Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa utendaji huu mzuri uliotukuka, naomba tuwapongeze sana. Naomba nichukue fursa hii
kumpongeza sana kaka yangu Profesa Mbarawa pamoja na Naibu wake Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii, pamoja na watendaji wote wa Wizara yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze sasa katika mchango wangu, nitaanza na barabara ya kutoka Kinyarambo A - Salavanu – Saadani - Madibila – Rujewa. Barabara hii inaunganisha Wilaya mbili, barabara hii inaunganisha mikoa miwili na inaunganisha Wilaya ya Mufindi na Wilaya ya Rujewa, Mkoa wa Iringa na Mkoa wa Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kama tulivyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 2000, kwamba itajengwa kiwango cha lami, 2005 itajengwa kwa kiwango cha lami, 2010 itajengwa kwa kiwango cha lami, na 2015 itajengwa kwa kiwango cha lami; lakini hizo ahadi zimekuwa hewa mpaka leo hakuna hata kilometa moja iliyojengwa kwa kiwango cha lami, katika barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ikijengwa itasaidia kwa kiwango kikubwa sana kukuza uchumi katika eneo hili na barabara hii ni shortcut ya barabara ya kutoka Mbeya itapunguza zaidi ya kilometa 60, hii ni manufaa makubwa sana katika uchumi huu. Kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake atueleze sababu zipi zimepelekea barabara hii inaonekana kwenye Ilani ya Uchaguzi kwa vipindi vitano, lakini mpaka leo haijajengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, inakuwa vigumu sana kurudi kwa wananchi wetu kuwaambia kwamba mpaka leo hii hatuna hoja za msingi kama watu wa CCM, watu wa Serikali, kwa nini vipindi vitano mfululizo mpaka leo haijajengwa? Naamini kabisa kaka yangu Profesa Mbarawa atakuja kuniambia maneno haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kesi ya pili ninayotaka kuzungumzia ni barabara ya kutoka Mtili – Ifwagi – Mdaburo
– Ihanu – Isipii – Tazara – Mlimba. Barabara hii inaunganisha Wilaya mbili, inaunganisha Wilaya ya Mufindi na Wilaya ya Kilombero, ina urefu wa kilometa 116, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi haina uwezo wa kujenga barabara hii.
Mheshimia Naibu Spika, katika vikao vyetu vya mwaka 2013, 2014 na 2015 tulipitisha katika Wakala wa Barabara wa Mkoa wa Iringa na Mheshimiwa Rais ambaye alikuwa Waziri wakati uliopita alikubali kupeleka wataalam kwa ajili ya kufanya utafiti kuona kama ina hadhi ya kupandishwa kuwa barabara ya TANROADS, lakini mpaka leo hii Mheshimiwa Waziri hawajaleta wataalam wa aina yoyote katika hili eneo. Namuomba sana kaka yangu atakapo kuja atuambie ni lini atatuletea hao wataalam kwa ajili ya kuja kufanya upembuzi yakinifu na barabara hiyo iweze kupandishwa kiwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala la barabara kutoka Jets corner - Kibao mpaka Mgololo, barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya ya Mufindi na uchumi wa Mkoa wa Iringa kwa ujumla. Eneo hili lina viwanda vingi vya mbao pamoja na chai, lakini ni muda mrefu hakuna hata kilomita moja ya barabara ya lami iliyojengwa katika eneo hili, ukichukulia kuna makampuni ambayo yanalipa mabilioni ya pesa kwenye kodi ya Serikali katika nchi hii. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali itupie macho mawili eneo hili kusudi tuweze kupata barabara ya lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la uwanja wa ndege wa Mkoa wa Iringa wa Nduli. Huu uwanja ni muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Iringa ukichukulia Iringa ni sehemu ambayo ina- base kubwa sana ya utalii. Kwenye eneo hili naomba niunganishe na barabara ya Ruaha National Park. Ruaha National Park ni mbuga ya pili kwa ukubwa katika Bara la Afrika, baada ya mbuga ya Kruger ya South Africa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuna haja ya kuukuza uchumi wa nchi hii katika eneo la Ruaha National Park kwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami. Kuna watalii wengi sana wanapenda kutembelea katika maeneo haya, lakini tatizo kubwa linakuwa hatuna barabara ya lami na hakuna uhakika wa kufikika kwenye hili eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama barabara hii itapata kiwango cha lami nina uhakika kabisa ile mbuga ya Kruger haina sifa ambazo Ruaha National Park inazo. Automatically Ruaha National Park inaweza kuwa mbuga ya namba one kwa ukubwa katika Bara la Afrika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana kaka yangu Profesa Mbarawa kwa kufungua kituo cha reli pale Mpanga Tazara ambacho kilikuwa kimefungwa, sasa hivi kinafanya kazi. Ninachomuomba ndugu yangu wakifanyie ukarabati kile kituo cha reli pamoja na kukifanyia ukarabati kituo kidogo cha pale Kimbwe kusudi wananchi katika eneo hili waendelee kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa Sheria za Barabara zifanye kazi, kwa sababu uharibifu mwingi unatokana kwa sababu zile sheria watu hawaziangalii, watu wanaharibikiwa magari yao, wanaacha magogo matokeo yake barabara zinaendelea kuharibika; hata ile dhana bora ya kutaka tupate barabara nzuri katika nchi hii inakuwa haina maana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye masuala ya mawasiliano, kuna maeneo matatu ni muhimu sana katika Jimbo langu ya Mufindi Kaskazini. Eneo la kwanza ni eneo la Ikwera, tayari mnara umeishajengwa, lakini kwa masikitiko makubwa huu mwezi wa sita sasa hivi ule mnara haufanyi kazi. Eneo la Mapanda mnara umeishajengwa lakini kwa masikitiko makubwa mpaka sasa hivi mnara haufanyi kazi. Eneo la Isipii mnara umeishajengwa lakini kwa masikitiko makubwa mpaka sasa hivi minara haifanyi kazi.
Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba utakapokuja kuhitimisha bajeti yako, utuambie kwa nini mpaka leo minara hii haifanyi kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache naomba niunge mkono hoja.