Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii. Naomba nianze na Utumishi na hasa nikiendeleza lile suala langu la asubuhi linalohusiana na ajira.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa kauli yake mwezi wa Sita mwaka 2016 kwamba inasitisha ajira huku ikifuatilia suala la watumishi hewa na kwamba zoezi hilo likiisha, ajira mpya zingetoka. Mpaka leo suala la ajira mpya halizungumzwi.
Mheshimiwa Spika, juzi wamezungumzwa wachache, walimu wa sayansi kama 4,000 na kidogo lakini kwenye orodha iliyotoka juzi, kuna walimu wawili wa masomo ya book-keeping na commerce, history na kiswahili na wao wameajiriwa kwenye hiyo orodha ya walimu wa sayansi.
Siwaonei wivu, lakini nataka kujua tu kwamba na hii history na kiswahili siku hizi ni sayansi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ifike mahali ituambie, uhakiki wa wafanyakazi unaisha lini na ajira mpya zinatoka lini? Watu wasikae na matumaini tu bila kujua wanaajiriwa au hawaajiriwi katika Awamu ya Tano. Nilitaka nizungumzie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba sekta ya elimu haina wafanyakazi/walimu wa kutosha. Afya haina wafanyakazi wa kutosha, kwa hiyo, Serikali itoe ajira na wale watoto walioko mitaani wanaendelea kuichukia tu Serikali bure bila sababu, wakati ajira zingeweza kutoka.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, wale hewa walioondolewa 18,000 kazi zao wanafanya nani leo? Hakuna replacement, pamebaki wazi au inakuaje? Hao wangeweza kuajiriwa wengine ingetusaidia kupunguza idadi ya ambao hawana ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la vyeti fake. Hili nalo limekuwa kizungumkuti katika nchi hii. Kuzungumzia vyeti fake nchi hii mpaka uwe na roho ngumu kwa sababu kuna cheti kimoja hapa sasa kimekuwa ni tatizo kabisa. Hiki cheti cha Bashite kina shida gani? Kina tatizo gani imekuwa sasa kinachafua mpaka jina la watu wakubwa kabisa. Hata mtu akifungwa magoli manne bila kitu chochote, wanasema ni
nne kwa Bashite; yaani tunaongeza misamiati isiyo na sababu. Hiki cheti cha Bashite kinalindwa kwa sababu zipi?
(Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Waziri wa Utumishi utakapoanza kushughulikia vyeti kwa watu wasio na vyeti na kuchukua hatua, hiki cha Bashite sijui kitabaki wapi. Ingawa siyo mamlaka yako, lakini najua utashauri kwa utaratibu fulani ili na Bashite naye awajibike pamoja na wale walio na vyeti
fake na ionekane, isije ikatokea double standard katika hili.
Huyu achukuliwe hatua zake na huyu apate haki zake, tumalize suala la Bashite nchi hii.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kuzungumzia kidogo suala la utawala bora. Ukiona haki inapotea…
SPIKA: Mheshimiwa Bilago, hiyo Bashite ndiyo kitu gani? Mheshimiwa endelea kuchangia tu, endelea. (Kicheko)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Ni cheti cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambacho siyo cha kwake, alisomea cheti cha mtu mwingine. Kwa hiyo, nilitaka nacho kiangaliwe na Waziri anayehusika.
Mheshimiwa Spika, suala la utawala bora; ukiona haki inapotea; haki inakwenda sambamba na amani. Hawa maaskari wetu waliofariki Mungu awaweke mahali pema Peponi; mkiangalia kwenye mitandao, kwa nini baadhi ya wananchi wamefurahia? Yaani binadamu wenzetu
wanapoteza maisha, lakini baadhi ya watu wanafurahia kwenye mitandao? Ni kwa sababu kuna baadhi ya haki zinapotezwa na hao watu wanaokufa. Sasa wakifa, watu wanapumua kidogo. Kwa hiyo, tuangalie mahusiano, tulete mahusiano mazuri kati ya wananchi na vyombo vya dola vyote, Usalama wa Taifa, Polisi, Jeshi tuwe na mahusiano mazuri.
Shirikishi, watu walikuwa wanakwenda vizuri. Leo hii ukipita kwenye mitandao unaona watu wanakufa, wengine wanashangilia. Siyo kitu kizuri, hata mimi sikipendi. Siyo kitu kizuri, lakini chanzo chake ni pale ambapo haki ya watu inapotezwa, watu wengine wanaona sasa likitokea la
kutokea wapate mahali pa kupumua. Maandamano ya moyoni hayo, yanaendelea moyoni, watu wanaandamana.
Mheshimiwa Spika, nilitaka nizungumzie upande wa afya kidogo sana, kwamba Waziri wa TAMISEMI atusaidie namna bora ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kule kwenye Halmashauri zetu. Sasa hivi takwimu zinafikia kama 550.
Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, tunapolizungumza kwenye Kamati yetu, tunaona kama lilihitaji Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI awepo na sijui kuna siku utatupa hiyo offer tumpate Waziri wa TAMISEMI kwenye Kamati yetu, wawepo pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Afya. Tukizungumzia la afya na elimu wote wakiwepo pamoja, nadhani inaweza ikawa na mantiki nzuri kwenye Kamati yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilitaka nizungumzie suala la Wakala wa Barabara Vijijini, nimeliona. Suala hili linaweza kutufikisha mahali pazuri kama litasimamiwa vizuri, kwa sababu kuna baadhi ya barabara zinashindikana kutengenezwa kule kwenye Halmashauri zetu na hasa zile
zinazotokana na Madiwani wa Upinzani. Kwa mfano, Jimboni kwangu, ninazo barabara za kufungua Jimbo na nchi jirani ya Burundi; Rumashi - Burundi, Malenga - Burundi, Kiga - Burundi, Kimiha - Burundi, Katanga – Burundi; zile ambazo zina Madiwani wa CHADEMA hazitengenezeki kwamba zitaendelea kuwapa umaarufu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wakala huyu hawezi kuwa na tabia kama hiyo, nadhani atakuwa na tabia nzuri kuliko hii. Kwa hiyo, ni vyema hili jambo likaenda vizuri tukapata huyu Wakala wa Barabara Vijijini, anaweza akatusaidia kuliweka vizuri ili wananchi wapate barabara bila
kujali itikadi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni ushuru wa mazao. Mheshimiwa Rais aliwahi kutoa maelekezo ya ushuru utozwe namna gani katika hotuba yake, akihutubia wananchi kwenye Mkutano wa Hadhara, likaanza kutekelezeka, lakini bado lina mkanganyiko. Ni ujazo gani unatakiwa kutozwa ushuru katika mazao haya ya nafaka na kadhalika? Maana debe moja halitozwi ushuru. Kule kwangu Kakonko, ukienda baadhi ya vijiji wanatoza ushuru debe moja, baadhi ya vijiji hawatozi debe moja. Kwa hiyo, kunakuwa na mkanganyiko.
Mheshimiwa Spika, hebu tupate uniformity nchi nzima; mazao yatatozwa ushuru wa ujazo wa kiasi fulani ili kuondoa huu mkanganyiko katika nchi.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni elimu. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, tuepuke madeni ya walimu yasiyo na sababu. Mkurugenzi anaamua anahamisha walimu 50, 60 hana hata senti tano, anawaambia nendeni tu mtalipwa.
Watalipwa na nani? Kama huna hela ya kuwalipa watu, usiwahamishe. Kuna walimu 85,000 mwaka jana walipanda madaraja; tena madaraja ya kufungua vidato (E to F; F to G; G to H; H to I). Wale watu wage bill yao ya mwezi ni shilingi bilioni 21; inaendelea ku-pile up tangu mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika, ni vyema Serikali ingelipa hili deni likasimama kwanza wakabaki wanadai hizi nyingine. Yaani likasimama kwa sababu kila mwezi kuna shilingi bilioni 21 na ndiyo inakwenda kufika kwenye shilingi trilioni 1.06 wanayodai Walimu nchi hii.
Mheshimiwa Spika, sasa na Walimu wenyewe wamesema wanadai, imeanza kufanyika uhakiki; uhakiki huu ni kama una dalili za delaying tactics, yaani unafanya uhakiki polepole ili usifikie wakati wa kulipa, lakini mwisho wa siku deni lile lipo na walimu wanaendelea kuhangaika nchi hii, wanafanya maandamano moyoni, wanafanya mgomo wa kutofundisha moyoni. Hawa watu kama hawajatekelezewa mambo yao, hawawezi kufanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, mimi ni mwalimu, nimefundisha darasani, nafahamu namna ya kugoma polepole. Kwa hiyo, tuwatekelezee mambo yao. Mwalimu huyo huyo, kimshahara hicho kidogo, halafu hata madai yao, zaidi ya Walimu asilimia 70 wote wana madai.
Taarifa....
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, ni ukweli usiopingika kwamba mimi ni mtu mzima, nina zaidi ya nusu karne. Kata hizo ninazozizungumza barabara zake, inaanzia ndani ya Kata inaenda mpakani mwa Burundi; haiwezi kupita kwenye Kata nyingine. Lazima ianzie ndani ya Kata kwenda mpakani. Sijazungumza barabara za ndani, niko makini na hilo. Kwa hiyo, nilikuwa nalizungumza hili kwamba huyu Wakala wa Barabara Vijijini anaweza akatufikisha mahali pazuri kama kweli utaratibu utakwenda kama ulivyopangwa.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa bado naendelea na hoja ya walimu nikitaka kuzungumzia juu ya motisha kwa walimu. Tuliwahi kutoa wazo wakati niko Chama cha Walimu na walimu wa nchi hii niwaambie wana matumaini makubwa sana na Serikali hii.
Kwanza, wakijua Rais ni mwalimu, Waziri Mkuu ni mwalimu, tena kiongozi aliyekuwa wa Chama cha Walimu kama mimi, huenda hata mimi tutakaposhika Serikali nitakuwa Waziri Mkuu, kwa sababu ndiyo Makatibu wa Chama cha Walimu wameanza kuwa Mawaziri Wakuu.
Kwa hiyo, walimu wana matumaini makubwa sana juu ya hili, tunaomba Serikali iwasikilize. Najua na sekta nyingine, sawa wana madai lakini tuangalie hii population kubwa ambayo inagusa karibu kila kijiji, kuna mwalimu anayekuwa na madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, motisha ambayo tulikuwa tunazungumzia ilikuwa ni teaching allowance. Teaching allowance mpaka leo haizungumzwi kabisa. Naomba Waziri anayehusika anaposimama atueleze, teaching allowance lengo lake ilikuwa; muda wanaofanya kazi walimu ni tofauti na sekta nyingine. Walimu walioko shule za bweni (boarding) wanatakiwa kuangalia watoto usiku mpaka asubuhi. Mtoto
akiugua, mwalimu anampeleka hospitali. Muda wa kusahihisha, mwalimu hawezi kusahihisha shuleni akamaliza kazi, lazima kazi ile aende nayo mpaka nyumbani, itamfuata mpaka nyumbani.
Kwa hiyo, ndiyo maana tukasema teaching allowance iwepo ku-offset hizi gharama za overtime na kadhalika. Nayo ilifanywa vizuri tu wakati ule wa Tume ya Makweta, ikaja ikatuletea taarifa nzuri kama hiyo na Walimu wakawa wanapata teaching allowance. Wale tuliofundisha zamani
kama mimi, nilikuwa napata 55 percent ya mshahara wangu, kwa sababu mimi ni mwalimu wa sayansi.
Kwa hiyo, Serikali ikifanya hilo, ita-motivate walimu, itawafanya waipende kazi yao na wafundishe watoto wa nchi hii ili tuweze kupata wataalam wazuri katika nchi hii.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kuzungumzia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante.