Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu kuna hali ya kutisha kwa sababu ya utekwaji wa watu (wananchi) lakini Serikali imenyamaza kimya, mfano kutekwa kwa Ben Saanane. Naiomba Serikali ishughulikie suala hili na hasa kumleta Ben Saanane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zetu za jinai zimesisitiza kwamba utekaji nyara kwa lengo la kuua au kuumiza mtu ni kosa kubwa la jinai. Chini ya Kifungu cha 248 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kwa mfano;
“Mtu yeyote ambaye anamteka nyara au kumtorosha mtu yeyote ili mtu huyo auawe, au aweze kutupwa ili kuwekwa katika hatari ya kuuawa, atakuwa anatenda kosa na anawajibika kwa adhabu ya kifungo cha miaka kumi”
Kwa mujibu wa kifungu cha 250 cha sheria hiyo, kuteka nyara kwa lengo la kumuumiza mtekwa nyara ni kosa la jinai vilevile na adhabu yake ni kifungo jela kwa muda wa miaka kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuwazuia watu wasiwe na uhuru wa mawazo ni kukiuka Katiba ya nchi Ibara ya 18(a) inayosema:-
“Kila mtu-
(a) Anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na kamatakamata ya baadhi ya Wabunge na wananchi wengine kwa sababu ya kueleza au kutoa mawazo yao ya kuikosoa Serikali. Naishauri Serikali kusikiliza mawazo hayo na kuyatendea kazi kwani ni kwa njia ya kukosolewa Serikali inaweza kuboresha utendaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ndoa za utotoni, naiomba Serikali kurekebisha Sheria ya Ndoa ili kuwatendea haki watoto wa kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzuia mikutano ya hadhara, hapa naona Serikali inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 20(1) inayosema:
“Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iruhusu mikutano ya vyama vya siasa kwani hii ni kulingana na Katiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.