Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Joyce John Mukya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee alipoishia mwenzangu Mheshimiwa Zubeda kuhusu walemavu. Walemavu wamekuwa wakidhalilishwa sana, walemavu wamekuwa hawasaidiwi kimatendo. Kwenye hotuba ya Waziri Mkuu katika ukurasa wa 47 amezungumzia
suala la walemavu lakini hakuna mkakati wowote unaoonesha kwamba walemavu watasaidiwa kimatendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kama ambavyo tunatoa asilimia 10 kwenye Halmashauri zetu kutoka kwenye own source, naomba kwenye asilimia hizo hizo 10 iwe ni lazima kwa wanawake asilimia tano wawepo walemavu at least watano au 10 kwenye watu 30 na walemavu wengine watano kwenye watu 30 ambao ni vijana. Naomba sana kwa sababu walemavu hawa wanaonekana kwa macho tofauti na wanawake na vijana ambao mara nyingi wamekuwa wakitumika kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanasiasa mara nyingi wamekuwa wakiwatumia wanawake na vijana kwa ajili ya kuwatafutia kura kwa vipindi vya uchaguzi vijavyo lakini naomba sana suala la walemavu wamekuwa hawana msaada dhahiri unaoonekana. Naomba sana suala la walemavu, aliliongelea sana Marehemu Dkt. Elly Macha, naomba tumuenzi marehemu Mheshimiwa Macha kwa kuwasaidia walemavu wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hela za maendeleo; ni dhahiri kwamba Serikali yetu imeshindwa kabisa kuisaidia nchi hii kwa hela za maendeleo. Asilimia 34 tu mpaka bajeti inakwisha ya mwaka 2017, hakuna hela za maendeleo ambazo zimeenda kwenye Halmashauri zetu ambazo
zinaenda kuwasaidia moja kwa moja wananchi kule chini. Ingekuwa hakuna own source katika Halmashauri zetu, mfano, Arusha Mjini tunaendesha Halmashauri kutokana na own source zetu wenyewe. Mpaka Februari mwaka 2017 imeenda shilingi milioni 320 kati ya bilioni tatu ambayo ni asilimia 11 tu iliyopendekezwa mwaka 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tunavyoendelea hivi tunaenda kuua zile Halmashauri zetu, wananchi hawatapa maendeleo na kwa Halmashauri ambazo ziko vijijini hawana own source za maana, wanashindwa kuendesha vikao, wanashindwa kulipana hela za vikao, wanashindwa kufika kwenye vikao kutokana na umbali ama distance kulipana mafuta na gharama za usafiri kwa sababu tu Serikali haipeleki hela za maendeleo kule chini. Naomba sana hili mliangalie kwa jicho la pekee sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongele suala la utawala bora; kumekuwa na tabia mbaya sana Viongozi wa Serikali wanachukua madaraka mikononi na kuanza kutumia hela za Halmashauri au hela za Mikoa na Wilaya walizopangiwa kuanza kutumia bila kuwashirikisha Kamati za Fedha na Uchumi za Halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili limetokea mwaka jana Septemba. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Mrisho Gambo aliita Walimu wa AICC pale Simba Hall akaongea nao, wakahojiana, Walimu 701 wakampa madai yao akamuamuru Mkurugenzi wa Jiji, Ndugu Athuman J.
Kihamia awalipe wale Walimu shilingi 169.8 milioni, hii siyo sawa. Hata kama Walimu wale walikuwa wanatakiwa walipwe zile pesa lazima ilitakiwa vikae vikao vya Kamati ya Fedha na Uchumi, lazima vikae vikao lakini siyo Mkuu wa Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anaumia sana na wale Walimu angeingia kwenye Mfuko wake wa Mkoa na kutoa hela kwa ajili ya kuwalipa wale walimu. Hilo alilofanya siyo sawa, alipoambiwa akasema nawakomesha na hapa nimeanza tu lakini mtakoma. Pesa zile zilikuwa kwa ajili ya kuwalipa Madiwani, ilikuwa ni stahiki za Madiwani kwa ajili ya vikao, kwa ajili ya vocha, kwa ajili ya usafiri lakini Madiwani ambao wanaongozwa na Chama cha CHADEMA walivumilia yote na leo wanaenda kwenye vikao wanalipwa sh. 40,000 mpaka
sh. 60,000 mbali walivyokuwa wanalipwa sh.120,000 kwa kikao kimoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la Faru Fausta; Serikali hii imejitanabaisha kuwa inapunguza matumizi na mpaka sasa hakuna mtu yeyote ambaye analipwa milioni 17 kwa mwezi, lakini Faru Fausta analipwa milioni 64 kwa mwezi hiyo ni mara tatu. Gharama za Faru Fausta huyo ambaye ni Mzee ana miaka 54 ni kwa ajili ya gari lake ambalo linabeba chakula chake, kwa ajili ya chakula kinachotoka nchini Kenya aina ya LASEMI, kwa ajili ya kulipa Walinzi 15 ambao wanamlinda kwa masaa 24 na nguvu za Kijeshi. Faru Fausta huyu ni Mzee lakini ukiongea na Wizara ya Maliasili wanakwambia eti kwamba anaingiza fedha nyingi za kigeni sawa na bilioni 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini kama Wazungu au Watalii wanakuja Tanzania kumuangalia Faru Fausta peke yake. Naamini Watalii wanakuja Tanzania kuangalia utalii, kujifunza kutalii Tanzania lakini wakifika Tanzania wanakutana na Faru Fausta. Naomba sana Serikali kwa sababu inajidai kwamba inapunguza gharama na kutumbua majipu, ianze kumtumbua Faru Fausta ambaye ni Mzee sana sasa hivi na wanasema kwamba nyumba yake ikishakamilika atatumia milioni 20.4 tu sawa sawa na milioni 244 kwa mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado gharama hizi ni kubwa sana. Kule chini Ngorongoro wale Wamasai na wale wakazi wa Ngorongoro wanahangaika, hawana mahali pa kulisha mifugo yao, Serikali imeshindwa hata kuwajengea majosho kule juu kwa ajili ya kulisha mifugo yao, Faru Fausta ambaye ni Mzee anahudumiwa kwa milioni 64 kwa mwezi, hii siyo haki na siyo sawa kwa wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie katika suala la elimu bure; elimu bure ni kwenye makaratasi tu, ukienda kule chini elimu bure hakuna cha elimu bure zaidi ya kulipa ile UPE. Walimu wamekuwa kwanza wanahangaika, hakuna walimu wa sayansi, hakuna walimu wa hisabati, imefikia wazazi wakae vikao na walimu na wanafunzi kutafuta walimu wa hisabati na walimu wa sayansi. Inabidi walimu wakae vikao na wanafunzi na wazazi kulipa walinzi, kulipa maji kwa ajili ya wanafunzi wao waweze kusoma, hii siyo sawa kabisa hapa hakuna elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Ma-DC na Ma-RC badala ya kupigana na Wapinzani kwenye Wilaya zenu na Mikoa yenu, tafuteni njia mbadala ya kusaidia a elimu bure ambayo ni sera ya Serikali yenu. Kama mnaweza kuchangisha hela za Mwenge, Mheshimiwa Gambo Arusha alinunua pikipiki 200 kwa kusaidiana na wadau wa Mkoa wa Arusha sasa Mheshimiwa Gambo fanya hili la elimu bure kwa watoto ambao wanakua sasa hivi. Naomba sana hili mliangalie kwa jicho la pekee kabisa, hakuna elimu bure hapa ni utapeli tu wa makaratasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende katika suala la utalii; suala la utalii tangu kodi na tozo za utalii zipande limekuwa halina faida kwa nchi yetu. Kama mnavyofahamu nchi ya Kenya ndiyo imekuwa mpinzani mkubwa sana kwetu kwa suala la utalii. Nchi ya Kenya imeondoa kodi ya VAT, nchi ya Tanzania imeweka kodi ya VAT, nchi ya Kenya imeondoa kodi kwenye magari ya utalii wakati wa matengenezo, nchi ya Kenya imeondoa Visa kwa watoto na kuwafanya watalii ambao wana familia waende Kenya na siyo Tanzania. Nchi ya Kenya imeondoa Park fees Tanzania vyote hivyo mmeviweka, Tanzania mnataka utalii wa aina gani ninyi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Tanzania, naomba sana nchi yetu, naomba sana Waziri Mkuu anavyokuja kujibu utalii Tanzania umeshuka katika ukurasa wa 20 amesema kwamba utalii umepanda kwa asilimia 1.2 siyo kweli. Wageni hawa ambao wanaingia nchini ni wageni ambao wanakuja kwenye mambo ya kibiashara na mikutano lakini takwimu za utalii zinasema wageni wote wanaokuja Tanzania ni watalii siyo kweli, siyo watalii wa vivutio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wageni wengi wanatokea Rwanda, wanatokea Burundi, wanatokea South Africa na hii ni kwa sababu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu anapopewa takwimu zipitie na watu wako, anapokuja hapa kwenye Bunge ziletwe
takwimu ambazo ni sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee mimea vamizi katika crater ya Ngorongoro. Kumekuwa na mimea vamizi sana katika crater ya Ngorongoro. crater ya Ngorongoro kuna uoto wa asili. Mimea vamizi imeharibu crater ya Ngorongoro, Waziri January Makamba alienda lakini
hali ni mbaya na mbaya zaidi mimea hii inakua kwa kasi sana. Sehemu ambako mimea hii inakua, wanyama hawawezi kwenda kula. Sasa inaharibu uoto wa asili kule. Naomba sana Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Waziri Mkuu ashirikiane… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)