Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakukushuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kumpa pongezi kubwa sana mtoa hoja, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa na timu yake yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nielekeze pia pongeze zangu kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua zake thabiti na za dhati katika kuhakikisha kwamba analifufua Shirika letu la Simu la TTCL, imewekwa pale management ya vijana, management nzuri kabisa. Ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, muasaidie sana hawa katika kuwaongezea mtaji ili waweze ku-compete vizuri katika soko hili ambalo lina ushindani mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nianze kujielekeza katika katika kuchangia hotuba hii. Katika hiki kitabu, ukurasa wa 49 na 50 unazungumzia ujenzi na ukarabati wa vivuko mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Mafia, sisi kule hatuna namna yoyote, lazima tupate boti au meli ya aina yoyote ili kututoa kwenye kisiwa kikubwa na kutuleta huku sehemu ya bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mwaka 2016 wakati nachangia hotuba hii, nilimuomba Mheshimiwa Waziri, naye anakumbuka kwamba sisi watu wa Mafia tuna matatizo sana ya usafiri wa kuingia na kutoka Mafia. Akatuahidi kwamba ile iliyokuwa MV Dar es Salaam, ambayo ilikuwa imeegeshwa pale, haina shughuli yoyote, tulipoiomba akatukubalia, lakini akasema ina matatizo kidogo ya kimkataba na ya kiutaalam; wakishayamaliza watatuletea Mafia iweze kutusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumesikia tangazo, mwenye mamlaka ameichukua ile meli, amewapelekea watu wa Jeshi, hatuna tatizo na hilo. Tatizo letu ni kwamba je, Mheshimiwa Waziri baada ya kutuondolea ile MV Dar es Salaam, katika hotuba yako, nimeisoma na kuirudia hapa kwenye maeneo ya vivuko hivi na ferry mbalimbali, hakuna mkakati wowote wa kuondoa tatizo la usafiri baina ya Nyamisati na Kilindoni katika kisiwa cha Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwa sababu naye anatokea kisiwani vilevile, baadhi ya maeneo mengine yamepangiwa kwa alternative route, wengine wanaona kama vile kuzunguka; mnawajengea vivuko wafupishe safari zao, lakini sisi hatuna namna, lazima tupande boti. Sasa hatusemi kwamba maeneo mengine wasipelekewe vivuko, lakini haya maeneo ambayo yana alternative route japokuwa ya kuzunguka, yasubiri kwanza mtupe kipaumbele sisi ambao hatuna namna yoyote, lazima tuvuke maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa majibu ya kusema kwamba jaribuni kuwashawishi private sector waje wasaidie, tumefanya sana na Mheshimiwa Waziri ni shahidi, tumeongea na Bakhresa, tumeongea na Zacharia, bado wanasitasita kuleta usafiri baina ya Kilindoni na Nyamisati. Sasa hili moja kwa moja ni jukumu la Serikali sasa, mtuletee huduma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwenye kiti chako hapo, uniandike jina langu kabisa, nitazuia shilingi mpaka nipate majibu, ni lini Serikali itakuja na mkakati thabiti kabisa kuhakikisha kwamba inapatikana meli au boti ya kisasa ili kuondoa tatizo la usafiri baina ya Nyamisati na Kilindoni Mafia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, gati la Nyamisati. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, walituahidi mwaka 2016 hapa wametenga shilingi bilioni 2.5 na kweli zimekuja tumeona mkakati unaanza pale, wataalamu wapo, utafiti wa udongo umeshaanza na ujenzi na tenda imetangazwa wiki iliyopita na ujenzi utaanza hivi karibuni. Tunaipongeza sana Serikali na tunashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa gati lile utachukua mwaka mmoja kukamilika. Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, wananchi bado wanapata matatizo. Bandari ya Nyamisati haina sehemu ya abiria, kuna banda tu bovu bovu pale, hakuna vyoo, hakuna maji, hakuna hata ngazi ambayo inaweza ikarahisisha abiria kupanda kwenye boti na kushuka. Tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri kupitia Mamlaka ya Bandari, naamini wapo, watusaidie pale. Na mimi binafsi nimefanya juhudi, nimeandika barua kwa Katibu Mkuu wa Ujenzi na nimemsikia asubuhi hapa akitambulishwa, Ndugu Nyamuhanga kwamba tunaiomba ile ngazi iliyokuwa pale inatumika kwa ajili ya MV Dar es Salaam ambayo haifanyi kazi kwa sasa, mtuletee Nyamisati kwa kipindi hiki cha muda wa mwaka mmoja wakati ujenzi unaendelea, isaidie. Sijajibiwa ile barua, wala sina taarifa zozote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, ninaamini Serikali ni sikivu na Mheshimiwa Waziri sasa nalileta kwako rasmi, tunaomba sana mtupatie ile ngazi angalau kwa muda huo wa mwaka mmoja tuweze kuondoa tatizo la kupanda na kushuka katika gati la Nyamisati.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi, kilometa 55 ilikuwa ni ahadi ya Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alipokuja kuomba kura Mafia mwaka 2005 na 2010 tena na kwenye Ilani ya Uchaguzi, 2015 - 2020 imo, kwamba barabara ile itafanyiwa upembuzi yakinifu. Nimekiangalia hiki kitabu kuna mahali nimeona kuna shilingi bilioni 1.5. Tafsiri yake sijaipata, lakini naomba utakapokuja kuleta majumuisho hapa, uniambie labda hiyo ndiyo kwa ajili ya usanifu na uchambuzi wa kina kuhusu barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, hususan Mheshimiwa Naibu Waziri yeye alikuja Mafia na tukamwambia kwamba Mafia ni kisiwa, kuna tatizo la udongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kuikarabati ile barabara, wataalamu wanasema udongo uliobaki utafaa kwa miaka miwili tu, baada ya hapo utakuwa umekwisha na mkitaka kujenga barabara ya lami itabidi udongo muutoe Dar es Salaam gharama itakuwa ni kubwa sana.
Kwa hiyo, naomba sana mtuharakishie ujenzi ule wa barabara ya lami Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi kilometa 55 tu ili tusije tukakumbwa na tatizo la ukosefu wa udongo ambao unakwisha kutokana na matengenezo ya kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu alifanya ziara Mafia Septemba, 2016, tukamwambia kilio chetu, ATCL ije Mafia, usafiri ni taabu, ni gharama kubwa sana usafiri wa ndege Mafia. Round moja tu ya kwenda one way ni shilingi 160,000; kwenda na kurudi inakwenda shilingi 300,000 mpaka shilingi 320,000. Tumeona ATCL wameanza route ya kwenda Mtwara, tunaomba sana ile ya kwenda Mtwara ipitie Mafia
– Mtwara; ikitoka Mtwara – Mafia – Dar es Salaam; itatusaidia sana kutuondolea tatizo hili la gharama kubwa ya usafiri wa ndege. Tukifika sisi Magharibi pale, jua likizama Mafia, huna namna ya kutoka. Akipatikana mgonjwa huna namna ya kutoka kwa sababu ndege zinazokuja pale ni ndogo na usiku uwanja ule hauna taa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nukta hiyo labda nizungumzie tena huu Uwanja wa Ndege. Tunaishukuru Serikali iliutanua, lakini bado kuna hilo tatizo la taa. Uwanja hauna taa na ikifika usiku, akitokea mgonjwa amepata dharura, basi mjue huyo mgonjwa chance za kupoteza maisha ni kubwa zaidi kwa sababu hakuna namna ya kutoka ndani ya Mafia ila ni kupitia bahari na ukiingia kwenye boti ni safari ya saa tano mpaka sita.
Kwa hiyo, tunaomba sana na Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja Mafia, tukakwambia hili jambo, ukasema utalitilia kipaumbele. Nimejaribu kuangalia kwenye kitabu hiki, sijaona uwekaji wa taa na utanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia. Naomba sana wakati unakuja kuhitimisha hoja yako utuelezee mikakati ya kuhakikisha kwamba Uwanja wa Ndege wa Mafia unawekwa taa na unaongezwa ukubwa ili kuongeza fursa za kitalii pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, wiki mbili zilizopita nilileta swali hapa...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.