Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipatia nafasi hii nami nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii au hoja tuliyonayo mezani. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba nilikuwa na afya iliyotetereka kwa takriban miezi sita iliyopita, lakini sasa naendelea vizuri na ndiyo maana nimeweza kusimama kwenye Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze moja kwa moja kwenye barabara za Jimbo la Vunjo. Mwaka 2016 Mheshimiwa Waziri aliniahidi kuhusu barabara ya Kawawa - Nduoni mpaka Marangu Mtoni. Barabara hii ina kilometa 29, imeshajengwa zaidi ya nusu kwa upande wa Kawawa –
Nduwoni kuna bado kilometa 4.8 na mwaka 2016 mliahidi kwamba kilometa hizo zitaingizwa kwenye Bajeti ya mwaka huu. Kwa bahati mbaya sana hizo kilometa 4.8 nimejaribu kukagua kila mahali japo sikuwa kwenye Kamati, mpaka sasa hazikuweza kuingizwa kwenye Bajeti ya mwaka huu. Naomba majibu sahihi, ahadi ya Mheshimiwa Waziri hii itatekelezwa vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya Kilema Road kwenda Hospitali, tunashukuru angalau zile kilometa mbili zimejengwa lakini hazijakamilika vizuri, ambapo zilikuwa ni eneo korofi sana. Ahadi ya Rais wakati wa uchaguzi aliahidi kwamba barabara ya Kilema kilometa 13 itajengwa yote kwa lami na siyo eneo lile ambalo ni korofi tu. Pia barabara ya Mabogini kwenda Kahe mpaka kutokea Chekereni ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Barabara za Himo Mjini ni ahadi za Mheshimiwa Rais, kwamba zote zitajengwa ili Mji Mdogo wa Himo uweze kufanana na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 nilishauri, maeneo yenye milima au maeneo yenye miinuko kwa mfano Mkoa wa Kilimanjaro, barabara zinajengwa lakini sehemu ya kutolea maji (drainage system) na maji ni adui mkubwa wa barabara. Namna gani Wizara yake na Serikali za Mitaa wanashirikiana pamoja ili Serikali za Vijiji wawe wanasafisha hiyo mitaro mara kwa mara? Kwa sababu wasipofanya hivyo, hili jukumu la Serikali Kuu, hawawezi kutekeleza wao wenyewe na mkikaa pamoja, tukishirikiana pamoja na Serikali za Mitaa wakahimiza hasa vijijini ili isafishwe hii mitaro barabara zitadumu zaidi, kwa sababu maji ni adui mkubwa wa barabara na uharibifu huu wa barabara kwa kiasi kikubwa tunazungumzia ujenzi wa barabara kitaalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumzia vizuri Mbunge aliyemaliza sasa hivi, Mheshimiwa Chenge. Ni namna gani tunafanya maintenance ya barabara? Namna gani kwenye mikataba yetu tuna-include local component capacity basic ya Wahandisi wetu ili hawa wakubwa wakishaondoka waweze ku-maintain barabara hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mikubwa kwa mfano ya reli ya kati ni namna gani tunaweka Wahandisi local component tuwanjengee uwezo wale wakiondoka waweze ku-maintain barabara hizo? Namna gani tunaiwezesha TANROADs? Nawapongeza sana TANROADs kwa kazi kubwa wanayofanya na hasa Mkoa wa Kilimanjaro, nawapongeza kweli kweli, wanafanya kazi nzuri ya kitaalam na ya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Engineer wa TANROAD wa Mkoa wa Kilimanjaro na timu yake anafanya kazi nzuri na Ma-engineer wote kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Ni namna gani tunawawezesha, tunawapa capacity ya kutosha ili waweze kuhakikisha miundombinu hii inaendelea kuwepo? Ni namna gani sasa hivi tunajenga reli ya standard gauge? Ni namna gani tunaandaa wafanyabiashara na namna gani ya kupitisha mizigo kwenye reli ukilinganisha na kwenye barabara, kwa sababu uharibifu wa barabara hizi ambazo zimefunguka karibu nchi nzima, uharibifu wake unakwenda kwa kasi kubwa? Angalia mvua zilivyonyesha sasa hivi barabara zinavyoharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la environmental impact assessment ambalo kwa kiasi kikubwa nimeisoma kwenye hoja ya Mheshimiwa Waziri, sioni likiwekewa kipaumbele cha kutosha. Nitatoa Mfano ili nieleweke. Ukiangalia upanuzi wa Airport ya Dodoma, suala la environmental impact assessment lilizingatiwa kiasi gani? Angalia uharibifu mkubwa uliotokea kwa binadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mwingine nieleweke. Barabara inayopita Serengeti iliyokuwa ijengwe, dunia ilipiga kelele kuhusu kusumbua wanyama wa Serengeti. Je, usumbufu wa binadamu ukoje? Miundombinu sawa ijengwe vizuri, lakini suala la kukuza utu na kuzingatia maadili ya uharibifu wa mazingira nao upewe kipaumbele cha kutosha, ambapo nikiangalia kwenye hoja ya Mheshimiwa Waziri, sioni suala la environmental impact assessment na mitigation missions zake ziko kubwa kiasi gani? Au utazingatiwa kiasi gani ili miundombinu hii iendane sambamba na inclusiveness ya wote ambao ni watumiaji wa barabara hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za Taifa letu la Tanzania, zipo kwenye classification mbalimbali zikiwepo barabara za Mkoa wa Kilimanjaro. Tusipozingatia kilimo cha matuta katika Mkoa wa Kilimanjaro, uharibifu wa udongo wakati wa mmomonyoko ambao ukija kwenye barabara unaharibu barabara hizo. Sasa ni namna gani sheria zetu, kanuni, tamaduni na mila zetu zinaweza kulinda barabara hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipoweza kuzingatia tamaduni, tukawa ni copy and paste ilimradi tumeona mradi fulani huko Ujerumani au huko Japan tukauleta hapa kwetu, wakati component ya maintenance na kutunza miundombinu hii hatujaizingatia vya kutosha, tutapata matatizo makubwa sana mbele ya safari. Tutakuwa na miundombinu ambayo iko kwenye class A, lakini namna gani ya kui-maintan ibaki class A itakuwa ni shida ili ile ya class B iende kwenye class A, class C iweze ikafanya hivyo, lakini hapo unaweza kukuta ule uelewa wa ujenzi wa miundombinu tunaendelea kusema, hii ndio class E iende class A, wakati ya class A bado inaendelea kuwa na uharibifu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, angalia barabara inayotoka Morogoro kuja Dodoma, barabara zinazotoka Dar es Salaam kuja Dodoma, angalia barabara sasa zinazojengwa za Dar es Salaam ambayo ni maendeleo mazuri tu, lakini ni namna gani ya kuhifadhi barabara hizo, namna gani ya kuzingatia wale wote ambao watatumia barabara hiyo? Ninachozungumzia hapa, narudi kwenye central education; elimu kwa matumizi ya barabara, elimu kwa matengenezo ya barabara, elimu kwa ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, angalia uwanja wa Airport. Nitatoa mfano nieleweke vizuri. Ukiangalia Airport ya Amsterdam, ndege zote zinazoruka pale, wakazi wa Aalsmeer wote imebidi wapewe compensation ya kutosha na ujenzi wa nyumba zao za sasa hivi lazima uzingatie masuala ya sound proof ili waweze kuishi vizuri katika nyumba hizo. La sivyo, miaka 10 mpaka 20 ijayo, japo tunazingatia kwenye miundombinu, tusipofikiri kwa mapana kitaalam, tutapata shida kwa ajili ya kutokutoa haki kwa uhalisia wa binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujue leo hii duniani, uharibifu mkubwa zaidi ya asilimia 96 unafanywa na binadamu. Sasa kama unafanywa na binadamu, zile known-known risk, know- unknown risk and unknown-unknown risk ambazo ni act of God; lakini kuna nyingi hapa ambazo tunasema ni act of God while is not an act of God! Ni uzembe wetu tu sisi binadamu, ndiyo tunaosababisha mambo ya mafuriko, hatuna mitaro mizuri na matatizo mengine. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri lakini namwomba, chonde chonde!
Mheshimiwa Naibu Spika, nihitimishe kwa kusema tena kwamba barabara za Bunju ambazo Mheshimiwa Waziri aliahidi mwaka 2016 ahakikishe zinapewa kipaumbele ili tuweze tukazungumza vizuri na ukizingatia kwamba mimi ni Shadow Minister wa Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu akubariki, ahsante sana.