Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Kabla sijasema, namshukuru Mungu kwa nafasi hii ambayo amenipa ili niweze kusimama kwenye Bunge hili na kusema machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuwapongeza sana watoa hoja, Waziri wetu wa TAMISEMI pamoja na Waziri wa Utumishi, Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Mheshimiwa Kairuki kwa kuwasilisha bajeti yao vizuri na bajeti ambazo kwa kweli zimebeba mambo mengi sana ambayo tunayaendea kwa mwaka wa fedha unaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tunatofautiana kutazama kitu kimoja, mimi nianze kwa kutoa shukrani kwa Serikali kwa kazi kubwa inayofanyika Bukombe. Wewe ni shahidi, kwa muda mrefu fedha za dawa zilikuwa hazipatikani kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali zetu, leo ninavyosimama hapa Wilaya ya Bukombe tulikuwa na mahitaji ya fedha za dawa kwenye vituo vya afya na zahanati zaidi ya shilingi milioni 600 na tunafurahi kusema kwamba sasa hivi tumeshapata shilingi milioni 512. Hii ni kazi kubwa sana, inahitaji kushukuriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hatukuwa na magari kwa ajili ya wagonjwa, Wilaya yetu ya Bukombe tumepata magari mawili kwa ajili ya wagonjwa yatakayokuwa yanahudumia kwenye Kituo cha Afya cha Uyovu pamoja na cha Ushirombo. Tumepata fedha kwa ajili ya kupanua shule ya msingi Ibamba, shule ambayo imeandikisha watoto wa darasa la kwanza peke yake 1,200. Wasikivu hawa, tulipowafuata
kuwaomba pesa, wametupa pesa shilingi milioni 92 kwa ajili ya kupanua shule hiyo. Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Bukombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shule maalum mbili Wilaya ya Bukombe, shule zenyewe ni shule ya msingi Uyovu pamoja na Ushirombo. Nafurahi kusema kwamba Serikali wametusikiliza, wametupatia fedha kwa ajili ya shule hizi shilingi milioni 100 tumekwisha patiwa kwa ajili ya kuhudumia watoto hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojaribu kuhangaika kuona vijana tunawasaidia vipi kwenye nchi yetu, Wilaya ya Bukombe maombi tuliyopeleka kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, tayari Serikali imetusikia imetupatia, imetupatia shilingi milioni 51 za kuanzia kuwapatia mikopo vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ni lazima tuyaseme, usipoweza kushukuru kwa kidogo, huwezi kushukuru kwa kikubwa hata kama utapatiwa. Naomba kwa moyo wa dhati, niishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya na Mawaziri wake ambao kwa kweli Wabunge wote hapa na wananchi ni mashahidi, tunawaona wanavyohangaika kuona
Tanzania inapata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, niseme machache ambayo sasa yanahitaji kuangaliwa na Serikali ili tuweze kuboresha. Jambo la kwanza, kwenye Wilaya yetu ya Bukombe tumekuwa tukiomba watumishi kwenye Idara ya Afya, hatujapatiwa watumishi wa kutosha na bahati mbaya sana hata hao wachache waliopo, wanapewa uhamisho bila kuletwa watumishi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, Wizara ya TAMISEMI wamehamisha madaktari saba wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe. Nimeuliza hili jambo hapa Bungeni, nimewafuata na ofisini kuwauliza, jamani mnapohamisha madaktari saba kwa mara moja kwenye Wilaya ya Bukombe mnatarajia nini kwa wananchi wetu? Ninaomba kupitia bajeti hii, Waziri wa TAMISEMI utusaidie, madaktari wetu saba wale
mliowahamisha mara moja mnatuletea lini fidia ya madaktari hao? Kwa sababu hali iliyopo kule siyo nzuri, wananchi wanahitaji huduma, lakini watoa huduma ni wachache sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeomba vile vile Hospitali yetu ya Wilaya ya Bukombe ambayo ni Hospitali ya Wilaya ipanuliwe, theatre yake ni ndogo. Ilikuwa ya mwanzo, kwa ajili ya kutumika kwa muda tu, baadaye watajenga theatre nyingine. Nasikitika, toka miaka hiyo ya 1990 haijawahi kupanuliwa. Naomba hili jambo na lenyewe liangaliwe ili wananchi hawa waweze kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madai ya watumishi wa Idara ya Afya, wanadai fedha nyingi, on-call allowance. Wanadai allowance zao hizi hawalipwi, wanadai mishahara yao na malimbikizo yao, tunaomba na hili Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI utakapoanza kuhitimisha hoja yako, utuambie watumishi hawa wanaanza kulipwa lini? Kwa sababu bila hawa, wananchi wetu hawawezi kutibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niongelee suala la elimu na kwenye hili nitaongelea elimu yenyewe lakini nitaongelea walimu. Hakuna muujiza wa kukomboa elimu hii kama hatuwezi kuwaangalia walimu wa Tanzania. Fanya kila unachoweza, unaweza ukawa na darasa lina vigae, masofa na television, lakini kama hakuna mwalimu aliyepewa motisha, kazi inayofanyika pale haiwezi kuleta matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wa Tanzania wana malalamiko yao mengi, tusipoweza kuyapatia majibu kwa awamu hii, dawa ya elimu ya nchi hii hatuwezi kuipata. Walimu 80,000 wa nchi hii wamepandishwa madaraja, hawajarekebishiwa mishahara yao. Leo nakuomba Waziri wa TAMISEMI utusaidie, uwape tumaini walimu wa Tanzania, madaraja yao haya mnaanza kuyarekebisha lini na kuwalipa mishahara yao?
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo walimu ambao wamepandishwa madaraja, baada ya kuwa wamepandishwa madaraja, wameonja mshahara mpya, mmewarudisha nyuma kwa sababu ya uhakiki. Mheshimiwa Waziri tunakuomba utuondoe kwenye kitendawili hiki. Wale waliopanda madaraja, wapatiwe mishahara yao ili waweze kiushi sawa sawa na jinsi ambavyo walikuwa wanatarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri
hili aliangalie. Wakati mwingine unaweza usiwe na fedha, lakini lugha nzuri kwa watu inaweza kuwapa
motisha wa kufanya kazi. Wapo watendaji wa Serikali na nichukue nafasi hii kumshukuru sana na
kumpongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, nilimuona kwenye television, anawatia moyo
walimu wa Tanzania. Wapo watu wengine wanafunzi wakifeli, analaumiwa Mwalimu Mkuu, unamvua madaraka
Mwalimu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya mwanafunzi kufeli siyo kama kufyatua tofali kwamba utaweka udongo kwenye kibao cha tofali, tofali litatoka, haiwezekani! Nataka nikwambie unaweza kumlazimisha mwalimu kuhudhuria kazini, huwezi kumlazimisha mwalimu kufundisha. Suala la kufundisha ni suala la mapenzi. Walimu wakati sisi tupo nyumbani tunaangalia television, wao wamejifungia kwenye vyumba vyao wanajiandaa kwa ajili ya watoto wetu kesho yake. Walimu hawa hawana mishahara mikubwa, wanajinyima fedha zao waweze kuchukua fedha hizo wakanunue vifaa vya kufundisha na maandalizi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapowavunja moyo kwa kuwaambia maneno ya kejeli, ninaomba Mheshimiwa Waziri unaposimama, ulikemee jambo hili walimu wa Tanzania wasikie. Walimu hawa wanahitaji kuthaminiwa, kuheshimiwa, unamvua Mwalimu Mkuu madaraka kwa sababu ya kufeli mwanafunzi, mwalimu pekee sio sababu ya mwanafunzi kufeli, zipo sababu nyingi zinazosababisha mwanafunzi kufeli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kwanza inaweza kuwa mzazi, sabab ya pili inaweza kuwa mazingira ya kazi na ya tatu inaweza kuwa mwanafunzi mwenyewe na sababu nyingine anaweza kuwa mwalimu. Unachukua sababu moja ya mwalimu peke yake, unamvua madaraka!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya walimu wa Tanzania na kwa niaba ya walimu wa Bukombe naomba nipaze sauti yao, tabia hii iachwe ya baadhi ya watu, wanaichafua na wanaigombanisha Serikali na walimu wa Tanzania, hatuwezi kukubali kama Bunge tukaona walimu ambao sisi wametufikisha hapa wanaendelea kudharauliwa na kuonewa kwa maneno ya kutungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Utumishi ukemee hili kwa sauti kubwa, watendaji kule chini wasikie na mimi nafahamu wewe Mheshimiwa wa Utumishi unafahamu ni watu gani wamefanya haya. Walimu wa Tanzania hatuwezi tukakubali wakaendelea kuonewa kwa kiwango hiki.
Tuwasaidie walimu kwa kuwapatia vifaa vya kufanyia kazi kwa kuwapatia fedha za kutosha, zile stahiki zao kama kupanda madaraja yao walipwe kwa wakati, mambo ya kuwapiga danadana inatosha, sasa hivi nao wanahitaji wapate chao mkononi na wafanye kazi kwa kujituma zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Mfuko wa Barabara. Wilaya yetu ya Bukombe upande wa Kusini tunapakana na milima, maeneo ya Imalamagigo, Mchangani na Nifa, maeneo yote haya tumeomba fedha kwa ajili ya Mfuko wa Barabara turekebishe barabara hizo hatuwaji kupata hata shilingi moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda TAMISEMI mara kadhaa kuwaomba ndugu zangu watusaidie, watu wanateseka, wanafunzi wanashindwa kwenda...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.