Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwa hai na kuwa salama tukahudhuria kikao hiki kujadili Mpango wa miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa. Pili, ninashukuru kupata nafasi hii ili na mimi kutoa maoni yangu kuishauri Serikali juu ya Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, uongo usiokanushwa hugeuka kuwa ukweli. Maelezo ambayo yametolewa hapa kwamba hawatotambua, hawatofanya nini, hayo yanazungumzwa na wengi, lakini kutotambua Serikali wamefanya kama watu ambao wamekula soro ya kizamani, maana soro ya kizamani inavyoliwa huwa yule mlaji hufunikwa kanga haonekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wanasema hawatambui lakini sasa kinachotoka Serikalini wanasema ni haki yao, sasa ni wajibu wa nani? Ikiwa wewe kwako haki ina maana kwamba ni wajibu wa mwingine, sasa hapo tayari umeshatambua Serikali ukitaka usitake. Kama wewe kweli hutambui kama Mungu yupo kwa nini unavuta hewa yake, imetengenezwa na nani? Wewe unasema hiki kitu hakipo kwa nini wewe unatumia na unasema hakipo, sasa hayo ni maneno tu ya mtu ambaye tuseme ni maneno ya mfa maji. (Makofi)
Kuna maneno hapa yanazungumzwa kwamba labda CCM wangetuachia sisi, sasa ninyi mnataka kushindanisha nazi na machicha katika kutoa tui? Hata mkimsimamisha 2020 na 2025 yale ni machicha, machicha ni machicha tu, yamebakia kuanikwa sasa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo langu ni kuchangia Mpango huu na nimelenga kuchangia katika suala la financing strategy ambayo imeelezwa kama ni mpango wa upatikanaji wa fedha katika kugharamia huu Mpango. Wazungumzaji wengi wameeleza katika kuchangia kuinua maendeleo ya nchi hii lazima tukope, hata nchi zingine nazo zinakopa katika kufanya mipango yao, Marekani wanakopa China, Japan wanakopa China na wote hawa wanakopa ili ku-finance mipango ambayo ipo wameiweka ili kuendeleza mataifa yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia suala ya deni la Taifa ambalo limewahi kuzungumziwa na wachangiaji, kuna msemo mmoja wanasema mcheza ngoma isiyo yake daima ataharibu, hawi sawa na wenzake kutwa huwa kwenye taabu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika,una mtu anazungumza deni la Taifa kwamba kutokana na ile percent ambayo ameizungumza Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ni asilimia 36.8 ya Pato la Taifa, anasema ni kubwa na halitofaa, wame-comment mengi. Lakini niwafahamishe tu vile ni vigezo vya Kimataifa siyo vigezo ambavyo labda vimezaliwa hapa Tanzania peke yake, ni vigezo vya Kimataifa na kila nchi inatumia vile vigezo, hilo ni jambo moja kwanza lifahamike.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili watu wafahamu kwamba Deni la Taifa kuwa himilivu vile ndiyo vigezo vyake, watu wafahamu kwamba Japan ni nchi ambayo inaongoza hata hapa Tanzania kwa kutupa misaada, lakini deni lake la Taifa kwa Pato la Taifa ni asilimia 246. Marekani asilimia 105 mwaka jana, mwaka huu asilimia 104, sisi ni asilimia 36.8. Kwa hiyo, ili kuweza kufanikisha malengo ambayo yapo katika mpango huu ni lazima tukope, wanaita leverage, ukitaka kubeba kitu kizito ni lazima uweke lever. Kwa hiyo, lever ni huu mkopo ambao utatusaidia kubeba mzigo wa maendeleo ambao tumejipangia wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kitu kimoja katika kukopa. Tumepanga kukopa ndani pia tumepanga kukopa nje, ninatoa ushauri kwa Serikali katika kukopa ndani bora zaidi tukope nje kuliko kukopa ndani, kwa sababu tutakapo kopa ndani mwenendo wa riba unaweza ukaongezeka, tulichopanga kwamba tuna sekta binafsi tunazitarajia nazo zishamirishe ukuaji wa uchumi. Kwa hiyo, mwenendo wa riba ukiwa juu ambao utasababishwa na kukopa ndani utainua riba ikiwa Serikali inakopa ina maana kutakuwa free risk, ile free risk kila mmoja atapenda aikopeshe Serikali, hatopenda kukopesha watu binafsi, hapa riba zitapanda juu kwa maana hiyo watu binafsi ama sekta binafsi zinaweza zikaanguka, hivyo nashauri tukope nje zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tukope nje zaidi tujaribu kutizama mikopo nafuu, mikopo nafuu ipo lakini pia Serikali inaweza ikaingia katika International Financial Market ikakopa, hiyo ipo, lakini tunasahauri pia tena kuwa jambo hili kwamba ile sovereign credit rating ifanyiwe haraka ya Tanzania imalizike ili riba tutakayokopa kutoka nje iwe chini. Hili jambo tunaishauri Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utakapokopa mwaka huu, utakapofanya maendeleo kama umekopa ni muhimu kwetu kuonekana kile tulichokopea kimefanyika. Kikiwa kimefanyika lile deni litakuwa halina shida kulipwa kwa sababu tayari kilichokopewa kimefanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika aina za financing strategies ambazo zimeelezwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, moja ni kufanya FDI (Foreign Direct Investment). Katika hili watu wa nje kuja kuwekeza mitaji yao moja kwa moja tujaribu kuchambua, tuchambue mapema ili tusije tukaja tukapata hasara kama inayowakuta watu wengine. Kwa sababu kuweka moja kwa moja Foreign Direct Investment bila ya kuchungulia chungulia au kaungalia tunaweza tukaja tukajitwisha mzigo ambao baadaye unaweza ukaja ukatugharimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi Foreign Direct Investment zinafanyika lakini tuangalie mazingira yatakayotupa nafuu katika kufanyika kwake. Kwa mfano, hivi sasa tunaweza tukawaita watu kuja kufanya hiyo Foreign Direct Investment kwetu, lakini baadaye ikaja ikawa mzigo wakataka kuweka mishahara wanayotaka wao, wakaweka mazingira magumu ya kazi, wanaweza wakawa wanabeba faida wanaenda nazo kwao, lakini jambo baya zaidi wanaweza wakaja wakafanya transfer pricing waka-quote bei kubwa kwa kupeleka kule kwao halafu sisi tukaja tukaathirika zaidi. Kwa hiyo, hili tujaribu kuliangalia ili tuweze kufaidika na hii Foreign Direct Investment tuchuje, kwa sababu wanaweza wakaja kutokana na hamu kubwa tuliyonayo tukawapokea haraka bila ya kuwachuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa niongelee ni kuhusiana na viwanda ambavyo Tanzania tumelenga kuviweka. Nchi yetu ya Tanzania siyo kisiwa, tuna ushirikiano wa Kimataifa, tuna ushirikiano wa Kikanda na kuna makubaliano mengine ambayo yamefanyika ya Tanzania na nchi nyingine, kupanga ni kuchagua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokusudia kufanya viwanda hapa kwetu tujaribu kufanya comparative advantage analysis, kwamba ni jambo gani tunaweza sisi katika kuzalisha kwetu likatunufaisha zaidi kuliko kitu kingine, ni viwanda gani ambavyo ni vya kuweka hapa kwetu kuliko kuweka viwanda vya aina zote, tusije tukaja tukakurupuka. Kwa mfano, alizeti inazalishwa Tanzania, wafanyabiashara wa mafuta ya alizeti au wazalishaji wa mafuta hayo hapa Tanzania wanahitaji nafuu fulani. Tunaweza tukasema kwamba tuna-block pengine bidhaa za kutoka nje, lakini ku-block kwetu bidhaa za kutoka nje tuna ushirikiano wa Kikanda, tuna ushirikiano wa Kimataifa, tujaribu kupima ile comparative advantage yetu na wenginge, tuzalishe kitu gani zaidi hapa ndani ili tuweze kutunufaisha zaidi, tujaribu kutazama kitu ambacho technology yake tunaiweza. Tujaribu kutazama kitu ambacho rasilimali zake zinapatikana hapa kwetu, pia kuangalia masuala mengine kama vile demand, kitu ambacho pengine kinahitajika sana na mambo mengine ya sera za kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili la viwanda linahitaji sera. Watu wa viwanda wanasema wanahitaji sera, kwa hiyo, tuwawekee sera ambayo itaweza kuwapelekea wafanyabiashara wetu wa hapa waweze kuzalisha, watakapoweza kuzalisha basi itakuwa ni nafuu kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu alizungumza kwamba uchaguzi uliofanyika Zanzibar ni uchaguzi haramu. Mimi napata taabu sana kwa kitabu kipi? Wamesema hakuna kitabu kilichozungumza CUF na CCM ama CHADEMA hakuna! Sasa ni kitabu kipi kilichotaja habari za uchagzi huu haramu na huu halali?
Mimi ninavyofahamu uchaguzi uhalali wake na uharamu wake ni kwa Katiba na Sheria. Tuliwafundisha hawa ndugu zetu hapa wakatulia, wakajua kwamba uchaguzi unakwenda kwa Katiba na Sheria, leo unakuja kusema uchaguzi ni haramu! Ni haramu kwa sababu ya kukosa kwako wewe! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yote umeyataka mwenyewe, iliyobaki shauri yako. Kwa sababu kama kuna kitu ambacho kimefanyika nje ya utawala bora ni mtu kuwazuia watu haki yao ya kwenda kupiga kura. Hili ndilo kubwa ambalo limefanyika. Sasa mtu aina kama hii atachukuliwa kama nani wakati jambo la vyama vya siasa ni jambo la Muungano, unazungumza wewe kama kiongozi, unawazua watu wasiende kupiga kura, matokeo yake unawakataza na wenzako wasishiriki, unawakataza wasigombee, matokeo yake watu wanalia huko! Hili ndilo ambalo wenzetu liliwasibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mtaka nyingi nasaba hupata mwingi msiba. Sasa huu msiba waache tu waende nao waomboleze, kwa nasaba kubwa walioitaka waache wapate msiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuzungumzia suala moja ambalo ni muhimu, ulinzi na usalama ni kitu muhimu sana katika nchi yetu. Utakapokuwa unatega mabomu sasa unataka watu wasifuatiliwe? Mabomu yanalipuka nchi nzima usifuatiliwe, usiguswe, wewe ni nani? Mimi ninaomba iwe hivyo hivyo. Mheshimiwa Mawe Matatu nenda nao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru.