Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninamshukuru Mungu kunijalia na mimi leo kuwa mchangiaji katika hoja hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu tumekuwa tukipanga mipango kadhaa, waswahili wanasema mpango siyo matumizi, tumekuwa tukipanga lakini hatutumii, ni vema tujiulize tunapokosea ni wapi katika mipango hii, bila shaka kuna makosa tunayoyafanya ambayo yanatupelekea tunapanga vizuri lakini hakuna matokeo mazuri ya mipango yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii katika Mpango kuna jambo zito kubwa sana ambalo linajielekeza kuifanya Tanzania iwe ni nchi ya uchumi wa viwanda. Kusema tumesema sana juu ya hili na siyo mwanzo leo kusema kwamba nchi hii haiwezi kuendelea bila kuwa na mpango madhubuti wa kuendeleza viwanda vyetu. Leo hii yalaiti mimi nataka niseme wazi CCM mmemsaliti Mwalimu Nyerere, mimi siko radhi na Watanzania hawako radhi, mmemsaliti Mwalimu Nyerere kwa nini, kwa sababu Mwalimu Nyerere nchi hii alijitahidi kuwaonesha mfano, kwamba viwanda ndiyo vitakavyotutoa hapa tulipo na kwenda mbele. Matokeo yake mmekuja na sera zenu za ajabu, mmeua viwanda vyote, sasa mnafufua viwanda kwa maneno matupu, neno tupu hakuna utekelezaji unaofanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani, ndugu yangu Mheshimiwa Silinde, alizungumzia habari ya kusema lengo la Wachina kujenga pale Kurasini Logistic, ni kuifanya nchi hii kuendelea kuwa madalali, dampo ni kweli! Lakini imekosolewa vikali, hata mimi nataka niseme kwamba Mheshimiwa ndugu yangu Silinde mzoea udalali hawezi kazi ya duka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukubaliane nao hivyo hivyo, kwa sababu tukisema tunakataa Wachina kujenga pale, uwezo wa kujenga viwanda kushnei, hakuna! Tutasema tumekaa humu, tutapita, watakuja na watakaopita, kwa Itikadi hii na utendaji huu wa Sera za Chama cha Mapinduzi, hebu ndugu zangu igeni yale mazuri yetu, ambayo tunawapa mawazo ninyi muyafuate, nchi hii ni yetu wote, nchi hii hakuna kitabu chochote kitakatifu kilichotaja CCM wala CUF wala CHADEMA, vitabu vyote vimewataja waja wa Mwenyezi Mungu atakao waweka sehemu moja aliyopenda yeye, tumejichagulia majina tumejiita Watanzania, wa Afrika katika dunia hii, lakini hakuna hilo andiko liko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposhauri tuna malengo mazuri, nataka kusema kwamba ndugu zangu, tufuateni yale mawazo bila kujali anayeyatoa ni nani. Lile zuri na wewe Mheshimiwa Naibu Spika nimesikia huko, Bwana Mkubwa kamtumbua Wilson Kabwe, jamani tulisema hapa, Ezekiel Wenje alisema mpaka povu likamtoka, ninyi wenzetu huko mlifanyaje, sisi tulikuwa wabaya, leo mnatulaumu eti vyama vyetu hivi vya UKAWA vilimsimamisha Mheshimiwa Edward Lowasa kuwa mgombea wa Urais, Mheshimiwa Edward Lowasa akiwa CCM akitembea mnampokea kama malaika ninyi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninyi alienda Tanga nilikuwepo Katibu Mwenezi wa CCM alimpiga mtu kutaka kumuua kwa sababu kamkaripia Lowassa, kweli uongo? Mliimba nyimbo nzuri za kumpamba, mpaka mkatusadikisha kweli yaweza kuwa yale maneno yetu hatuko sawa, hebu tumuangalie. Leo tumefanya kosa kubwa, miaka yote mliokuwa naye alikuwa mzuri, mbaya kwetu, kwenu kizuri, tutakuwa naye na tutakufa naye Lowassa na Mungu akimuweka 2020 ndiye huyo huyo, mkipenda msipende dozi ni hiyo hiyo, mkinywa mkitema shauri yenu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie jambo moja lililonigusa sana. Mheshimiwa Zungu siyo mara ya kwanza, siyo mara ya pili, siyo mara ya tatu amekuwa akishauri toka Bunge lililopita. Makampuni ya simu yanaiibia nchi, hii nataka niwaulize yeye yule siyo mpinzani, Mheshimiwa Zungu ni Mbunge wa CCM. Mheshimiwa Zungu alichokisema ni kwa maslahi ya nchi hii, mlifanya yapi, mmetekeleza lipi, hamna! Tutawasifu wafanyao mazuri na tutawakosoa wanafanya mabaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waliopewa jukumu la kusimamia suala hili hawajaitendea haki nchi hii, kama mu-watumbuaji wazuri wa majipu angalieni hili siyo jipu ni busha! Lazima tuangalie kile kinachokosesha mapato nchi hii, tukiangalia bila kuoneana haya, kuna tatizo gani kuandaa wataalam wetu makini, wakaona ni kwa kiasi gani Tanzania inapoteza mapato kutokana na makampuni ya simu. Yupo nani nyuma ya makampuni ya simu tuambieni, yuko nani? Siyo bure iko sababu. Siyo bure kwa sababu tafadhalini tunayoyasema hapa siyo kwa ajili ya ushabiki ni kwa ajili ya kuisaidia nchi hii, itoke ilipo iende mbele. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia juu ya maamuzi ya kukurupuka yanayochukuliwa na watendaji wa nchi hii. Nchi hii mmeingia mkataba wa himaya moja ya forodha kufanya mizigo ya Congo sasa hivi iwe inalipiwa kwao kabla ya kutoka katika Bandari ya Dar es salaam, jambo ambalo limechangia kushuka kwa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam kufikia asilimia 50. Hebu niwaulize tumefanya yale kwa faida ipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nchi ya Congo, mimi niliwahi kuwa mjasiriamali nilikaa pale Congo katika Mji wa Lubumbashi, nchi ile haijasimama utawala wake sawa sawa, pale unaweza kupeleka containers akaja Kanali tu wa Jeshi akatoa amri pitisha hizo kontena tano na zinapita. Sasa wafanyabiashara wale wa Congo mnapoweka vile vikwazo ambavyo haviisaidii nchi hii, wametafuta bandari ya Beira, wametafuta bandari za nchi nyingine wameiacha Dar es Salaam imedoda, mnapata faida gani? Mambo ya Wacongo yanawahusu nini ndugu zangu, msiba wa Kichina Mmasai anaingiaje? Waacheni wenyewe sisi tukusanyeni kodi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimesoma gazeti moja, nimeona taarifa Serikali inasema kwamba imeliona hili na mnalifanyia kazi, nawaomba sana ndugu zangu shitukeni mapema, kule Beira wakizoea utamu wa kule hakuna atakayerudi hapa, anzeni sasa kuchukua hatua msisubiri kesho na kesho kutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie suala la utawala bora. Suala la utawala bora lina mtazamo mpana sana. Mojawapo ikiwa ni wananchi wenyewe wafaidike na utawala bora wenyewe. Nasikitika kwa kituko ambacho kimefanywa na Serikali yenu ya kuzuia matangazo haya wananchi wa Tanzania wasione wawakilishi wao wanasema nini, amesema mwenzangu hapa mmoja kwamba ule umaarufu Dkt. Chegeni mliokuwa mkiupata kwenye TV sasa hamtoupata tena. Kila Mbunge aliyeingia hapa mpaka ukiitwa Mbunge tayari wewe ni maarufu tu, ukaonekana kwenye TV usionekane kwenye TV wewe tayari ni maarufu tu. Wengine tuna umaarufu wa ziada.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mwenyewe ni maarufu kwa sababu ni baba watoto nina familia na watoto wasiopungua 12, nina mke wangu ambaye naweza kumfanya Waziri Mkuu, mimi Rais wa familia na watoto wangu Baraza la Mawaziri, siyo umaarufu mdogo huo? Kila umaarufu una ngazi yake, leo umaarufu wangu siwezi kuufananisha na Mheshimiwa Magufuli lakini hata umaarufu wa Mheshimiwa Magufuli hauwezi kuwa zaidi ya Mheshimiwa Barrack Obama, hauwezi kuwa sawa! Kwa hivyo, humu hamna uwezo wa kutupunguzia umaarufu tulionao, mimi ni maarufu, mimi ni Rais kwenye familia yangu, watoto 12 ninao ni Baraza tosha kabisa la Mawaziri na mama watoto Waziri Mkuu wangu, ninataka umaarufu gani tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tafadhalini sana fikirieni tena kwa makini, hatutafuti umaarufu tunataka Watanzania wajue wawakilishi wao waliowachagua wanasimamia vipi yale wanayoelekeza wawakilishe kwa Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo katika utawala bora kwa masikitiko tu ni kwamba leo hii nchi inayoitwa Zanzibar, nilisema kabla ya Bunge hili, kabla ya uchaguzi haramu uliofanyika mara ya pili Zanzibar, nilisema kwamba jamani tufikirieni maneno ya nchi wahisani wanayosema juu ya kuikatia misaada nchi yetu. Hili jambo misaada hii tusikae tukisema tutakula mihogo, mihogo ipo siku zote mbona hatukushiba? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo jamani Watanzania wenzangu, Wabunge wenzangu, niwaambie wazi watu wasiozidi kumi Zanzibar wanaifanya nchi hii iingie katika historia nyingine ya kuonekana nchi isiyo na demokrasia, wakati tunajidai ni nchi ya demokrasia. Kisiwa cha Zanzibar ambacho Mheshimiwa Ally Keissy alisema ukiwaita kwa filimbi wanakusanyika tunapatikana, wanainyima mamilioni ya Watanzania misaada katika nchi hii, siyo haki na tusijidai. Tumekuwa na matatizo, madeni yameongezeka, muda wote wakati ambapo tulikuwa tukipewa misaada, kuondoka kwa misaada hii ni tatizo, fikirieni tena.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge hili, napenda kuwaambia wananchi wangu wa Jimbo la Konde, kwa sababu kule kwetu Zanzibar hata kufanya mikutano hatufanyi, ile nchi imekaa ndivyo sivyo, kile kisiwa kimekaa ndivyo sivyo, utawala bora haujulikani. Kwa mfano, leo akitokea CCM mmoja katika Jimbo akienda ku-report tu wale wana-CUF wameniangalia kwa jicho baya, kijiji kizima wanapelekwa askari wanakwenda kukisomba wanakiweka ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, siropoki! Tarehe 17 siku tatu kabla ya uchaguzi, mwana CCM mmoja katika Jimbo langu, alizua kwamba amechomewa nyumba hakikuungua hata kibakuli kimoja, walikuja kuchukuliwa wazee wa kijiji 30 wakaswekwa ndani kwa sababu tu ya amri ya kisiasa ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba. Utawala bora gani mnaoujadili nyinyi hapa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba alitoa tangazo la kupiga marufuku wananchi wa Mkoa ule wasitembee usiku, ana mamlaka gani kisheria na Kikatiba kutangaza hali ya hatari katika Mkoa? Nchi hii ina Majemedari Wakuu wa Majeshi, Amiri Jeshi Wakuu wangapi? Hebu niambieni maajabu hayo kuna Amiri Jeshi wangapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema na ninawaambia wananchi wa Jimbo la Konde kwamba dini zote zinakataza mtu kushirikiana na dhalimu, dini zote zinakataza kabisa mtu kushirikiana na mtu aliye dhalimu kwa njia yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, nawaomba wananchi wangu kuanzia mimi mwenyewe wasishirikiane na madhalimu muda wote wa uhai wa maisha yao, wasishirikiane nao. Kama wanauza watii masharti ya leseni kwa sababu inataka lazima kuuza, lakini kununua ni hiyari yao na hakuna atakaethubutu kuwaingilia, waendelee kufanya wanaloweza kuhakikisha madhalimu hawakamatani nao, hawashirikiani nao katika lolote na hilo nawaunga mkono mia kwa mia.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwape mfano tu mimi mwenyewe nimeanza, Mwakilishi wa CCM haramu aliyechaguliwa tarehe 20 alinipigia simu nikamwambia ukome kama ulivyokoma kuzaliwa mara ya pili kwenye tumbo la mama yako, na nilimwambia asinisogelee na akinisogelea hamtaniona tena hapa Bungeni, tutamalizana huko huko, hamtaniona. Haiwezekani, unakaaje na watu wanaodhulumu haki za watu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii imejijengea historia sasa ya kuifanya ile Zanzibar ni kichaka, leo ninyi mnatafuta watalii wakija wakiwinda vitalu na kupiga wanyama badala yake ninyi mnachukua Jeshi lenu mnalipeleka Zanzibar kuwalinda mama zetu na baba zetu, haki iko wapi? Wameleta magari yote ya Tanzania Bara kuja katika Kisiwa cha Pemba; mnawawinda nini, mnawatakia nini mama zetu, ndugu zetu, watoto wetu, tuna lipi baya, kukataa tu kuiunga mkono CCM ndiyo kosa letu? Kama hilo ndiyo kosa niwahakikishieni hata dunia iundwe mara ya pili CCM hatutaikubali na hatuitaki!
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.