Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii niweze kuchangia hoja ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utawala Bora.
Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kusimama ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili naomba nichukue nafasi kuwapa pole wananchi wenzangu wa Wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji kutokana na matukio yaliyojitokeza, lakini niliona nilisemee hapa kwa sababu tukio la mauaji linaloendelea Wilayani Kibiti na Rufiji kwa kiasi kikubwa limeathiri uendeshaji wa Halmashauri za Kibiti na Rufiji na naiomba Ofisi ya Rais, TAMISEMI waiangalie kwa jicho la huruma Halmashauri mpya ya Kibiti, wameshindwa kukusanya mapato kwa sababu katika maeneo ambayo mauaji hayo yanajitokeza mara kwa mara eneo la Bungu na Jaribu Mpakani ni eneo ambalo lina vyanzo vingi vya mapato na linalochangia mapato kwa kiwango kikubwa.
Kwa hiyo, naomba Serikali itambue Halmashauri ile ni mpya, inahitaji pesa ya uendeshaji wa Halmashauri na ina maeneo maalum ya ukanda wa delta. Kwa hiyo, naomba sana Waziri aitazame Halmashauri ile kwani kwa sasa hata malipo ya posho za Madiwani zitakuwa ngumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa pia wanaopata madhila hayo ni baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji, naomba pia Mheshimiwa Waziri aangalie namna gani viongozi wa maeneo yale watakavyokuwa wanawajibika. Hapa hapa niwasemee viongozi hawa wa vijiji na vitongoji pamoja na Waheshimiwa Madiwani ambao ni wasimamizi wa shughuli mbalimbali za maendeleo kuwaongezea posho. Kwa mfano, Wenyeviti wa Vijiji hawana posho yoyote. Pia naipongeza Halmashauri yangu ya Chalinze kwa uamuzi wa kuwapa Wenyeviti wetu wa Vijiji shilingi 30,000 kila mwezi kwa ajili ya kuwawezesha kufanya shughuli mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii pia ni Ofisi ya Rais, naomba nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na kwa Mkoa wa Pwani tunaishukuru ziara yake aliyoifanya mwezi wa Tatu. Ziara ile ilionesha azma yake ya ujenzi wa viwanda nchini kutimia ndani ya Mkoa wa Pwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mazingira mazuri, tunavyo takribani 82 vinavyoendelea kujengwa kikiwemo kiwanda cha tiles ambacho kimekamilika Mkuranga, lakini kuna kiwanda cha tiles kinaendelea Chalinze, lakini pia kuna kiwanda cha usindikaji matunda Msoga, Chalinze. Kwa hiyo, hii inaonesha bado wawekezaji wana imani na Serikali hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwamba anaendelea kukubalika na Jumuiya ya Ulaya imeshatoa msaada, imeahidi kuendelea kuisaidia nchi yetu dola milioni 205, ameshasaini. Pia Benki ya Dunia inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya ujenzi wa flyover Dar es Salaam, kuendelea kwa ujenzi wa mradi wa mwendokasi Dar es Salaam, yote hayo yanaonesha namna gani Mheshimiwa Rais wetu anaaminika na Benki ya Dunia, African Development Bank na wadau mbalimbali wa maendeleo. Tuendelee kumuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye suala la elimu bure. Naipongeza sana Serikali, jambo hili siyo jepesi. Kwa bajeti ya mwaka huu, zaidi ya shilingi bilioni 201 zimetengwa kwa ajili ya elimu bila malipo. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa kutoa ufafanuzi mzuri namna ya kutofautisha elimu bure na elimu bila malipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo baadhi ya wananchi wengi tu katika maeneo mbalimbali wameanza kulitekeleza hilo la kutoa michango yao. Hapa naipongeza Halmashauri ya Bagamoyo na Chalinze, Kibiti, Mkuranga, Mafia, Kisarawe kwa wananchi mbalimbali, tumeanza ujenzi wa miundombinu ya elimu ili kuchangia jitihada za Serikali. Kwenye Halmashauri ya Chalinze ninayohudumu tumetenga shilingi milioni 400 ya ujenzi wa miundombinu kwa mapato ya ndani kwa elimu ya msingi, shilingi milioni 400 ujenzi wa miundombinu kwa mapato ya ndani kwa elimu ya sekondari. Hii inaonesha namna gani sisi wawakilishi wa wananchi; Madiwani na Wabunge tunavyoona umuhimu wa kuisaidia Serikali katika suala zima la elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo naiomba Serikali kwenye suala hili la elimu bure, ukiangalia namna ambavyo hizi fedha zimetengwa kwa uhalisia, uwiano wa wanafunzi katika Halmashauri zetu, uwiano wa walimu na uwiano wa uhaba wa mindombinu; hapa naomba Mheshimiwa Waziri aangalie ile randama kwenye Halmashauri zetu za Mkoa wa Pwani. Kwa mfano, Halmashauri ya Chalinze na Mkuranga inaongoza kwa idadi ya wanafunzi, inaongoza kwa idadi ya walimu, inaongoza na kwa idadi ya uhaba wa miundombinu, kwa hiyo, nadhani katika ule mchanganuo haujakaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta Halmashauri nyingine idadi yao ni ndogo na hapa nia ni kufanikisha; kwa hiyo, naomba nimletee Mheshimiwa Waziri ile taarifa yetu kamili ya kuonesha namna gani ule mgawanyo ulivyo ili waweze kurekebisha. Ukizingatia hasa Halmashauri ya Mkuranga kwa kweli uhamiaji ulikuwa mkubwa na wanafunzi ni wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo pia naipongeza Serikali hususan Wizara hii ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya kwa namna ambavyo wameanza mgao wa vifaa tiba kwenye hospitali zetu. Hivi karibuni tumeona Serikali imenunua vifaa tiba vya thamani ya takribani shilingi 2,900,000,000 ambapo kila Halmashauri itapata vitanda 20, vitanda vitano vya kuzalishia, magodoro 25 na mashuka 50. Kwa kweli hii ni hatua nzuri katika kuboresha huduma za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwenye ukurasa wa 34 wa hotuba ya Waziri wa TAMISEMI, ameonesha ni namna gani Serikali kwa kushirikiana na hizi Wizara mbili itakavyokarabati vituo vya afya 100 ili kuboresha mazingira ya upasuaji kwa ajili ya afya za akina mama. Mpango huu utagharimu shilingi bilioni 63. Naipongeza sana Serikali.
Kwa hapa nizisemee Halmashauri zetu mpya Kibiti na Chalinze; Halmashauri hizi hazina Hospitali za Wilaya, lakini kwa Chalinze bahati nzuri Mheshimiwa Rais wetu Mstaafu wa Awamu ya Nne amejitahidi tumepata majengo kwa Kata ya Msoga, lakini changamoto kubwa ni uhaba wa watumishi. Hatujapatiwa watumishi kwenye hospitali yetu ile ya Wilaya na majengo yamekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata Basket Fund tumepata takriban shilingi milioni 488, lakini mpaka sasa kiasi cha shilingi bilioni 105 kinashindwa kutumika kwa kuwa hakuna hospitali yenye hadhi katika Halmashauri ya Wilaya wakati tunayo tayari na majengo tayari pia yamekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikisemee Kituo cha Afya cha Chalinze. Kituo hiki kinapokea majeruhi wengi, naomba sana Serikali ijitahidi kutuboreshea wodi ya upasuaji, maana hakuna wodi hiyo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima la uwezeshaji wa wananchi, naipongeza sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba Mkoa wangu wa Pwani umepokea shilingi milioni 104 kwenye Mfuko wa Vijana, lakini sambamba na hilo, Mkoa wetu wa Pwani umetoa takribani shilingi milioni 477 ambayo ni asilimia 10 ya mapato yake ya ndani. Hapo naomba nishauri; kwa kuwa marejesho ya mfuko huu hayaonekani wazi wazi kwa kuwa hakuna akaunti maalum, naomba Serikali sasa ione namna ya kuanzisha akaunti maalum kwa ajili ya marejesho tu ya mikopo hii ya asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwa kuwa fedha zinazotengwa ni nyingi, Serikali ione uwezekano wa kuanzisha benki za wananchi katika mikoa yetu. Kwa mfano, mwaka huu tulitenga shilingi 1,800,000,000; mwakani tumetenga shilingi 2,400,000,000; hizi zinatosha kabisa kuanzisha benki za wananchi katika mikoa ili kurahisisha na wakati huo sheria itakuwa imerekebishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nadhani pia ile mikopo ya shilingi milioni 50, sijasikia neno kutoka kwa Waziri wa TAMISEMI, lakini nadhani Wizara yake ndiyo itakuwa inaratibu, inaweza pia ikaongeza nguvu katika mikopo hii ya asilimia 10 kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwasemee walimu pia. Nampongeza sana Mheshimiwa Biteko na Waheshimiwa wote waliosemea hili, lakini hapo niseme tatizo lililopo sasa hivi la uhamisho. Walimu wengi wamepata watu wa kubadilishana nao, lakini vikwazo mbalimbali vinatokea na sekta hii kwa kweli na watumishi wengi wanakwama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nampongeza Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa namna alivyosimamia zoezi hili la uhakiki wa wafanyakazi, uhakiki wa vyeti fake, lakini ifike wakati sasa zile haki za kimsingi, hata zile ambazo hazihusiani na masuala ya malipo, walimu wenyewe wameomba kuhama kwa hiari yao, wamepata wa kubadilishana nao, basi TAMISEMI itoe hiyo orodha ili walimu wetu na kikwazo kingine masuala ya ndoa yaweze kufanyika vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.