Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Mnamo tarehe 5 Mei, 2016 nilisimama katika Bunge lako Tukufu kuwatetea watoto ambao wanaolewa wakiwa na umri chini ya mika 15. Nami naomba niahidi kwamba nitaendelea na ari hii hii ya kuwatetea watoto wa kike ambao wamekuwa wakipoteza ndoto zao wakiolewa katika umri mdogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utangulizi huo, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaonekana ni sheria ambayo inambagua mtoto wa kike ambapo katika kifungu kile cha 13 na 17, kinamtaka mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 wakati mtoto wa kiume anaoa akiwa na umri wa miaka 18. Ukiangalia katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 13 nitanukuu, inasema:-
“(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria”.
(2) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweka sharti lolote ambalo lina ubaguzi wa dhahiri au kwa taathira yake.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sheria hii ya Ndoa ya mwaka 1971 utaona ni kwa namna gani inakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumbagua mtoto wa kike ambaye anatakiwa kuolewa na umri wa miaka 15 ilihali mtoto wa kiume anatakiwa kuoa akiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea. Ni jukumu letu sasa sisi kama wanawake na wawakilishi wa watoto wa kike na wanawake wote Tanzania nzima lakini tukishirikiana na Waheshimiwa Wabunge wote bila kujali rika na kujali jinsia kuwatetea watoto wa kike ili na wao pia waweze kutimiza ndoto zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona madhara ya ndoa yakiwemo ya kiafya. Watoto wengi wa kike wanapokuwa wanaolewa na umri mdogo wa miaka 15, kiafya watoto hawa wanakuwa hawajapevuka katika maumbile yao na hivyo basi kitu hiki kinasababisha watoto hawa wanapopata ujauzito, hizo tunaziita ni mimba za utotoni kwa sababu zile ni mimba ambazo bado yule mtoto hajapevuka maumbile yake na madhara makubwa ambayo yanatokea ni vifo vya akinamama. Naamini kabisa Serikali haitapenda kuona vifo vya wanawake vikiendelea kutokea ambavyo vinasababishwa na sheria hii ya ndoa za utotoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia madhara mengine ya ndoa za utotoni ni vifo vya watoto wachanga ambao wanazaliwa na akinamama ambao bado hawajapevuka. Kitu kingine, wasichana wanakosa elimu na kuna msemo unaosema kwamba unapompa elimu mtoto wa kike umesaidia jamii nzima, hili linaonekana wazi kabisa. Wapo Waheshimiwa sasa hivi humu ndani wakiamua watoe shuhuda zao kwa kweli kila mtu atastaajabu. Basi ni jukumu letu sisi Waheshimiwa Wabunge kuiomba au kuishawishi Serikali iweze kutusaidia kurekebisha Sheria hii ya Ndoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na madhara ambayo yanawakuta wasichana, kwa sababu wasichana ndiyo waathirika wakubwa, wanapoolewa na umri mdogo, kwa nini tunasema Sheria ya Ndoa ibadilishwe. Mchakato wa kuomba Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ifanyiwe
marekebisho haukuanza leo. Hivyo naamini kwamba Bunge hili halitakuwa la kwanza kuishawishi Serikali kuleta mabadiliko ya Sheria ya Ndoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato huu ulianza mwaka 1984 ambapo Umoja wa Wanawake Tanzania waliishauri Serikali kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria kwamba Serikali irekebishe Sheria hii ya Ndoa kwa sababu walizunguka Tanzania nzima na wakaona kwamba watoto wengi wa kike wanapata hasara kubwa sana wanapoolewa na umri mdogo. Kwa hiyo, utaona kwamba mchakato huu haukuanza leo ulianza siku nyingi sana mwaka 1984 wakati sheria imeundwa mwaka 1971, mchakato huu ulianza mapema sana. Wanawake Tanzania waliona ni kwa namna gani watoto wa kike wanaathirika katika kuolewa na umri mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato huu pia mwaka 1994 Tume ya Mabadiliko ya Sheria baada ya kupokea maoni mbalimbali kutoka kwenye NGO’s mbalimbali walileta pia mapendekezo yao. Kama ningepata nafasi ya kukuletea hapo mezani na wewe pia ukayapitia mapendekezo ya Tume hii ambayo ilishauri kwamba Serikali ifanyie marekebisho Sheria hii ya Ndoa. Pamoja na changamoto zote ambazo zinaonekana za kimila na za dini lakini bado Tume hii ilishauri Serikali kufanyia marekebisho Sheria hiyo ya Ndoa ili kuwanusuru watoto wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumeingia mikataba mbalimbali ya kimataifa ukiwepo Mkataba wa Haki za Watoto, Mkataba wa Kutokomeza Aina Zozote zile za Ubaguzi hapa Nchini Tanzania na kwingineko. Pia Sustainable Development Goals inazingatia sana kutokomeza ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2030. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, juzi juzi tu hapa ilitoka hukumu dada mmoja anayeitwa Rabeca Gyumi alipeleka mapendekezo yake Mahakamani kuhusiana na kubadilishwa kwa Sheria hii ya Ndoa. Kama tunavyofahamu Mahakama ndiyo sehemu pekee ambayo wanaweza
kutusaidia kutafsiri sheria na hapa ninayo nakala ya hukumu. Katika hukumu hii iliyotolewa na Mahakama inapendekeza Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kubadilisha Sheria hii ya Ndoa kile kifungu cha 13 na 17 ambacho kinapendekeza umri wa mtoto wa kike kuolewa kuwa miaka 15 na wa kiume kuoa akiwa na miaka 18. Kwa hiyo, hukumu imetoka ikieleza au ikiitaka Serikali kubadilisha vifungu hivyo vya Sheria ya Ndoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo sina mengi sana ya kuongea lakini naomba nihitimishe kwa kusema kwamba, sisi Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tukikaa kimya bila kuwasemea watoto wa kike kwa kweli watu wengi huko nje watabaki wanatushangaa. Nasema hivi kwa sababu nimekuwa nikifuatilia sana kwenye TV, wanawake wanalia na kutoa machozi tena wanabaki wanauliza, wako wapi wanawake wa Tanzania waweze kututetea watoto wetu wasiolewe katika umri mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ndoa hizi wanaoathirika sana ni watoto wetu wa kike. Japokuwa kuna juhudi za Serikali ambazo kwa kweli zimeonekana na siwezi kukataa kwamba juhudi za Serikali hazijaonekana. Tunaona marekebisho ya Sheria ya Elimu ya mwaka 2016 ambayo inataka watoto wasiolewe chini ya umri wa miaka 15 au wakiwa wako shuleni. Hata hivyo, ukiangalia sheria hii inawabagua wale ambao wapo nje ya mfumo wa elimu. Kwa hiyo, ni ombi langu kwa Serikali kutusaidia tu kutekeleza hii hukumu ambayo imekwisha kutoka au la sivyo naomba wanapokuja kuhitimisha hoja yao…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.