Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo langu la Kigoma Kusini naomba nichangie Wizara hii nyeti yenye masuala ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza niipongeze Wizara hii chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa pamoja na Naibu wake, lakini pia niwapongeze watendaji wote wa Wizara hii, kwa kweli kwa Jimbo langu mimi la Kigoma Kusini Wizara hii imetutendea mema mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nianze kuzungumzia barabara ya Simbo – Kalya. Barabara hii ya Simbo – Kalya kwa muda mrefu sasa inatengenezwa kwa kiwango cha changarawe. Sasa tulikuwa tuna ombi, kwanini Wizara isifike sasa mahali ikaona namna gani inaweza ili ikafanya kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami ili kuondoa usumbufu wa kufanya maintenance ya mara kwa mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba pia nizungumzie kipande cha barabara kutoka Uvinza kwenda Malagarasi kilometa 51.1. Barabara hii ina muda mrefu sana, hawamalizii kile kiwango cha lami kinachokwenda kuunga mpaka Malagarasi. Nimeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri anazungumzia kwamba tunatarajia pesa za wafadhili kama mfuko wa Abudhabi na mifuko mingine. Sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri aone namna ya kutusaidia wananchi wa Uvinza kumalizia hizi kilometa 51.1, na ikizingatiwa kamba barabara hii ni barabara kubwa inayopita Ma-semi trailer yanayobeba mizigo ya kwenda Congo na kwenda Burundi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie vile vile kipande cha kilometa 40 kinachotoka Chagu hadi Kazilambwa. Kipande hiki ni korofi sana wakati wa mvua, na tumekuwa tunaomba hapa, hata bajeti iliyopita nilimuomba sana Mheshimiwa Waziri aone ni jinsi gani wanaweza wakatafuta namna ya kumalizia hizi kilometa 40. Kwa hiyo ninaomba sana Mheshimiwa Waziri utusaidie wana Uvinza namna ya kutumalizia kipande hiki cha Chagu – Kazilambwa Wilaya ya Kaliua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie vile vile barabara ya kutoka Uvinza kwenda Mpanda ambayo tuna kilometa kama 60 zinazokwenda Mishamo. Sisi tunacho kijiji kinaitwa kijiji cha Ubanda. Wananchi wa kijiji cha Ubanda wanatoka kata ya Kalya hawawezi kusafiri kwa njia yoyote zaidi ya kutumia hii barabara ya Mpanda. Kwa hiyo, tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri aone namna ya kuangalia hizi barabara za vijijini, hali ya huko vijijini si nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba atumalizie hicho kipande cha kilometa 60, na ikiwezekana basi waweze kuanza ujenzi wa hizi kilometa 35 kama alivyotenga kwenye kitabu chake, kwenye taarifa yake hii ya bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie masuala ya uchukuzi. Jimbo langu nina vijiji kama 33 viko Ukanda wa Ziwa Tanganyika. Nimeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri amezungumzia ujenzi wa gati tatu; gati ya Sibwesa, gati ya Lagosa na gati ya Kalya; na amesema kwamba gati ya Sibwesa na gati ya Lagosa ujenzi umekemilika kwa asilimia 50. Mheshimiwa Waziri mimi nikuombe sana, nimeshaomba sana hapa, nimeomba kwenye bajeti iliyopita lakini nimeomba pia katika maswali ya nyongeza. Wananchi wa Ukanda huu wa Ziwa Tanganyika wanapata tabu mno. Usafiri wanaotumia ni meli ya Liemba, hatuna gati hata moja inayofanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna gati ambayo ilitakiwa ijengwe, hiyo ya Kalya, Sibwesa, gati ya Mgambo, gati ya Lagosa na gati ya Kirando, hakuna iliyokamilika hata moja tangu uhuru, miaka 56. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, nilikuwa napitia kwenye kitabu chako nimeona baadhi ya maeneo wana magati matatu, wana magati manne; nini tatizo kwenye Jimbo la Kigoma Kusini kutupa hata gati tatu zikamilike ili meli ya Liemba iweze kupata maeneo ya kuegesha na abiria wapate kutoka kwenye usumbufu?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie Daraja la Ilagala. Tumekuwa tunapata shida sana na Daraja la Ilagala na Mheshimiwa Waziri umetuahidi kwamba Wizara yako inafanya mkakati wa kutujengea daraja la muda mfupi ili wananchi pamoja na magari waweze kuvuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mimi ni mkazi wa Kigamboni. Sambamba na daraja langu la Ilagala naomba pia nizungumzie Daraja la Nyerere – Kigamboni. Tuna kilometa
3.8 kutoka Tungi kwenda Kibada; hivi karibuni tumekwama pale siku tatu tunashindwa kufika kwenye daraja kwa sababu ya mvua nyingi zinazonyesha pale Kigamboni. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri, maadamu umezungumzia kwamba kuna pesa zimetengwa za kujenga hizi kilometa 3.8 kutoka Tungi kwenda Kibada tunaomba basi uweze kutekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nitoe pongezi kwa Serikali kwa ujenzi wa meli mpya ambayo inatarajia kuanza hivi karibuni, ambayo itakuwa inabeba abiria pamoja na mizigo kwenye Ziwa Tanganyika; natoa pongezi sana, lakini pia natoa pongezi kwa ukarabati wa meli ya Liemba ambapo wote tunajua hii meli ya Liemba kihistoria ni meli ya Wajerumani na nimeona kwamba Mheshimiwa Waziri anasema wanataraji kusaini mkataba hivi karibuni ili maintenance hiyo iweze kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo naomba pia nitoe pongezi kwa Serikali kwa ununuzi wa ndege mbili. Wananchi wa Kigoma tulikuwa tunapata taabu sana na usafiri, lakini tangu Mheshimiwa Rais, amenunua hizo ndege mbili kwa kweli wananchi wa Kigoma tunamshukuru sana tena sana kwa kuturahisishia usafiri wa Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo naomba pia nizungumzie ujenzi au upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma. Mheshimiwa Waziri unakumbuka mwaka jana kulikuwa na mvutano wa wananchi wa Kibirizi na wananchi wa maeneo ya jirani ya uwanja wa ndege. Sasa tulikuwa tunaomba basi upanuzi uanze mara moja ili kuondoa ile kizungumkuti, kulikoni Serikali imelipa fidia wananchi lakini hakuna lolote linaloendelea la kupanua uwanja wa ndege wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nizungumzie reli. Kwa sababu ujenzi wa reli hii ya standard gauge inapita pia kwenye Jimbo langu kwa maana Uvinza kwenda Msongati, Mpanda mpaka Karema. Hizo kilometa 150 ambazo mpo katika hatua ya kufanya upembuzi yakinifu, Mheshimiwa Waziri mimi nipongeze sana kwa jitihada hizo. Lakini pia nipongeze jitihada za reli yetu ya kati ambayo inatoka Kaliua
- Mpanda - Tabora – Kigoma kilometa 411; nipongeze pia kwani hiyo pia ni jitihada nzuri kwa sisi wananchi tunaotumia reli ya kati.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: ahsante sana.