Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii muhimu ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Waziri Jenista na kaka yangu Mavunde kwa kazi nzuri wanayoifanya. Tunawashukuru kwa kutupa ushirikiano mzuri
katika kuwahudumia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Magufuli, Mheshimiwa Makamu wa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na dira ya miaka mitano ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mawili katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kipengele cha hali ya uchumi nchini ukurasa wa 13 mpaka 40 kuna mambo ambayo hotuba imeyazungumzia ningependa kuchangia mambo mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala; kwenye mjadala sasa hivi kuna mjadala kuhusu size ya Bajeti ya Serikali. Katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017, Serikali ilitenga trilioni 29.5 na katika mwaka ambao unakuja wa Mwaka wa Fedha 2017/2018, bajeti hii itapanda kutoka 29.5
kwenda kwenye trilioni 31.7.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mijadala kuhusu size ya Bajeti ya Serikali naona Serikali kwa sababu dhamira yake na nia yake ni kutatua changamoto za Watanzania kwa kasi, si mbaya kuwa na malengo marefu na kwa vile Serikali ya Awamu ya Tano tunajua ina dhamira ya kuhakikisha inatumia vizuri fedha za umma, nadhani Waheshimiwa Wabunge tujikite kwenye kusimamia kile ambacho Serikali inakikusanya kama kinaenda kwenye kutekeleza miradi ya maendeleo. Sio mbaya kuwa na malengo if you aim higher na ukaweka jitihada ya ufanya kazi ili kwenda kwenye hayo malengo mapana ni jambo la kupongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani TRA ilikuwa inakusanya takriban bilioni 800, lakini Serikali ingependa ikae kwenye kusifiwa kwamba inatimiza malengo ya kila mwezi, basi tungejiwekea target za bilioni 800, tunaendelea kupongezana kila mwezi lakini Serikali ikajipa challenge ikasema tujivute twende kwenye trilioni 1.2. Kwa hiyo, unaona kwamba ni hatua nzuri, unakuwa na malengo marefu, lakini unajitahidi kwenda kwenye hayo malengo marefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo naiona kwenye uandaaji wa bajeti ni kwamba asilimia kubwa ya Watanzania, kikundi cha wananchi ambao wako vijijini, asilimia kubwa ya wale Watanzania ni kwamba uchumi unakua lakini hauwagusi wale asilimia kubwa. Kwa mfano, katika mpango wa maendeleo wa 2017/2018 na katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukiangalia kwa upande wa kilimo kwanza kwenye ukuaji wa Sekta ya Kilimo 1.7% ni kidogo mno. Hatuwezi kuona social economic transformation kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Sekta hizi ambazo zinaajiri Watanzania walio wengi kama tutaendelea kupata ukuaji wa 1.7%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuiomba Serikali katika Bajeti za Kisekta ambazo zinakuja, tuone bajeti ya kutosha imetengwa kwa ajili ya pembejeo, tuone kuna mpango wa kupata maafisa ugani wa kutosha ili vijiji vyetu vipate maafisa ugani, tuone bajeti ya kutosha kwenye kilimo
cha umwagiliaji. Mwaka wa Bajeti wa 2017 ilitengwa hela kidogo sana kwenye kilimo cha umwagiliaji. Katika Bunge hili baada ya ukame ambao ulitupata kule Karagwe, niliomba Serikali ije kwenye kata kumi ambazo zina vyanzo vya maji tutathmini kuona kama tunaweza kufanya kilimo cha umwagiliaji, lakini mpaka hivi sasa sijapata timu ya wataalam kufanya hii tathmini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ili tuweze kwenda kwenye uchumi wa viwanda na kwenda kwenye middle income country status lazima tufike mahali tuone jitihada za kibajeti zinazolenga kutoa bajeti ya kutosha kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili Watanzania wengi hawa ambao wanajishughulisha kwenye hii sekta tuweze kuwasaidia kujikwamua kutoka kwenye umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mazao ya biashara, kodi kero 27 kwenye zao la kahawa tumeondoa kodi moja tu ya ada ya leseni ya kusindika kahawa ya dola 250 tu. Tuko kwenye rekodi, kwenye Ilani tumeahidi kwamba tutaondoa hizi kodi kero kwenye zao la kahawa. Mheshimiwa Rais alikuja Kagera akaahidi kwamba kwenye bajeti hii ya 2017/2018 tutaziondoa hizi kodi kero. Mheshimiwa Waziri Mkuu
nakushukuru ulikuja Karagwe tukaahidi lakini sijaona jitihada ya Serikali kuondoa hizi kero kwa sababu kwenye hotuba ya Waziri Mkuu hazitatajwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye kusaidia yale makundi ya wananchi ambao wako vijijini pia kuna haja ya kuangalia wajasiriamali wadogo na wa kati na kuweka mazingira wezeshi ili kuwasaidia kukua. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inatambua kwamba 56% ya
wananchi ni nguvu kazi ya vijana, lakini kwa sababu tumekuwa na malengo ya kukusanya mapato ya kila mwezi kwa mfano, kumekuwa na aggressive behavior katika kukusanya mapato kiasi kwamba haya makundi ambayo tunategemea kuwasaidia kuwakwamua kutoka kwenye
umaskini tunajikuta zile aggressive behavior za kukusanya kodi kwa mfano upande wa bodaboda, ukija Karagwe, bodaboda awe kwenye gulio, msiba au shambani, pikipiki zinawindwa na askari wa usalama barabarani kwa sababu wana target ya mapato kiasi fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo matokeo yake unakuta badala ya kumsaidia yule kijana ambaye tumeshindwa kumpatia ajira kwa sababu tatizo la ajira ni la nchi nzima na si Tanzania tu ni Afrika na dunia nzima, wale vijana ambao wanajiajiri tunatakiwa kuwawekea mazingira wezeshi ya kukua. Kama amejiajiri kama bodaboda basi tumsaidie ili aweze kukua. Kwa hiyo, matokeo yake, kwa sababu ya target za mapato unakuta tunawaathiri yale makundi maalum ambayo tulitakiwa kuwasaidia kuwawekea mazingira wezeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa, niende kwenye changamoto zlizoko kwenye Jimbo la Karagwe na nimezileta kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ili nimwombe aweze kunisaidia yapate attention inayostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mradi wa maji wa Rwakajunju. Huu mradi ni ahadi ya muda mrefu, Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni tuliwaahidi wana Karagwe katika hii Serikali ya Awamu ya Tano tutatekeleza mradi huu. Serikali ikatenga dola milioni 30 kwenye Mwaka wa Fedha 2016/2017, lakini nashangaa kwenye bajeti ya mwaka huu 2017/2018, fedha hizi sizioni sasa sijui zimeenda wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu nakumbuka ulivyokuja karagwe tuliwaahidi wana Karagwe kwa vile zilikuwa zimeshatengwa kwenye bajeti ya mwaka uliopita, tukawaahidi pale tulikofanya Mkutano pale Kihanga tena ukamwomba Mkurugenzi wa Halmashauri aje kwenye jukwaa awaambie kwamba wananchi wa Kata ile ya Kihanga na wenyewe watapata huduma ile ya maji kutoka
kwenye mradi wa Rwakajunju. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mradi huu usipotekelezwa kwa kweli kuna hali ya hatari huko mbeleni. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu anisaidie katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu. Naipongeza Serikali katika elimu ya bila malipo, tunakwenda vizuri na Serikali inaendelea kurekebisha pale ambapo tunakwama lakini ili tuweze kwenda vizuri, naomba Bajeti ya 2017/2018, tutenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuajiri walimu. Wilaya ya Karagwe peke yake tuna deficit ya walimu 840 wa shule za msingi, tuna deficit ya walimu wa sayansi 96.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la afya. Katika malengo ya Serikali ya kuwa na kituo cha afya kila kata nadhani ni malengo mazuri lakini hatuwezi kuyatimiza kwa muda mfupi. Nipende kuishauri Serikali angalau tulenge kuwa na kituo cha afya kwa kila tarafa ili katika kipindi cha miaka mitano tuweze kuonesha kwamba tuna malengo ya muda mrefu lakini katika kipindi cha miaka mitano tumeweza kuwa na kituo cha afya cha kila tarafa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na migogoro ya ardhi. Pale Kihanga tulipofanya mkutano, zile hekta 2000 ambazo Mheshimiwa Waziri Mkuu alielekeza Serikali irudishe kwa wananchi mpaka hivi sasa bado. Walienda pale wakasema tunawapa hekta 2000 lakini zimelenga sehemu
ambapo wananchi tayari wanakaa, hazijatolewa kutoka kwenye ranch ya Kitengule na wenye ma-block, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu asiingilie katika hili suala ili tuweze kurudisha hekta 2000 kwa wananchi kama tulivyowaahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.