Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kunipa afya njema na kupata nafasi ya kusema machache kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini pia na Kamati ambazo ziliwasilisha maoni yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na kwenye hiki kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 21. Waziri Mkuu ametoa takwimu za upatikanaji wa chakula kwa mwaka uliopita na akagusia kwamba mwaka huu kuna maeneo ambapo hali ya hewa haikuwa nzuri sana. Nilichokuwa nakitegemea hapa kidogo na nitoe ushauri ni kwamba kutokana na hali hiyo kutokuwa nzuri, kwanza nilitarajia nione hapa kama kuna akiba kiasi gani sasa ya chakula lakini tunakitumia kwa namna gani ku-control bei inayoendelea kupanda kwenye soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza jana Mwanza gunia la mahindi lilikuwa shilingi 125,000 na wakati kelele za uhaba wa chakula zinaanza gunia la mahindi lilikuwa shilingi 80,000. Hii maana yake ni nini? Kadri tunavyokwenda kuja kufikia mwezi wa kumi kama hakuna
mechanism ya Serikali ku-control bei ya mahindi yatafika shilingi 160,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachozungumza hapa sio njaa, hatuzungumzi njaa tunazungumzia kwamba bei ya chakula inapanda kwa sababu Serikali ni kama haijachukua position yake ya ku-control bei ya chakula kwenye soko. Wakati tunazungumza wakati ule bei ya mchele ilikuwa
shilingi 1,200 leo ni shilingi 2,500, Mwanza ni shilingi 1,800. Maeneo yote haya ninayoyazungumzia hawakulima kwa sababu mvua hazikuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ombi langu Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama tunayo stock ya chakula kwenye godowns, Wizara ichukue position yake, chakula kingie kwenye masoko na bei elekezi itolewe ili kisiendelee kupanda, vinginevyo purchasing power ya wananchi
inapungua. Wananchi kipato ni kilekile, chakula kinapanda, matokeo yake watajikuta hata hiyo shilingi 2,000 ya kula kwa siku inakosekana. Hilo ndiyo lilikuwa ombi langu kwenye huu ukurasa wa 21.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 25 amezungumzia kuhusu hekta 38,567 za wachimbaji wa madini. Tatizo langu mimi sio utengaji wa maeneo, nilimwambia Waziri wa Nishati na Madini, alikuja Geita akazungumza takwimu kubwa za
kuwapa watu maeneo ya kuchimba. Nikamwambia tatizo kubwa lililoko hapa wanaopewa ni walewale. Ukiingia kwenye database utamkuta Kanyasu huyu ana-appear kwenye karibu kila eneo dhahabu inapotokea wale ambao wanatakiwa kabisa wapewe maeneo haya hawapewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza na wewe tuna vikundi zaidi ya 100 Geita vimejiandikisha vinasubiri maeneo ya kuchimba havipewi, lakini ukienda kwenye takwimu za Wizara atakutajia kubwa ya watu ambao kimsingi ni walewale wachimbaji wakubwa ambao wanahama toka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana, ni ahadi yetu kwenye Ilani ya CCM, tutawapa watu maeneo ya kuchimba, lini? Huu ni mwaka wa pili sasa. Kama yapo tunaomba yaanze kutolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 28 limeongelewa suala la umeme. Geita kila siku umeme unakatika. Hivi ninavyozungumza na wewe umeme hakuna, unakatika zaidi ya mara nne. Nimezungumza na Waziri na Naibu Waziri, wana matengenezo ya kutoka Busisi kwenda
Geita karibu miaka miwili hayaishi. Nataka kufahamu hili tatizo la umeme Geita linakwisha lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo, kuna maeneo tumepeleka umeme wa REA baada ya umeme wa REA kufika kazi imeisha, jirani akiomba umeme TANESCO hakuna vifaa. Ina maana REA peke yake ndiyo sasa inafanya kazi ya kusambaza umeme, TANESCO wenyewe hawana uwezo? Naomba sana eneo hili lifanyiwe kazi vizuri kwa sababu linakatisha tamaa, kama umeme umefika kijijini, kuna watu wanne wamepewa umeme, jirani hapewi umeme kwa sababu TANESCO hana vifaa, nadhani hapa kuna mipango mibovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la fao la kujitoa. Mimi natoka Geita na naomba Waheshimiwa Wabunge wote wanisikilize vizuri sana. Geita pale karibu nusu ya watu wanaofanya kazi pale Geita Mjini ni watumishi wa mgodi. Kinachotokea kwenye mgodi pale ni kwamba
hakuna mwenye ajira ya kudumu. Kuna watu pale wanafanya kazi kwa mikataba ya miezi sita, miaka miwili, miaka mitatu. Anapofukuzwa kazi hawezi kupata kazi ya aina ile tena katika nchi hii, kuna wengi ni vibarua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watu wanafukuzwa kazi, kwa sababu kandarasi iliyokuwa imempa kazi mkataba wake umekwisha, imeondoka imekwenda South Africa. Akienda kufuata pesa zake NSSF anaambiwa hizo pesa hawezi kupewa mpaka afike umri uliolezwa. Mtu leo ana
miaka 25 au 30 asubiri pesa hizi mpaka afikishe miaka 55 ndiyo aweze kulipwa na hana kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja ametoa hoja kwamba wapewe asilimia 25, hapana. Ziko kada ambazo wanaweza wakasubiri, ukimwambia mwalimu, polisi, daktari asubiri sawa. Pale mgodini kuna tabia supervisor akikuchukia anaku-blacklist,
akiku-blacklist huwezi kuajiriwa mgodi wowote duniani. Sasa unakaa unasubiri hiyo pesa mpaka utakapofikisha miaka 60 unaendelea kuwa maskini kwa misingi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri, sekta ya madini iangaliwe kwa jicho tofauti. Kuna watu pale wanaacha kazi kwa sababu ni wagonjwa. Mgodi ule hauchukui watu wagonjwa, ukitibiwa mara mbili unaumwa kifua wanakufukuza, Mheshimiwa Jenista unafahamu nilikuletea watu wanaumwa, walipokuwa vilema walifukuzwa kwenye kazi, wana miaka 25, 30 halafu wananyimwa zile pesa wanaambiwa wasubiri mpaka watakapozeeka, anazeeka hizo pesa aje atumie nani? Ushauri wangu ni kwamba sekta ya madini ichukuliwe kwa namna tofauti, hatuwezi kuwa na jibu moja kwenye maswali yote magumu, lazima tuliangalie hili suala tofauti. Kama tuna nia ya kuwekeza NSSF wana mitaji mikubwa waangalie sehemu nyingine, lakini haya maisha ya watu kwa pale Geita tutawafanya kuwa maskini zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna gereza pale Geita Mjini, uwezo wake ni kuchukua watu 100 na zaidi, hivi sasa lina watu 800, sababu kubwa ni wachimbaji wadogo wadogo ambao wanatafuta pesa ndogo ndogo ya kula, akikamatwa anarundikwa pale. Kuna tatizo sasa hivi kwenye Jeshi la Polisi na watu wa Idara ya Sheria, kesi ya madai inageuzwa inakuwa jinai wanarundikwa mle, matokeo yake watu wanalala wamesimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu Mheshimiwa Waziri Mkuu na nafikiri nilizungumza na wewe, pale kuna tatizo tuna OC-CID hafanyi kazi yake vizuri, kazi yake ni kukusanya pesa, anachokifanya yeye ni kuhakikisha kwamba kila anayetuhumiwa pale, iwe ni jinai, iwe ni civil lazima
abambikwe kesi ambayo itamuweka magereza zaidi ya miezi mitatu, gereza limejaa. Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe alikuja aliona, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ulikuja uliona, tunaomba mtusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna hizi kesi ndogo ndogo za kupita tu mgodini anakamatwa mtu anawekwa ndani miezi sita. Unapita tu na baiskeli unakamatwa unawekwa ndani miezi sita. Serikali ina pesa za kuchezea, kwa nini hizi pesa ambazo zinakwenda kulisha watu humo
wasipewe hawa wanasheria wakapeleka hizi kesi haraka? Mimi nadhani kuna haja ya kuisaidia Wilaya ya Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni uwepo wa migodi mingi sana kwenye Mkoa wa Geita na tatizo la huduma za afya. Wilaya ya Geita peke yake ina watu 800,000 kwa sensa ya mwaka 2012, lakini hospitali yetu iliyokuwa ya Wilaya tuliigeuza kuwa ya Mkoa, matokeo yake hatuna tena Hospitali ya Wilaya. Sasa ufikirie population ya watu 800,000 wa Wilaya moja na ile hospitali imegeuka kuwa ya mkoa, watu milioni mbili matokeo yake ile hospitali imezidiwa kabisa uwezo. Tuna vituo viwili vya afya tumeanza kuvitengeneza, tunaomba support yako Mheshimiwa Waziri wa Afya, tunakushukuru ulitupa gari lakini hatuna madaktari. Daktari aliyepo pale kuna specialist mmoja ambaye ni surgeon waliobaki wote ni AMO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru sana Serikali, tulitaka kuleta muswada hapa wa kuwaondoa Madaktari Wasaidizi kwenye mfumo wa madaktari, lilikuwa ni kosa kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule vijijini madaktari wetu ni ma-AMO na ndiyo wanaofanya kazi usiku na mchana. Ukiwaondoa wale kwenye mfumo wa madaktari waliobaki wengine wote ni mabosi wakienda kwenye wilaya kazi yao ni research, hawakai kwenye ofisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi namuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu mtusaidie sana Hosptali yetu ya Mkoa wa Geita ianze ili Hospitali ya Wilaya irudishwe Wilayani ili gharama za matibabu ziweze kupungua. Hivi sasa navyozungumza na wewe gharama za matibabu ziko juu sana kwa sababu tunalipa… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.