Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Kojani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuchangia katika hotuba ya bajeti ya TAMISEMI na Utawala Bora.
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah Wataallah kwa kunijalia uzima nikasimama hapa leo kwa ajili ya kuchangia hotuba hii.
Baada ya shukurani hizo, pia naomba nikipongeze chama changu kwa kukamilisha ziara ya Wilaya zote za Unguja na Pemba kwa kuimarisha chama, ziara hiyo iliyofanywa na Katibu Mkuu wa Chama Maalim Seif Sharif Hamad. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba niende moja kwa moja katika suala zima la utawala bora. Hapa naomba nigusie kipengele kizima cha uhuru wa kuabudu.
Mheshimwa Spika, naelewa kwamba suala la uhuru wa kuabudu ni suala la kikatiba, lakini pia katika suala zima la utawala bora ni suala ambalo limejadiliwa kwamba suala la ibada ni suala ambalo linadumisha amani ndani ya nchi. Ni suala ambalo haliangalii itikadi za vyama, ni suala ambalo linawakutanisha watu wa vyama vyote.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba katika suala hili la ibada ndani ya Jimbo langu lilizua mtafaruku mkubwa sana kwamba katika kufanya ibada upande wa chama kimoja walilazimisha kwamba lazima atajwe Mheshimiwa Rais kwenye hotuba ya Ijumaa, suala ambalo
lilizua mtafaruku mkubwa sana, ikabidi kwamba Mkuu wa Wilaya aingilie kati, achukue Jeshi la Polisi livamie kijiji kile, masuala ambayo ni kinyume na taratibu na sheria na nchi.
Mheshimiwa Spika, suala la ibada tunajua kwamba ni suala ambalo ni huru, jamii inatakiwa iabudu yenyewe kwa kufuata dini yao ambavyo inawaelekeza. Sasa Mkuu wa Wilaya aliamrisha Jeshi la Polisi livamie kwenye msikiti ule na baada ya kuvamia ule msikiti kwa kweli ikawa ni tafrani kubwa sana ndani ya Jimbo lile.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba Jeshi la Polisi tunaomba lifuate masuala mazima ya utawala bora, lisiingilie masuala ambayo yako nje na mamlaka yao. Suala la ibada ni suala la uhuru wa kila mtu.
Mheshimiwa Spika, baada ya Jeshi la Polisi kuvamia, lilikamata watu wawili. Naomba niseme kwamba kuna mzee wa miaka 65 alikuwa anahuzunisha, lakini pia kuna kijana wa miaka 35. Huyu kijana kwa sababu wazee wake walikuwa ni CCM, Mkuu wa Wilaya alikwenda akamtoa ndani.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba Jeshi la Polisi lisivae magwanda ya kijani, litumie sheria, yule mzee maskini jamaa zake walifika kumwombea dhamana, lakini kwa sababu RPC alikataa katakata, siku iliyofuata alipelekwa mahakamani na akawekwa ndani kwa muda wa wiki mbili. Yule kijana alitolewa baada ya dhamana ya Mkuu wa Wilaya. Hivi kweli Mkuu wa Wilaya anatoa dhamana kwa mshitakiwa
aliyefika polisi au polisi ndiyo wanaotoa dhamana? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Wizara husika ya Utawala Bora, Mheshimiwa Waziri alisema hapa kwamba anatoa mafunzo kwa viongozi wa polisi. Wawaelimishe kwamba watende kazi zao bila kuangalia itikadi za vyama.
Mheshimiwa Spika, naomba niende kipengele kingine. Suala hili la utawala bora nilisema kwamba linaingia katika taasisi mbalimbali. Tuliona hapa kwamba suala la vyama vya siasa kuingiliwa na Msajili wa Vyama ni kukiuka suala zima la utawala bora. Tulieleza kwa kina hapa kwamba
Profesa Lipumba alijiuzulu kwa hiari yake na baada ya kujiuzulu, Msajili wa Vyama akaingilia kati kumrejesha kwenye chama.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme jamani au naomba niulize Wizara ya Utawala Bora, Katiba ya Chama; kuna Katiba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuna Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, naomba mtueleze ni Katiba ipi kati ya hizi tatu inayota uhuru wa mtu yeyote
ambaye ni kiongozi kujiuzulu halafu akarudi katika nafasi yake? Mtueleze kama kuna kifungu ambacho kinaeleza, basi mtuambie kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano kifungu namba fulani kinamruhusu mtu kujiuzulu halafu akarudi katika nafasi yake au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaruhusu mtu kujiuzulu halafu akarudi katika nafasi yake?
Mheshimiwa Spika, iweje leo Msajili wa Vyama aingilie maamuzi ya chama yaliyofanywa kihalali? Yeye anasema kwamba kikao kilikuwa ni halali, kilifikia quorum lakini maamuzi yalikuwa ni batili. Hii ni sawa na kumchanganya nguruwe na kuku ukawapika mahali pamoja halafu ukasema kwamba kuku ni halali, nguruwe ni haramu. Hiyo naona itakuwa haileti tija jamani. Tuangalie suala zima la utawala bora.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli suala la utawala bora ni suala lenye uwanja mpana sana na ni suala ambalo linastahili kuangaliwa kwa macho yote kwa kweli. Wenzangu walizungumzia hapa kwamba hata ajira zinatolewa kwa kuangalia itikadi za vyama.
Mheshimiwa Spika, hivi kweli mnalipeleka wapi Taifa hili kama kweli mpaka leo hata ajira inaangalia mtu kwa chama jamani? Hivi tutalipeleka wapi Taifa leo? Ina maana kwamba watendaji ambao ni wa vyama vya upinzani hata kama ana sifa kiasi gani, asiajiriwe ndani ya nchi hii kwa
sababu yeye ni mpinzani? Nafikiri tutakuwa hatulitendei haki Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wanaoajiriwa kwa dini; kwa sababu inayohusika na Utumishi na Utawala Bora ni Wizara ya Utumishi
na Utawala Bora. Ndiyo niliyosema kwamba naongelea suala zima la Wizara ya Utumishi na Utawala Bora. Nilipoanza utangulizi wangu nilisema hivyo.
Mheshimiwa Spika, samahani. Sikusema wanaajiriwa kidini, nilisema wanaajiriwa kufuatana na itikadi za vyama na hili nilisema hata kule kwetu Zanzibar linafanyika, kwa sababu binafsi nina mwanangu alifanya usaili wa benki, lakini wakawa wanafuatiliwa majumbani kwao. Wanaulizwa hasa, wewe baba yako ni nani, mama yako ni nani, yuko chama gani? Kwa kweli unafikia mahaliā¦
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ulitaka ushahidi. Sasa nilikuwa nakupa hata ule ushahidi kwamba haya yameanza hapa mpaka Visiwani yameendelea. Ahsante, namalizia suala hilo la ajira.
Mheshimiwa Spika, sasa nije kwenye suala zima la TASAF. TASAF kwa kiasi fulani wameonesha mwelekeo mzuri kwenye suala zima la kunusuru kaya masikini, lakini pia katika ajira za muda. Kwa kweli katika kaya maskini, wamesaidia pakubwa sana, isipokuwa niseme kwamba kwa upande wetu kule Zanzibar kuna suala zima la usimamizi wa hizi kaya maskini. Usimamizi wa kaya maskini umelengwa zaidi kwa upande wa Masheha. Tunakuta kwamba baadhi ya Masheha wanazitumia vibaya nafasi zao kwamba wanaingiza watu ambao hawastahili kwa sababu ni jamaa zao. Kwa hiyo, TASAF walifuatilie suala hili