama tatizo limeshaonekana na kwenye kituo cha afya kuna huduma ya upasuaji, mama huyu anatakiwa apangiwe ni lini na siku gani atakayofanyiwa upasuaji ili kuweza kuokoa maisha yake yeye kama mama lakini pia na maisha ya mtoto yule ambaye anamleta duniani. Kina mama wengi sana wamekuwa wakipoteza maisha yao lakini mtoto anabaki kwa sababu ya kutoa damu nyingi na matatizo mengine
mbalimbali ambayo yanawakumba akina mama wakati wa kujifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika hotuba ya Waziri Mkuu wameeleza ni namna gani bajeti ya vifaa tiba pamoja na dawa imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 hadi shilingi bilioni 251. Katika kuongezeka kule sisi Mkoa wa Mwanza naiomba tu Serikali katika bajeti hii ya mwaka huu iweze kutusaidia CT Scan, Mkoa wa Mwanza hatuna CT Scan. Ukiangalia CT Scan inasaidia katika mambo mengi sana si tu wanawake. Kuna watoto wanazaliwa kule na vichwa vikubwa Mkoa wa Mwanza lakini na Kanda ya Ziwa kwa ujumla… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naunga mkono hoja.