Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuchangia hii hotuba ya Waziri Mkuu. Awali ya yote niweze kwanza kumpongeza Rais mpya wa TLS ndugu yangu Mheshimiwa Tundu Antipas Lissu kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana. Kwa hiyo, pongezi sana japokuwa mchakato huu ndugu yangu Mwakyembe alitaka kuingilia, bahati mbaya akawa amelemewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo naomba sasa niweze kujikita kwenye hotuba ya Waziri Mkuu na naomba nianze na suala moja la wakulima wa zao la kahawa. Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati yupo kule kusini alifanya mambo mazuri sana kwenye suala la watu wa korosho akapunguza tozo kwenye korosho na mambo mengi sana, lakini kiukweli kabisa amewasahau wakulima wa zao la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Mbozi pamoja na Mkoa wa Songwe na Mikoa yote ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wanaolima kahawa wana maeneo mengine wanasema kwamba kama Waziri Mkuu hatapunguza tozo na kodi kwenye zao la kahawa maana yake Waziri Mkuu
atakuwa ameonesha upendeleo wa hali ya juu sana na atakuwa amefanya ubaguzi ambao kwa kweli hatutegemei kuuona. Wao pia wanasema kwamba amefanya hivyo kwa sababu kule ni nyumbani kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakulima wa zao la kahawa wanasema kwamba wanategemea kusikia atakapokuwa anahitimisha na hapa nimepokea meseji kama 200 hivi kutoka Jimboni kwangu; wanategemea kusikia anapunguza kodi na tozo mbalimbali kwenye zao la kahawa.
Zipo tozo nyingi sana; kuna ushuru Bodi ya Kahawa, iko tozo kwenye TaCRI na iko tozo kwenye Halmashauri kule asilimia 0.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wanaomba tafadhali suala hili Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kulichukulia kwa umakini sana maana kule kwake nadhani ameshamaliza sijui ndio alikuwa anatengeneza mazingira lakini kwa kusema ule ukweli kwenye mazao mengine kama kahawa nahitaji kuona anapunguza tozo na kodi mbalimbali kwenye zao la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwetu Mbozi kahawa ndio dhahabu yetu; kahawa ndio kila kitu, mtoto anapokwenda shule lazima unaangalia kwenye kahawa na mtoto anapotaka kuoa unaangalia kwenye shamba la kahawa, kila kitu kahawa. Kwa hiyo, tafadhali suala hili ajaribu kuliangalia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu wakulima wetu wa kahawa sasa wamefika mahali wamekata tamaa na wameanza kung’oa miche ya kahawa kwa sababu bei kwanza ni ndogo na hizo tozo na kodi zimekuwa nyingi hivyo wanategemea atatoa majibu mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu kama hatozungumza lolote kuhusu kahawa mimi na Wabunge wengine tunaotoka kwenye Majimbo na maeneo wanayolima kahawa tutahamasishana kuwaleta wote hapa Dodoma ili waje kupewa majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kuzungumzia kidogo suala la maafa amegusa kwenye ukurasa wa 48. Suala la maafa tunajua ndugu zetu wa pale Bukoba tetemeko lilitokea wakapata matatizo makubwa sana. Cha kusikitisha Rais wa nchi hii amechukua muda mrefu
kwenda pale kuwafariji wananchi wale. Kibaya zaidi zipo fedha ambazo zilichangwa bilioni sita kutoka EU na lakini ziko pesa ambazo tulikatwa hapa Bungeni kwa ajili ya ndugu zetu wa Bukoba, hizi pesa zimeliwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujui hatujaambiwa hadi leo lakini inaonekana fedha hizi zimepigwa. Tulifanya mechi pale Dar es Salaam uwanja wa Taifa; Wabunge tumecheza mechi hadi miguu imeuma, tumepata zaidi ya milioni mia mbili na kitu pesa hizi zinaonekana kama mmeshazipiga. Sasa hatujui kwa nini watu wanapata matatizo badala ya Serikali kuchukua fedha zile kuwasaidia, mnaamua kuzitumia kinyume na matarajio, kinyume na ile kazi ambayo tulikuwa tunategemea zifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kabisa kwamba pale wananchi wanapopata matatizo, Rais wa nchi, Serikali iweze kutoa lugha nzuri. Leo kama Rais wa nchi anasema mimi sikuleta tetemeko, hatutawasaidia chakula ina maana kwamba Taifa hili tumekosa Rais. Nadhani suala
hili tujaribu kuliangalia sana. Naomba niwe muwazi kabisa kwamba Rais wetu lugha anazozitoa watu wanapopata matatizo…
KUHUSU UTARATIBU.....
MHE.PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba, mara ya kwanza ulisema kuwa hutatoa taarifa yoyote ila nasikitika umetoa taarifa kwa huyo bwana. Labda inawezekana ilikuwa kasoro kwa Simbachawene tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo nililokuwa nalizungumza hapa ni kwamba watu wanapopata matatizo wananchi wakipata maafa, Serikali inatakiwa ikae karibu na wananchi. Sasa kama Serikali fedha zinachangwa inafika mahali fedha zile zinatumika kinyume ni lazima tuhoji, lazima
tuulize. Sasa leo hii tusipouliza unategemea nani atauliza suala hili sisi ndio tunaowakilisha wananchi; tumekaa hapa huu ni mkutano wa hadhara wa wananchi nchi nzima hawawezi kukusanyika wote hapa.
TAARIFA....
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uweze kulinda muda wangu na najua bado nina dakika kama saba hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kuzungumzia suala lingine, suala ambalo Waziri Mkuu amelizungumzia kwenye ukurasa ule wa 11 kuhusu kufanya siasa za kutuunganisha badala ya kufanya siasa za kutugawa. Naomba sitanukuu sana kile alichokisoma pale Waziri Mkuu,
naomba niseme tu kwamba nchi yetu ilipofikia siasa za kuwagawa Watanzania zimeasisiwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siasa hizi zimeasisiwa juzijuzi hapa kwenye vyombo vya habari, imeripotiwa tu Mwenyekiti wa CCM Taifa anasema kwamba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ni marufuku kwenda kumwona Mbunge mwenzao Mheshimiwa Godbless Lema aliyekuwa amewekwa ndani. Siasa hizi za kutugawa Watanzania…
TAARIFA....
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu na naomba niseme kwamba ninachochangia hapa sichangii kitu ambacho hakipo, nachangia Hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale ambao labda hawajasoma hotuba hii vizuri wangepata muda waweze kusoma vizuri, hapa kwenye ukurasa wa 11 amezungumza vizuri sana Waziri Mkuu, kwamba tufanye siasa za kutuunganisha badala ya kufanya siasa za kutugawa na
nilichokizungumza mimi, siku ambayo Mwenyekiti wa CCM Taifa amewaasa baadhi ya Wabunge wasiende kumtembelea Mbunge mwenzao vyombo vya habari vilitangaza, magazeti yaliandika, Kituo cha Utangazaji cha TBC kilitangaza, ITV walitangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa nashangaa sana, labda inawezekana kuna wengine ambao inawezekana hawafuatilii vyombo vya habari, labda hawajasoma na Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, naomba tafadhali usiingie kwenye mtego, hii Hotuba ya Waziri Mkuu naichangia vizuri sana, hii ninayo hapa, ni ukurasa ule wa 11. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba nizungumze; wapo ndugu zetu wengi ambao walifukuzwa siku za hivi karibuni Msumbiji, Mheshimiwa Waziri Mkuu nadhani anakumbuka na Wabunge wote mnakumbuka kwenye Bunge hili. Wale Watanzania wamefukuzwa Msumbiji wamepelekwa mpakani pale wengine wamepoteza maisha, wengine wamebakwa. Rais wa nchi, naomba niseme tu kwamba kiongozi mkuu wa nchi, maana yake mmesema tusimtajetaje, sijajua tatizo ni nini, anasema kwamba walikwenda kwa njia za panya warudi kwa njia za panya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea viongozi wetu, watu wetu wanapopata matatizo tuwe wa kwanza kwenda kuwasaidia, tuwe wa kwanza kwenda kuwatia moyo. Watanzania wengi wanaoondoka nchini hawaendi nchi za huko mbali kwa ajili ya kwenda kutalii, wanatafuta
maisha, wanatafuta fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkuu wa mkoa alipojaribu kupeleka hata gari lile la jeshi kwenda kuwabeba wale watu alikatazwa akaambiwa kwamba usiwabebe, waache kama walivyo, walikwenda kwa njia za panya warudi kwa njia za panya. Suala hili kwa kweli linasikitisha sana na kwa jinsi hali ilivyo kwenye nchi yetu kama tutaendelea kwenda hivi, mimi naamini kabisa kwamba tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ambao wametuchagua sisi Wabunge na ambao wamemchagua Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na ambao wametuchagua sisi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba tu kwamba ifike mahali sisi viongozi ambao ndio tumaini la Watanzania tufanye kazi ya kuwawakilisha wananchi wetu vizuri na tufanye kazi ya kuwatetea, tufanye kazi ya kuwasemea, lakini inapofika mahali unasema kwamba
sikuwatuma mimi kwa kweli hatuwatendei haki hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala lingine ambalo linapatikana ukurasa ule wa 21 wa Hotuba ya Waziri Mkuu kuhusu ziada ya chakula ambayo ameizungumza kwenye hotuba hii. Mheshimiwa Waziri Mkuu anafahamu yeye na Wabunge wote wanafahamu kwamba
takribani halmashauri 55 zina tatizo la njaa japokuwa sasa hatujaambiwa, hatujaletewa taarifa rasmi Bungeni kwamba kwa sasa tumefikia wapi, lakini taarifa iliyokuwepo siku za nyuma ni kwamba halmashauri 55 zina njaa. Imefika mahali tunaambiwa kwamba chakula hakitapelekwa, sasa watu waliotuchagua leo tu…
MWENYEKITI: Nakuongeza dakika moja!
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, dakika zangu nadhani umenipunja kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka nizungumze tu kwamba sasa tuulize, wakati Watanzania wanapata njaa kipindi cha Nyerere alikipata wapi chakula cha kuwapelekea, wakati Watanzania wamepata njaa kipindi cha Mkapa, kipindi cha Mwinyi, kipindi cha Kikwete, chakula kilitoka wapi na hii Serikali leo kwa nini inashindwa kuwapelekea Watanzania chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la njaa halina baunsa, mtu yeyote anaweza akapata njaa kutokana na kwamba inaweza kuwa mvua labda haijanyesha, kumetokea ukame, kumetokea matatizo mbalimbali, sasa leo Serikali inasema kwamba sisi hatutapeleka chakula kwenye maeneo ya njaa, hii ni fedheha kubwa sana kwa Taifa letu na nina… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)