Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushukuru kwa kupata nafasi na pia nipende kuwapongeza Mawaziri wanaofanya kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Mheshimiwa Jenista alifika mpaka kule Jimboni Mafinga akazungumza na wajasiriamali na akina mama kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia Baraza la Uwezeshaji, pia ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde hakuwa na ziara rasmi lakini alivyopita pale akasimama stand akaongea na vijana kuwatia moyo, kwa hiyo, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tunajadili hotuba ya Waziri Mkuu ambayo ndani yake kuna Bunge, moja kwa moja nizungumzie kuhusiana na ufanisi wa ufanyaji kazi wa Bunge. Tumeshuhudia siku zilizopita badala ya kukutana wiki tatu tumekutana wiki mbili. Kwa mujibu wa Katiba, wajibu wa Bunge ni kuisimamia na kuishauri Serikali na sehemu mojawapo ya kuisimamia ni kupitia tunavyokutana kwenye
Kamati, lakini pia tunavyokagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali. Niombe bajeti hii pamoja na jinsi ambavyo tumeambiwa imeongezwa, iliangalie Bunge katika namna ambayo italiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aeshi amezungumza hapa kuhusu Bunge Sports Club, sisi tulioenda Mombasa kwenye mashindano ya Bunge tunajua kilichotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumechagua Wabunge wa EALA ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika masuala mazima ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo suala la michezo. Tumekwenda kule kuna watu tulikuwa tunapanda kwenye karandinga, huu ni ukweli mpaka kuna watu
wametuuliza ninyi ni Wabunge kweli maana we were seen like a second citizen wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niombe kwa nia ya kufanya kazi kwa ufanisi, tumeona hapa wakati wa kukagua miradi Wabunge wanasafiri na double coaster zinaharibika njiani. Hata security yao, pamoja na kuwa wanakuwa na maaskari mle ndani lakini kuna healthy
security, afya yao katika kusafiri kwenye mazingira ya magari ambayo basically yamejengwa kwa ajili kuwa school bus sio jambo jema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba ili Bunge lifanye kazi kwa ufanisi hebu kile kinachotengwa kipatikane. Kwa sababu sisi hatufanyi kwa kujipendekeza, tunafanya kazi kwa mujibu wa Katiba iliyowekwa. Naomba hilo tulitizame sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu pembejeo. Wamezungumza Waheshimiwa hapa na kaka yangu Mgimwa amesema. Tumesikia kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu amekutana na watu waliokopesha pembejeo, ni kweli matajiri wakubwa walikataa kuwahudumia
wakulima wetu, wafanyabiashara wadogo wadogo wakajitokeza. Kwa hiyo, mimi niombe baada ya uhakiki watu hawa walipwe pesa zao. Kwa sababu ni kupitia kilimo watu wetu kwa mfano mimi kule Mafinga kuanzia Bumilainga mpaka Itimbo watu wale hawana shida, wewe wape
mbolea tu ni wapiga kazi wazuri. Vijiji vyote Isalamanu na Kitelewasi watu wanalima mwaka mzima lakini wapete tu mbolea kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hawa ambao wamekopeshwa wapewe fedha zao kwa wakati ili kusudi wakati ujao waweze kuwa na moyo wa kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi wetu. Kwa hiyo, niombe sana Ofisi zinazohusika, najua itakuja Wizara ya Kilimo tutalisemea, lakini suala la pembejeo ni suala linalogusa maisha ya watu.
Kwanza, mbolea zifike kwa wakati kwa sababu msimu unajulikana. Sasa mbolea ya kupandia iende mwezi wa pili sio jambo zuri, wananchi wanaona kama tumewatelekeza.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa nadhani wa 16 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu umezungumzia kuhusu kutenga maeneo kwa ajili ya biashara. Mimi niombe mamlaka zinazohusika, Halmashauri zetu kwa hali ilivyo baada ya kutoa ule utaratibu wa retention haziwezi kuwa
na fedha kwa ajili ya kutenga maeneo, kwa sababu tunaposema kutenga haiishii tu kutenga ni pamoja na kuyapima maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa Halmashauri hazina nguvu hii tena tuje na utaratibu ambao tunaweza tukazisaidia, zikatenga maeneo yakapimwa yakajulikana haya ni maeneo ya biashara, haya ni maeneo ya wafanyabiashara wadogo wadogo na yakajengewa
miundombinu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotuba yake amempongeza Alphonce Simbu, huyu ni mwana michezo.
Sasa katika kutenga maeneo pia tuzisaidie Halmashauri zitenge maeneo kwa ajili ya michezo. Kwa sababu ni kupitia michezo vijana wanapata ajira na kupitia michezo tunapata akina Samatta na hawa akina Simbu. Bila kuwa na miundombinu kwa maana ya viwanja hatuwezi kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kupitia michezo tumeona hapa utalii umeongezeka kwa asilimia 12 lakini kupitia michezo tunaweza tukafanya promotion kwa wepesi zaidi. Leo hii Simbu ameshinda Mumbai Marathon ni Wahindi wangapi India wameweza kuifahamu Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba Halmashauri bado hazijaweza kuwa na nguvu especially kama ya Mji wa Mafinga. Wananchi wamejitahidi wamejenga zahanati, juzi tunashukuru Ubalozi wa Japan umetusaidia tujenge theatre. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwenye Halmashauri kama hizi ambazo ni mpya na wananchi wamejenga maboma itie nguvu yake katika kuhakikisha kwamba zahanati zinakamilika. Vilevile kama ambavyo Serikali imefanya kwenye utaratibu wa kuwapata walimu wa sayansi na hesabu pia tuweke utaratibu na tupate vibali ili
kusudi watumishi wa kada ya afya nao waweze kuongezwa katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa haya yote tunayoyasema na kuyatekeleza na tutakayoyatekeleza yatafanikiwa tu ikiwa Serikali kwa macho mawili itaangalia welfare ya watumishi wa umma. Chochote tutakachofanya kama watumishi wa umma morale wako chini nadhani
kwamba hatuwezi kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa tutazungumza kwenye Wizara husika lakini Serikali iangalie kama wamepata promotion, waweze kulipwa zile haki zao zinazoendana na promotion zao na welfare yao kwa ujumla watumishi wa umma. Kwa sababu hawa pamoja na
rasilimali fedha ni watu muhimu kuhakikisha kwamba tumefanikisha mipango tuliyoipanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.