Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
Ex-Officio
Constituent
None
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu anayetuwezesha Wabunge kutekeleza majukumu yetu hapa kama ambavyo tunamuomba kila siku wakati wa dua. Baada ya kusema hayo pia niseme moja kwa moja kwamba niwapongeze Waheshimiwa Wabunge ambao kwa kutumia haki zao za Kikatiba wameamua kuchangia uboreshaji wa Mpango huu wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano ambao ni Mpango halali Kikatiba na kisheria.
Ninaunga mkono moja kwa moja hoja hii ya Mpango huu wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kutoa ufafanuzi na kushauri baadhi ya maeneo ya Kikatiba na kisheria ambayo yameguswa wakati Waheshimiwa Wabunge wakichangia hapa Bungeni. Moja ni hoja ya kwamba ilipaswa Mpango huu uletwe pamoja na Muswada wa sheria. Naomba kushauri kweli kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63(3)(c), inaeleza kwamba Bunge hili litajadili mpango wa muda mrefu au wa muda mfupi na kutunga sheria, lakini pia Ibara hiyo 63(3)(d) inaelekeza juu ya kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kutungwa kwa sheria. Kwa hiyo Ibara hizi lazima zisomwe zote pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme hivi, tayari ipo sheria mahsusi ya kusimamia utekelezaji wa mpango, uwe wa muda mrefu au wa muda mfupi, na hii ni Sheria ya Tume ya Mipango ya mwaka 1989. Ukisoma ile Sheria Kifungu cha 5 kinachoelezea ile kazi ndiyo unaona sasa kazi ya Tume ya kusimamia utekelezaji, vipimo, ile monitoring and evaluation hiyo ni sheria ya jumla inayosimamia utekelezaji wa mpango wowote ule, uwe wa muda mrefu au wa muda mfupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 tuliyoipitisha Waheshimiwa Wabunge hapa, ukisoma vifungu, kuanzia kifungu cha 7, kifungu cha 8, 9, 11, 13, 15, 19, 21, 20 na 26 na 32 vinaeleza vizuri. Lakini zaidi ya hizi sheria Bunge lenyewe kwa mujibu wa Katiba limepewa mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa Mpango wowote ule ni wakati huo linapojadili bajeti kwa kipindi kama hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hakukuwa na sababu ya kuja na Muswada wa sheria mahsusi wakati unapoleta mpango hapa, kwa sababu hata Mpango wenyewe haujapitishwa sasa utauleteaje na Muswada wa sheria? zaidi ya hizi Sheria zipo sheria hii ya bajeti imetaja vizuri katika vifungu nilivyovisema.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huu wa miaka mitanp una nyumbuliwa katika Mpango wa mwaka mmoja mmoja na Mpango wa mwaka mmoja mmoja huu ndiyo unatengenezewa bajeti na ili Mpango huu upitishwe, ili utekelezwe ndiyo unatungiwa sheria ya Finance Act. Lakini pia unatungiwa Sheria ya Appropriation Act na Sheria nyinginezo. Zaidi ya hapo Mpango huu unatekelezwa kwa kusimamiwa na sheria mbalimbali za kisekta.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wenyewe maana yake ni nini? Mpango ni mkakati wa Kikatiba na kisheria wa kukuza uchumi na mapato ya Serikali kwa ajili ya kuleta Maendeleo ya Wananchi. Kwa sababu hiyo, zipo na sheria mbalimbali nyingine za kisekta ambazo zinasimamia utekelezaji wa Mpango. Kwa hiyo hakukuwa na sababu ya kuleta muswada mahususi kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nizungumze juu ya Zanzibar, Uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika kwa amani na kuwepo kwa majeshi Zanzibar, suala la ulinzi na usalama ni la Muungano. Kwa hiyo, Majeshi yaliyopo Zanzibar yalisimamia amani na utengemano Zanzibar, kwa sababu ni suala la Muungano siyo kwamba watu wamepelekwa tu kule na ndiyo maana uchaguzi ukafanyika kwa amani na utengamano. Mkuu wa Mkoa wa Pemba aliyetoa maagizo yale aliyatoa kihalali pia chini ya Sheria ya National Security Council. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Waheshimiwa Wabunge, wamezungumza juu ya kufanyiwa ukaguzi juu ya Deni la Taifa, hii ni mamlaka ya wazi kabisa ya Control And Auditor General iko pale hawezi kuzuiliwa hiyo haikupaswa kuletwa hata kuzungumziwa humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie kuhusu Mheshimiwa Rais. Ukisoma Ibara ya 35 wamezungumza juu ya Good Governance ya utendaji wa Rais. Ibara ya 35 ya Katiba inasema hivi shughuli zote za utendaji katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitatekelezwa na watumishi wa Serikali kwa niaba ya Rais. Ibara ya 36 inampa Rais kuteua viongozi hawa wote na kusimamia hata nidhamu yao hata kama kuna mamlaka nyingine imesema nidhamu yao itasimamiwa na mamlaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma Ibara 36(4) haimnyimi Rais kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wanaokiuka maadili yao. Kwa hiyo, haya ndiyo ambayo wananchi wanataka. Kama sisi watumishi wa umma wajibu wetu ndiyo tunatekeleza majukumu yetu kwa niaba ya Rais, Rais hayuko tayari kuangushwa na watumishi ambao hawafanyikazi kwa kuzingatia sheria. anachokifanya Rais anamsimamisha hata kukiwa na tuhuma ya hadharani kama ya juzi hakumfukuza moja kwa moja, alisema asimamishwe akachunguzwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa kuchunguzwa mtu anaweza akajitetea hajachukua nafasi ya mtu kwamba labda anaingilia nafasi ya mtu yeyote, vyovyote vile mtu anaweza akaenda Mahakamani. Kwa hiyo, niliona niyaseme hayo kwa sababu ya muda mfupi ulionipatia lakini pia ningechukua nafasi hiiā¦
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, basi naunga mkono hoja.