Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, 2016/2017 hadi 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi hii ili kuchangia hoja iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango tarehe 20 Aprili, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, kwa kuniamini na kunichagua kuwa Naibu Waziri wa Wizara wa Fedha na Mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda natoa shukrani zangu za dhati kwa wapiga kura wangu wa Jimbo la Kondoa, kwa kuniamini na kunichagua kuwa Mbunge wao. Nawaahidi kwamba sitawaangusha kwa yale yote niliyowaahidi.
Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao walichangia hoja hii kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa Mpango wa kuyafikia malengo tarajiwa. Serikali imepokea ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wote na itaufanyia kazi kadri itakavyoonekana inafaa kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja zilizotolewa ni nyingi lakini nitajikita katika kufafanua baadhi ya hoja hizo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza, uwepo wa vipaumbele vingi na vinavyofanana kwenye Mipango ya Maendeleo tokea uhuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa vipaumbele vingi na vinavyofanana tangia uhuru kumetokana na lengo na nia ya Taifa katika kupunguza umaskini nakufikisha nchi kwenye uchumi wa kati. Hata hivyo Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano umeainisha maeneo manne ya vipaumbele ambayo ni haya yafuatayo:-
(i) Kukuza Maendeleo ya viwanda;
(ii) Maendeleo ya watu na mabadiliko ya jamii; na
(iii) Kujenga mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji katika viwanda pamoja na vile vinavyowezesha utekelezaji wa Mpango wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ilisema Serikali ijikite katika kufadhili miradi ya maendeleo ambayo haiwavutii sekta binafsi kuwekeza. Serikali imedhamiria kutanzua vikwazo vya maendeleo kwa kujenga miundombinu msingi ikiwemo ya nishati, barabara, maji na reli ili kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa sekta binafsi kuwekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu hii ni ya gharama kubwa kama tunavyofahamu na hivyo mara nyingi Serikali inachukua jukumu la kuitekeleza. Mpango wa Kwanza ulianza kutekeleza maeneo haya kama njia muhimu ya kufungua fursa za kiuchumi na Mpango wa Pili unalenga kumalizia pale tulipoishia kwenye Mpango wa Kwanza na kuendelea kutekeleza maeneo mengine manne mapya kama nilivyobainisha hapo juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, bado sekta binafsi ina nafasi pia ya kuweza kushiriki katika uwekezaji huu mkubwa maalum utakaowezesha sekta binafsi na wananchi kufaidika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya tatu ilikuwa Serikali iweke utaratibu mzuri wa kuwaandaa wananchi katika kutumia shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na jinsi ya kurejesha fedha hizo. Baraza la Taifa la Uwezeshaji limepewa jukumu la kuandaa mfumo mahsusi utakaotumika katika kugawa na kusimamia fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za kiuchumi kutegemeana na fursa za vijiji husika. Kazi hiyo inaendelea na kila kijiji kitapatiwa utaratibu na mfumo huo mara utakapokuwa tayari chini ya usimamizi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja namba nne, uchumi unakua lakini maisha ya watu wa kawaida yanazidi kuwa magumu. Sekta zinazochangia kukua kwa uchumi wa Tanzania kwa kiwango kikubwa ni sekta ambazo zinaajiri idadi ndogo ya watu. Baadhi ya sekta hizo ni ujenzi ambao inakua kwa asilimia 15.9; biashara na matengenezo kwa asilimia 10; usafirishaji na uhifadhi mizigo asilimia 12.5 na fedha na bima asilimia 10.8 kwa takwimu za mwaka 2014. Sekta inayoajiri idadi kubwa ya Watanzania ambayo ni kilimo inakua kwa wastani wa asilimia 3.5 kwa mwaka.
Kiwango hiki cha ukuaji wa sekta ya kilimo ni kidogo hivyo hauwezi kupunguza kiwango cha umaskini kwa haraka. Pia katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 iliyopita tuliwekeza zaidi kwenye misingi ya kiuchumi na mazingira rafiki yanayofungua fursa za kiuchumi na kuchochea uwekezaji kama vile elimu na miundombinu ya barabara. Matokeo yanayoakisi uwekezaji huu huonekana baada ya muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba ili kiwango cha umaskini kiweze kupungua kwa kasi wastani wa kiwango cha kukua kwa uchumi katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 kinatakiwa kisiwe chini ya asilimia 10 kwa mwaka. Hivyo basi, wastani wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa asilimia 6.7 kwa mwaka hautoshi kupunguza kiwango cha umaskini kwa haraka kama ambavyo imekuwa ikielezwa na wadau wengi wa maendeleo.
Mwisho, tunapoangalia viashiria vya kupunguza umaskini hatuangalii kimoja tu cha ukuaji wa uchumi. Pamoja na viashiria vingine, tunaangalia pia kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012; kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu ilikuwa ni asilimia 2.7 kwa mwaka. Ukuaji huu wa idadi ya watu ni kubwa na hivyo ni changamoto kwa Taifa hususani pale tunapochukua hatua za kupunguza umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya tano, Serikali haijawahi kufikia lengo la kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani jambo ambalo limeacha miradi mingi kutokamilika kutokana na kutegemea fedha za wahisani ambazo hazitolewi kwa wakati. Katika kipindi chote cha utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo Serikali ilitenga fedha za maendeleo kwa asilimia 27 kwa mwaka ikilinganishwa na lengo la wastani wa asilimia 35 kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa bajeti una changamoto mbalimbali kama tunavyofahamu ikiwa ni pamoja na mapato kuwa chini ya makadirio na sehemu kubwa ya matumizi kuelekezwa kwenye matumizi ya kawaida. Kama Serikali, changamoto hii tumeiona na ndiyo maana kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 tumeamua kuongeza bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 27 hadi asilimia 40. Ni matumaini yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge, mtatuunga mkono uamuzi wetu huu wa Serikali mara tutakapo wasilisha rasmi makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya sita, huduma za masuala ya fedha ni muhimu ziimarike mabenki mengi ya biashara pamoja na Benki ya Kilimo zipo mjini wakati walengwa wako vijiji hakuna huduma. Huduma za mabenki ya kibiashara zimejikita zaidi maeneo ya mjini kufuatia uwepo wa shughuli nyingi za kiuchumi na hivyo kuwa rahisi katika utoaji wa huduma za amana na mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Benki ya Kilimo kilichoanzishwa ni Makao Makuu tu ya benki hii na sasa Serikali inajipanga kuanzisha matawi Mikoani na katika Kanda mbalimbali kulenga wateja walipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya saba, kilimo kufuatia umuhimu wake kiuchumi, kitaifa na maisha ya kaya na mtu mmoja mmoja kingekuwa ni miongoni mwa maeneo ya kipaumbele ya Mpango. Kwa maana nyingine ni kuwa Mpango unapaswa kuwa na mikakati kamili ya kutekeleza azma ya kuendeleza sekta ya kilimo kuliko kuwa na kauli mbiu zisizotekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huu kama ilivyo dhima yake unatilia mkazo maendeleo ya viwanda ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya kipaumbele ya Mpango yamebainisha kwa kuzingatia dhima hii ya mpango yaani kusukuma kasi ya maendeleo ya viwanda kwa maendeleo ya uchumi na maendeleo ya jamii ya Watanzania. Njia pekee ya kufikia azma hii ni kuwa na mfumo wa maendeleo ya viwanda, unaotoa fursa kwa wananchi wengi kushiriki katika maendeleo tarajiwa. Wananchi wengi nchini wanaishi kwa kutegemea kilimo kwa tafsiri pana zikihusisha kilimo cha mazao, ufugaji, misitu na uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya yote yamebainishwa kuwa kama ya kipaumbele katika ukurasa wa 43 hadi 44 kwa kitabu cha Mpango na umuhimu wa kuhusisha kilimo tunafahamu katika maeneo ya kipaumbele umezingatia yafuatayo: -
(i) Fursa kubwa ya maliasili za uzalishaji kwa maendeleo ya kilimo;
(ii) Uwezekano kwa wananchi waliowengi kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kama wazalishaji wa malighafi na upatikanaji wa chakula kwa wafanyakazi wa viwandani na wakazi wa mijini; na
(iii) Kupanua soko la ndani kwa bidhaa za viwandani kama walaji, wazalishaji zana za kilimo na pembejeo na pia kupunguza umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ili kilimo kiweze kuchangia katika uchumi ni lazima tija ya uzalishaji iongezeke na ili uongezeke Mpango umejielekeza katika kuongeza tija ya kilimo kwa mambo yafuatayo:-
(i) Kubadili kilimo kuwa cha kibiashara;
(ii) Upatikanaji wa mitaji;
(iii) Upatikani rahisi na kwa wakati wa pembejeo;
(iv) Kufungamanisha kilimo na sekta ya viwanda ili kuimarisha soko la ndani la bidhaa za kilimo; na
(v) Kuimarisha huduma za utafiti, ugani, na masoko ya mazao yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu wa kipekee niwaombe wadau wote wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, kuendelea kutuunga mkono na kushiriki katika jitihada za kujenga na kuimarisha uchumi wetu. Pamoja na mipango mizuri tulionayo ni dhahiri kuwa maendeleo hayapatikani kirahisi wala siyo ya kwenye makaratasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maendeleo yanahitaji nidhamu katika uwajibikaji kwa kufanyakazi kwa bidii, maarifa, ubunifu na ufanisi katika kufanikisha utekelezaji wa mipango na programu za maendeleo. Tushirikiane sote kwa pamoja katika kutafsiri mapendekezo ya Mpango na bajeti ya Serikali yaliyowasilishwa mbele yetu ili yawe shirikishi na yenye kutekelezeka kwa manufaa ya wananchi wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge ni wadau namba moja katika ufanisi wa utekelezaji wa Mpango huu wa Pili wa maendeleo uliowasilishwa mbele yetu. Tanzania yenye neema inawezekana chini ya Serikali inayoongozwa na Kiongozi shupavu na mwenye uthubutu kama Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu pia maendeleo ni mchakato na tayari tulishaanza mchakato huu tunaomba mtuunge mkono, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais wetu katika utekelezaji wa kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi tu!
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.