Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Mwanne Ismail Mchemba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami pia kwa kunipa nafasi nichangie hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza nianze na pongezi. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anayoifanya, asirudi nyuma, ana uhakika na kitu anachokifanya nasi tunamuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri Mkuu kazi aliyoifanya katika nchi hii ni kubwa sana, siyo hilo tu uamuzi wake wa kuhamia Dodoma inataka ujasiri, ametekeleza jinsi Mheshimiwa Rais alivyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze tena ndugu yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, amesimamia vizuri sana uanzishwaji wa Makao Makuu na Serikali kwa ujumla akiambatana na Naibu wake Mheshimiwa Antony Mavunde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitatenda haki kama sitatoa pongezi kwa Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, wewe Mwenyekiti na Viongozi wote ambao wameweza kufanya kazi ya Bunge hadi sasa tuko vizuri ingawa Bunge lilikuwa katika hali ngumu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah amefanya kazi nzuri, tumetembea, tumefanya kazi kwenye miradi na Kamati zimekwenda vizuri, niwapongeze sana kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kuisimamia Bunge. Pia nimpongeze tena AG kwa kazi nzuri ya kusimamia sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, niwapongeze Mawaziri wote, wamezunguka Tanzania hii kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM inafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie hoja sasa ya kuchangia Bajeti hii. Mimi nichangie moja kwa moja kuhusu viwanda, bahati nzuri au mbaya Waziri wa Viwanda hayupo. Tabora tuna matatizo makubwa sana ya viwanda, tulikuwa na kiwanda cha nyuzi hakipo, nimpongeze Waziri wa Viwanda amesema kwamba wako njiani na yule Mwekezaji anakuja kuzindua kiwanda hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hicho kinasikitisha, kina historia kubwa sana katika Mkoa wa Tabora, kiliwezesha kuwapa ajira vijana wetu lakini sasa tumerudi kwenye umaskini. Tuna kiwanda kingine cha Manonga, kila siku nazungumza na sitachoka kuzungumza. Kiwanda cha
Manonga cha Rajan mpaka sasa kina matatizo ambacho kiko Wilaya ya Igunga. Naomba katika uwekezaji sasa iangalie suala zima la viwanda katika Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunasindika asali, tunarina asali nyingi sana katika Mkoa wa Tabora na zamani tulikuwa na kiwanda cha Kipalapala ambacho kilikuwa kinasindika mpaka tunauza nchi za nje lakini kimekufa, kwa hiyo natangaza soko na ombi la wawekezaji kama watakuja kuwekeza ardhi ipo na ipo ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo suala zima la afya. Tuna tatizo sana la hospitali za Wilaya, Manispaa ya Tabora, Kaliua, Uyui mpaka sasa Hospitali za Wilaya hazipo. Niombe Serikali iangalie kwa jicho la huruma kwa sababu tabu wanayopata wananchi wa maeneo hayo Mheshimiwa Waziri Mkuu aiangalie. Wilaya ya Kaliua haina Hospitali ya Wilaya, wanakwenda Urambo kutibiwa lakini wazingatie pia
kwamba kuna huduma ambayo inatakiwa akinamama na mtoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Igunga kuna kituo cha Afya ambacho ni cha Jimbo la Manonga. Kimekamilika, kilikuwa kimefadhiliwa na ADB mpaka sasa hakifanyi kazi, hakuna vifaa vya kufanyia kazi, hakuna gari la wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima la maendeleo kwenye maeneo yetu. Serikali imefanya kazi kubwa sana kuondoa umaskini kwenye kaya maskini hususan TASAF, imefanya kazi nzuri sana. Imezunguka na imesaidia miradi ya awamu ya kwanza na ya pili ambayo haijakamilika tungeomba sasa awamu ya tatu Serikali iangalie na ikamilishe miradi yote hususan vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali kusimamia na kuhakikisha mradi wa MKURABITA unakwenda vizuri na wanapewa pesa za kutosha ili angalau wapunguze umaskini kwenye kaya ambazo ziko chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie asilimia 10 ya Wanawake na Vijana, Serikali imefanya vizuri. Niwapongeze Wakuu wa Mikoa, niwapongeze Halmashauri na Majiji nchi nzima, kwa sababu naomba nichangie kama Makamu Mwenyekiti, nina uhakika na ninachokizungumza kwa sababu wamekuja kwenye Kamati yetu, tumeona bajeti waliyopanga na mafanikio yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, karibu Halmashauri zote zimetenga asilimia 10 kwa sababu mwaka 2016/2017 tuliwapa masharti kama Kamati, wamefanya kazi nzuri, nawapongeza na kwenye bajeti wameonesha. Kwa hiyo, kazi wanaifanya, hatuwezi kusema hawafanyi, asilimia 10 ipo.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna baadhi ya Halmashauri imeweza kutenga katika asilimia 10 imesaidia makundi maalum. Kwa mfano, Tanga tumekuta wale wenzetu kwenye makundi maalum wasiosikia wametengewa fedha. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie jinsi gani ya kutenga asilimia 10 angalau asilimia mbili waweze kupata wenye makundi maalum. Ukurasa wa kumi na sita Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema, naungana naye na ni kweli hii fedha imetolewa, tuombe tu Serikali iangalie ni jinsi gani sasa ya kusaidia kuhakikisha fedha zile zinaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni barabara niipongeze sana Serikali, barabara ya kutoka Itigi kwenda Tabora imetengewa fedha, lakini bado kazi ile inasuasua. Kwa hiyo niombe barabara ya kutoka Chaya kwenda Tabora ipewe kipaumbele. Niombe tena barabara ya kutoka Puge kwenda Ndala, Nkinga hatimaye Manonga, hii barabara tumeiombea sana iweze kutengenezwa, Nkinga kuna hospitali kubwa sana ambayo inasaidia wananchi wa Mkoa wa Tabora kwa ujumla. (Makofi). Kwa hiyo, niombe sana Serikali iangalie… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.