Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na neema kwa kutujalia uzima na afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Simbachawene, lakini pia na Naibu wake Mheshimiwa Jafo pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Angellah
Kairuki. Napenda kuwapa moyo mnafanya kazi nzuri, endeleeni na moyo huo huo na kazeni buti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo moja kwa moja nijielekeze kwenye hoja iliyopo mezani nikianza na suala la elimu bure. Napenda kuipongeza Serikali kwa mafanikio makubwa waliyoyapata kwa muda mfupi kwa kutoa elimu bure. Jambo hili limejidhihirisha wazi, kwa mwaka 2017 jumla ya wanafunzi milioni 3.8 wa darasa la awali na la kwanza waliweza kuandikishwa. Uandikishaji huo ni sawa na
ongezeko la wanafunzi 300,000 ambao waliweza kuandikishwa kwa mwaka 2016. Ongezeko hilo limechangiwa na wazazi wengi kuhamasika na Waraka wa Elimu Bure na kupeleka watoto wao shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini elimu bure imekuja na changomoto zake zikiwepo uhaba wa madawati, vyumba vya walimu, vyumba vya madarasa, upungufu wa walimu na matundu ya vyoo. Mfano kwa Mkoa wa Singida kuna upungufu wa madarasa 5,547 na nyumba za walimu 5,580. Idadi hii ni kubwa sana ambapo kwa bajeti zilizotengwa katika Halmashauri zetu haziwezi kukamilisha ujenzi wa miundombinu kwa kukarabati shule zetu zilizoko vijijni na hata zilezilizojengwa chini ya mpango wa MMEM I na MMEM II. Hali ni mbaya na hasa kwa shule zetu zilizopo vijijini ambazo hazimfanyi mwalimu kufundisha kwa utulivu, lakini vile vile hazimfanyi mwanafunzi kupokea kile anachofundishwa na
mwalimu. Bila mazingira bora ya kufundishia hakuna elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa Wilaya ya Ikungi tu pekee, ina uhaba wa shule 568 na upungufu wa walimu 490, vilevile ina uhaba wa vyumba vya madarasa 568. Hivyo, naiomba Serikali yangu sikivu kuangalia mpango mahususi ambao utawezesha ujenzi wa miundombinu hii ya elimu kukamilika, lakini pia kuboresha mazingira ya kufundishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuweza kujenga maabara 5,562, lakini ni ukweli usiopingika, miundombinu ya maabara zetu bado hazijakaa vizuri na hasa maabara zilizopo katika Mkoa wangu wa Singida.
Naishauri Serikali kukamilisha miundombinu hiyo kwa haraka iwezekanavyo ili kuwawezesha wanafunzi hao kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo, lakini pia kwa ukamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda, bila ya kuwandaa wanafunzi wetu kuwa wanasayansi, ni vipi tutayafikia malengo yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuchangia ni suala la watumishi wa umma. Wapo madaktari na wauguzi ambao wanatazama afya za Watanzania, lakini pia wapo walimu ambao pia ndiyo msingi wa maendeleo kwa kwa Taifa letu. Bila elimu bora hakuna maendeleo na bila walimu bora hakuna mambo yatakayoweza kufanyika kwa weledi, ujuzi na ufanisi. Watumishi hawa wamekuwa
wakifanya kazi kubwa na ngumu na bado maslahi na stahiki zao zimekuwa ni ndogo sana ukilinganisha na kazi wanazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuchangia na ninaona siyo zuri pia kwa watumishi, ni watumishi wengi kutokupandishwa madaraja kwa wakati. Jambo hili linawavunja sana moyo watumishi wa umma. Ninatambua kwamba zoezi la uhakiki wa watumishi wa umma limekamilika, hivyo basi ni wakati muafaka wa kuwapa watumishi wetu kile kinachostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la afya. Sera ya Afya ya mwaka 2007 imehitaji kila kijiji kuwa na zahanati moja, lakini katika Wilaya ya Singida ambayo ina kata 21 kuna zahanati 26 tu ambazo hazikidhi mahitaji ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile zahanati zilizopo zina upungufu mkubwa wa vifaa tiba lakini pia na wataalamu. Jambo hili linasababisha msongamano sana katika hospitali zetu za Wilaya, lakini pia vilevile msongamano katika hospitali yetu ya rufaa ya Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali inakuwa ni mbaya zaidi pale mama mjamzito anapohitaji huduma ya afya katika zahanati zetu ambapo hakuna huduma za upasuaji, hakuna theatre, hakuna huduma za damu safi na salama. Unategemea mama mjamzito aende wapi iwapo atakumbwa na kadhia hii ya kwenda kujifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuchangia ucheleweshaji wa fedha za miradi ya maendeleo. Nakubaliana na mfumo wa Serikali kwamba baadhi ya mapato kuingizwa moja kwa moja kwenye mfuko wa Serikali Kuu na naipongeza sana Serikali, lakini mfumo
huu una changamoto zake. Moja ya changamoto ni kusababisha baadhi ya Halmashauri kutokutekeleza majukumu yake kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua hapo awali kabla ya kutumika kwa mfumo huu kulikuwa na mianya mingi ya rushwa na upotezaji wa fedha za umma, lakini kwa sasa hali ya fedha za miradi ya maendeleo zitoke kwa wakati ili kusaidia kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu Madiwani wetu. Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia wamechangia kuhusu Madiwani. Madiwani wanafanya kazi ngumu; wa ndio kiungo kati ya Wabunge na wananchi. Tunapokuwa huku Bungeni kufanya shughuli
zetu, wenyewe wanakuwa karibu na wananchi. Hivyo, naomba Serikali iangalie Madiwani wetu na Wenyeviti wa Vijiji kwa jicho pana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.