Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote nianze kumshukuru Mungu kwa nafasi hii, lakini vile vile niendelee kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Muhambwe kwa kunituma kuja kuwatumikia kama Mbunge wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitamani sana nizungumze kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Pamoja na mambo mazuri yaliyoongelewa kwenye hotuba yake, lakini nina ushauri mdogo sana ambao ningependa niutoe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la Private Public Partnership (PPP); nitaongelea hasa kwa Jiji la Dar es Salaam kama ushauri. Naamini Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi itaupokea. Kuna suala la ujenzi wa kipande cha barabara kutoka Dar es Salaam mpaka Chalinze, sina tatizo na hiyo; na kuna kipande cha barabara kutoka Oysterbay ambacho kitakwenda mpaka Ocean Road. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri mdogo tu kwa Serikali yangu kuhusu kipande cha barabara ya kutoka Oysterbay mpaka Ocean Road. Ni kweli kwamba kile kipande kinajengwa kwa ajili ya kusaidia kupunguza foleni katika Jiji la Dar es Salaam, lakini kwa maamuzi ya Serikali ya
kuhamisha Makao Makuu kuja Dodoma, naona uwezekano wa foleni hasa kipande cha kutoka maeneo ya Bunju mpaka Mjini ikiwa inapungua. Nilikuwa Dar es Salaam juzi nimeona kabisa kwamba foleni inapungua na hapa wamehama wafanyakazi wachache sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini watakapohama kabisa, kile kipande cha barabara kutoka Oysterbay kwenda Ocean Road ambacho kikimalizika itatakiwa watu wawe wanalipia ili kufika mjini, kinaweza kukosa pesa ya kurudisha kwa ajili ya kuwalipa wale private na hivyo tukaiingiza Serikali kwenye gharama ya kulipia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba kama kuna uwezekano, kama hatujafika mbali sana kwenye hatua hiyo, basi Serikali iangalie namna ya kuzitoa hizo pesa zije huku Dodoma zijenge miundombinu tutanue mji wetu ambao hakika sasa hivi tunaanza kuiona foleni hapa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ushauri huo, niingie kwenye hotuba ya TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utawala Bora. Kwanza nawashukuru sana Ofisi ya TAMISEMI; Mheshimiwa Waziri Simbachawene na Msaidizi wake Mheshimiwa Jaffo kwa kazi nzuri sana wanayoifanya.
Wamekwishatembelea sana sehemu mbalimbali za nchi yetu na kwangu Wilaya ya Kibondo wameshafika. Nashukuru sana kwa shughuli mbalimbali wanazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea sana Kituo cha Afya cha Kifura katika Wilaya yangu ya Kibondo. Kituo hiki cha Afya kimesahauliwa sana kwa muda mrefu.
Miundombinu yake imekuwa chakavu, lakini hicho kituo kimezidiwa kiasi ambacho kinasababisha hata Hospitali ya Wilaya nayo izidiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke tu hii hospitali ya Wilaya ya Kibondo inatumika kama Hospitali ya Rufaa kwa Hospitali ya Kakonko kwa jirani yangu Mheshimiwa Bilago.
Wale pale hawajawa na Hospitali ya Wilaya inayoitwa Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, rufaa zao zote wanazileta Kibondo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya yangu ya Kibondo pale, kwa takwimu za mwaka 2012 ina watu 290,000. Kwa sasa hivi lazima watakuwa wameshazidi, lakini tuna Kambi ya Wakimbizi ya Nduta ambayo Hospitali yao ya Rufaa na wao ni Hospitali ya Wilaya ya Kibondo, ambayo miundombinu yake bado ni ya mwaka 1969. Naomba sana Serikali iangalie hilo iweze kupanua miundombinu katika hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile miundombinu ya maji katika Wilaya yetu ya Kibondo ambayo ni ya toka mwaka 1973, bado inaendelea kutumika mpaka sasa hivi.
Kumbuka mwaka 1973 tulikuwa na wakazi wasiozidi 64,000, sasa hivi tuna watu zaidi ya 290,000 ukiondoa watumishi wanaokuja kuhudumia wakimbizi ambao tunao wengi sana; kwa hiyo, huduma ya maji ni ya kiwango cha chini sana katika Wilaya yetu ya Kibondo. Tunaomba sana Serikali iliangalie hilo tuweze kupata miundombinu ya maji ya kuweza kutosheleza watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulijaribu kuongea hata na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani asaidie kuhusu suala la kuwabana UNHCR ambao ndio wameleta wakimbizi pale wasaidie katika suala hilo. Naamini Waziri wa Mambo ya Ndani bado analishughulikia suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe shukrani ya dhati kwa Wizara ya Afya kwa kutuletea gari moja ya kuhudumia wagonjwa (ambulance). Gari hiyo imekuwa ni ya msaada mkubwa sana kwa akinamama na watoto ambao walikuwa wanapata shida sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie kwenye suala la ahadi za Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais wakati anafanya kampeni zake, mwaka juzi, 2015 alipita pale Wilayani Kibondo akaahidi ujenzi wa kipande cha lami cha kilometa sita. Kila nikienda kule, huwa nadaiwa. Naomba sana, TAMISEMI waangalie namna ya kuweka kwenye mahesabu yao, hicho kipande cha barabara kiweze kujengwa, kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo aliwaahidi wananchi wa Wilaya ya Kibondo na Wilaya ya jirani ya Kakonko, nakumbuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine aliloliahidi Mheshimiwa Rais ambalo natamani sana lifanyiwe kazi ni suala la pensheni kwa wazee. Mheshimiwa Rais akiwa jukwaani aliahidi wazee wote ambao hata kama siyo wafanyakazi, wafugaji, wakulima, anapotimiza miaka 60
watapewa pensheni ya kila mwezi. Naomba sana hilo suala lifuatiliwe na lianze kutekelezwa. Japo nimeangalia katika bajeti sioni utaratibu wowote ambao umesababisha hili suala liweze kuwa la kutekelezeka. Naomba sana Serikali iliangalie hili suala ili tusipate shida sana na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la TASAF. Mpaka sasa hivi, katika Wilaya yangu ya Kibondo kiujumla bado naona lina utata mkubwa sana. Ni kweli kwamba kuna baadhi ya watu walipewa hizo fedha, lakini hawakuwa wanastahili; nashukuru kwamba kuna baadhi
wameondolewa; lakini utekelezaji wa suala hilo umewagusa hata wale ambao walikuwa wanahusika katika kupewa hiyo pesa ya TASAF. Wameondolewa bila utaratibu maalum. Sijajua utaratibu uliotumika kuwaondoa baadhi ya watu ambao wanastahili kabisa kuwemo katika utaratibu wa TASAF. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, Serikali iangalie tena upya wale ambao wanastahili kuwemo kwenye utaratibu wa kulipwa na TASAF, waendelee kulipwa bila kubaguliwa na wale ambao hawastahili waondolewe kweli. Natamani sana watumike viongozi wa Serikali za Vijiji, lakini
huu utaratibu naona TASAF kwenye Ofisi za Wilaya kule wanaamua wenyewe wanavyotaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kidogo kuhusu suala la usambazaji umeme kwenye taasisi za umma. Tunashukuru sana Serikali kwamba imekuja na REA awamu ya tatu, tunaamini watasambaza umeme katika vijiji vyote. Utaratibu wa REA, wanapitia kwenye barabara kuu na kwamba watakwenda kushoto na kulia kilometa isiyozidi moja na nusu kusambaza umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muktadha huo, umeme unapita karibu na shule au zahanati, sijaona kama Wilaya zile ambazo kipato chake ni kidogo, zimesaidiwaje kuhakikisha kwamba shule za sekondari, msingi na zahanati zinaingiziwa umeme kwenye Taasisi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali ihakikishe kwamba shule za sekondari hasa zile za kata zinaingiziwa umeme ili kutupunguzia mzigo sisi Wawakilishi kwa kuwa tunadaiwa kila tunapokwenda, tuingize umeme na kufanya wiring moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna upungufu wa Walimu katika sekondari zetu; hilo najua limeshapigiwa kelele sana na Waheshimiwa Wabunge, naamini Serikali italifanyia kazi, mimi nitaongelea sana kuhusu suala la wahudumu wa afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna changamoto kubwa sana. Nalipigia sana kelele hili kwa sababu katika Wilaya ya Kibondo kuna ongezeko la watu zaidi ya 200,000 ambao tunalazimika kuwahudumia katika suala la…
NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.