Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia hii nafasi nami nipate kuchangia kwenye hii Wizara yetu ya TAMISEMI. Ni Wizara ambayo ni pana, kubwa na inahangaika sana na makundi mengi ya kijamii yaliyoko kijiji, lakini ni Wizara ambayo haina uwezo, yaani kifedha imekuwa hoi, lakini inashughulika na watu moja kwa moja kwenye vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayeongea hapa natokea kwenye vijiji; tena vijiji hasa kule kusikokuwa na barabara, kusikokuwa na maji, wala huduma ya afya, wala kilimo bora wala na kilimo cha umwangiliaji. Ndiyo huko ninakotoka. Kwa hiyo, hata kwenye hivi vitabu wakiandika, wanaenda kuboresha barabara vijijini kwa kuweka zege na nini, mimi nashangaa, wanaboresha wapi? Mijini au vijijini? Kwa hiyo, ni muhimu watakapokuja hapa kuleta majibu ya kila eneo waeleze ni namna gani wataenda kuboresha haya maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kibaya zaidi sasa, huko nilikotoka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, mpaka tunakuja hapa kwenye hili Bunge, ni asilimia 25 tu ya pesa za maendeleo zimepelekwa huko. Sasa nashangaa, tunakuja kupitisha tena, hiyo asilimia 75 mtapeleka lini? Labda mtuambie, kabla hatujamaliza mwaka huu wa fedha mnapeleka lini hizo hela ili tupate maendeleo?
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wamejenga maboma, lakini Serikali haijamalizia. Mnasema mnaboresha OND, lakini wananchi wameshafanya; Serikali mna mpango gani wa kumalizia hayo maeneo ambayo wananchi wameshafanya kazi ya kutosha? Matokeo yake mvua zinakuja zinaharibu majengo, kwa hiyo, nguvu za wananchi zinapotea bure. Sasa ni vema kila bajeti mkija, hapo muwe na majibu ya uhakika mlifanya nini na kila Jimbo mtuambie mmefanya nini? Hiyo jumla jumla wakati wengine tunaumia huko, haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya mipaka katika vijiji ipo. Kwa mfano, Ofisi ya Waziri Mkuu inajua, TAMISEMI mnajua. Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero; Kijiji cha Ngombo kiko Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, lakini mpaka leo Serikali haijaleta majibu Ngombo inaitika wapi? Matokeo yake mnatuachia ugomvi; Malinyi wanagombana na Kilombero. Naomba mnipe majibu, Ngombo iko wapi ili tupate maendeleo kwa wananchi wa Ngombo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sasa vijiji, tangu mwaka 2014 tulivyoingia kwenye uchaguzi wa vijiji, kuna vijiji viwili havijafanya uchaguzi mpaka leo. Kijiji cha Idandu na Kijiji cha Miomboni. Majibu ya Serikali mnasema kwamba eti kule kuna uwekezaji; mimi nashangaa, hivi mahali kwenye uwekezaji ndiyo watu hawachagui uongozi wao? Kwa hiyo, wale watu wanataabika, maendeleo yao hawajui wanafanya nini? Naomba majibu ya Serikali, ni lini mtaruhusu katika vile vijiji watu wafanye uchaguzi? Ni aibu, ni Serikali ambayo inasema ina utawala bora, lakini kule katika vile vijiji kwani wanakaa wanyama? Nataka majibu ya Serikali
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mkoa kuisimamia Halmashauri, sasa nimpe taarifa Waziri wa TAMISEMI kama hajui. Katika Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Kilombero, wananchi wa Wilaya ya Kilombero tumenunua gari la Mkurugenzi, lakini gari hilo nakwambia mpaka sasa ni miezi sita liko kwa Mkuu wa Mkoa. Leo mnasema Mkoa usimamie Halmashauri, utasimamiaje wakati wenyewe ndiyo unakwenda kubembeleza unachukua gari kwenye Halmashauri? Hawa watu wataweza wapi kuisimamia Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini msiboreshe? Kama kweli ninyi ni waungwana, kwa nini mnaishia kununua ndege, hamboreshi Ofisi za Wakuu wa Mikoa ili waende wakasimamie hizo Halmashauri? Matokeo yake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro hana gari, amechukua gari la Kilombero, moyo unaniuma na wananchi wa Kilombero tumenunua lile gari kwa pesa zetu? Pelekeni gari la Mkuu wa Mkoa pale Morogoro ili gari letu lirudi Kilombero likafanye kazi. Miundombinu yetu ni mibovu, tunahitaji gari, acheni ubabaishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo namwambia hivi, ajue nataka majibu ya Serikali apige simu kule atajua mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya awali.
Usicheke hayo ndiyo mambo, mnatuumiza sana ninyi, haki ya Mungu! Yapo maneno mengi kwenye vitabu, lakini utekelezaji huko chini hamna.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya awali na msingi; sawa mnasema elimu bure, lakini nendeni field mkaone. Haki ya Mungu, watoto 400 wa chekechea na darasa la kwanza wapo nje, Walimu hakuna. Hii nini? Kwa nini hamwajiri Walimu? Tatizo liko wapi? Leo nimeona kwenye vyombo vya habari eti Mheshimiwa Rais, wale Madaktari wa Kenya Wamekataliwa, ninyi ndiyo mnasema mnaajiri. Ninyi mna matatizo gani? Kwani ninyi hamna mpango wa kuajiri mpaka wakataliwe Kenya ndiyo mwajiri?
Mheshimiwa Naibu Spika, leo mnasema mnapeleka Walimu wa Sayansi katika shule zetu, lakini mkae mkijua, Walimu wengi hata wa masomo ya kawaida, wamepungua katika maeneo ya Vijijini, labda wamejaa Mjini. Tunataka ajira kwa Walimu, tunataka ajiwa kwa Madaktari, tunataka ajira kwa Manesi. Mtahakiki mpaka lini? Hii ni Serikali ya kuhakiki! Haiwezekani! Leteni ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, uendeshaji wa Miji na Vijiji. Nilimwomba Mheshimiwa Jafo, hebu tembelea Jimbo la Mlimba. Kwa nini hamtembelei? Ninyi mkifika Ifakara, ndiyo mnaona mmefika Wilaya ya Kilombelo, lakini mjue kuna kilometa 265 kutoka ifakara mpaka kufikia Jimbo la Mlimba. Kwa nini hamji? Mnaogopa nini? Mnaogopa barabara kwa sababu mbaya! Njooni, tena vizuri mje wakati wa masika mwone kama hamkulala njiani siku tano na magari yenu hayo. Fikeni kule, nendeni mkahudumie wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mlimba lina miji kama sikosei miwili au mitatu. Mlimba yenyewe, Ngeta na Chita, lakini mpaka leo hakuna mwendelezo, hakuna upimaji watu wako hovyo hovyo, hamtusaidii. Yaani Mlimba inastahili kuwa Halmashauri, Kilombelo na Ulanga na Malinyi inastahili kuwa na Mkoa, lakini leo mnatuchakaza. Sisi watoto wa wakulima hamtupi mkoa, hamtupi halmashauri, hamtupi miji, mna matatizo gani? Tunahitaji Halmashauri ya Mji wa Mlimba, tunahitaji Mkoa wa Morogoro ugawanywe mara mbili uwe Mkoa wa Kilombero. Tumeshateseka sana, sasa tunasema basi.
Mheshimiwa Naibu Spika, utawala bora uko wapi? Mkuu wa Mkoa kuteremka kwenye Kijiji, kuna mkutano mkubwa wa wananchi kutoka Kata mbalimbali, halafu anatangaza: “nimevunja Serikali ya Kijiji.” Huo ndiyo utawala bora? Wapeni Semina Elekezi, wanaenda kutuvuruga vijijini.
Hiyo imetokea kwenye Kijiji cha Ikule; Kata ya Mngeta Mkuu wa Mkoa alienda akiwepo na Mheshimiwa Waziri Mwinyi huyu hapa. Hivi alivyofanya vile Mkuu wa Mkoa pale ni sahihi; kwenda kuvunja Serikali ya Kijiji kwenye Mkutano wa wananchi Kata yote? Ni aibu! Waambie, wapeni elimu; wanatutesa wananchi. Wapeni Semina Elekezi, kuna umuhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi, kwenye hiyo hotuba ya Kambi ya Upinzani naiunga mkono. Huyu Mheshimiwa Mama Mollel waliyempiga hapa, alistaafu kazi miaka mitatu iliyopita, mtu asiyekuwa na takwimu, yaani usipofanya utafiti huna right ya kusema wewe. Leo anampiga Mheshimiwa Mama Mollel, eti amestaafu siku tano; achana na hizo habari wewe! Mengine kuna watu wamekuwekea kiporo, watakuja kumalizana na wewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya vijijini kwetu ni mbaya; mnapoenda kuzuru maeneo na Waziri Mkuu anajuwa, kwenye kile kijiji mnasema kuna uwekezaji wa sukari, lakini mpaka leo wananchi wanahangaika. Vijiji havijafanya uchaguzi. Nendeni sasa mkalete hao wawekezaji, wananchi wapo tayari kuwa wakulima wa nje ili wapate maendeleo yao.
Mheshimiwa Simbachawenye naongea na wewe kila siku; tunahitaji, ingawa unasema sasa hivi huyu jamaa hataki utawala mpya. Sisi tumeshaumia sana watu wa huku; hivi wewe Jimbo moja lina kilometa karibu 300, leo linakwenda ku-report Makao Makuu ya Wilaya kilometa 265, hamwoni kama mnawatesa wananchi wale?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji utawala, tunahitaji Halmashauri ya Mji wa Wilaya ya Mlimba; tunahitaji Miji midogo ikaendelezwe; na hizo bajeti mnazosema, tunahitaji tuzipate; Vituo vya Afya ndiyo usiseme, balaa. Juzi juzi hapa tumepata shilingi milioni 500 kuendeleza Kituo cha
Afya cha Mlimba lakini hakitoshi, kwa sababu Jimbo lina kilometa zisizopungua…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)