Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Savelina Slivanus Mwijage

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Na mimi napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia, napenda kupongeza Shirika la UN walioweza kuwajengea watu wa Bukoba waliopata tetemeko. Wale wasiojiweza wamewajengea mabanda ya kujihifadhi wazee na maskini, napenda kuwapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie kwenye pesa za mchango wa tetemeko Bukoba. Hizo pesa walisema zinakwenda kujenga miundombinu ya shule za Iyungo na Nyakato. Ni jambo la kusikitisha pesa ipo na majengo hayajajengwa, wamevuruga tu wakaacha hivyo hivyo, hao
wanafunzi wataweza kurudi kusoma au ndiyo mwisho?
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanashangaa sana kwa sababu hizo pesa zilichangwa kwa ajili ya kuwasaidia watu waliopata madhara, lakini ikaamuliwa kwenda kwenye miundombinu. Mimi sijawahi kuona watu wanatumiwa pesa za kuwasaidia katika matatizo yao zinapelekwa sehemu nyingine. Je, tetemeko lisingetokea miundombinu isingejengwa? Naomba kama pesa hizo zimeshapelekwa kwenye miundombinu basi shule zijengwe tuweze kujua hiyo pesa imefanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Watu wengi wameongea kwamba Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wamekuwa Miungu watu katika Wilaya na Mikoa yetu. Wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira magumu kwa sababu ya
kutishwa kuondolewa kazini. Kwa hiyo, tunaposema semina baadaye wanabadilisha kwamba tunabeza, wanapaswa wapewe semina, wasiwe Miungu watu kuwatisha wafanyakazi. Wafanyakazi tunawategemea na wanafanya kazi katika mazingira magumu, unakuta Mkuu wa Wilaya
ndiye analeta migogoro ya ardhi ndani ya Halmashauri.
Nilishawahi kumletea Mheshimiwa Waziri Lukuvi tatizo la Mkurugenzi wa Bukoba Vijijini anavyovuruga Halmashauri, wapewe semina wajue mipaka yao, wasipende kuwavuruga wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye malipo ya wafanyakazi na walimu. Hatujabeza elimu bure ila tunazungumzia mazingira ya walimu, mazingira yaliyoko katika shule, ukienda kwenye shule nyingi watoto hawana vyoo watapata akili gani ya elimu bure na kuendelea kupata
elimu nzuri. Hawana mahali pa kujihifadhi, hawana maji, unakuta wasichana na wavulana matundu ya vyoo yamepakana na magonjwa kuambukizana inakuwa ni rahisi.
Hatubezi, bali tunaongelea mazingira yalivyo na walimu wanadai pesa zao na wewe Naibu Spika, sisi tukikosa posho yetu hapa tunalalamika, niambie mwalimu anayekwenda kumfundisha mtoto hajui chochote anakosa pesa yake atakuwa na akili gani ya kuweza kumfundisha yule mtoto? Naomba sana pesa za walimu zikalipwe ili waweze kuwa na nguvu za kuweza kufundisha watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Hospitali za Wilaya. Bukoba Mjini tumepata Hospitali ya Wilaya iko mbali kabisa na mji, haina miundombinu, njia yenyewe shida. Tuliomba Serikali kwamba Hospitali ya Wilaya waboreshe yale majengo ya Zamzam ili mgonjwa akitoka kwenye Hospitali ya Mkoa iwe rahisi kuingia kwenye Hospitali ya Wilaya. Hivi sasa watu wanateseka imebaki kuwa hospitali ya majanga
kwa sababu juzi ndiyo imesaidia kipindi cha tetemeko. Naomba sana hata yakiwa majengo mawili, matatu lakini yako karibu na wananchi siyo hospitali iko kijijini kabisa kule, miundombinu ya shida, watu hawaijui iko wapi. Wakifika mkoani pale wakakuta wodi zimejaa, wanaambiwa nenda kwenye Hospitali ya Wilaya kufika shida na dawa shida. Juzi wakati wa mafuriko haya watu wamehangaika, kuna daraja limepelekwa na yale maji wanavuka kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya wanashindwa kwenda mtu anakaa pale pale anakosa hata mahali pa kwenda kutibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye tunaosema utawala bora. Tunasomesha wanafunzi wetu, vijana wanapata elimu wanakwenda kwenye vyuo lakini inafika wakati wa kupata ajira wanakosa ajira, unakuta vijana wana vyeti vyao vizuri tu lakini wanaendesha bodaboda, ni aibu. Juzi umeona wametangaza kuwapeleka Kenya madaktari wengi walijitokeza na sisi hatuna madaktari katika nchi yetu inakuwa ni shida ni kwa sababu ya kukosa ajira. Kwanza tuwape ajira watu tuliowasomesha kwa pesa za Serikali ili waweze kulitumikia Taifa lao na sisi tufaidike na watoto wetu tunaowapeleka shule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea suala la Madiwani. Madiwani wanapata shida kwa sababu sasa hivi mapato ya Halmashauri zetu ni madogo sana. Unakuta barabara za kuunganisha Wilaya kutoka Bukoba Mjini kwenda Bukoba Vijijini na kutoka Misenyi kwenda Karagwe barabara ni mbovu hawana, hata pesa zile za maendeleo. Serikali inatenga pesa lakini hazifiki kwa wakati. Tumekagua
miradi mingi tumekuta pesa zinazoahidiwa na Serikali hazifiki kwa wakati kwa hiyo miradi inakuwa viporo. Sasa tunaiomba Serikali pesa zinazotengwa wakati huu zikipatikana wamalize viporo ndiyo waweze kuanza miradi mipya. Tukiendelea kuongeza miradi mipya na viporo ni vingi hatutaweza kwenda mbele. Ndiyo maana unakuta wengine tukisimama hapa tunasema Serikali imeshindwa ni kwa sababu ya kupanga mipango mipya ya zamani tunaiacha ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka leo hii Madiwani wanakopwa na Serikali kwa vikao wanavyokaa. Diwani anatoka zaidi ya kilometa 30 anakwenda Halmashauri kwa mfano kama Bukoba Vijijini. Wilaya ya Bukoba Vijijini iko Bukoba Mjini na tayari walishatenga viwanja vya kujenga Wilaya lakini mpaka leo hii hakuna mipango mikakati inayokwenda, anatembea kilometa zaidi ya 30, 40 anakuja Bukoba Mjini kwenye vikao, hapati posho zake, hana hata nauli ya kurudi kule, unamkuta amepanda ule usafiri wa mtaji wa maskini nguvu zake mwenyewe (baiskeli) kutoka kule ni mbali sana. Naomba Bukoba Vijijini Halmashauri ijengwe katikati ya Wilaya, wametenga kiwanja kikubwa tu Mgaza.
Diwani kukopwa na Serikali ni aibu, wapate posho zao, kile wanachokipata ni kidogo sana. Wangekuwa na pesa za maendeleo, wanapesa wanakusanya vizuri katika makusanyo yao ya Halmashauri ingekuwa ni nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Hospitali ya Mkoa. Hospitali yangu ya Mkoa pale, namshukuru Mheshimiwa Jafo anajitahidi sana akifika Bukoba anazunguka sana, nampongeza sana na ukimletea tatizo lako anaweza kukusikiliza. Tatizo letu mpaka hivi sasa Bukoba
Mjini hatuna mahali pa kuhifadhia maiti, kachumba ni kadogo, vijokofu hamna mpaka tunasafirisha maiti kupeleka Bugando. Ni aibu Hospitali ya Mkoa kukosa chumba cha kuhifadhia maiti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna wodi ya wazazi
pale, ni ndogo sana, ina vitanda sita, wewe
Naibu Spika ni mwanamke unakuja unaumwa uchungu unamsubiri mwenzako ajifungue ndio na wewe uingie, itawezekana, si utajifungulia kwenye simenti pale. Serikali ilishajiandaa kujenga lakini leo hii wamekaa kimya na hivi sasa nitaomba msaada kwa watu wa MSD waweze kutusaidia hata vitanda viwili angalau viwe nane waweze kupata mahali pa kujifungulia au hata ipanuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwa wanafunzi ambao wamemaliza chuo na wanafunzi wengine, nikimaliza kuchangia hapa nitakwenda kwa Mheshimiwa Waziri wa Elimu, wanafunzi wanazuiwa kufanya mitihani kwa kuwa wanadaiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshiniwa Waziri yuko pale napenda nimueleze kwamba mpaka sasa hivi Chuo cha Mwalimu Nyerere watoto wameshindwa kufanya mitihani kwa sababu wanadaiwa. Wameomba wakaambiwa jazeni fomu mtafanya mitihani mpaka sasa hivi wako nje hawajafanya mitihani kwa semester ya kwanza na ya pili. Tunaposema elimu bure basi tuwajali na wanafunzi wetu na wale watoto pesa wanapewa na wazazi kwenda kulipia karo, wawavumilie wafanye mitihani ikifika wakati wa kupata vyeti wawanyime vyeti mpaka walipie ile pesa yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye matatizo yanayotokea Mkoa wa Kagera, nimalizie na hili. Watu wakimuongelea Rais mnasema kwamba tunamuongelea, hatumuongelei yeye bali yale matamshi. Vitabu vya dini vinasema mdomo unaumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nampenda sana, ni jirani yangu, amefika katika maafa anawaambia watu wa Kagera mimi sikuleta tetemeko, kweli mdomo unaumba. Kwa hiyo, naomba afute kauli yake ndipo watu wa Bukoba watakuwa na heshima na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba afute kauli ya kuwaambia mwafa, hilo
jambo limekuwa kero kwa Watanzania na kwa wananchi wa Kagera. Kwa kweli wanaumia sana na jambo hilo. Hata Waziri Mkuu akisimama hapa afute hiyo kauli ili wananchi wa Mkoa wa Kagera waweze kuwa na imani na Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.