Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakupongeza wewe na timu yako jinsi unavyotuongoza. Pia nampongeza Waziri wa Fedha na Mipango kwa kazi nzuri aliyoifanya inayoonekana kwenye Mpango wa Miaka Mitano aliouleta. Aidha, naipongeza Kamati ya Bajeti kwa maoni yao yanayoleta nuru zaidi katika mikakati ya Maendeleo iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuokoa muda nitachangia kwa kuuliza maswali ya kimkakati (strategic questions) ambayo naamini yakijibiwa yataboresha Mpango mzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi sasa imepata Rais ambaye pia ni Kiongozi. Kwa hiyo, tuna mtu wa kutuonesha njia ili tujue tunakwenda wapi. Juhudi za Kinabii ambazo Rais, John Pombe Magufuli (JPM) anafanya nchi yetu inaweza sasa kuwa na mpango na kuutekeleza. Pia ninapochangia kwa kuuliza maswali naamini Mheshimiwa Waziri atayafanyia kazi na yale yanayohitaji mwongozo wa Kiongozi wa nchi atayawakilisha. Kwa mantiki hiyo, nauliza kimkakati yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, aya ya 12; kama mfumuko wa bei umepungua kutoka asilimia 9.8 mwaka 2011 hadi alimilia 5.6 mwaka 2015, kwa nini riba katika mabenki yetu yote imebaki juu sana? Riba kubwa ya tarakimu mbili haiwezi kusaidia kusukuma shughuli za uzalishaji katika sekta husika (productive investments) riba za tarakimu mbili ni kwa wachuuzi wasiochangia uzalishaji mali na uwekezaji. Nini mkakati wa Serikali kutatua changamoto hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, aya ya 14; umaskini; ni jambo jema kwamba kama Taifa tumepunguza umaskini. Hata hivyo, ili jambo hili liaminike takwimu za umaskini ziwe zinatolewa kimkoa na kiwilaya ili mikakati iwekwe kulingana na eneo husika, ili mikakati iwekwe kulingana na eneo husika. Katika Jimbo langu la Muleba Kusini hali ya umaskini imeongezeka. Katika Jimbo langu Tunahitaji mikakati maalum inayohusu maisha na shughuli zetu, Mpango wa Miaka Mitano unahitaji kugatuliwa kwenda ngazi za wilaya na hata vijiji ili tupambane vizuri na hali halisi na kuweza kuboresha maisha yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja linalochangia Wilaya kama Muleba kubaki nyuma kimaendeleo ni kwa Taifa kutokuwa na specific program za Wilaya kubwa kieneo (geographic size) na wingi wa watu population size. Kwa Tanzania bara mgao wa fedha za maendeleo hauzingatii vigezo hivyo. Kwa hiyo, bajeti ya maendeleo inawasaidia zaidi wenye maeneo madogo kuliko wenye maeneo makubwa na watu wengi. Matokeo ni kugawa Mikoa, Wilaya, Vijiji na Majimbo vipande vipande, yaani hivi sasa kwa mtazamo wa kiuchumi kuna utitiri wa maeneo ya utawala.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la wazi kwamba, maeneo ya utawala yakiongezeka na gharama za uendeshaji wa Serikali zitaongezeka. Ingawaje kuna sehemu ambapo ugawaji wa maeneo yataleta ufanisi tusisahau kuwa teknolojia ya mawasiliano, usafiri na miundombinu bora inaondoa umuhimu huo. Kwa mfano, ilikuwa inachukua masaa 36 kuendesha gari kutoka Dar es salaam kwenda Bukoba, hivi sasa ni masaa 16. Kwa hiyo, kinachotakiwa ni mpango mkakati wa kuwa na Mipango ya Maendeleo ya Miaka Mitano na bajeti za kuitekeleza iliyojikita na inayozingatia na yenye uwiano wa ukubwa wa eneo na wingi wa watu waliomo kwa Tanzania Bara. Bila hivyo utakuta umaskini unaongezeka katika Mikoa na Wilaya kubwa.
Hii ni tofauti kabisa na malengo ya kuiendeleza Tanzania kwa misingi ya usawa iliyokuwa wenye Mpango wa Maendeleo wa Kwanza wa 1964-1963 (1st Year Development Plan) Mikoa kama Kagera ilitakiwa kupiga mark time kusubiri wengine, sasa imerudi nyuma na inashika mkia.
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano unatakiwa kuwa na uchambuzi huu wa usalama na uwiano wa maendeleo ya mikoa- (regional equality). Bila hivyo umaskini na kutokuwa na usawa vinaweza kuwa chanzo cha vurugu na kuharibu amani na utulivu wa nchi yetu. Mheshimiwa Rais Magufuli, ana uwezo na upeo wa kurekebisha hali hii isiyoridhisha aliyoirithi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Uwekezaji (Ibara ya 28); Mpango unakiri kuwa uwekezaji wa sekta binafsi haukufikia malengo. Hili ni jambo zito linalohitaji kuchunguzwa kwa kina. Haitoshi na ni kujidanganya kujivunia uwepo wa rasilimali nyingi chini bila kuwa na uwezo kifedha, kiteknolojia na kiutawala (managerial capacity) kuziendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Maendeleo unahitaji kuweka bayana mikakati ya kuondoa balaa hili, kuwa na rasilimali ardhi bila uwezo wa kuitumia. Badala ya mashamba tuna mapori, tuna rasilimali maji, lakini samaki wanavunwa na Mataifa mengine kwa sababu ya uvuvi duni. Tuna rasilimali misitu lakini hatuna wataalam wa kuvuna misitu na kutengeneza fenicha za kuuza nje, tunaishia kuuza magogo na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango ya Matokeo Makubwa Sasa; jambo hili linahitaji kuangaliwa kwa kina lisijekutwa ni jipu. Mishahara mikubwa inayodaiwa kulipwa kwa Watendaji wa Sekretarieti hiyo ni vyema iwekwe wazi na katika kufanya hivyo sera na mpango wa mishahara endelevu ufafanuliwe kwa wote. Gharama za uendeshaji zikizidi mapato hatuwezi kwenda mbele, tutakwamba. Naunga Mkono uamuzi wa Mheshimiwa Rais, kutangaza mshahara wake na kupendekeza suala la mishahara mikubwa sana kuangaliwa upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu; kinachohitajika ni reli, reli, reli kila mahali. Bila hivyo ni vigumu kuendelea na kushindana katika kilimo. Aidha, barabara za vijijini (access roads) zipewe kipaumbele. Barabara ya Muleba – Kinyambogo - Rubya. Kwa kiwango cha lami ni mfano hai wa jinsi barabara za vijijini zinavyosahaulika. Naamini Mheshimiwa Magufuli atatusaidia kutekeleza jambo hili ambalo alilifanyia kazi alipokuwa Waziri wa Ujenzi.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naamini maswali yangu yakijibiwa tutafanya maendeleo.