Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ngoja nibadili uelekeo kidogo basi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika bajeti ya TAMISEMI na mimi napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia na mimi nakuombea angalau hukuwa na hasira leo, mambo yameenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, nina machache sana kuhusu bajeti ya Wizara hii. Kwanza nianze na fedha za Mfuko za Wanawake na Mfuko wa Vijana zile asilimia kumi ambazo zinapaswa kukatwa katika mapato ya Halmashauri (own source) ili ziweze kusaidia wanawake na vijana.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu katika Kamati zetu ambapo TAMISEMI tumekuwa tukisisitiza sana kwamba Halmashauri hizi ziweze kutenga fedha hizi ili 5% na 10% iweze kuwasaidia wanawake na vijana katika kuboresha maisha yao, kufanya biashara na hivyo kujiajiri na kuwaondoa mitaani ili waweze kuwa na shughuli za kufanya.
Mheshimiwa Spika, baada kuweka msisitizo huo, Halmashauri nyingi sasa zinaanza kutenga fedha hizo. Binafsi nimekuja na mawazo yangu haya nikiitaka TAMISEMI na kuuliza swali. Fedha hizi ambazo zinatolewa kwa makundi mbalimbali ya wanawake na vijana huwa zinarudishwa au tunatoa zaka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu ziko fedha nyingi ambazo zinatolewa kwa vikundi katika nchi hii, lakini mifuko hii iko wapi? Zinarejeshwa wapi? Katika akaunti ipi? Je, kama hatutoi sadaka au kama hatuzitoi kama ruzuku, kama TASAF ni kwa nini hazina return yake?
Mheshimiwa Spika, ukienda katika Halmashauri utawaambia toa fedha na hata CAG hata siku moja hajawahi kuonyeshwa namna fedha hizi zinavyorejeshwa.
Fedha zinapelekwa kwa makundi, basi zinaishia pale. Kila mwaka Halmashauri itasisitiza, tunaziweke msimamo kwamba mchange fedha hizo mpeleke kwa makundi, lakini hatuangalii hizi fedha zinarejeshwa vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, binafsi nilikuwa nawaza kwamba kama mabenki yanaweza kukopesha fedha kwa watu na baadaye mwisho wa mwaka wanatuonyesha kwamba sasa benki hii tulikopesha shilingi bilioni tano, lakini tumezalisha hivi, tumekuwa na mfuko endelevu. Ni kwa nini ndani ya Halmashauri yetu hakuna kitu kama hicho?
Mheshimiwa Spika, nimegundua kwamba fedha hizi zinapotea kiholela, hakuna anayeziona na hata kwenye Halmashauri hatukuambiwa kwamba ziko kwenye akaunti ya deposit, wapi? Kwa hiyo, naomba Wizara itazame ni jinsi gani huu mfuko unaweza ukasimamiwa ukawa endelevu.
Mimi siupingi, naupenda sana, lakini fedha za walipa kodi ndani ya Halmashauri zinapotea bila ninyi kujua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hebu jaribu kufanya research kidogo muone kama hizi fedha huwa zinarejeshwa au zinapotea jinsi zinavyopelekwa? Maana yake Halmashauri zina-respond sasa hizi, zinapeleka shilingi milioni 200, shilingi milioni 300, shilingi milioni 400, that is the end of the story, zinaenda wapi? Hakuna mahali ambapo zinarejeshwa, hakuna return yoyote, hakuna Bunge hata kuelezwa kwamba Halmashauri ya mahali fulani ilikopesha shilingi milioni 500, mwisho wa mwaka tumekuwa na shilingi milioni tano na tumeweza kuendeleza mfuko huu na kama tungefanya hivi, tumekuwa tumeacha hii biashara. Hii biashara ya kuwaambia Halmashauri itenge kila mwaka, kuwasisitiza, kungekuwa na mfuko wao ambao umekuwa endelevu.
Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nimegundua, hii mifuko haina sheria. Hii mifuko inaendeshwa kiholela ndani ya Halmashauri. Kwa vile hakuna sheria, hakuna kanuni na hakuna kamati. Hizo kamati zinaundwa hata Madiwani wa Viti Maalum hawapo. Kwa hiyo, unaweza
kuona ni kwamba pamoja na kusisitiza kwamba fedha hizi zipelekwe, lakini hazina uangalizi hata kidogo. Kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali na TAMISEMI kwamba sasa twende mbali, tutunge sheria, tuwe na kanuni, lakini mifuko hiyo iwe endelevu, ionyeshe faida, izae tupate mfuko maalum ndani ya Halmashauri ambapo fedha zake zinakwenda zina-rotate zinakopeshwa kwa wadau.
Mheshimiwa Spika, kama Serikali hii inaamua tuzitoe kama zaka, tuwatangazie watu wote ziwe sadaka tujue kwamba Halmashauri inatoa sadaka kwa watu na hazirudishwi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije kwenye kodi ya majengo. Amesema vizuri Msemaji wa Kambi ya Upinzani, amejaribu kutoa ushauri. Ninachotaka kukwambia ni kwamba kweli Kamati ya Bajeti imetuambia kwamba hizi fedha zitakuwa zinarejeshwa kwenye Halmashauri kutokana na jinsi
walivyoweka makadirio. Binafsi nikajiuliza, je, kuna sheria inayo-guide kwamba Halmashauri inaweza kupata kiwango fulani? Maana yake mimi nilikuwa kwenye RCC tarehe 2 Machi katika Mkoa wangu wa Kagera, wakatupa taarifa kwamba fedha za kodi ya ardhi hazijarejeshwa mpaka Disemba mwaka 2016, mkoa ulikuwa haujapata hata senti tano.
Mheshimiwa Spika, pale kuna sheria ambayo inasema kwamba asilimia 30 itarudi katika Halmashauri na hata Mfuko wa Barabara una sheria yake; ni kwa nini kwa upande wa majengo hakuna sheria ambayo ina-guide kiasi ambacho kitarudishwa ndani ya Halmashauri? Tunaacha tu holela. Ni kwamba Serikali inaweza ikaamua. Nilikuwa naongea na Mbunge wa Tunduma hapa, ameniambia karibu shilingi milioni 78 za ardhi hazijarudishwa katika Halmashauri yake. Kwa mtindo huo na kwa style hiyo ni kwamba hata hizi fedha za majengo hazitarudishwa, kwa sababu hakuna sheria, hakuna kitu chochote kinacho-guide Halmashauri ikajua kwamba itapata kiwango hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali ifikirie namna ya kuweka sheria ambazo zitawezesha Halmashauri wajue angalau katika kodi itakayokusanywa ndani ya Halmashauri yetu tunastahili kupata asilimia au asilimia 50. Kutoka hapo hata Wabunge wanaweza kuwa mandate ya kusaidia kudai ili Halmashauri zao ziweze kupata fedha.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ngoja niendelee.
Mheshimiwa Spika, leo limetoka swali hapa linalohusu miradi ya maji la Mheshimiwa Kaboyoka, tukapewa majibu; majibu haya wakati mwingine ya kimzaha mzaha hii Serikali ya CCM inatoa.
Mheshimiwa Spika, nilianzia katika Kamati ya TAMISEMI, leo niko kwenye Kamati ya LAAC kwa hiyo, napata chance ya kukagua miradi. Tena nashukuru wewe huendi huko, kwa sababu ungekuwa unaenda, ungekuja huo upara umeota nywele. Hakuna miradi ya maji.
Mheshimiwa Spika, tena nakusihi usijaribu kwenda kule. Nakwambia karibu asilimia 43 ya miradi ya maji haifanyi kazi katika nchi hii.
Ukienda kule utakuta mambo ya ajabu. Hakuna umwagiliaji, hakuna mabwawa, mabilioni ya pesa yamelipwa yaani unabaki kushangaa. Mimi nataka Serikali iwe inatujibu swali kwa nini? Msituambie michakato. Ni kwa nini Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilishindwa kusimamia miradi hiyo?
Mheshimiwa Spika, kuna mkanganyiko kati ya Wizara ya Maji, kuna mkanganyiko katika Halmashauri; ukienda wale wanakwambia aah, sisi wapembuzi yakinifu walitoka kwenye Wizara ya Ardhi. Wamekuja pale wamefanya Wizara ya Maji, wamekuja wamefanya upembuzi yakinifu wanaondoka, wameacha Wakurugenzi hawajui cha kufanya hata fedha wakati mwingine... Halafu na ninyi mna tabia ya kuingilia ingilia mambo ya watu, msini-distract mimi.
Taarifa...
Mheshimiwa Spika, halafu hii tabia ya Mawaziri kujibu kabla ya majumuisho kwa kweli inatupa shida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilichosema, nilikuwa kwenye RCC yangu Mkoa wa Kagera tarehe 2 Machi taarifa ile ninayo. Mimi naenda kwenye vikao mwenzako, nilikuta wanadai tangu Disemba Mkoa wangu wa Kagera hakuna chapa; sasa kama umepeleka jana, hewala. Kwa hiyo, ninachojua ni kwamba hizo fedha haziendi na siyo kwangu tu. Sehemu zote mkifuatilia mtakuta hizi fedha haziendi; na siyo ajabu hata
kwako. Kama umepeleka, basi ni ubinafsi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachosema ni kwamba, nilikuwa naongelea kuhusu mambo ya miradi ya maji, akanipeleka huko, mnani-distract memory kitu ambacho sipendi kwa kweli.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama miradi ya maji haitekelezeki, Waziri atuambie ni kwa nini Serikali inashindwa kusimamia? Wasituletee mambo ya michakato hapa. Watuambie ni kwa nini, miradi hiyo imekwama?
Mheshimiwa Spika, maji ni kero katika nchi hii. Ninyi hamjaona, nendeni katika majimbo yenu labda mahali pengine hamuendi. Kuna mahali nimewahi kwenda kusimamia kampeni sitawasema, watu hawaoshi vyungu, yaani kile chungu kinapika maharage, kinapika na kahawa
ya kunywa. Kwa hiyo, unaweza ukaona ni namna gani nchi hii ilivyo katika matatizo makubwa ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachowaomba hakikisheni nchi hii iweke priority katika kazi hii na msimamie mabilioni ya pesa, mabilioni; na mabilioni hayo ni pesa za watu, ni mikopo, watakwenda kulipa Watanzania. Kwa hiyo, kama mnaona kuna miradi hewa, unakwenda Mkurugenzi anakutembeza hata mradi haujulikani mahali ulipo.
Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo mambo ambayo nilisema nichangie machache…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ya pili eeh, ahsante sana.