Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Dua William Nkurua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. DUA W. NKURUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara yetu ya TAMISEMI. Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na afya njema nikaweza kuchangia muda huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekutana hapa kuviangalia vipaumbele vya Taifa hasa katika matumizi ya pesa yetu kwa muda wa mwaka wa fedha 2017/2018. Kwa hiyo, vipaumbele vya Taifa vipo na mimi kama Mbunge nitajaribu kuviongezea vile ambavyo Wizara labda
hamkuviona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niishukuru Wizara kwa kuruhusu baadhi ya Halmshauri kutumia asilimia 60 kwa ajili ya kuendesha Halmashauri na asilimia 40 kwa miradi ya maendeleo. Suala hili kwa mtu ambaye hajadumu sana Halmashauri anaweza akaliona ni dogo, lakini Halmashauri nyingine hazina uwezo wa kuendesha Halmashauri zao. Kwa hiyo, unapowaambia watumie asilimia 60 kwa maendeleo kinachotokea ni kwamba wanakwenda kuathiri pesa zingine na cha kwanza kinachokwenda kuathiriwa ni pesa za mikopo ya akina mama na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kuziruhusu baadhi ya Halmashauri kutumia asilimia 40 kwenye maendeleo na asilimia 60 kuendeshea Halmashauri yao itasaidia kufuata kanuni ambazo Serikali imeweka kuliko pale mwanzo ambapo mlikuwa mnalazimisha asilimia 60 ambazo zilikuwa hazifanyi kazi. Mkumbuke hapo mwanzo ilikuwa asilimia 60 inakwenda kwenye maendeleo, asilimia 20 inakwenda kwenye vijiji na asilimia 10 ilikuwa mikopo ya vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utakuta asilimia 90 imekwenda kwenye mpango ambao Serikali imeelekeza lakini matokeo yake yalikuwa hayaendi vizuri. Kwa hiyo, hilo nalipongeza sana kwa mtazamo huo na nafikiri Halmashauri ya Nanyumbu itakuwa ni mojawapo ambayo itawekwa katika asilimia 40 ili waweze kuendesha vizuri Halmashauri yao na waweze kusimamia pesa nyingi ambazo Serikali inapeleka kule Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa kwanza naenda kujikita kwenye elimu. Nafahamu kwamba Taifa lolote ambalo elimu haijakaa vizuri, basi tutakuwa na matatizo mengi kwa sababu elimu ndiyo kama taa, ndiyo kama mwongozo wetu wa kuweza kupambana na maisha
haya ya dunia. Sasa Serikali yetu imeweka vipaumbele vingi katika elimu, imetuonesha katika Bajeti yake mambo gani ya msingi yatakwenda kuzingatiwa ili tuweze kuisimamia vizuri elimu. Sasa nayaunga mkono yote hayo na nataka nisisitize baadhi ya machache.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, Serikali iweke utaratibu wa wazi wa kuweza kuboresha miundombinu ya shule. Tuna matatizo ya madarasa, nyumba za Walimu na Walimu. Maeneo haya matatu yanatusumbua sana katika Serikali yetu. Naiomba sana Serikali isaidie Halmashauri katika ujenzi wa shule, nyumba za Walimu na vyoo katika shule zetu zote za nchi nzima. Katika eneo hili itatusaidia kuwa na shule
zenye ubora, lakini pia kuwa na Walimu wenye moyo wa kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka Serikali itilie mkazo ni malipo ya Walimu. Nimeona mkakati ambao Serikali imeuweka, naupongeza, lakini naomba sana Serikali isisitize kuhakikisha kwamba Walimu wetu wanapata malipo yatakayowasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine katika elimu ambalo naomba sana Serikali iliangalie ni uhaba wa Walimu. Wilaya ya Nanyumbu, kwa matokeo ya Darasa la Saba mwaka jana tulifanya vibaya sana katika Mkoa wa Mtwara, lakini pia hata Kitaifa hatukwenda vizuri. Sisi kama Wilaya tulikaa tukayaangalia matatizo yetu ya ndani tujue ni kwa nini tumefika hapo? Tukayabainisha na tumejipanga kukabiliana nayo. Tunayo timu kule ya watu, tunao Madiwani, tunaye Mkuu wetu wa Wilaya, anafanya kazi vizuri sana. Tunahakikisha yale matatizo ya ndani tutakabiliana nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo matatizo ya nje ambayo lazima Serikali itusaidie. La kwanza, tuna uhaba mkubwa wa Walimu. Wilaya ya Nanyumbu inahitaji Walimu zaidi ya 1,100 lakini ina Walimu kama 600 hivi. Kwa hiyo, tuna upungufu wa Walimu zaidi ya 450. Kwa hiyo, unakuta kwamba uhaba huo wa Walimu ambao umekithiri, huwezi kuwa na wanafunzi watakaofanya vizuri. Ni sawa na timu isiyo ya kocha, haita-perform vizuri. Kwa hiyo, naomba sana Serikali katika mgao wa Walimu awamu hii ihakikishe kwamba Nanyumbu inapata Walimu wa kutosha ili tuweze kuwa na elimu bora ambayo Serikali inalenga kuifikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka nilichangie ni afya. Nafahamu Wizara hii ina kazi kubwa, inasimamia afya zetu na za wananchi wetu pia. Afya inafanana na elimu. Tuna uchache wa Zahanati na Vituo vya Afya. Sera ya chama chetu ambayo ndiyo inaongoza
nchi hii, tulikubaliana kwamba tutajenga Zahanati katika kila kijiji, lakini nafahamu kwamba safari hii ni ndefu, hatuwezi kujenga leo wala kesho tukamaliza vijiji vyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri zitaweka vipaumbele wapi ikajengwe; lakini naomba sana, Serikali iweke mpango maalum utakao-support Halmashauri kukamilisha lengo hili. Halmashauri zetu nyingi hazina uwezo wa kukamilisha hili. Kwa hiyo, Serikali iweke mpango ambao utaruhusu pesa nyingi kwenda Halmashauri ili kujenga hizo Zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi huo hautatusumbua sana. Wananchi wamejiandaa kujenga zahanati, tusifikiri kwamba Serikali itakwenda kujenga complete hii zahanati. Wananchi wamejitoa sasa, kwa hiyo, cha msingi ni Serikali kupeleka pesa na wananchi watajenga, pale ambapo Serikali itahitaji isaidie, tutamalizia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali tupeleke pesa ambazo zita-support jitihada za wananchi katika ujenzi wa zahanati katika vijiji vyetu. Tuliahidi wenyewe; nina uhakika kwa kasi ambayo tunayo ya ukusanyaji wa mapato na seriousness ya Serikali yetu na Rais
wetu, suala hili tutalikamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna watu wanafikiri ni ndoto, lakini nina uhakika kwamba kwa kasi ya Serikali yetu na kwa kasi ya Rais wetu, suala hili litafanikiwa na wanaobisha tutakutana 2020; watahakikisha! Tutafikia pakubwa, kwa sababu pesa ndiyo itakayofanya haya na
wananchi wetu tumeweza kuwaandaa vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitahukumiwa na wananchi wangu wa Nanyumbu kwa jinsi nitakavyohamasisha na Serikali itakavyoniletea pesa ya kumalizia majengo hayo. Kwa hiyo, naiomba Serikali tutenge pesa maalum kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati na Vituo vya
Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni watumishi. Tuna uhaba mkubwa wa watumishi wa zahanati zetu. Naomba sana Serikali ijipange kuhakikisha kwamba tunaweza kumudu kuwatuma watumishi katika zahanati zetu kwa sababu tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi katika zahanati zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka nilichangie ni posho ya Waheshimiwa Madiwani. Madiwani wetu wana kazi kubwa sana na wengi hapa wamegusia namna ambavyo Madiwani wanasimamia pesa ambazo Serikali inapeleka kule. Sasa huwezi kumtuma mtu akasimamie pesa, mwenyewe amechanganyikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, posho ya Madiwani ni ndogo, sisi tulikuwa huko, tumeiona ni ndogo sana kiasi kwamba wanakosa moyo wa kuweza kusimamia vizuri pesa ya Serikali ambayo ni nyingi inayokwenda kule kwenye Halmashauri. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ihakikishe
kwamba posho ya Madiwani inapanda. Imepanda siku nyingi sana; tuliomba mwaka 2016 na mwaka huu sijaona kama imeendelea vizuri. Kwa hiyo naomba sana posho ya Madiwani izingatiwe ili tuwape motisha Madiwani hawa waweze kusimamia vizuri pesa ya Serikali ambayo inakwenda kule katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la mwisho, ni posho pia au niite mshahara wa viongozi wetu wa vijiji. Ni eneo lingine ambalo tumelisahau. Tuna vijiji vingi nafahamu, mzigo ni mkubwa lakini twende tuanze tuwaoneshe njia. Tuna Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Vitongoji. Hao wote
wanafanya kazi katika Serikali yetu kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na amani na wanakuwa na maendeleo, wanasimamia maendeleo kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali katika mipango yake ituambie namna gani inafikiria kuhakikisha kwamba wananchi hasa Viongozi wa Vijiji na Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wanapata posho au mshahara ili wawe na moyo wa kuweza kutumikia vizuri Serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.