Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bismillah Rahman Rahim.Nakushukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa mwanzo katika siku ya leo katika hotuba iliyo mbele yetu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama walivyotangulia wenzangu na mimi napenda nikukumbushe kwamba kama ambavyo tuliagizwa kwamba tukumbushe hakika ya ukumbusho unawafaa wanaoamini.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ulipoapa kuwa Mbunge ulishika Msahafu na kauli yako ya mwisho ukamwomba Mwenyezi Mungu akusaidie na ulipoapishwa kuwa Waziri Mkuu ulishika tena Msahafu na kauli yako ya mwisho ikawa unamwomba Mwenyezi Mungu akusaidie. Na sisi
tunamwomba Mwenyezi Mungu akusaidie inshaallah. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yako ukurasa wa 52 na 53 umezungumzia suala la amani, lakini amani haiwezi kuwa amani ya kweli kama haijasimama kwenye nguzo zake na nguzo kubwa ya amani ni haki, Katiba na kufuata sheria. Ni dhahiri Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali ambayo sasa wewe ndiye Kiongozi Mkuu wa Serikali hiyo kwa maana ya Mtendaji Mkuu wa Serikali, Serikali
yako au nchi yako unayoisimamia sasa hivi, siyo salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nje ya mipaka yetu hatuna vita, lakini ndani ya nchi yetu wananchi hawaishi kwa amani kabisa. Kila mmoja wetu ana hofu ya nini kitatokea baadaye? Kuanzia Mawaziri na watendaji wote wa Serikali hakuna mmoja anayefanya kazi yake akiwa na amani ndani ya nafsi yake akiamini kwamba jua litatua hajatumbuliwa. Wafanyabiashara kuanzia wakubwa na wadogo, hawana amani na biashara zao wakiona kwamba wakati wowote biashara zao zitapotea. Wafanyabiashara wakubwa, wamachinga wenye vibanda vidogo vidogo, anaweza
akaamka asubuhi, biashara yake haipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bomoa bomoa za nyumba, mtu ana nyumba yake amejenga kwa miaka 20, 30 anaishi inakuja kubomolewa ndani ya dakika tano. Watanzania hawaishi kwa amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vifo vinavyotokana na
watu wenyewe kupigana, wakulima na wafugaji, wanyama kufa kwa kukatwa mapanga ama sumu, vimezidi kuendelea katika nchi yetu, lakini njaa inayoendelea kwa sababu mbalimbali za ukame, mafuriko ama wanyama waharibifu na ndege, inazidi kuendelea katika nchi yetu na wananchi wakisema wana njaa majibu ya Serikali yanakuwa hayaeleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi sana, nchi hii siyo salama. Baya zaidi hivi sasa kinachotia hofu ni hii kamata kamata, utekaji na uuaji unaoendelea katika nchi yetu. Wilaya za Mkuranga na Rufiji sasa hivi watu wanapigwa risasi, viongozi wa Chama cha Mapinduzi ambao ni Wenyeviti wa Vijiji wanapigwa risasi, hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inanishangaza sana kuona polisi wanatumia nguvu kubwa kuondoa mashamba ya bangi huko, lakini watu wanakufa kwa risasi ndani ya nchi hii. Kwa umri wangu wa miaka 54 sasa sishangai suala la utekaji, wala uwekwaji ndani wa watu, wala kupotea watu
wasionekane kama Ben Sanane, sishangai na sitashangaa. Waheshimiwa Wabunge, haya yalianza Zanzibar. Miaka ya 1964 mwanzoni, akina Abdallah Kassim Hanga, Mlungi Ussi, Abdulaziz Twala, Othman Sharrif na Twaha Ubwa walipotea katika mazingira ya kutatanisha na hadi leo
hawajaonekana. Mwaka 1972 mwasisi wa Jamhuri ya Muungano Abeid Aman Karume amepigwa risasi, akauawa. Kesi ikawa inaoneshwa live katika televisheni ya Zanzibar wakati huo ndiyo televisheni ya mwanzo kwa Afrika, ikionesha kesi ile. Mshtakiwa Mr. ‘X’ hajulikani ni nani, kesi ile ikaishia. Wanaotuhumiwa kuwa wauaji wakahifadhiwa na Jamhuri ya Muungano hadi kufa kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeshuhudia kifo cha Edward Sokoine kimeacha maswali mengi sana. Kifo cha Imran Kombe aliyekuwa Mkuu wa Usalama wa Taifa, kapigwa risasi kama ngedere katika shamba lake, lakini pia Horace Kolimba alipotea katika mazingira ambayo yameacha maswali mengi; Balali aliyekuwa Gavana Mkuu wa Serikali kapotea, lakini Wazanzibari hadi leo tunajiuliza kifo cha Dkt. Omar Ali Juma kupotea kule na familia yake imetelekezwa hadi leo. Kwa hiyo, sishangai Ben Sanane, sishangai kukamatwa kwa Wabunge na watu wengine kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haya ni mazoea! Naona ni utamaduni, kwa hiyo, hili silishangai. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninayasema haya kukwambia kwamba Serikali yako pamoja na kwamba unazungumzishwa hapo hunisikilizi, lakini sishangai na napenda tu nikwambie kwamba Serikali yako unayoisimamia ndani ya mwaka mmoja na nusu, haina amani ndani ya nchi
yako na ujue kama wewe ukiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali iko siku utaulizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mtihani, uongozi ulionao ni mtihani; uzima ni mtihani; watoto ni mtihani; madaraka ni mtihani; na iko siko utaulizwa juu ya neema hii aliyokupa Mwenyezi Mungu umeitumia vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadithi fupi tu; Nabii Nuhu aliishi katika dunia kwa miaka 950. Siku anakufa, Mwenyezi Mungu anampelekea malaika wawili kuzungumza naye, anaulizwa, Yaa Nuhu, hebu tupe habari za duniani? Nuhu akasema yeye asiulizwe mambo ya duniani, kwa sababu
hakika ya dunia ni kama nyumba, ameingia kwa mlango wa mbele akatoka kwa mlango wa nyuma. Hajui kilichomo ndani. Miaka 950, seuze sisi wenye miaka 60 na 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nizungumzie suala hili linaloitwa mgogoro wa Chama cha Wananchi CUF. Chama cha Wananchi CUF hakina mgogoro. Mimi ni kiongozi ndani ya Chama cha Wananchi CUF, naingia katika vikao vyote vya Chama cha Wananchi CUF, Chama cha Wananchi CUF kinaendesha vikao na shughuli zake kama kawaida. Unaoitwa mgogoro ambao umepandikizwa na system kwa kutumiwa Msajili wa Vyama vya Siasa na Profesa Ibrahim Lipumba, huu sisi hatuuiti mgogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo lake kubwa huu unaoitwa mgogoro kwa kutumia watu hao ni kuzuia haki ya Wazanzibari ya tarehe 25/10/2015. Hawawezi kuzuia haki hii Profesa Ibrahim Lipumba na Msajili wa Vyama na mwingine yeyote kwa sababu ni haki na maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar na haki ya WazanzibarI itapatikana muda mfupi unaokuja. Msijidanganye wala wasijidanganye katika hili, hamuwezi kuzuia haki ya Wanzibari ya tarehe 25. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie kwa kumwambia bosi wangu, keshakimbia eeh, Mheshimiwa Magdalena Sakaya juzi wakati anachangia hapa alisema anawashangaa Wabunge kwamba ni wanafiki. Nataka nimuulize na kwa sababu kakimbia lakini yupo kibaraka
mwenzie atamfikishia huu ujumbe, ni nani mnafiki? Yeye akikaa na Profesa Ibrahim Lipumba anasema kwamba…
KUHUSU UTARATIBU....
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa mwongozo wako. Ninachotaka kusema, hii pilipili usiyoila sijui yakuwashia nini Mheshimiwa Jenista. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema, anapokaa na Profesa Ibrahim Lipumba anasema kwamba Profesa Ibrahimu Lipumba anamuunga mkono na wako pamoja. Akiondoka Profesa Ibrahim Lipumba anawaita Wachungaji anawaambia nimechoka kutumia pesa yangu, Mwenyekiti
akija hapa akiondoka analeta masuala mengine. Nawaomba Wachungaji mwende mkaongee na Seif Sharif suala hili limalizike ili mimi nisitumie pesa zangu, mnafiki ni nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nawaambia tena Msajili wa Vyama vya Siasa, mpango wake alioupanga taarifa tunazo asitegemee kwamba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)