Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipatia fursa hii ili nami niweze kuchangia. Kubwa nakushukuru kwa jinsi ulivyoliongoza Bunge lako Tukufu asubuhi kwenye sala ama dua. Wabunge tuna tabia tunapofika hapa asubuhi shughuli zetu kabla hazijaanza tunaanza na sala au dua. Unapotafakari maneno mazuri yaliyopo kwenye ile sala hakika huwezi kuamini kwamba baada ya muda mfupi tu ule tunaweza kusahau commitment yetu kwa Mungu tukaanza ku-behave kama watu ambao hatukutambua mamlaka ya Mungu tunayemwomba kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa ya kuchangia hapa na aendelee kutukuzwa sana. Pia nimshukuru Waziri na kumpongeza Mheshimiwa Profesa Kabudi kwa hotoba hii nzuri ya bajeti yake ambayo naiunga mkono. Kusema kweli imezungumza mambo ya msingi ambayo yanalihusu Taifa hili. Kwa sababu hiyo, naungana nawe Mwenyekiti kwa ushauri wako ulioutoa mbele ya Bunge lako Tukufu muda mfupi uliopita kwamba hotuba hii imesheheneza mambo ya msingi kwa mustakabali wa Taifa hili. Laiti Wabunge tungeelekeza michango yetu kwenye mambo mazuri yanayosimamiwa na Wizara ya Katiba basi tungeweza kuishauri Serikali vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu ambacho napenda kusema hapa kwamba Bunge kama Bunge tunapaswa tutambue wajibu wetu. Wakati fulani huwa nakaa hapa nasikiliza sana kwa makini, lakini hatuwezi kuligeuza Bunge hili kuwa sehemu ya burudani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mambo ya msingi yanazungumzwa kwa mustakabali wa Taifa hili halafu baadhi yetu tunageuza Bunge hili kuwa sehemu ya burudani na watu wengine wanaleta sauti za wanyama kama ulivyosema fisi, wakati fulani najiuliza mimi kama Mshauri wa Sheria wa Serikali hii hivi tutumie Sheria ya Afya ya Akili? Maana tunayo Sheria ya Afya ya Akili ambayo tunaweza kuitumia kuangalia kama baadhi yetu akili zetu ziko sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mtu ambaye akili yake iko sawa na anashiriki mjadala kuna namna ya kushughulika na mjadala, mjadala ama ni kwa kuzungumza au kwa maandishi lakini siyo kwa kuzomea au kwa kupiga kelele. Unapofika hatua hiyo katika mjadala sisi ambao tumeshiriki sana kwenye mjadala, mimi nilikuwa Mwenyekiti debating club shuleni, ujue huyu mtu ameishiwa hoja za msingi na kwenye hotuba kama hii hamkupaswa kuishiwa hoja za msingi yapo mambo mengi ambayo yalipaswa yazingatiwe.
Mheshimishiwa Mwenyekiti, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mambo mengine inataja mihimili mitatu ya dola na mgawanyo wake katika Ibara ya 4; Bunge linatunga sheria, Mahakama inatafsiri sheria na kutoa haki na Serikali inasimamia utekelezaji wa sheria. Sasa humu ndani yamezungumzwa mambo ambayo mengine yameingilia kwenye mihimili mingine kwa mfano yale mambo ambayo yako Mahakamani, hayo hayapaswi kuletwa hapa Bungeni. Moja, yamezungumzwa hapa mambo ya kesi ambazo ziko Mahakamani.
Huyu Msemaji wa Kambi ya Upinzani yeye mwenyewe ana kesi nne Mahakamani analeta hoja hapa kuhusu mambo ya Mahakamani.
Godbless Lema ana kesi mbili Mahakamani. Hawa ambao wanashtakiwa kwa sababu ya kukiuka Sheria ya Makosa ya Mitandao wana kesi Mahakamani. Kwa hiyo, mambo yote haya ambayo yako Mahakamani tuyaachie mhimili wa Mahakama iyashughulikie. Bunge haliwezi kugeuka kuwa ndiyo mtunga sheria, Jaji na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna tuhuma, Bunge linapotunga sheria hapa maana yake zifanyiwe kazi. Bunge hili lilitunga Sheria ya Cyber Crimes Act, Electronic Transactions Act na sheria chungu nzima, kama wapo watu ambao wamekiuka zile sheria, Serikali iliyopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria lazima ichukue hatua ipasavyo. Watu hawa wanaposhtakiwa Serikali isichukuliwe kwamba ni dikteta au inanyanyasa, ndiyo wajibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri, katika hotuba hizi zote na michango yote hii yale mambo ambayo yako Mahakamani Kiti chako kisiyatilie maanani na wananchi wayapuuze kwa sababu upo mhimili mahsusi kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Subira Sungura amezungumza juu ya utata wa umri wa mtoto wa kike kuolewa. Hili pia limezungumzwa na Mheshimiwa Kiteto Koshuma, ni hoja za msingi sana lakini Serikali imekuwa ikichukua hatua. Jana Waziri wa Katiba na Sheria alizungumza na atazungumza lakini suala hili jinsi lilivyo Serikali imeshachukua hatua. Moja, kuna kesi Mahakamani. Kwa hiyo, kwa vile kuna kesi iko Mahakamani Kanuni zetu na Katiba vinakataza tusiyazungumze haya humu ndani jamani. Tuna prejudice Mahakama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba hii Ibara ya 30(2)(d) inasema kwamba:-
“Kulinda sifa, haki na uhuru wa watu wengine au maisha binafsi ya watu wanaohusika katika mashauri mahakamani; kuzuia kutoa habari za siri; kutunza heshima, mamlaka na uhuru wa mahakama”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na michango yao mizuri kuhusu huu utata wa umri wa kuolewa kwa sababu kuna kesi Mahakamani, naomba kulishauri Bunge lako Tukufu Wabunge wavute subira, tuiachie fursa Mahakama, Mahakama itaamua, tuishie tu pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimba za utotoni pia Serikali imeshachukua hatua. Kwanza, kuna Sheria ya Kanuni ya Adhabu ambayo inapiga marufuku mtu kujamiana na mtoto wa kike ambaye yuko chini ya umri wa miaka 18. Ukifanya kitendo hicho basi unakuwa umetenda kosa la kubaka na adhabu yake ni miaka 30 na kama yuko chini ya miaka 12 ni kifungo cha maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumerekebisha Sheria ya Elimu kama alivyosema Mheshimiwa Koshuma, mwaka 2016 hapa, tukaweka kwenye kifungu cha 60A kwamba ikawa ni marufuku mtu kuoa au kuolewa na mwanafunzi au kuozesha au kwa namna yoyote kumfanya mwanafunzi aache kusoma, ni kosa la jinai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo, tuliwapa jukumu wakuu wa shule kwamba kila robo wawe wanatoa taarifa za incidences case za ndoa, za utoro kwa Afisa Elimu wa Wilaya. Kwa hiyo, Serikali kama Serikali imechukua hatua za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hilo, Serikali pia imechukua hatua za kisera, moja, imejenga sekondari za Kata kila sehemu; sekondari nyingine zipo mpaka vijijini. Pia ikaifanya elimu hii ya msingi mpaka sekondari kuwa bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukingo ule uliowekwa unamwezesha huyu mtoto asome. Ni wakati gani anapata umri wa kuolewa? Polisi hawezi kuwa kila wakati, lakini Sheria ya Mtoto (The Law of the Child, 2009) kifungu cha (8) na (9) kinatoa jukumu kwa mzazi kuhakikisha kwamba mtoto wake anapata elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa Serikali imeweka sera hizi za elimu bure, imejenga shule, imetunga sheria, ombi langu kwa wazazi sisi, tuipe Serikali ushirikiano ili tuisimamie hii sheria na watoto wetu wapate elimu. Kwa hiyo, wazazi tuna jukumu hilo la msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sabreena Sungura amezungumzia juu ya Serikali… (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza masuala ya kidini, Waheshimiwa Wabunge hatuwezi kutumia Bunge hili kuleta mtafaruku wa kijamii kwa kutumia Bunge hili kuwafanya watu ambao ni ndugu wasielewane. Unapozungumza, unailaumu BAKWATA hapa, sasa unatambua taasisi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba yetu Ibara ya 19 inasema, masuala ya kidini na ya imani hayawezi kuingiliwa na Serikali. Eeh, hatuwezi kwenda huko. Katiba iko wazi, kama kuna mgogoro uende kwa Kabidhi Wasii Mkuu, ndivyo sheria zinavyosema. Hamwezi kutumia Bunge hili kupanda mbegu za chuki kwa wananchi wa Tanzania. We cannot allow this. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashangaa hata mnayoyaleta humu ndani, nawe Mheshimiwa Kubenea, unajua vitu vinazungumzwa hapa, ngoja nianze kuwashauri. Hili la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam lazima tuheshimu Sheria na Katiba tulizozitunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo sheria hapa, inaitwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Sheria hii inatoa fursa kwa sisi viongozi wa umma tunaokiuka kushitakiwa kule. Meya wa Ubungo amefungua kesi dhidi ya huyo RC, iko pale. Kwa hiyo, tusiwe na haraka. Mnavyoiharakisha, mnaiharibu.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mnataka Mheshimiwa Rais achukue hatua gani dhidi ya huyu mtu wakati tayari iko kwenye mamlaka nyingine inashughulikiwa? Ile Tume ikiona kuna mambo ya jinai, itapendekeza, kwa sababu ina mamlaka mle ya kupeleka PCCB, kupeleka polisi. Eeh, msiwahishe hivi vitu. Mnajua mkiingilia hizi kesi Mahakamani, mnaziharibu. Sisi tunaoendesha kesi, kuna kitu kinaitwa mis-trial; na mimi naende kule tunasema bwana umeshahukumiwa, hiyo kesi unaiharibu. Kwa hiyo, isije ikawa ni mikakati ya kuharibu hizi kesi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, vuteni subira. Utawala wa Sheria mnaoutaka ni lazima mzingatie hamwezi kuwa mnaisema Serikali tu, na ninyi hamtaki kuizingatia hiyo kitu. Kwa hiyo, RC anayo mamlaka yake ya uteuzi na sasa hivi sijui ametuhumiwa amevunja, amepelekwa kwenye hiyo Sekretariati. Let us be patient, hatuwezi kuwa tunahukumu tu hivi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aaah, Mheshimiwa Shahari amezungumza hili la mashehe. Hili suala liko mahakamani na ni ushauri wangu tu ni kwamba tuliache Mahakama ichukue hatua. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wetu sisi tutajitahidi kuharakisha uendeshaji wa kesi hii, ama upelelezi ukamilike mapema hatima yake ijulikane, lakini hili siyo jambo la kuzungumzia humu ndani, unajua masuala ya kuzungumzia kesi zilizopo Mahakamani, mnaziharibu halafu mnaingilia uhuru wa Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ya Mheshimiwa Maige na Muswada binafsi tuliupokea ule Muswada unashughulikiwa na Serikali. Kwa wakati muafaka atashirikishwa, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Maige uwe na subira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ester Mmasi ametushauri vizuri sana Serikali. Ushauri wa Mheshimiwa Mmasi ni mzuri sana, kuna kila sababu ya sisi Serikali kuchukua mambo mazuri anayoyatoa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho naweza kuahidi, moja, tunachoweza kufanya, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini atazungumza wakati wa Bajeti yake, kuna umuhimu wa kuirekebisha ile sheria ili nako tuweke fursa local content kwa maana ambayo itazingatia ajira, fursa nyingine, goods and services na kadhalika; na hapa Watanzania anaowazungumza watapata hizo fursa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kwenda kwa undani, lakini ninachoweza kusema ni kwamba ni ushauri mzuri, Serikali itautafakari na muda muafaka Waheshimiwa Wabunge mtaona matokeo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli niseme tu kwamba Mheshimiwa Mchengerwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria amelisaidia sana Bunge hili. Kwa hiyo, sisi kwa upande wetu tumeunga mkono mchango wake katika hili na tuseme tu kwamba kama Wabunge wote mkiwa mnatoa michango ya aina hii ingetusaidia sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, haya mambo ya kuzungumza viongozi wa mahakama yakome. Kambi yenu ya Upinzani na hasa Msemaji wenu wa Upinzani ana tabia sana ya kuwasema Majaji Wakuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumekuwa hapa kwenye Bunge, kila akiwemo Jaji Mkuu, alikuwa anamshambulia sana Jaji Mohamed Chande amekuja huyu, naye anamshambulia tu. Sasa uliwahi kuona anaingia humu ndani? Kwa hiyo, acheni. Wananchi, muwapuuze hawa watu. Huyo anayekaimu ana mamlaka sawa na Jaji mwenyewe in full. Ndivyo tafsiri ya sheria inavyosema na wananchi waendelee kuwa na imani na mahakama yao. Hakuna kitu chochote kinachovurugwa. Kama ni mashauri waende mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la ushauri, tuzingatie sana sheria. Haiwezekani Serikali ambayo imepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria, inapochukua hatua za kusimamia zile sheria mliozitunga ninyi wenyewe, mnasema hii ni Serikali ya kidikiteta, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unavunja sheria, unashitakiwa. Huwezi kushitakiwa halafu ukasema ni dikiteta. Mwalimu Nyerere alisema hivi, Serikali ni sheria. Hakuna kitu kinaitwa Serikali bila sheria na sheria zikishatungwa ni lazima zifuatwe. Ndiyo msingi wa utawala wa sheria mnaousema Mheshimiwa Shahari na ndiyo msingi wa Ibara ya 26 ya Katiba ya nchi yetu inayotaka kila mtu kuzingatia Katiba na sheria za nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa hakuna cha dikteta. Nchi hii inaongozwa kwa demokrasia na taasisi zake zote za kidola likiwemo Bunge, Mahakama na Executive, vinafanya kazi kwa ufanisi; na Ma-Rais walioko madarakani, wameingia madarakani kidemokrasia kwa Uchaguzi Mkuu. Eeh, Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa Rais Shein, wala hapa hakuna cha Udikteta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ya kubadilisha Mawaziri na yenyewe ni kitu cha kawaida. Mheshimiwa Rais amepewa mamlaka ya kuteua Mawaziri wake na hatukuweka sheria ya ukomo kwamba huyu ata-serve kwa muda fulani na akimbadilisha anampeleka Wizara fulani. Msianze kuwatisha viongozi. (Makofi)
Mazingira hayo mnayojenga kwenye jamii ya watu kwamba kuna hofu imetanda, mwache. Kwa sababu huko nyuma mliwahi kusema kwamba mtaifanya Serikali isitawalike, haiwezekani. Mliwahi kusema mtafanya nchi isitawalike, haiwezekani. Wakati ule mlichukua vitendo, sasa mnaleta hoja kwamba hofu hofu, wakati mambo yanaendelea hapa. Shughuli zote za kijamii, kiuchumi, kisiasa zinaendelea kama kawaida, halafu mnasema eti kwamba kuna hofu. Haya lazima tuyapuuze. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kushauri, haya mambo yote ambayo yametajwa hapa kwamba kesi sijui na vitu gani, haiwezekani ninyi mnashabikia wengine washitakiwe, ninyi mkishtakiwa mnasema sijui tunaonewa. That cannot be the case. Kesi nyingine mnayosema walifikishwa mahakamani wakaachiwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.