Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, na kushukuru sana kwa kunipa fursa nichangie na mimi Bajeti ya hii Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na nianze kwa kueleza na kukubaliana kwamba ninaunga mkono hoja zote katika ripoti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye hoja ya suala la Daraja la Kigamboni. Hili mimi nitaendelea tu kulisemea tu sana kwa sababu imekuwa ni changamoto kubwa. Tozo katika Daraja la Kigamboni zimekuwa kero kuliko msaada, gharama zinazotozwa pale kwenye lile daraja ni kubwa kuliko hali halisi ya wananchi wa Kigamboni. Tulitarajia kama ambavyo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati anazindua lile daraja alivyosema, kwamba daraja lile lifungue fursa za kuwasaidia Watanzania, wananchi wakazi wa Kigamboni kubadili mfumo wa maisha yao lakini pia kujipatia fursa za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama wakazi wa Kigamboni bado ni aina ya wananchi ambao wanawaza watoto wao watakula nini, watapata wapi ada ya shule, lakini pia wanawaza hata namna ya kugharamia mavazi ukilinganisha na hali halisi ya uchumi ilivyo leo na ukiangalia hali halisi ya uchumi wa Tanzania, mimi nafikiri bado hatujafikia mahali pa kulipia tozo za huduma muhimu na nyeti kama barabara na madaraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hili naomba kabisa Mheshimiwa Waziri litazamwe upya, ikiwezekana kama iko lazima sana kwa sababu daraja hili limejengwa kwa ubia wa NSSF na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania basi lile eneo la NSSF lifanyiwe utaratibu fedha zile ambazo zilitolewa kama mchango wa NSSF kwenye ujenzi wa lile daraja zilipwe, kwa sababu daraja hili kulingana na jinsi ambavyo nimesoma kwenye hotuba yako itakuwa ni connection ya interchange ile barabara ya haraka ya Chalinze, sasa kama ndivyo je, ni eneo lile tu la kuvuka pale kwenye daraja litakuwa linalipiwa ama na barabara zote za interchange zitakazo unganisha na daraja la Kigamboni zitakuwa zitalipiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama zote zitalipiwa bado tufahamu kabisa kwamba ni changamoto kubwa kwa Watanzania wa sasa hivi na hali ya uchumi ilivyo jamani hatujafika huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie baadhi ya vipaumbele ambavyo vimeoneshwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu eneo la Kigamboni nikianzia na barabara ya Kongowe – Mjimwema – Kivukoni ambayo kulingana na taarifa zilizopo katika kitabu cha Waziri ni ya kilomita 25 na imepangiwa shilingi bilioni 1.290. Mheshimiwa Waziri niombe sana kwamba barabara hii ni muhimu sana kwetu na tangu mwaka jana ilikuwa katika bajeti yako, lakini kwa bahati mbaya nadhani ilipata fedha kidogo mno ambapo utaratibu wa upanuzi ulianzia tu eneo la pale kwa Mwingira mpaka kufika Mji Mwema na imeishia hapo.

Kwa hiyo, nikuombe sana katika bajeti yako ya utusaidie kutengwa fedha za upanuzi wa hiyo barabara kwa sababu ndicho kiunganishi kikubwa cha kutoka eneo la Kivukoni mpaka kwenda kuunganisha na Kongowe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimeona Mheshimiwa Waziri amelitaja daraja la Mzinga, nikuombe sana lile daraja msimu wa mvua tunapata matatizo makubwa sana, na mwaka juzi daraja lile lilikatika kabisa tuliishi kwa msaada wa ujenzi uliofanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Kwa hiyo, nimeona umetenga fedha pia kwa ajili ya daraja hilo, tunaomba pesa hizo zipatikane na hilo daraja lijengwe ili kuweze kuwa na connection baina ya wakazi wa Kigamboni na eneo la Temeke; lakini ukizingatia na hiyo express way ambayo nimeona mnaijenga, nimeona inakwenda mpaka eneo la Mbagala ambayo na amini ile barabara ya Kongowe itakuwa ni feeder road kwenda kwenye hiyo interchange ambayo umeizumzumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye barabara ya Tungi – Kisiwani – Kibada. Mheshimiwa Waziri wakati wa hotuba yako wakati wa uzinduzi wa daraja la Kigamboni kwa maneno yako mwenyewe kabisa ulisema umejipanga na utakwenda kumalizia lile eneo la kilomita 1.5 lililobaki baada ya daraja kwenda mpaka pale kwa Msomali, na ulisema fedha zipo na ujenzi ungekamilika mapema iwezekanavyo. Hata hivyo lile eneo limebaki na sura kama alivyosema Mheshimiwa Shabiby jana, kwamba umevaa koti zuri safi na tai lakini chini umevaa kaptula na makobazi.

Mheshimia Naibu Spika, ukubwa wa barabara inayotoka darajani ni kubwa mno ya njia tatu pande zote mbili lakini inakwenda kuingia katika barabara ndogo halafu mbaya na chafu sana, tena wakati huu wa mvua ukifika eneo lile hata kupita na gari ndogo ni shughuli kubwa na pevu. Kwa hiyo tunaomba kipande hicho cha kilometa 1.5 kimaliziwe kama ambavyo uliahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba hiyo hiyo ya Mheshimiwa Waziri ya siku ya uzinduzi wa daraja la Kigamboni alisema lile eneo la darajani, mpaka pale kwa Msomali kwa maana ya kuunganisha barabara ya Kivukoni kupitia Tungi, Vijibweni mpaka Kibada usanifu umeshakamilika na barabara ile ilipaswa kuanza, ujenzi ungeanza Mei 2016 lakini mpaka ninavyozungumza leo hakuna kinachoendelea eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sielewi kilichotokea yawezekana ni ufinyu wa bajeti lakini tunaomba sasa msimu huu kwa maana bajeti hii inayokuja mtusaidie eneo lile liweze kukamilika na barabara ile ikamilike kwa sababu ndio barabaara ambayo ina wasaidia wananchi wengi wa kazi ya maeneo ya Kisarawe II, kata za Kibada, Mji Mwema kupita kwa ajili ya kuja kukutana na eneo la daraja la kuvuka kuja mjini. Barabara ile ya sehemu ile ni mbaya sana na kisehemu cha lami kilichojengwa kuanzia Tungi mpaka Vijibweni karibu kuelekea hospitali eneo limeshaharibika kabisa lina hali mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia nizungumzie au ni muulize Mheshimiwa Waziri atusaidie. Katika bajeti iliyopita ulitupangia fedha kwa ajili ya barabara ya Kibada - Mwasonga kuelekea Tundwi Songani. Najua unaufahamu umuhimu wa barabara hii, ndiyo barabara ambayo magari makubwa sana ya yanayotoka Kimbiji kuelekea Kiwanda cha Saruji cha Nyati yanakopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile kwa kweli imepata uharibifu mkubwa sana kutokana na matumizi makubwa ya yale maroli na kwa hiyo wananchi wa kawaida na usafirishaji wa kawaida unashindwa kuendelea kabisa katika eneo lile kwa sababu mara nyingi yale magari yanapoharibika au yanapokwama katika barabara ile wakazi wanashindwa kuendelea na maisha yao ya kawaida. Kwa hiyo, sasa sielewi imekuaje kwamba barabara hii ya Kibada – Mwasonga – Tundwi kuelekea Kimbiji haijatengewa fedha msimu huu wala haujaizungumzia wakati 2016/2017 ilikuwepo kwenye bajeti yako Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia nizungumzia barabara ambayo nimeona umeizungumzia katika kitabu chako ukurasa wa 35, barabara ya bandari ambyayo ni ya kilomita 1.2 lakini barabara ya Mivinjeni kilometa moja na Dock Yard kilometa 0.7. Barabara ile Mheshimiwa Waziri nikusihi sana kwamba tungependa itengewe fedha lakini itanuliwe kiasi cha kutosha, kwa sababu msongamano wa yale maroli pale bandarini unatupashida shida sana.

Mheshimiwa Naibu Soika, kweli unafiri ni haraka sana kutoka Kigamboni kwa kuvukwa kwa daraja na kuondoka haraka kufika mjini lakini ukishaondoka darajani tu unakutana na hii barabara ya bandari imejaa foleni ndefu, unakutana na barabara ya Mandela imejaa foleni ndefu, kwa hiyo, shughuli ile inabaki kuendelea kuwa shughuli vilevile. Hata kama kungekuwa na nafuu barabara ya bandari bado utaratibu wa kuegesha magari yale makubwa ni mgumu mno na barabara hii inashindwa kupitika. Kwa hiyo, tunaomba mtusaidie utaratibu wa kutengeneza parking maalum ya yale magari ili barabara zibaki huru zitembee kwenda na kurudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikushukuru sana, nimeona umetenga bajeti yako pia ukurasa wa 214 umetenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa gati ya pale Kivukoni, Kigamboni. Eneo lile nalo ni shida kubwa sana, vivuko vile tunashukuru vinafanya kazi na vinatusaidia sana kwa sababu sisi kwa bahati mbaya tumejikuta na hilo janga la kujikuta barabara kwa maana ya daraja tunalipia na kivuko tunalipia, hewala kama ndivyo ilivyowapendeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikuombe basi mtusaidie sana Bajeti hii fedha za utanuzi wa gati pale zipatikane kwa sababu hata kama pantoni imefika imetia dock pale utaratibu wa utokaji wa magari unakuwa taratibu mno kwa sababu eneo ni finyu mno. Kwa hiyo, pantoni kupakia ruti nyingine iende inachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru kwa haya ya leo, ahsante.