Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kupata nafasi hii tena ya kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Namshukuru sana Waziri Mkuu kwa speech yake nzuri yenye maelekezo mazuri. Naipongeza Serikali kwa kazi nzuri mnazofanya, kazi zenye changamoto nyingi sasa hivi, kwa kweli mna changamoto nyingi lakini endeleeni kuzifanya, endeleeni kulisaidia Taifa hili tuweze kufika mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kutoa mchango wangu, naomba nitoe ushauri mdogo, ushauri unaotuhusu baadhi yetu sisi. Tuna bahati nzuri sana katika nchi yetu katika kipindi hiki cha Awamu ya Tano, tumepata Rais mwenye sifa kubwa tatu, hizi sifa tulizihitaji muda mrefu. Sifa ya kwanza ana nia thabiti ya kuleta maendeleo kwa wanyonge. Sifa ya pili, anaamua papo kwa papo, hacheleweshi na sifa ya tatu anataka watu wafanye kazi, ndiyo maana ya msemo wa Hapa Kazi Tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa hizi baadhi yetu tumezitumia vibaya, tumeshindwa kuzitumia kuzi-harness ili nchi yetu isonge mbele. Nasema hivyo kwa sababu baadhi yetu Wabunge wa Upinzani, Chama cha Mapinduzi, baadhi yetu Mawaziri siyo wote na baadhi yetu Wasaidizi wa Rais tumeshindwa kusema kweli. Tumeshindwa kushauri kwa ukweli, tumekuwa wanafiki, hili jambo litatuua sana, badala ya kutengeneza ushauri uliokamilika, unatengeneza ushauri nusu nusu, unampelekea Rais anaamua palepale unafikiri kitatokea nini? Tunahitaji uchambue ushauri wako uupime, uutengeneze uende umekamilika na Rais wetu huyu anayefanya papo kwa papo akiamua nchi inasonga mbele.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi haya yote tunayoyaona ni kwa sababu unafiki umezidi miongoni mwetu, nasema kweli. Mimi ni mwathirika wa mambo haya, mtu anaenda kusema anasema Dkt. Kafumu, Kafumu, Kafumu, jambo hili siyo zuri sana. Tumsaidie Rais kusonga mbele tutafika, tukifanya vinginevyo kwa kweli tutarudi nyuma. Ushauri wangu jamani tumsaidie Rais, tumshauri tumshike mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa aliamini katika ujamaa lakini waliomzunguka hawakuamini, tumeufikisha ujamaa wapi, Mzee amekufa ameondoka anaamini peke yake na sasa tuna bahati hii, hebu tuitumie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, naomba nitoe mchango wangu sasa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama ilivyo kwa Wabunge wa Tabora nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, suala la tumbaku lilikuwa linatusumbua kweli lakini umelimaliza ahsante sana. Tunakushukuru sana endelea kuja Tabora kwa watani zako utusaidie na mambo mengine.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kifungu cha 46 kinazungumzia miundombinu, haya ninayoyasema nayaleta kwa Waziri Mkuu ili anisaidie kumwambia Waziri wa Miundombinu, Wilaya ya Igunga na Jimbo la Igunga, tuweze kupata miundombinu, tuweze
kupata barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu sina barabara kabisa, unajua ni kwa sababu za kijiolojia. Miaka 60,000 Kabla ya Kristo Igunga asilimia 80 ilikuwa ni ziwa na ziwa hilo lilipokauka limeacha tope, ukifika Igunga ni mbuga ambayo ukitaka kujenga barabara ni lazima uweke tuta zito kubwa la juu. Halmashauri haina uwezo, tunajikuta hatuwezi kujenga barabara. Ukikwangua hiyo barabara ni ya kiangazi tu, wakati wa masika barabara hakuna kabisa na hasa Jimbo la Igunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Igunga halina barabara ya TANROADS, kuna kipande cha kilomita nadhani kumi kutoka Itunduru kwenda Igurubi. Hakuna barabara ya TANROADS kwenye Jimbo la Igunga, wakati wa masika lile Jimbo halipitiki kabisa. Naleta hili kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, uwatume wataalam wakaangalie na hasa wakati wa masika wakienda, hatuwezi kabisa. Mimi huwa sifanyi kazi wakati wa masika, nasubiri kiangazi ndiyo niweze kuwafikia wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia barabara Jimbo la Igunga tunazungumzia, Kata 16 za Wilaya ya Igunga ambazo hakuna barabara ya TANROADS na wakati wa masika hakuna barabara. Nataka nizungumze habari za barabara Wilaya ya Igunga na nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu, anisaidie kabisa ikiwezekana atume wataalam wakatembee sasa Igunga. Kwa kweli hakuna barabara na wale waliofika Igunga waliofanya kampeni wanajua hakuna barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa tunatumia ‘mapanda ya ng’ombe’, ni njia za ng’ombe hatuna barabara kabisa. Wakati wote nimeomba kuna barabara ya kutoka Shinyanga, kupitia Igurubi mpaka Igunga, na inapita inaenda mpaka Loya kwa ndugu yangu Mbunge wa Igalula. Hiyo barabara tumeomba ipandishwe hadhi mpaka leo angalau tupate barabara moja ambayo itatusaidia kwa ajili ya wananchi wa Igunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaongelea kitu kingine chochote, nataka niongelee barabara tu, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, tukimaliza Bunge hili, atume wataalam wakaangalie barabara Wilaya ya Igunga hususan Jimbo la Igunga. Kwa kweli kuna shida kubwa sana na nitaomba akiwa hapo akimaliza hii nitaenda hapo pembeni labda kesho kutwa niende kumwonesha vizuri Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba sana sitaki kusema mambo mengine nasema barabara. Barabara Igunga ni mbaya, barabara Igunga hakuna, barabara Jimbo la Igunga hakuna kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mliofanya kampeni Upinzani huku na huku CCM, mliona barabara hamna mapanda du wanasema Wasukuma, kwa hiyo ni kazi kubwa kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirudie tena, ningeweza kusema mambo mengi, mambo ya maji lakini naomba barabara, hiki ni kilio cha wananchi na najua wanasikiliza, tuna shida kubwa kweli tusaidieni. Mheshimiwa Waziri Mkuu, naona majirani zangu wananiambia nizungumzie Ziwa Victoria lakini sitaki, naomba barabara, barabara, barabara, barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba barabara Mheshimiwa Waziri Mkuu tafadhali sana.