Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na mimi nichangie Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na naomba nianze kwa kutoa pongezi kubwa kwa kazi kubwa ainayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara zaidi ya kilometa 17,000 huwezi kutenganisha na Mheshimiwa Magufuli. Ujenzi wa viwanja vya ndege nchini unaoendelea, huwezi kuacha kumtaja Mheshimiwa Rais Magufuli; umeme vijijini ambapo tunamalizia vijiji hivi, huwezi kumuacha Mheshimiwa Rais Magufuli; mabasi yaendayo kwa kasi Dar es Salaam ni kwa sababu ya Rais Magufuli, ujenzi flyover leo Dar es Salaam, kwa kweli ni Mheshimiwa Rais Magufuli; Daraja la Mkapa, Daraja la Kikwete, Daraja la Kigamboni, Daraja la Kilombero huwezi kuyatenganisha na Mheshimiwa Rais Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa reli ya kati ya kisasa (standard gauge) ambayo mara ya mwisho reli hii imejengwa mwaka 1906 leo Mheshimiwa Rais Magufuli anaandika historia ya kujenga reli Tanzania. Kuimarisha Shirika la Ndege la ATC ni kazi ya Mheshimiwa Rais Magufuli, kudhibiti matumizi ya Serikali ni Mheshimiwa Rais Magufuli, ukusanyaji wa mapato ni Mheshimiwa Rais Magufuli. Leo tunaona elimu bure, ni Mheshimiwa Rais Magufuli, mabweni ya University of Dar es Salaam ni Mheshimiwa Rais Magufuli. Upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na Mtwara ni Mheshimiwa Rais Magufuli, kuanza kujenga upya uchumi wa viwanda ameanza Mheshimiwa Rais Magufulina na kudhibiti maliasili ni Mheshimiwa Rais Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo hakika kwa kazi kubwa inayofanyika ya miumbombinu, safari ya kuondoa umaskini wa Watanzania Mheshimiwa Rais Magufuli ameianza. Pia naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, ninayo hakika atayekuja kuandika historia ya Tanzania nina hakika jina la Mheshimiwa Rais Magufuli litaandikwa kwa wino wa dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nichangie baadhi ya maeneo; barabara ya Mwandiga - Chankere kwenda Kagunga, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri ameipandisha lakini fedha iliyowekwa ni kidogo sana kwa sababu barabara hii ni ndefu na inapita kwenye milima mikubwa sana. Pia suala la barabara ya
Mwandiga, fidia Mwandiga - Manyovu nakuomba sana Mheshimiwa Waziri Mbarawa, usimchonganishe Mheshimiwa Rais Magufuli na watu wa Kigoma Kaskazini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Magufuli alikuja kwenye kampeni, aliahidi kwamba lazima atawafidia ambao hawajafidiwa kwenye barabara hiyo ya Mwandiga
- Manyovu na barabara ya Mwandiga - Kidahwe. Nakuomba sana utekeleze ahadi hii. Pia barabara ya kutoka Simbo kwenda Ilagala kilometa kumi za lami naomba zianze kujengwa, Mheshimiwa Rais Magufuli alihaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi kwa nini nasema hivi? Mheshimiwa Rais Magufuli akiahidi anatekeleza. Naombeni ninyi watu wa Serikali, Wizara msimchonganishe Rais, kwa sababu aliahidi naombeni mtekeleze hizi ahadi zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Bandari ya Kagunga, nawapongeza sana watu wa bandari kujenga gati ya Kagunga. Nawaomba sana watu bandari, ili bandari ya Kagunga iwe na maana kibiashara ni lazima na soko la Kagunga mlichukue muweze kulifanyia kazi. Halafu baadaye Halmashauri ya Kigoma tutaungana na bandari, tutafanya revenue sharing, mkishamaliza kutoa fedha zanu, then mtaturudishia jengo lile, lakini nina hakika bandari ile itakuwa na maana kama tutakuwa na soko la Kagunga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, pale kwenye Soko la Kagunga tupafanye kuwa free trades zone area ili watu wote wapeleke bidhaa pale. Nina hakika Warundi na Wakongo watakuja pale kwenye soko lile na tutapata fedha nyingi sana kama nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nilitaka niliseme vizuri sana, ni suala la barabara vijijini na TANROADS. Nimesikia Serikali inataka kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini. Nashauri na naomba sana tayari tunayo TANROADS, inafanya vizuri sana, hivi badala ya kuanzisha Wakala mwingine ambao ni matumizi, ni fedha, ni mzigo, badala yake kwenye TANROADS pale fuwafanye waende mpaka Wilayani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wote hapa ndani mmekuwa mnaomba barabara zipandishwe, sasa kama tunaomba barabara zipandishwe, basi tuamue.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge, tuamue niombe Serikali kwamba sasa custodian wa barabara nchini iwe TANROADS peke yake ili fedha zote za mafuta tunazokusanya, badala kumpelekea TANROADS asilimia 67, tumpelekee asilimia 100 kwamba suala la barabara Tanzania tunashughulika na TANROADS peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashuri yapo mambo mengi ya kufanya, tuwanyang’anye hili la barabara. Nina hakika Wakala huu tukiupanua tukawapa fedha zote mtu mmoja, kwanza tutakuwa tume-save fedha za administration kwa sababu itabaki ni ile ile; kama ni Mkuu wa Taasisi atabaki ni yule yule, Wakurugenzi watabaki ni wale wale. Tukianza taasisi nyingine, hizi ni gharama. Na mimi ninaamini spirit ya Serikali hii ni kupunguza matumizi. Nani anataka kuleta habari ya kuanzisha mawakala wengi, wakati tunaweza kuamua ma-engineer wote tunawapeleka na one umbrella, wao ndio wafanye kazi ya kuhakikisha nchi yetu barabara zinajengwa na mtu mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa naibu Spika, mwisho ni suala la barabara ya kutoka Kibondo kuja Kasulu kwenda Manyovu. Nawaomba sana, nimeona kwenye kitabu mmeandika kwamba ipo under NEPAD. Habari ya NEPAD tumeisikiliza huu ni mwaka wa saba. Nadhani imefika wakati sasa, na kwa kweli jamani, tuliobaki hatujapata barabara ni sisi watu wa Kigoma. Naombeni sana mjitahidi tumalizie barabara hizo za watu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nataka kuwakumbusha tu watu wa Serikali, inawezekana Mheshimiwa Waziri Mbarawa labda hili hulijui vizuri sana. Reli
ya kati Tanzania; definition ya reli ya kati toka wakati wa Mjerumani ni Kigoma - Dar es Salaam. Toka 1906 ni Kigoma – Dar es Salaam. Halafu kuna matawi ya Tabora - Mwanza kuna matawi ya kutoka Kaliua kwenda Mpanda, haya ndiyo matawi. Naombeni tusi-diverge from the original reli ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi kwa nini nasema Kigoma? Ni kwa sababu moja tu; kwa sababu Kigoma tunayo bahati; Kigoma tuna Burundi na Kongo ambako huko kuna mzigo wa biashara. Investment hii inayofanyika ni kubwa sana, lazima tuanze kuifikiria kibiashara. Tutumie jiografia yetu kutengeneza pesa. Mungu ametuunga geographically tuko well located, tuitumie nafasi hii kufanya vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sana nimpongeze tena Mheshimiwa Waziri na watendaji wake kwa kazi kubwa sana wanayofanya. Nawapongeza watu wa bandari, wanafanya kazi kubwa sana. Tumeongea habari ya gati 13 na 14 nikiwa Bunge hili karibu miaka kumi. Sasa naona kuna mwanga, gati 13 na 14 linaenda kutekelezwa; gati namba moja mpaka saba inatekelezwa, kupanua mlango na kuchimba dragging ya Dar es Salaam inatekelezwa. Naombeni miradi hii iende kwa kasi ili nasi tuweze ku-compete katika biashara ya huko mbele tunakokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri.