Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi asubuhi hii ya leo na mimi naomba nianze kutoa pongezi nyingi na za dhati kabisa kwa Mawaziri wetu, Mheshimiwa Angellah, Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Simbachawene kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya kulitumikia Taifa letu. Ni Mawaziri wasikivu, wachapakazi na mara nyingi ukipeleka shida zako wanakusikiliza na wanakuelewa. Hongereni na chapeni kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayofanya.
Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi makubwa, amerejesha nidhamu ya kutumia fedha na nidhamu kwenye ofisi za umma. Mheshimiwa Rais amethubutu kufanya mambo mazito kwenye reli, anga na barabara. Mheshimiwa Rais
amethubutu kulipa madeni ya nje na leo Serikali yetu inaanza kuaminika. Tuendelee kumuombea nmwenyezi Mungu ampe afya njema na mwenyezi mungu amuongezee ujasili aweze kulitumikia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la Mvomero kwa upande wa elimu. Mvomero tuna upungufu wa walimu zaidi ya 200 kwenye shule zetu za msingi. Kabla sijaendelea naomba niseme kwamba walimu wa Mvomero walikuwa wanaida Serikali shilingi 137,000,000. Naomba niipongeze Serikali kwa kuleta fedha hizi na sasa hivi walimu wa Mvomero hawadai tena. Hongereni sana Mawaziri,
hongera sana Mheshimiwa Rais fedha zimekuja shilingi137,000,000 na walimu wote wamelipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu wa walimu kama 200 tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma.
Jiografia ya Mvomero imekaa vibaya, ukitoka Mvomero unakwenda mpaka Handeni unapakana na Mkoa wa Tanga na Kilindi, unarudi mpaka kwenye mbuga za wanyama za Mikumi, unakwenda mpaka na Chuo Kikuu cha Mzumbe na unapanda mpaka kwenye milima ya Mgeta unapakana tena na tarafa nyingine za Morogoro Vijijini. Jiografia ya Mvomero imekaa vibaya, naomba Waheshimiwa Mawaziri tuangalie
ni jinsi gani Mvomero tunaweza kuigawa aidha katika Halmashauri mbili au katika majimbo mawili. Mvomero imekaa vibaya tunatumia muda mwingi sana kutembea kupeleka huduma, naomba Serikali iliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika Wilaya ya Mvomero tuna tarafa nne lakini tuna sekondari mbili za Alevel.
Tunaomba Serikali itusaidie fedha ambazo tumeomba zile tarafa mbili zilizobaki tuweze kupata sekondari za A-level. Tarafa za Turiani na Mvomero zinazo shule hizo, lakini tarafa viongozi mtusikie katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la TASAF kwa ufupi kabisa. Fedha za TASAF zinazokuja katika zoezi la kusaidia kaya maskini zinakwenda muda mbaya.
Wataalam wetu wanatoka na fedha benki jioni saa kumi, wanatembea kwa zaidi ya saa mbili/tatu wanafika usiku, wananchi wengine wanakuwa wameshapata vinywaji wamechangamka kunakuwa na vurugu. Naomba Waziri, dada yangu Mheshimiwa Angellah uliangalie hilo na utoe maelekezo na waraka kwamba fedha zipelekwe muda wa mchana na muda mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la zahanati na afya. Mheshimiwa Waziri Wilaya ya Mvomero tuna upungufu mkubwa sana wa huduma ya afya. Tumejenga Hospitali ya Wilaya, jengo limekamilika lakini bado umeme. Bajeti ambayo wataalamu wetu waliiandaa tunahitaji shilingi 100,000,000 tuweze kuifungua hospitali ile ya Wilaya na fedha hizi tayari tumeziomba. Naomba Mawaziri mnaohusika muweza kutuidhinishia fedha hizo tuweze kufungua Hospitali ya Wilaya ya Mvomero. Nawaombeni sana fedha zilizotumika ni nyingi, idadi ya fedha iliyobakia ni ndogo, tunaomba bajeti ile idhinishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna Hospitali Teule inaitwa Turiani Hospitali. Hospitali ile wananchi ambao wanakwenda kupata huduma pale wanapata huduma kwa gharama kubwa. Hospitali ile haitusaidii chochote wananchi wa Mvomero. Fedha ambazo zinapelekwa bado hazisaidii, wananchi wanatozwa gharama mbalimbali na taratibu hazifuatwi. Huduma wanazopata mama na mtoto bado wanatozwa na sera ya Serikali inasema huduma ya mama na mtoto ni bure. Mheshimiwa Jafo uliniahidi kwamba tutakwenda pamoja Mvomero, naomba tekeleza ahadi yako, tukimaliza Bunge hili au Jumamosi moja chapa kazi twende zetu ukaone matatizo yaliyopo na uweze kutushauri na kutusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naomba niliseme, Wilaya ya Mvomero imebarikiwa ina mito mingi, maji mengi na ardhi nzuri sana. Tuna green land kubwa sana Mvomero. Wabunge karibuni, chukueni mashamba mlime.
Tatizo letu tunahitaji tusaidiwe na Serikali ili kilimo kile kiwe kilimo cha kisasa tuweze kupata fedha za kutusaidia baadhi ya maeneo tuweze kumwagia zaidi tuweze kuyatumia yale maji vizuri. Fursa kubwa ipo tatizo ni fedha tunazoomba haziletwi kwa wakati na zinakuja fedha ndogo. Naomba sana fedha hizo zije kwa wakati ziweze kutusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho kabisa na naona muda unakwenda, tunaomba sana Idara ya Ujenzi Mvomero inayoshughulikia barabara haina gari kufuatilia miradi ya barabara. Mheshimiwa Jafo tuliongea jambo hili ukaniambia tutakaa chini tutazungumza. Naomba kupitia bajeti ya Wizara yenu, Mvomero jiografia yake imekaa vibaya, tunaomba gari Idara ya Ujenzi tuweze kufuatilia barabara zetu tuweze kuleta maendeleo kwa Mvomero yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni na naunga mkono hoja mia kwa mia.