Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami kwa moyo mkunjufu, napongeza kwanza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa yale mambo mazuri ambayo yameandikwa na tumeendelea kuyasisitiza, Serikali myachukue myafanyie kazi maana kazi yetu ni kuwashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napongeza Majiji yote na Halmashauri zote zinazoongozwa na Upinzani. Mbali ya ufinyu wa fedha lakini wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana na hiyo inaonesha ni namna gani Watanzania hawakukosea kutupa kura na tunawahakikishia wakiendelea kutupa kura, haya mambo ya kuwaza mawasiliano ya simu, hakuna. Sisi tutawaza flyovers zenye nafasi na underground. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, sasa naomba niende katika Jimbo langu la Bunda. Kwanza, natambua kazi nzuri ambayo inafanywa na TANROADs Mkoa wa Mara, lakini pia nashukuru kwa baadhi ya barabara kwenye Jimbo langu ambalo tayari zimeshapandishwa hadhi, ila tu Mheshimiwa Waziri najua yeye ni mchapakazi na alikuja Bunda. Kuna barabara ambazo hazijapandishwa hadhi katika mwaka huu wa fedha, please, naomba mwakani ziangaliwe ziweze kupandishwa hadhi. Naomba sana, kwa sababu bado Halmashauri yetu ni changa, inahitaji kulelewa na inahitaji support yenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hiyo ni Sazira – Misisi – Kitaramanka, barabara ya Bitaraguru – Kiwasi na barabara nyingine zote hizo tunahitaji zipandishwe hadhi ili ziweze kupitika ili akinamama wanapokwenda kujifungua waweze kupita katika miundombinu iliyo salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie Mfuko wa Barabara. Katika Mamlaka ya Mji wa Bunda, mwaka 2016 tulitengewa shilingi milioni 710 mpaka sasa hivi zilizofika ni shilingi milioni 73 tu. Shilingi milioni 700 ndizo zilizokuwa zimetengwa, zilizofika ni shilingi milioni 73, tutazifanyia nini jamani?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni asilimia ngapi hiyo? Kumi kati ya 100! Please! Halmashauri yetu ya Bunda ni changa; na ukizingatia kwenye hizi Halmashauri, vyanzo vya mapato Serikali Kuu mmevichukua ambavyo vingesaidia hizi Halmashauri changa kujitahidi angalau basi kukarabati hizi barabara. Hamkuleta pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, TANROADs Mkoa wa Mara na wenyewe ni kilio. Mkoa wa Mara barabara zinazokarabatiwa sasa hivi ni vyanzo vya ndani. Kwenye RCC iliyopita, mpaka tuliunda Kamati ndogo kuja Wizarani kudai pesa. Miaka mitatu mfululizo mnachelewa kutupa pesa, Mkoa wa Mara tumewakosea nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nazungumzia Majimbo yote; na huu mkoa una historia katika kutafuta uhuru wa nchi yetu. Mara unazungumzia Baba wa Taifa, lakini leo hii Mkoa wa Mara, Makao Makuu ya Mkoa tukizungumza Uwanja wa Ndege, mara mnauweka katika ujenzi wa kiwango cha lami, mara mnautoa. Tatizo liko wapi? Please, tunaomba Uwanja wa Ndege wa Musoma ujengwe kwa kiwango cha lami, biashara ya kuuweka na kuutoa na kuanza kuukarabati kwa kiwango cha changarawe tumechoka. Mara ndege zinakuja, mara zinasimamishwa kwa sababu ya uwanja mbovu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa alianza kuusema Veda one, Veda two karudi. Sasa akaja tena Nyerere One; sasa sijui akirudi tena Nyerere two, ataendelea kuongelea huu uwanja!
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunazungumzia barabara ya Kisolya – Bunda – Nyamswa; barabara ya Nata ambayo inatokea Musoma Vijijini kwenda Serengeti, barabara ya Tarime – Mtomara mpaka Ngorongoro; lakini pia tunataka hizi barabara ambazo zinaenda katika mbuga zetu, kama kweli utalii ndiyo unaongoza katika pato la Taifa, kwa nini sasa tusitengeneza barabara ambazo zinaenda katika hizi mbuga zetu ili watalii waongezeke, Serikali iendelee kupata mapato tuweze kufanya mambo mengine? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa pia nimeona kwenye kitabu chako, nakupa hongera, barabara ya Tanga – Saadani – Bagamoyo, isiishie kutengewa fedha, zijengwe kwa kiwango cha lami. Barabara ya kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park, kutoka pale Tarangire, zote hizo ziwekwe lami ili utalii wetu ukue.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nizungumzie tu barabara ya Iringa kwenda Ruaha, zaidi ya kilometa 120, leo hii watu wanashindwa kwenda kule. Mvua ikinyesha wanatumia zaidi ya saa manne na hii Mbuga ya Ruaha ndiyo mbuga ya kwanza Afrika Mashariki kwa ukubwa na ina wanyama wengi. Kwa Afrika ni mbuga ya pili kwa ukubwa, lakini ni miongoni mwa mbuga tano zinazochangia mapato ya Serikali. Sasa kwa nini tunashindwa kuweka lami kwenye hizi barabara ambazo zinaenda katika mbuga zetu ili kukuza utalii wetu? Hilo pia ni jambo la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie fidia ya barabara ya kutoka Mwanza kwenda Musoma. Katika kipande cha Jimbo langu wananchi wamedai fidia kwa muda mrefu katika kupisha ule ujenzi na tena barabara ndiyo ilifuata nyumba za wananchi, siyo wananchi walifuata barabara, watalipwa lini? Hapa pia nimetumwa na mpiga kura senior, baba yangu Mzee Wasira, ana nyumba yake pale Manyamanyama, mlipeni. Lini sasa mtawalipa hawa watu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ukarabati wa hii barabara unaendelea, imekwisha, haijakamilika, tayari barabara zimeanza kuharibika. Hivi hawa Wakandarasi mnaowapa tender mnatumia vigezo gani? Kabla tu barabara haijakabidhiwa, tayari kuna mashimo kama mahandaki. Juzi niliuliza swali, hii barabara ya Dodoma, hapa Dodoma Waheshimiwa Wabunge wenyewe mnajua katika maeneo yetu, kila siku zinakarabatiwa. Kule Ununio, barabara ile ya Mbagala kule Dar es Salaam na yenyewe hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuone ni namna gani hawa Wakandarasi wetu wanajenga barabara zenye viwango! Hilo ni jambo la msingi sana Mheshimiwa Waziri. Kama wanashindwa kazi, washughulikieni. Siyo kwamba Wakandarasi wanachezea tu Serikali; mmewapa tender, hawafanyi kazi kama vile ambavyo inatakiwa na fedha za Serikali zinaenda bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni madeni ya Wakandarasi. Barabara nyingi zimesimama kwa sababu Serikali hamjalipa Wakandarasi fedha. Naomba sana… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri achukue, alikuja Bunda, tunahitaji Mkoa wa Mara tupate fedha za kutosha… barabara zetu. Ahsante sana.