Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Ahmed Juma Ngwali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ziwani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Kwanza nianze kwa kumpongeza Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa hotuba yake ambayo pamoja na mambo mengine neno Ngariba lilizua taharuki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hoja yangu kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nyuma huku kwenye Katiba katika orodha ya Mambo ya Muungano orodha ya kwanza, Kifungu Na. 15 kinachohusu mafuta na gesi, ambacho hivi karibuni mwaka 2015, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria tatu, Sheria ya Petroleum, Sheria ya Mafuta na Gesi ya Revenue na Sheria ya Ustawi wa Mafuta na Gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo linanisikitisha sana dhamira na lengo ya sheria hizi tatu ilikuwa ni kwamba, zinapitishwa sheria, baada ya kupitishwa sheria tunapitisha Katiba mpya, baada ya kupitishwa Katiba mpya, mafuta yanaondolewa katika Mambo ya Muungano. Jambo la kusikitisha ni kwamba, sheria zinaendelea kufanya kazi, kila mmoja kwa upande wake, lakini bado Katiba inatambua kwamba mafuta na gesi ni mambo ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni la ajabu sana, Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa mara ya kwanza kabisa na kwa ajabu kabisa, katika Sheria ya Oil and Gas Revenue Management Act ya mwaka 2015, Kifungu Na. 2 (2) kimetoa mamlaka kwa Baraza la Wawakilishi kutunga sheria, zinazohusiana na mambo ya revenue za mafuta na gesi. Jambo ambalo tunajiuliza Bunge la Jamhuri ya Muungano linapata wapi mamlaka ya kuitungia sheria, maana yake kuliagiza Baraza la Wawakilishi litunge sheria. Maana yake ni kwamba unafanya Baraza la Wawakilishi wanatunga sheria kwenye Mambo ya Muungano, jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 64 (3). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chukua Katiba uangalie, kwa hivyo sasa jambo hili limetutia mashaka sana na Baraza la Wawakilishi tayari wameshatunga Sheria ya Oil and Gas ya mwaka 2016, sheria Na 6, Sheria ambayo inafanana kabisa copy and paste na sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hivyo, Legislature mbili zina sheria mbili za oil and gas. Jambo ambalo ukisoma Katiba Ibara ya 63 ile sheria ya Zanzibar inakuwa batili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyofahamu mimi na wanaojua sheria na watu wengine, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, linatunga sheria kutokana na Katiba ya Zanzibar, kwa hivyo, kuiamuru maana yake hata ungeiamuru kwa mfano, sheria ile madhali imepewa amri na sheria nyingine ile sheria itakuwa ndogo haiwezi kuwa sheria sawa na hii. Kwa hivyo, jambo hili linaleta utata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hata ukizitazama hizo sheria zenyewe lengo lilikuwa ni kuyaondoa mafuta katika Muungano, lakini sheria zile ukiziangalia zote zinasema sheria hizi zitatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, sasa unajiuliza ikiwa lengo kuyaondoa mafuta katika Muungano mbona hizi sheria bado ni za kimuungano,. Hilo ndilo jambo ambalo ni la kujiuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la kushangaza Katiba mpya ambayo ilikusudia kuja kuondoa hayo mambo ya mafuta na gesi katika Mambo ya Muungano haipo. Ukitizama Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020, nimeipitia ukurasa kwa ukurasa, hakuna mahali popote panapozungumzia kutakuwa na Katiba mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna mahali popote ambapo kaahidi kuleta Katiba, ukifuatilia maneno yake, maneno yake yalisema kabisa kwamba Katiba siyo ajenda yake, lakini jambo la mwisho hata ukitazama fedha zilizotengwa kwenye bajeti hakuna fedha kwa ajili ya Katiba mpya. Kwa maana hiyo, Katiba mpya haipo. Kwa hivyo, zile sheria kuendelea kufanya kazi pande tofauti ni makosa, ni kuvunja Katiba na ninyi watu mnaohusika na Muungano mpo, Mawaziri mpo, Mwanasheria Mkuu upo! Pia unatunga sheria za Muungano mambo ya mipaka baharini huweki, sasa mafuta ambayo yatagundulika baharini itakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupendekeza kwamba, kwa sababu pesa hamna za kuanzisha Katiba mpya, leteni Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tutumie kipengele Namba 98(1)(b) tuondoe mambo ya mafuta katika mambo ya Muungano. Itakuwa kazi rahisi sana, tutapiga kura tu third majority kwa kila upande kwa Muungano, tutaliondoa jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nilisemee ni suala zima linalohusu fedha za misaada, nakusudia kusema GBS pia na nizungumzie suala zima linalohusu Pay As You Earn na mambo mengine. Fedha hizi za Pay As You Earn zimekuwa ni tatizo kubwa sana, haziendi kwa wakati unaotakiwa Zanzibar, kwa hivyo Zanzibar inapata shida sana kwenye fedha hizi. Tunawaomba fedha hizi zifike kwa wakati unaotakiwa ili Zanzibar ipate kufanya shughuli zake.
Pili; fedha ambazo zinatoka katika Institution za Muungano ambazo zina-genarate fund, hizi fedha haziendi kabisa, tunaomba Serikali ya Muungano kwamba fedha hizi mzipeleke kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Wizara ya Fedha, miradi ambayo imeiva Zanzibar ni miradi ya International kama UN na mambo mengine na misaada mbalimbali inayotoka nje za nchi. Mnapopelekewa miradi ile iliyoiva Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha anachelewesha sijui kwa makusudi tuseme ama vipi, lakini ile miradi inakaa mpaka inafika wakati sasa hata gharama hiyo ya miradi yenyewe inakuwa imekwenda sana. Kwa hivyo tuiombe Serikali jambo hili pia nalo mlifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la fedha za Mfuko wa Jimbo; fedha za Mfuko wa Jimbo zinazokwenda Zanzibar hazijawahi kukaguliwa, nasema tena hapa kwamba hazijawahi kukaguliwa kwa miaka saba, hii ni kutoka na sheria. Ndiyo maana Jaji Warioba alipokuja na Tume yake akasema, tuna sababu ya kuwa na Serikali tatu, kwa sababu sheria haimruhusu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano kukagua fedha zile katika Hazina ya Zanzibar, kwa hivyo, fedha zile hazijakaguliwa na aje mtu anisute. Kwa hivyo, fedha za Serikali zinatoka kutoka Serikali Kuu ya Jamhuri ya Muungano, kwanza zinachelewa, zinakopwa na Serikali ya Mapinduzi, lakini hazikaguliwi, kwa hivyo sasa ifanywe kama ambavyo imefanywa kwa MIVARF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye MIVARF baada ya kukamilisha utaratibu wa mchakato wa tenda wa kufanya kazi pesa za MIVARF ambazo zinatolewa na Benki ya Afrika pamoja na IFAD zinakwenda moja kwa moja katika akaunti ya……..
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.