Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda huu nami niweze kuchangia hotuba ya Mawaziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais; Waziri wa Nchi wa TAMISEMI na Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi yake nzuri anayoifanya katika kutekeleza wajibu wake na katika kuendesha nchi yetu ili wananchi tuweze kuwa na amani na tuweze kukuza uchumi wetu. Sisi Wanyamwezi tunapenda sana kupongeza jambo kwa kushangaa na maneno yetu ya kushangaa ni mawili tu, yaani ‘ish!’ na ‘jamani!’
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ametushangaza sana na tunamwona wa ajabu. Kwa mfano, Mheshimiwa Rais kanunua ndege mbili, sisi tukashangaa, ish! Pia, Mheshimiwa Rais amegundua wafanyakazi hewa wengi, tukasema, jamani! Mara tumesikia Mheshimiwa Rais huyu huyu anajenga reli ya standard gauge, tukasema, ish! Kapata wapi hela? Hatujakaa vizuri, Mheshimiwa Rais huyu huyu akasema tunahamia Dodoma, jamani! Wote tuko Dodoma!
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa UKAWA kule wamekosa maneno mazuri ya kumpongeza, lakini na wao pia wanashangaa. Wanamshangaa kwa mazuri anayoyafanya katika kutekeleza majukumu, wanabaki kusema Rais wa ajabu, kama ambavyo sisi tunasema Rais
wa ajabu kwa mambo mazuri anayoyafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko fujo zinazolalamikiwa na dawa hiyo ya kulalamikiwa fujo hizo, mimi niliileta katika Mkutano wetu wa Pili wa Bunge hili la Kumi na Moja. Nilileta kwa Mheshimiwa Spika Muswada wa Sheria wa Sekta ya Ulinzi Binafsi. Sheria ile ingeweza sana kutibu mambo ambayo tunayaona sasa. Vikundi mbalimbali vinavyojitokeza sasa ni kwa sababu hakuna sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alete sheria hiyo haraka ili tuweze kudhibiti vikundi ambavyo vinafanya fujo kwa wananchi, vinapiga na kukaba watu. Serikali na Waziri wa Mambo ya Ndani, kama nilivyosema, ni budi alete sheria hiyo ili tuweze kudhibiti matukio ambayo yanatokea sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nichagie ukurasa wa 65 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, kuhusu TAMISEMI. Katika DCC ya Wilaya ya Uyui pamoja na Halmashauri na Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC) tuliomba jina la Halmashauri ya Uyui libadilishwe kutoka Tabora District Council liwe Uyui District Council. Jambo hili linachanganya wakati wa maagizo ya kiserikali kutoka Serikali
Kuu, lakini pia tumeshuhudia fedha za Wilaya ya Uyui, Halmashauri ya Uyui, zikienda Manispaa ya Tabora. Kwa hiyo, mikutano yote miwili ya Wilaya pamoja na ya mkoa ilileta maombi kwa Waziri anayehusika na TAMISEMI ya kubadilisha jina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba atakapokuja Mheshimiwa Waziri hapa kujadili kufikia mwisho wa majumuisho yake, asiache kueleza kwa nini Halmashauri ya Uyui isiitwe Halmashauri ya Uyui badala ya Halmashauri ya Tabora? Kwa sababu hatuhitaji bajeti ya hela. Ni maombi yetu sisi wananchi wa Uyui na yeye ni kutoa kibali tu. Kwa hiyo, sidhani kama itakuwa tatizo kwa Mheshimiwa Waziri wa
TAMISEMI kutukubalia ombi letu hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nichangie kwenye Kifungu cha 33 kuhusu uboreshaji wa huduma za afya. Halmashauri ya Uyui na Wilaya nzima ya Uyui haina Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, tunategemea kituo kimoja cha afya ambacho hakifanyi kazi vizuri na hakiwezi kufanya upasuaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Naibu Waziri wa Nishati ambaye amenisaidia kupeleka umeme pale; umeme tunao sasa, lakini hatuwezi kufanya upasuaji kwa sababu ya matatizo makubwa. Hicho ndicho kituo pekee cha afya katika Jimbo langu na katika Wilaya nzima ya Uyui. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aje na msaada wa kusaidia kituo kile na hatimaye kusaidia majengo
yanayojengwa na Halmashauri ambayo yamejengwa kwa hela ya ndani ili tuweze kuyamalizia na tupate Kituo cha Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali, hasa Wizara ya TAMISEMI kuanzisha Mfuko au kuanzisha Kitengo cha Barabara, Uwakala wa Barabara Vijijini. Wilaya yangu ni mpya na Jimbo langu ni jipya, hatuna barabara za ndani kabisa. Tuna barabara ambayo ni lazima utoke barabara kubwa uende mjini, huwezi kwenda katika kijiji kingine. Hakuna barabara! Kwa hiyo, tumefurahi sana kusikia kwamba mwezi wa saba Serikali itaanzisha Wakala wa Barabara Vijijini. Tuna imani kwamba wakala huyu atafanya kazi sawasawa na Wakala wa TANROADS ambaye anafanya kazi nzuri. Wakiiga hivyo, basi Jimboni kwangu kutakuwa na barabara za kutosha ili kusafirisha mazao na kuweza
kuwasiliana. Nina imani kwamba wakala huyu atakuwa ndiye kichocheo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niongelee mambo ya utawala bora. Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais kuhusu mambo ya Utawala Bora, watu wengi, Wabunge wengi humu ndani na wananchi kule nje, wanalalamika sana kuhusu mpango mzuri ulioanzishwa wa TASAF. Kwetu umesaidia sana. Tulipoanza mpango huo ulifanya kazi nzuri sana, lakini baadaye mpango umekuja kuwafuta watu waliokuwa wamepewa hela; wanatakiwa wazirudishe kwa madai kwamba wamekosewa kupewa hizo hela, hawamo tena katika sifa za wanaopokea hela.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili limeleta mgongano mkubwa sana. Wengine wameomba Wabunge tuwasaidie, nasi hatuna hizo hela, lakini pia wananchi hawana hizo hela kuzirudisha tena. Kosa lililofanywa na TASAF lisahahihishwe kwa Maafisa wa TASAF na siyo kusahihisha kwa wazee. Wazee wengine wanaotaka kurudisha hela, kwa kweli, ukimwangalia hivi ni maskini na hawana uwezo kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri mhusika mwenye jukumu hilo atakapokuja kufanya majumuisho yake, aeleze tutafanyaje kuondoa matatizo ya wazee kuwaomba hela ambayo tuliwapa sisi wenyewe?
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono na nakushukuru sana kwa kuniruhusu kuchangia katika Wizara hizi mbili.