Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi nichangie kwenye Wizara hii ya Miundombinu. Naibu Waziri anajua lakini bahati mbaya sana alifika wakati wa kiangazi. Hapa ninaposema, ninaposimama, naogopa hata kwenda Jimboni kwa sababu kuna vilio, kuna vifo, Mheshimiwa Naibu Waziri ile barabara imekatika kabisa. Hata kama ulimuagizia engineer siku ile kwamba ile barabara ipitike mwaka mzima ukimuuliza sasa hivi; kwanza namshukuru Meneja wa Mkoa, yule mama anafanya kazi kubwa sana lakini hela hana. Makandarasi wako kule, lakini kama unavyojua ile barabara ya Jimbo la Mlimba ina mito mingi sana, kwa hiyo kuanzia pale Idete Kalia Gogo mpaka ukifika Taweta, kule karibu na Madeke, Njombe barabara yote inakatika, mkandarasi anahangaika, leo akiziba hapa kesho imekatika hapa mito kila kona. Kwa hiyo, Jimbo la Mlimba linatakiwa litazamwe kipekee kuhusu masuala ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninaposema, sisemi tu kwa kujifurahisha lakini nimeona kwenye kitabu chenu kwamba mnaboresha barabara ya mpaka Madeke - Njombe, mnaposema Madeke, Njombe ndiyo inapakana na Mlimba, na watu wa Njombe wanataka ile barabara iboreshwe na mnajenga kwa kiwango cha lami ili watu wa Njombe wapite Mkoa wa Morogoro waje Dodoma, sasa mtapoboresha kule barabara ya Njombe mpaka Madeke mkiiacha kutoka Madeke - Tanganyika - Taweta hadi Mlimba (Ifakara) mtakuwa hamjaitendea haki thamani ya ile barabara ya Madeke.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninachoomba mnasema iko kwenye upembuzi yakinifu na kweli kabisa lakini kwenye vitabu vyenu haijazungumziwa kabisa hiyo barabara, huo upembuzi yakinifu na wa kina umeisha au vipi? Mnatarajia kujenga kwa kiwango gani? Mnasema kiwango cha lami kuanzia Ifakara mpaka Mlimba, lakini mjue kwamba ili tulinganishe Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe inatakiwa barabara ifike Madeke kule Taweta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi naomba, tumeteseka kiasi cha kutosha miaka mingi tangu uhuru sasa na sisi angalau tufaidi matunda ya uhuru. Tunashangaa tu barabara za wenzetu lami, flyover, ndege, sisi hatutaki hata kuzungumzia ndege, tunataka barabara. TAZARA ipo inapita kule hivi wananchi wa kule wanaponea ki-peace cha kutoka Makambako mpaka Kilombero lakini ki-peace kinapita kwa wiki mara mbili au tatu.

Leo mama mjamzito anayetokea kule Masagati, Taweta, Njombe moyo unaniuma mimi, moyo unalia machozi akina mama wanakufa katika Jimbo la Mlimba, wanataka kujifungua hakuna hospitali ya uhakika, hospitali mpaka iwe Ifakara kilometa 230 hivi huyu mama mjamzito anafikaje kwenye hiyo hospitali? Wote mmezaliwa na wanawake, hebu muwaonee huruma wanawake wanaotokea katika Jimbo la Mlimba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanakufa kule jamani, kwa vile hakuna vyombo vya habari wangekuwa wanaripoti kila siku, lakini tunahangaika tu, hakuna tv nani apeleke tv yake kule sehemu ambayo haina barabara? Kwa hiyo, mimi naomba suala la barabara Mlimba ni kipaumbele. Naomba barabara, Mheshimiwa Naibu Waziri umefika Wananchi wamekushangilia ukamuagiza engineer lakini nakuambia leo hii hata hawa ma- engineer hawana bajeti ya kutosha, kinachotakiwa ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme sasa, kinachotakiwa ni kwamba barabara hii ya kilomita 230 kutoka Ifakara mpaka Madeke, mpakani na Njombe imekatika haina uwezo tena wa kupitika na haijapangiwa pesa za kutosha. Hata kama tunasubiri lami, basi tunaomba ipitike kwa mwaka mzima na nimeongea na wataalam, engineer anasema kwamba ili hii barabara ipitike kwa mwaka mzima inahitaji inyanyuliwe kwa kiwango cha juu sehemu zile korofi kilometa zisizopungua 50 angalau, lakini hela mliyoitenga kwa kukarabati hiyo barabara haisaidii, tutaendelea kuteseka wananchi wa Mlimba. Naomba mtuokoe tumo kwenye shimo, tunaonekana kama hatujapata uhuru ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kuna akina mama, kuna vijana na wazee wanahitaji huduma. Kwa hiyo basi maeneo ambayo barabara imekatika, ukianzia Jimbo la Mlimba utaanza katika kata ya Idete Kalia Gogo. Vilevile kuna maeneo mbalimbali ambayo hii barabara haipitiki, utaenda Idete, Kalia Gogo, Kiogosi, Kisegese, Tandale, Mbingu, Ngajengwa, Njage, Udagaji, Mgugwe, Mlimba Mpanga mpaka Madeke - Njombe, hili eneo lote ninalosema ni barabara ambayo ni ya TANROADS, mnatusaidiaje wananchi wa Mlimba? Hali ni mbaya tunateseka. Kwa hiyo, ni muhimu wakaliangalia kwa jicho la karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, ni Waziri wa kwanza uliyefika kuitembelea ile barabara, basi naomba uitendee haki, naomba tafadhali uitendee haki ile barabara ungepita wakati huu kwanza usingefika ingebidi urudi Ifakara, Mkuu wa Wilaya alikuwa anaenda Mlimba akashindwa akabakia pale Mgugwe maji yamejaa yanakatiza barabara akarudi Ifakara. Ndiyo maana nilikuwa nalalamika haiwezekani Mkurugenzi tumemnunulia V8 halafu gari mnamuachia Mkuu wa Mkoa, hivi huyu Mkurugenzi akitaka kuwahudumia wananchi wa Mlimba ataenda na usafiri gani? (Makofi)

Kwa hiyo tuna umuhimu wa vitu vyetu vibaki Kilombero. Yaani mimi hapa leo nalia na barabara, hela mlizotenga hazitoshi hata kwa haya matengenezo yanatakiwa linyanyuliwe matuta katika eneo korofi ya kilometa 50. Naomba mtutengee hela za kutosha. Ongeeni na wataalam wenu wanajua, na mimi haya nimeyapata kwa wataalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeomba barabara ya kutoka Mlimba, tuna Kata moja ya Uchindile ina mto mkubwa sana, huu Kilombero unaanzia kule, tunaomba ile barabara ichukuliwe na TANROADS sisi hatuna uwezo wa kuunganisha hiyo barabara kama Halmashari kutoka Mlimba mpaka Uchindile. Vilevile kutoka kijiji cha Tanganyika tumeomba mpaka mkoani ile barabara muichukue TANROADS, kuanzia Taweta mpaka Tanganyika kuna mto mkubwa wa Kilombero unakatisha. Kwa hiyo, wananchi wametengwa na kata zao, jimbo la na Mkoa wao. Chonde chonde nawaomba sana mtuangalie na mtupe haya maeneo tuhakikishe kwamba barabara inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini siyo hivyo tu kuna suala la TAZARA. TAZARA mmeandika kidogo sana. Jimbo langu limepitiwa na TAZARA, makao makuu ya TAZARA kiwilaya yako Mlimba, lakini TAZARA hiyo kuna wastaafu wanadai miaka kenda rudi, wengine mpaka wanakufa watoto wameshindwa kusoma, ninyi katika kitabu chenu sijaona mahali popote. Namna gani mnasema tu sasa hivi sijui ngapi, naomba kauli ya Mheshimiwa Waziri wale wastaafu wa TAZARA waliotumikia reli kwa muda mrefu, na watoto wao sasa hivi wanateseka na wenyewe wanateseka ni nini hatima yao nchi hii jamani? Watu waliotumikia kwa moyo mkubwa kwa imani bila wizi kwa nini mnawafanyia hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba muwaokoe wastaafu wa TAZARA. Mheshimiwa Waziri ukija hapa useme kidogo kuhusu wastaafu wa TAZARA, kama ndio wamesahaulika hawawezi kulipwa tena, basi mtuambie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mawasiliano, barabara hakuna simu wengine mpaka wapande juu ya miti, sasa haya mambo gani? Kuna maeneo ambayo huwezi ukapata simu, mimi mwenyewe nikienda Jimboni kipindi fulani utanitafuta hunipati, hakuna mawasiliano ya simu, naomba mtuangalie kwa karibu watu ambao tupo remote area. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mjini mnajenga mpaka ma-flyover nyie nini? Kwa nini wenzenu mmetusahau huko? Mnazungumzia tu viwanja vya ndege sisi havitusaidii. Hivi leo usafiri wa kule ni trekta, namshukuru kijana mmoja anaitwa Muddy Kindindindi wa Ifakara alinunua mabasi yake yanaitwa Muki yakawa yanaenda mpaka Mpanda lakini kutokana na barabara mbovu sasa hivi hayaendi tena, wanasafiri na trekta. Jamani, hivi bado tupo dunia hii ya leo? Mimi naomba Waziri kama ikiwezekana Naibu Waziri umruhusu akimaliza kupitisha hii bajeti twende mimi na yeye tuongozane mpaka kulekule alikofika mwanzoni aone hiyo barabara ndipo atapata uchungu akija ataona kwamba hii hela mliyotenga hapa sio lolote sio chochote. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, naomba tafadhali, hata kama huna mafuta mimi ntawaambia wananchi wa Mlimba wajichangishe tukuletee mafuta twende ukaikague hiyo barabara sasa hivi na watafurahi sana wakikuona. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilio changu ni barabara...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, barabara, Mlimba.