Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Upendo Furaha Peneza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii na namshukuru Mungu ambaye meniwezesha kufika katika Bunge hili la Bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajielekeza moja kwa moja kwenye mambo ya msingi ya kuchangia napenda niongelee suala moja. Hapa kuna miongozo kadhaa iliombwa na uliitolea ufafanuzi lakini utaratibu ambao umesema ufuatwe wa watu kwenda kwenye hizo taasisi za
ajira nadhani ni vizuri tukatambua kwamba hili suala sana sana linaelekea kwenye mambo ya human trafficking ambapo watu hawa wanasafirishwa kwa njia ambazo sio nzuri. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaangalia ni namna gani inawalinda watoto wetu kutokana na hiyo biashara haramu ili pia wasiweze kupatwa na matatizo. Kwa hiyo, suala hili naomba liangaliwe katika muktadha wa human trafficking.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni la mama yangu hapa Mama Mollel ambapo Baba yangu ninayemheshimu amelizungumzia lakini niseme tu mama alijiunga na CHADEMA katikati ya uchaguzi. Kwa hiyo, si vizuri kuwadhalilisha viongozi wetu ambao tunawaheshimu katika Bunge letu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa najielekeza katika suala ambalo lipo mbele yetu hapa. Tunafahamu kwamba nchi yetu na viongozi wetu ambao wako hapa wameweza kutueleza kiundani kuhusu masuala ya utawala bora. Hata hivyo, katika masuala ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji
ni vitu vya msingi sana vya kuweza kuzingatiwa ili kuweza kuupata huo utawala bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha nyuma wananchi kwa kiasi kikubwa sana wameshiriki kikamilifu kushirikiana na Wabunge kwa ajili ya kuiwajibisha Serikali. Naongea hivi kwa maana moja kwamba kipindi cha nyuma tulikuwa na Bunge live ambapo wananchi wamekuwa
wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge wakiweza kusikiliza vipindi vinavyoendelea ndani ya Bunge ambapo imewasaidia wao kwanza kuelewa hata sheria zinazopitishwa ndani ya Bunge, kuelewa bajeti ambayo inawagusa moja kwa moja lakini pia kuna mambo mengine ambayo yameweza kuwagusa wananchi moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge hili upande wa Chama cha Mapinduzi waliunga mkono sana suala la Bunge live kuondolewa, lakini kuna watu ambao ni wanawake ambao ndiyo waathirika wakubwa kwa kuliondola hili suala la Bunge live. Jana tumesikiliza jinsi ambavyo idadi ya wanawake imepungua katika Baraza la Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na nafasi mbalimbali za Kiserikali. Kwa hiyo, sisi kama wanawake tuna nafasi ya kwenda kugombea katika majimbo na katika jamii zetu zilizojaa mfumo dume, Bunge live limeweza kubadilisha
umma na kuona kwamba wanawake wanaweza. Pia kuna mambo ya msingi mengi ambayo wanawake tumeweza kuyainua ndani ya Bunge hili, kuna masuala ya ndoa za utotoni uelewa watu umeweza kubadilika, kuna masuala mbalimbali yanayowagusa mabinti zetu kule nyumbani
wananchi wameweza kubadilika taratibu kutokana na kwamba wanasikiliza Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile kuna ripoti ya TWAWEZA ya mwaka 2012 inayoonesha kwamba masuala ya ukeketaji yamepungua kwa asilimia 21 na inatokana na mchango wa Bunge. Kwa hiyo, wananchi waliokuwa wakifuatilia Bunge wameweza kubadilika na kuona kwamba kuna haja ya kuweza kupunguza masuala ya ukeketaji na hii inatokana na mchango wa Bunge ndani ya Bunge hili letu
Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba yawezekana ni maagizo tunasingizia kupunguza matumizi ya Serikali kwa masuala ambayo yanaathiri masuala ya kijamii na kijinsia. Kwa hiyo, kama wanawake sasa kuna haja kubwa ya kusimama na kudai hili suala la Bunge live kwa sababu linatuathiri. Hata kama hamuwezi kuteuliwa kwenye Baraza la Mawaziri basi tukapata nafasi za uwakilishi kule chini na nina imani wanawake kwa pamoja hebu tufanye mambo ya msingi kwa ajili ya maisha yetu na watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine ambalo napenda kuzungumzia katika masuala ya Serikali za Mtaa na niseme tu namshukuru Naibu Waziri Mheshimiwa Jafo kwa kuweza kufika Geita na kwa kujibu swali langu ambalo lilikuwa ni kuhusu masuala ya maji na bwawa. Napenda tu pia uje utuambie ni lini sasa hiyo Tume ambayo ulisema itaundwa itaenda kuchunguza ubadhirifu ambao umefanywa katika
eneo hilo hapo Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna suala lingine Waheshimiwa Mawaziri wa TAMISEMI ambalo napenda kulitolea ushauri na pia imeshalitolea ushauri ndani ya Halmashauri yangu ambayo ninatoka. Geita ni kati ya Halmashauri nyingi ambazo zinapokea service levy ya 0.3% kutoka Mgodi wa Geita Gold Mine kutoka kwenye gross revenue, pesa hizi zinavyotumika nyingi zinatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya kuendesha shughuli mbalimbali za Halmashauri. Niiombe Serikali, tumetoa mwongozo hatujatunga sheria kuhusu utaratibu wa 5% kwa wanawake na 5% kwa ajili ya wanaume. Hebu tuweke utaratibu sasa kwamba walau 70% ya pesa zote zinazotokana na service levy ziweze kwenda kwenye shughuli za maendeleo na 30% ziingizwe katika matumizi ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili litatusaidia, hapa tunasema kwamba wananchi bado wana wajibu wa kuchangia huduma mbalimbali za kihuduma katika maeneo yetu, lakini kuna hela ambazo zinatoka katika maeneo ya mgodi, kwa hiyo naiomba sasa Serikali iweze kutoa
mwongozo huo ili pesa hiyo iweze kusaidia shule za maana zipatikane. Kwa sababu hizo hela hazina mwendelezo miaka si mingi pesa hizo zitakata kwani mgodi utamaliza shughuli zake. Kwa hiyo, ni afadhali sasa hizo pesa ziwe zimeshaingizwa kwenye shughuli za maendeleo za wananchi ili hata miaka ijayo watoto wetu watuone tuna maana, tulizitumia hizi hela kwa ajili ya faida yao, wamekuta huduma nzuri za afya na shule kutokana na kutumia hizi pesa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwamba tuna tatizo kubwa sana nchi hii. Mheshimiwa Rais alipokuwa anaingia madarakani alikataza mambo ya semina elekezi suala ambalo limezungumzwa pia katika hotuba ya Kambi ya Upinzani kwamba mafunzo elekezi ni suala nyeti sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwetu kule tuna shida, Mkuu wa Wilaya anawafukuza Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wakati sheria iko wazi, Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa anaondolewa na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi Mheshimiwa Rais yeye mwenyewe alikiri akasema kwamba yeye huu urais amepata tu, simu alipiga ikaitika. Kwa hiyo, kwa lugha nyingine yeye mwenyewe alikuwa anastahili elekezi fulani, namheshimu sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaangalia suala la watumishi wetu Serikalini tumekuwa na watu tunaowalipa mara mbili mbili. Hapa tunajifunza kwamba scheme of service inasema mtu anakuwa promoted baada ya miaka mitatu kutokana na ripoti ya utendaji wake mzuri, lakini suala
hilo halifanyiki ni kwa sababu Serikali hamna pesa, fedha nyingi mnalipa Wakurugenzi wawili, ma-DED wawili, ma-DAS wawili tutafika wapi kwa namna hiyo? Kwa hiyo, watumishi wa Serikali wanakosa morali kazi hazifanyika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wa Serikali wanavunjika moyo na zaidi ya hapo bado tunawatumbua kiholela bila kuheshimu hata nafasi wala mamlaka walizonazo. Hata ndugu zangu hapo Waheshimiwa Mawaziri nyie pia mnakumbwa na hilo, heshima ya kuthamini utendaji
wa mtu inakuwa haipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iangalie hili suala kama hawa watu wanapangiwa maeneo wapangiwe wawe productive kuliko kukaa nyumbani. Serikali mnalipa watu mishahara ambao hawana kazi ya maana ambayo wanaifanya katika Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile haya masuala kwamba hatuna hela, Serikali ifanye mkakati itafute pesa watu tuwapandishe vyeo kutokana na ripoti na ufanyaji kazi wao mzuri ili tuweze kuwa na wafanya kazi wazuri ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi cha nyuma pamoja na kwamba Rais wa sasa alimbeza sana Rais aliyepita lakini alikuwa anatafuta viongozi au watu mpaka kutoka nchi za nje, watu wenye uelewa na wenye taalum fulani…
KUHUSU UTARATIBU...
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nadhani hata pamoja na kwamba tuna roho ya kuwatetea viongozi au mabosi wetu, lakini hebu tuwe wakweli, kama haya masuala hayakuandikwa hata kwenye vyombo vya habari mseme kwa sababu ni vitu ambavyo
vimeandikwa na vimesikika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niseme tu na hata nilivyozungumzia masuala ya semina elekezi hata kwa Mheshimiwa Rais mwenyewe si kawaida. Mheshimiwa Rais kweli, kuna kuteua Wabunge hapa si imeleta shida mpaka imebidi mtu tena mwenye ulemavu atolewe ni masuala ya shida hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni kijana, naomba niseme kwamba naipenda nchi yetu hii, lakini pia namheshimu sana Mheshimiwa Rais, ni jirani yangu, ni baba yangu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Peneza jambo moja tu, kwa sababu nimesema ili tusianze kwenda mbele na nyuma, Rais wa sasa kuhusu kumbeza Rais aliyepita. Naomba hilo uliweke sawa ili tuweze kusonga maana hiyo sentensi ndiyo yenye kuleta taabu hapa.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, labda sijui kama ni neno kubeza niseme basi alikuwa akizungumzia upungufu kwenye utawala wake na yeye hawezi kuyafanya kama yeye alivyofanywa, labda niseme kwa mfumo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nimalizie kwa kusema neno moja kwamba naipenda nchi hii, lakini nathamini pia viongozi. Pia niseme kwamba tunahitaji…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.