Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye hotuba ambazo ziko mbele yetu na niaze kwa kuunga mkono kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa nia yake thabiti ya kusaidia wanyonge, namshukuru Waziri Mkuu, sikupata nafasi ya kuchangia kwenye hotuba yake, lakini namshukuru sana kwa kutusikiliza, tunapokuwa na masuala anayashughulikia kwa haraka sana.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri, ndugu yangu Mheshimiwa George Simbachawene, Mheshimiwa Jafo na dada yangu Mheshimiwa Kairuki kwa hotuba nzuri. Nimepitia hotuba hizi na jedwali hili ambalo Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ametuwasilishia hapa, yapo mambo ambayo kwa kweli inaonesha kabisa Wizara imejipanga vizuri, na mimi nimefarijika sana kuona kumbukumbu nzuri ambazo pia zitatusaidia katika kutekeleza majukumu yetu. Kwa hiyo, nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kutoa mchango wangu kwa kuzungumza juu ya uratibu, hususan najikita kwenye hii Wizara ya TAMISEMI, kwamba Wizara hii inayo majukumu mengi lakini napenda tu nipate nafasi hii niweze kuomba sana katika kuratibu maeneo mbalimbali ambayo pia
yanasimamiwa na sekta nyingine kwa mfano kwenye kilimo waweze kuangalia vizuri ili watusaidie wananchi wetu. Sisi tunaotoka majimbo ambayo pia ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya kilimo, waweze kutusaidia. Kwa sababu najua wanasimamia upande wa pembejeo, tumekuwa na shida kubwa, tunahitaji uratibu uwe wa mapema ili wananchi wetu wapate pembejeo mapema tuweze kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, yapo maeneo mengine ambayo yanahitaji kufanya utafiti. Tunaona kuna suala hili la kuwa na akiba ya chakula, imefika wakati sasa Wizara ijaribu kuangalia kama tunaweza kupata fursa pia ya kuhifadhi chakula, tuwe na maghala kwenye upande wa Serikali za
Mitaa kwa maana ya Halmashauri zetu ili tuwe na akiba lakini pia tunaweza kufanya biashara kupitia zoezi hili la kuhifadhi chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia napenda kushauri kuhusu usimamizi wa mikopo kwa wakulima wetu kwa sababu Wizara hii kwa idara ambazo zipo kwenye Halmashauri zetu, ikisimama vizuri tutaweza kuwasaidia wananchi. Kwa sababu utaweza kuona kwamba mikopo ambayo inakwenda kwa wakulima kwa mfano wa zao la tumbaku, utaona ile mikopo na mikataba inayotolewa na vyombo vyetu ambavyo vinakopesha wananchi kumekuwa na biashara ndani yake ambayo inawaumiza sana wakulima.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano mikataba ambayo inakuwa imetengenezwa kwa kufuata fedha za kigeni, kwamba wakati wa kukopa unapopewa pesa kwenye kubadilisha pesa kutoka dola kwenda shilingi, pale kuna gharama ambazo zinakuwepo na wakati wa malipo
kadhalika kunakuwa kuna gharama ambazo mwisho wa safari wakulima wetu wanapata gharama kubwa kutokana na mikopo hii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda nishauri kwenye kuratibu, tuimarishe maeneo ambayo kwa upande wa idara ambazo zinasimamia wakulima hawa hususan hawa wa tumbaku tuweze kuona kwamba mikataba yao pia inakuwa mizuri kwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, nilitaka nizungumze juu ya uongezaji wa makusanyo katika Halmashauri zetu. Kwa maana hiyo, naiomba Wizara hii ya TAMISEMI iweze kutusaidia pale ambapo kwa upande wetu sisi kama Halmashauri tunavyokuwa na mipango ya kuwekeza ili tuweze kupanua
makusanyo katika maeneo yetu, kwa sababu hapa kuna tatizo kwamba tunavyotaka angalau tu-cross border, tuweze kufanya uwekezaji kwenye maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI anajua kwamba sisi tuna dhamira kubwa ya kutokutegemea ushuru tu wa mazao, tunapenda pia twende tufanye uwekezaji ili Halmashauri zetu ziweze kuongeza mapato.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tu Wizara hii iweze kufanya coordination nzuri ili tutakapofika kwenye maeneo ambayo tunataka kupanua vyanzo, basi watusupport ili tuweze kuongeza makusanyo. Kuongezeka kwa makusanyo ina maana huduma kwa wananchi wetu itakuwa inaongezeka.
Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze juu ya udhibiti wa ndani (internal controls), lakini nataka nijikite kwenye maeneo mawili; kuimarisha hili eneo la Wakaguzi wa Ndani na upande mwingine nitazungumza juu ya Kamati za Ukaguzi ambazo hazijafanya vizuri, zimeleteleza kutokuwa na udhibiti mzuri katika makusanyo na katika matumizi. Kwa hiyo, nafikiria nizungumze maeneo haya mawili.
Mheshimiwa Spika, nimeona kwamba katika maeneo yetu upande wa Wakaguzi wa Ndani bado tuna matatizo makubwa. Kwanza Wakaguzi hawa wa Ndani ni wachache sana, hawawezi kumudu kuwa na mawanda ya kutosha (scope) ili ule ushauri wao uweze kusaidia Halmashauri yetu.
Mheshimiwa Spika, nafikiri Wizara hii itazame sana eneo hili, kwa sababu ukiangalia Wakaguzi wa Ndani, hawana hata ule mpango. Sisi tunao Wakaguzi wawili; hawana hata ule mpango ambao utaonesha kwamba wamejipanga vizuri ili kuweza kupitia maeneo ya kutosha
na kuweza kushauri katika Halmashauri ili tuweze kufanya vyema.
Mheshimiwa Spika, utakuta Wakaguzi hawana hata ule ujuzi wa kutosha kuweza kuangalia labda kuwa na uwezo kwenye mifumo hii, ujuzi wa TEHAMA uko mdogo, hawawezi ku-access information kwenye EPICA, Lawson, kwenye PLANREP, kwa hiyo, utaona kwamba hili ni tatizo. Hawa Wakaguzi wa Ndani waongezwe lakini pia waweze kuwa na weledi wa kutosha waweze kuzisaidia Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, utakuja kuona kwamba hata bajeti, nilipokuwa nikipitia bajeti ya kwenye Halmashauri yangu, niliwauliza Wakaguzi wa Ndani kama fedha zinatosha.
Kwa hiyo, unaona kwamba hata pesa wanazopangiwa ni kidogo sana kuweza kumudu majukumu yao na pia wana shida ya vifaa, hawana kompyuta, hawana magari ya kutembelea maeneo mbalimbali, maeneo ya kwetu ambayo ni makubwa sana. Kwa hiyo, utaona kwamba ule mchango wao ni mdogo sana ambao kimsingi kama maeneo haya tutayaboresha, watatuwezesha pia Maafisa Masuhuli kufanya kazi zao vizuri kwa sababu watapata ushauri na kwa mapema zaidi.
Mheshimiwa Spika, hili eneo la Kamati za Ukaguzi utaona Kamati ya Ukaguzi ni muhimu sana kuwepo katika Halmashauri yetu, lakini bado hatujaziwekea msimamo mkubwa kuweza kuhakikisha kwamba Kamati hizi zinafanya kazi na kusaidia mambo mengi sana.
Kwa hiyo, utaona eneo hili ni muhimu sana, TAMISEMI ilitazame ili waweze kusaidia. Hizi Kamati zitamwezesha Afisa Masuhuli kutimiza wajibu wake kwa sababu ataweza kumshauri vizuri majukumu yake ya kiuongozi, zitasaidia sana kama zitaimarishwa. Pia tutapata ufanisi katika hiki kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kwa sababu hii Kamati ya Ukaguzi inamsimamia kwa ukaribu sana huyu Mkaguzi wa Ndani. Kwa hiyo, nafikiri eneo hili pia tuweze kulitazama.Mheshimiwa Spika, nizungumzie juu ya maboma.
Tunayo maboma mengi sana ambayo wananchi wametumia nguvu nyingi sana kujenga, katika hili TAMISEMI watusaidie sana kuyakamilisha haya maboma. Nilikuwa najaribu kuangalia kwenye haya majedwali, utaona kabisa kwamba kuna upungufu sana. Kwa mfano, nilikuwa najaribu kutazama nikaona upungufu wa madarasa katika shule za msingi na sekondari. Kuna upungufu mkubwa sana ukiangalia majedwali haya, lakini wananchi wamejitolea vya kutosha; yako maboma mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, ninazo nyumba 170 ikiwemo madarasa, zahanati, majengo ya utawala, nyumba za walimu, nyumba za wafanyakazi wa afya 170 ambazo zinasubiria kukamilishwa. Hii idadi ni kubwa sana, bila Serikali kutusaidia Halmashauri peke yake haiwezi. Pia yapo majengo 117 ambayo yako kwenye hatua mbalimbali; hatua ya msingi, hatua ya madirisha na hatua ya lenter Serikali naomba
itusaidie sana ili tuweze kupunguza huu upungufu ambao upo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana TAMISEMI watazame eneo hili kwani wananchi wameweka nguvu nyingi, watapata moyo sana kama Serikali itatusaidia kuweza kukamilisha masuala haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nilipokuwa nikipitia hili jedwali, nimeona kuna shule zimesahaulika. Nashukuru kwamba tumepata walimu wa sayansi wachache, lakini ninaamini kwamba sisi katika Halmashauri ya Ushetu tunayo shule ya high school inaitwa Dakama secondary school, haikupangiwa walimu na ina upungufu; haina walimu wa sayansi. Walimu wa physics, tunaye mmoja ambaye ndio Mkuu wa Shule, anafundisha kuanzia form one mpaka form six.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Hatuna mwalimu wa biology! Sasa naomba Wizara itazame ili tuweze kusaidia hawa watoto. Isipokuwa nimegundua kwamba ilisahaulika kwa sababu, ukiangalia hata katika majedwali kwenye mgao wa fedha za usimamizi wa mitihani, hatukupangiwa high school. Kwa hiyo, naamini kwamba shule hii ilisahaulika.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba uitazame hii shule ili tuokoe hawa watoto waweze kupata huduma na tuweze kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kumwomba Mheshimiwa Waziri TAMISEMI, kusaidiwa madaraja matatu…
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja.