Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilipata mtihani mkubwa sana wa kukuamini kama ni mtemi au siyo. Lakini ulilolifanya Mheshimiwa ndani ya Bunge lako hili kama Mwenyekiti umeonyesha kweli wewe ni mtemi. Fujo iliyotokea hapa hakuhitaji busara, ilihitaji nguvu na uwezo mkubwa sana nakushukuru sana na pole sana. (Makofi)
Mwishoni katika shukrani zangu nimshukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutusaidia chakula cha njaa. Tulipata matatizo sana sisi mwaka huu na nilipokwenda kuwaona nashukuru sana tulipata msaada huo, haukutosha lakini si haba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo chache naomba sasa nijadili hotuba ya Mheshimiwa Rais kuanzia ukurasa wa 16 mpaka 22. Mheshimiwa Rais ameongelea kuwaanda vijana kielimu, na mimi ningependa tukazanie hasa shule za ufundi (Technical Schools) na VETA.
Mimi ni zao la shule ya ufundi ya Moshi Technical na nipokwenda kuitembelea mwaka huu nikataka kulia. Shule hizi zimetoa watu wenye uwezo mkubwa sana, ma-engineer wengi waliopo sasa na wataalam wengi walipita katika vyuo hivi na shule hizi za ufundi lakini sasa hali yake imekuwa mbaya sana. Ningeomba Mheshimiwa Rais aelewe kwamba tunamuunga mkono sana katika hotuba hii, lakini vilevile ajue kwamba kuna vitu vya kufanya na shule za ufundi zipewe umuhimu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa unaofuata, Mheshimiwa Rais ameongelea kuwaandaa pia vijana kimtaji, akaongelea SACCOS vikundi vya kiuchumi vidogo vidogo lakini vyenye uwezo wa kuwezeshwa na mimi namuunga mkono kwa sababu mimi mpaka sasa ni Trustee wa NSSF kutokana na madaraka niliyonayo katika Chama cha Waajiri.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshaachia lakini naongelea nilivyokuwa kwamba ni muhimu sana Mheshimiwa Rais aungwe mkono na mifuko hii yote ya hifadhi ya jamii iweze kuwasaidia hawa vijana ambao Mheshimiwa Rais ametaka kuwasaidia kwa mpango ambao mifuko hii inao na ningependa tu kuitaja ni NSSF, PPF, PSPF na LAPF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais ameongelea katika hotuba yake gap linaloonekana sasa kati ya walionacho na wasionacho, maskini na wenye nacho. Wako watu ni kweli wametoka shuleni juzi au wamefanya mchezo fulani kwa kuacha kulipa kodi au kwa njia nyingine ya udanganyifu wamekuwa matajiri sana, kwa kufanya hivyo wamefanya watu wengine wawe maskini sana. Mheshimiwa Rais limemuuma sana hilo. Kwa hiyo, anafanya kazi kubwa ya kukusanya hela na kuzipeleka Hazina ili sasa aweze kuzigawa kwa wananchi wote. Suala hili mimi naliunga mkono na ninaomba watu wote tumpongeze Mheshimiwa Rais katika suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira katika ukurasa wa 16 Mheshimiwa Rais ameongelea kukuza ajira nchini ili vijana wenye uwezo wa kuajirika na uwezo wa kufanya kazi waweze kufanya kazi na hapa alikuwa anailenga sekta binafsi. Narudia tena sekta binafsi ndiyo engine au mhimili mkubwa sana wa kutoa ajira hapa nchini. (Makofi)
Lakini nao pia wamekuwa na malalamiko ya hapa na pale kwamba ziko tozo nyingi sana ambazo si za lazima ambazo pia Mheshimiwa Rais ameziongelea ziondolewe katika sheria ya 21 alizizozitaja kwamba kero kwa wananchi. Tozo moja kubwa iliongelewa leo asubuhi hapa ya Pay As You Earn, lakini pia ningependa kuitaja kero moja ya SDL. Sasa hivi Tanzania inafanya tozo la asilimia tano ambalo ni kubwa sana duniani, katika nchi zinazozunguka zote tozo kubwa kabisa katika nchi za jirani hapa ni asilimia 1.2. Sisi waajiri wanatozwa kila kichwa cha mwajiriwa asilimia tano, hicho ni kiasi kikubwa sana na imefanya tusiwe competitive katika nchi jirani tunapoajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Rais katika hotuba yake amegusa mambo ya maji, na Kanuni zinanikataza kurudia mambo yaliyoongelewa lakini ningependa kuchangia kidogo tu kwamba ule mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kupitia Shinyanga na Kahama unapita Makao Makuu ya Wilaya ya Uyui pale Isikizya ambako wafanyakazi wameshindwa kuhamia kwa sababu hakuna maji. Lakini vilevile mradi huu utagawa maji kilomita sita kushoto na kulia kwa barabara, tungependa mradi huu upanuliwe kuenda kilomita 25 ili kupeleka maji kwenye kituo cha afya cha Uyui Jimbo la Tabora Kaskazini na kituo kimoja tu cha afya Uyui na ambacho akifanyi kazi kwa sababu hakuna umeme na hakuna maji. (Makofi)
Katika suala hilo pia itasaidia kupeleka maji katika zahanati ya Ikongolo pale, kijiji cha Majengo na Kijiji cha Kanyenye. Vilevile umeme limekuwa tatizo kubwa sana katika Jimbo langu la Uyui mimi ningeomba wapiga kura wangu walionichagua walikuwa wanajua kwamba najuana na Mawaziri wengi na ni kweli hakuna Waziri humu ndani ambaye hanijui, tunajuana sana lakini hatupeani kazi kwa kujuana tunapeana kazi kwa mahitaji. Naomba Mheshimiwa Profesa Muhongo aangalie sana kupeleka umeme katika hiyo zahanati na kituo pekee cha afya pale Upuge.
Mwisho, ili niwaachie wenzangu waongee wananchi wa Uyui wanapata taabu sana na ikumbukwe kwamba Uyui ndiyo mkulima wa tatu wa tumbaku, lakini bahati mbaya sana tumbuka na sheria ile ya ushirika, ndiyo maana asubuhi nilitaka kuchangia hapa bahati mbaya sikupata nafasi. Ile Sheria ya Ushirika imetoa fursa kwa watu fulani kuwaibia wanyonge inaumiza sana, kwamba mkulima anayelima tumbaku analazimika akauze kwenye Chama cha Ushirika ambacho hakikopesheki na kama kinakopesheka kina madeni makubwa, anakatwa hela ambazo hajakopa. Mwaka jana amekatwa na mwaka huu amekatwa au wengine wamepeleka tumbaku hawalipwi chochote kwa sababu sasa wanadaiwa tumbaku ya miaka mitatu iliyopita kama vile hawana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linaumiza sana na wananchi wamekata tamaa kabisa, nafurahi nafurahi Waziri wa Kilimo anakutana na sisi kesho, mimi nimeandika paper ambayo inaeleza matatizo yote na itakuwa jambo la kuongelea kwenye mkutano wa kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala dogo sana lililobakia naomba Serikali ifanye juhudi kubwa kutambua au kutumbua majibu katika Vyama vya Ushirika ili vyama hivi viweze kuwatambua wafanyakazi wabaya ili wananchi waweze kuuza tumbaku na waweze kulipwa tumbaku imetusomesha sisi lakini sasa leo tumbaku imetia umaskini wazee wangu wote katika vijiji vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru niwaachie wenzangu waongee. ahsante sana. (Makofi)