Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kutumia fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniruhusu kusimama hapa ili kuweza kuhitimisha mjadala wa Bunge lako Tukufu kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano kuanzia 2016/2017 mpaka mwaka 2020/2021.
Pili, nikushukuru wewe binafsi, pia Mheshimiwa Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha vizuri majadiliano kuhusu Mpango huu ambao niliuwasilisha tarehe 20 Aprili, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutambua michango iliyotolewa kwanza na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, lakini pia Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, ambaye ni Naibu Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, waliochangia ama kwa kuzungumza au kwa maandishi. Ukiacha Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, jumla ya Wabunge 44 wamechangia hoja yangu ambapo Waheshimiwa Wabunge 34 wamechangia kwa kuzungumza na 10 wamechangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi na kwa niaba ya watumishi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango, tumefurahishwa sana na mjadala juu ya Mpango huu ulivyoendeshwa. Kwa ujumla sisi tunaona kwamba mjadala umechukua mwelekeo wa Tanzania kwanza ambapo hoja nyingi zilizotolewa zilitanguliza zaidi maslahi ya Taifa. Ni matarajio yangu kwamba mwelekeo huu utaendelezwa katika majadiliano yote ya Mkutano huu wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sehemu kubwa michango ilikuwa yenye tija ikilenga kuboresha Mpango wenyewe, lakini pia kulikuwa na michango ya kukosoa ili kujenga (constructive criticism) na mingine ilikuwa ni ya kuomba ufafanuzi ili kuongeza uelewa. Nafikiri huu ndiyo utaratibu ambao Watanzania wangependa kuona ndani ya Bunge lao na nawapongeza kwa dhati na kuwashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wachache ambao walichukua mkondo tofauti na baadhi walichangia kwa jazba. Ninaomba wajiangalie tena na wabadilike na hasa huku tunakoendelea na Bunge hili la Bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba niwashukuru kwa dhati Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa ufafanuzi mzuri wa hoja ambazo zinagusa sekta wanazoziongoza. Nafikiri hii inathibitisha kuwa Serikali yenye dhana ya Hapa Kazi tu inazingatia siyo tu uwajibikaji lakini pia teamwork. Ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nirejee kwa kifupi masuala kadhaa ambayo yalisisitizwa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tumesikia msisitizo mkubwa sana juu ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani na ni kweli hiki ni kipaumbele kikuu cha Serikali ya Awamu ya Tano. Tumesikia mmesisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa mapato, kwamba Serikali ibuni vyanzo vipya na kujumuisha sekta isiyo rasmi katika mfumo wa kodi na tuangalie sekta zinazoibukia. Tumesikia kwamba ipo haja ya kuchukua hatua madhubuti kuziba mianya ya kukwepa kodi na tozo mbalimbali na hasa kwenye sekta ambazo zinakua haraka kama mawasiliano (telecommunications), madini na sekta ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia umuhimu wa kuimarisha matumizi ya vyanzo mbadala vya mapato kama vile hati fungani za miundombinu (local government bonds). Pia ushirikiano wa taasisi za fedha katika kukopesha (loan syndications). Mkazo umewekwa kwenye maeneo ambayo bado tunaweza tukakusanya vizuri zaidi na hasa mapato yanayotokana na rasilimali za nchi yetu, ikiwa ni pamoja na rasilimali za bahari, ardhi, misitu na utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikiliza ushauri kwamba ni lazima sasa zoezi la kutathimini uwezo wa kukopa (credit rating) ili kupanua wigo wa sekta binafsi na Serikali kukopa, hili tumelisikia. Ipo pia haja ya kuboresha baadhi ya sheria ikiwemo ile ya mikopo, dhamana na misaada, namba 30 ya mwaka 1974.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia msisitizo kuhusu umuhimu wa kujenga mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na Waheshimiwa Wabunge wamesisitiza sana tuhakikishe upatikanaji wa malighafi; kuendelea kujenga na kuimarisha miundombinu yetu kwa ajili ya viwanda vilivyopo na tunavyotarajia vianzishwe, wamesisitiza upatikanaji wa ardhi kwa maendeleo ya viwanda katika mikoa yote na miji yote na kushughulikia changamoto ambazo zilijitokeza katika kutekeleza Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Waheshimiwa Wabunge, wamesisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa sekta ya kilimo, kama msingi wa maendeleo ya viwanda, kilimo cha umwagiliaji, umuhimu wa kuimarisha masoko ya mazao na upatikanaji wa bei nzuri kwa wakulima wetu. Tumeendelea kupokea ushauri kuhusu umuhimu wa kuongeza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo na pia Benki ya Wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, umetolewa ushauri mbalimbali kwamba iko haja ya kuimarisha Mpango huu upande wa mikakati ya kuendeleza viwanda ikiwa ni pamoja na kulinda viwanda vya ndani, kuhakikisha tunaongeza thamani ya bidhaa tunazozalisha viwandani, pia kukamilisha tathimini ya viwanda vilivyobinafsishwa ili kuweza kuviendeleza na kufufua vile ambavyo vimekufa kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamesisitiza uboreshaji wa rasilimaliwatu na hususani tuhakikishe kwamba rasilimaliwatu inaendana na mahitaji ya viwanda. Kwa kuboresha mitaala ya elimu na kadhalika. Pia kufanya jitiahada ya kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja na mitaji kutoka nje. Kwa kweli nawashukuru sana kwa michango hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nitoe ufafanuzi wa hoja chache, nikitambua kwamba siyo rahisi kufafanua hoja zote ambazo zilisemwa au kuandikwa. Kama ulivyosema nitatoa ufafanuzi wa baadhi tu ya hoja kuongezea pale ambapo Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri walipoishia.
Moja, kulikuwa na hoja kwamba namna gani Mpango umejikita katika kupunguza utegemezi?
Mheshimiwa Naibu Spika, utegemezi una madhara mengi sana ikiwa ni pamoja na kukosa uhuru. Naomba uniruhusu nitoe mfano wa kule nilikozaliwa. Akinamama kutoka Mkoa wa Kigoma wanafahamu vizuri kwamba ukiazima kitenge cha rafiki yako, ukaenda harusini na umefuatana naye, basi pale unapojimwaga mara nyingi anakukumbusha kwa kusema; “ucheze vizuri usije ukachana kitenge changu.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli utegemezi unaendana na masharti na wao wenyewe wanasema there is no free lunch. Baadhi ya wafadhili wanaingilia hata maamuzi ya mambo yetu ya maendeleo. Upatikanaji wa hizi fedha za misaada hauna hakika na hivyo ni lazima kuchukua hatua kupunguza utegemezi kwa kuongeza kiwango cha fedha za ndani kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tunafanya hivi. Mwaka 2011/2012 tulitenga shilingi trilioni 1.87 kwa ajili ya maendeleo, lakini kufikia mwaka huu wa fedha tunaomalizia tulikuwa tumetenga shilingi trilioni 4.2 na nia yetu kwa kweli ni ya dhati kabisa. Ni lazima tuendelee kuongeza fedha yetu ya ndani ambayo tunaitumia kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana wakati nikiwasilisha mapendekezo ya ukomo wa bajeti nilisema wazi na ninarudia, tumeamua kutenga shilingi trilioni 8.7 kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha ambayo ni asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hivyo tu, bado tumeendelea kuwa na dhamira ya dhati ya kuongeza kiwango cha makusanyo ya mapato ya ndani ya kodi na yasiyo ya kodi. Kwa hiyo, mwaka 2014/2015 wastani wa makusanyo ya kodi katika Pato la Taifa ilikuwa ni asilimia 12.01 mwaka 2020/2021 ambao ndiyo mwisho wa Mpango niliouwasilisha dhamira yetu ni kwamba sasa ifike asilimia 18 ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumeendelea kupunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima na kuelekeza hizo fedha kwenye maendeleo, lakini hasa kwenye ujenzi wa viwanda ambapo maana yake tunajenga uwezo wa nchi yetu kujitegemea zaidi na hatimaye tuweze kuondokana kabisa na utegemezi. Tumesisitiza umuhimu wa kujenga mazingira ya uendeshaji biashara na uwekezaji nchini na hiyo yote ni dhamira kwamba, hatimaye tutakapokuwa tumekuza uwekezaji nchini tutakuwa tumejinasua kwenye utegemezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie hoja hii tu kwa kusema na kuwahakikishia Watanzania kuwa dhamira ya Serikali yetu ya kuondokana na utegemezi, ni thabiti kabisa na wale wenzetu wanaotaka tuendelee kubebwa hadi uzeeni mimi nawasihi wajitambue maana dunia imebadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunataka uhusiano wa kibiashara na washirika wa maendeleo, tunataka uhusiano wa uwekezaji zaidi na huu ndiyo uhusiano endelevu, huu ndiyo utatuhakikishia uhuru wa kiuchumi na ndiyo uhusiano ambao unaheshimika yaani wenye dignity kama nchi na ndio utakaotuhakikishia sovereignty ya nchi yetu inabakia kuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwepo hoja, kwa nini Serikali inaleta Mpango mpya wakati Mpango uliopita umetekelezwa kwa asilimia 26 tu? Kitaalam tathmini ya utekelezaji wa Mpango wowote unatumia vigezo vingi, upatikanaji wa rasilimali fedha ni moja tu ya vigezo. Viko vigezo vingi kama muda wa utekelezaji, thamani halisi ya hicho tulichopata, lazima tuangalie malengo, outcomes and impact (matokeo). Lazima pia tutathimini madhara yaliyotokana na utekelezaji na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo siyo sahihi hata kidogo kutumia kigezo kimoja tu kuhukumu Mpango kwamba haukufanikiwa. Tathimini ya utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano ipo na Waheshimiwa Wabunge, tuliwagawieni kitabu ambacho kimeeleza kwa kina tulivyotathimini utekelezaji. Kwa kweli tulibaini kwamba ukizingatia viashiria vingi itakapofika mwezi Juni, 2016 utekelezaji utakuwa ni takribani asilimia 60 na tuliweka wazi sababu ambazo zilipelekea Mpango huu usifike asilimia 80 au 90. Isitoshe ulimwenguni kote hakuna Mpango unatekelezwa asilimia 100. Hata Mpango wako binafsi haufiki asiliamia 100. Ndiyo ukweli wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulibainisha sababu kubwa zilikuwa ni upungufu wa rasilimali fedha, ushiriki mdogo wa sekta binafsi na udhaifu katika usimamizi. Serikali ya „Hapa Kazi tu‟ ni Serikali inayosema ukweli kwa maana ya kutaka kujirekebisha, ndiyo maana hatufichi sababu ambazo zilipelekea utekelezaji usifike kule ambako tungetaka na ndiyo maana katika Mpango huu tumesisitiza maeneo ambayo tumeona yalikuwa na udhaifu. Hivyo Mpango niliouwasilisha utaendelea kutekeleza miradi muhimu kama miundombinu, nishati, usafirishaji na maendeleo ya rasilimali watu ambayo ni lazima tuendelee kutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kuwa Serikali ina mikakati gani kupata fedha kwa ajili ya ugharamiaji wa Mpango. Nafikiri nimeshalieleza. Kuna aya mahsusi katika kitabu cha Mpango ambayo inaeleza vyanzo mbalimbali kwa ajili ya ugharamiaji wa Mpango, lakini kikubwa ni lazima tuelekeze nguvu ku-tap resources zilizoko kwenye sekta binafsi (PPP).
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za Serikali nilisema zinatumika kama chambo, Kiingereza kizuri ni leveraging private capital. Hiyo ndiyo itakayotupeleka mbele. Miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kati, kuijenga kwa Bajeti ya Serikali nilieleza katika Bunge lililopita ni kazi ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, palikuwa na hoja kwamba kuna ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na Makampuni ya Simu. Ni hoja nzuri ambayo tunaendelea kuifanyia kazi. Lakini naomba niseme kuwa hizi hisia zipo kwamba makampuni haya hayatupatii takwimu sahihi juu ya muda wa maongezi (airtime) unaotumiwa na wateja na hivyo wanavujisha mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda wateja walikuwa wanatumia kadi (scratch cards) na hapo ilikuwa ni rahisi kuweza kufuatilia mapato ya kampuni za simu na kuhakiki au kulinganisha idadi ya kadi ambazo zilikuwa zimenunuliwa hapa nchini na zile walizokuwa wameagiza, zilizotumika na zilizobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa teknolojia imebadilika; siku hizi unaweza ukanunua airtime kwa njia ya kielektroniki. Sasa hapa changamoto inakuwa ni kwamba, unajuaje mauzo halisi ya muda wa maongezi kwa Makampuni ya Simu kwa siku, kwa mwezi na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, simu za mkononi sasa zinatumika kwa ajili ya kusafirisha fedha na ni kwa kiwango kikubwa na haya makampuni yanapata mapato kutokana na hizo transfers. Serikali imefanya juhudi kupitia TCRA ili kuwezesha mapato haya kwa maana ya commission charges hasa kwa upande wa foreign traffic na hili limewezekana kwa kufunga mtambo ambao unaitwa TTMS (Telecommunication Traffic Monitoring System).
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo tulilonalo ni kwamba mfumo huu umetusaidia sana kujua hayo mapato kwa zile simu za international. Kazi ambayo inafanyika hivi sasa ni kuhakikisha kwamba muda wa maongezi kwa simu za ndani yaani local traffic nazo ziwe zinaweza kutambuliwa katika mfumo huu. Kwa hiyo, tunahitaji kuunganisha hii TTMS na mfumo mwingine unaoitwa Airtime Revenue Monitoring Solution (ARMS). Na kazi hii itakapokamilika hapo ndipo tutaweza kuwabana na kuwa na uhakika huo wa muda ambao kwa sasa hatuwezi kuu-capture vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Jumamosi hii nimeitisha Mkutano kati yetu Wizara, Wizara ya Uchukuzi, TCRA yenyewe na Mamlaka ya Mapato Tanzania ili tuharakishe kazi hii ya kuhakikisha kwamba huu mfumo wa ARMS unakuwa integrated na huu wa TTMS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme mambo mengine mawili. Moja, kuna Mheshimiwa Mbunge anasema wanawake wamesahaulika. La hasha, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba kwetu sisi tukisema viwanda, kwetu sisi tukisema umeme vijijini, tukisema maji, focus yetu ni akinamama. Kwa kweli Mheshimiwa Rais alinipa Naibu Waziri mwenye uwezo mwanamama. Sasa kama na yeye amejisahau nitashangaa kweli kweli! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna hakika kabisa wala hatubabaishi akinamama ndiyo wamebeba uchumi wa nchi hii. Mpangaji yeyote wa mipango katika nchi kama ya kwetu ambaye hatambui mchango mkubwa wa akinamama katika uchumi wa Taifa, basi huyo hafai kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya kati. Naomba niseme kwamba umuhimu wa kujenga reli mpya ya kati na matawi yake yote hapa nchini hauna mjadala hata kidogo. Ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga reli mpya kwa kiwango cha standard gauge haraka inavyowezekana. Ndiyo maana pamoja na hali ngumu tuliyonayo, tumeamua kwamba tutatenga shilingi trilioni moja mwaka unaokuja kwa kuanzia tuone uwezekano wa kujenga angalau kilometa 50 mpaka 100 za reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Kwa sababu reli hii ni fursa itakayotuwezesha kutumia fursa pekee ya Tanzania tuliyonayo kijografia yaani ni unravel opportunity ambayo Taifa hili inayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya kati ndiyo itatuwezesha kuhakikisha kwamba biashara ya mazao yetu ya kilimo, ya chakula na ya biashara, uendelezaji wa madini lakini pia utalii. Vile vile kuhakikisha kwamba utangamano katika Afrika Mashariki na nchi zinazotuzunguka unaimarika na ni ukweli ulio bayana, Tanzania tunafaidi kutokana na utangamano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumewekeza katika baadhi ya miundombinu na reli hii ndiyo itatusaidia kuhakikisha kwamba tunafaidi. Naomba nisisitize tu kwamba tatizo letu kubwa hapa nilieleza kikao kilichopita reli hii inakadiriwa ili kuijenga itatumia kati ya dola za Kimarekani bilioni 7.5 mpaka bilioni 9.0. Hizi ni fedha nyingi, siyo fedha kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, challenge kubwa inayotukabili kama Taifa ni kutafuta financing kwa ajili ya kujenga reli ya kati. Mjadala siyo kuijenga, hapana. Kazi kubwa tuliyonayo ni kupata fedha. Trilioni moja hii tuliyotenga ni kuonesha resolve tuliyonayo kama Serikali kwamba lazima tujenge hii reli na kwa hiyo nayo tunaitumia kama chambo kuvutia wawekezaji ili waone seriousness tuliyonayo ya kujenga reli yetu ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe tu, kilicho muhimu Waheshimiwa Wabunge, ni kuwa na mkakati ambao ni credible wa kujenga hii reli. Kwa ushauri wangu tusijidanganye kusema kwamba sisi “lets do it alone” tujitazame tu ndani. Tukijenga matawi ya ndani peke yake haitatosha. Hatuna mzingo wa kutosha nchini kufanya ujenzi wa reli yetu ya ndani uwe sustainable. Kwa hiyo, ni muhimu na niwaombe Waheshimiwa Wabunge, maana wale wanaosema tusifikirie kujenga na extension ya kwenda Rwanda, jamani mbona hawasemi tufunge ile barabara ya kwenda Rwanda ambayo mizigo inapita hapa. Transit-trade peke yake inatuingizia mapato in foreign currency na sasa ni sekta ya pili kwa ukubwa kutuingizia mapato ya kigeni hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwaombe tu, tutafute strategy ambazo ni credible na sidhani kabisa kwamba strategy ya kujenga reli inayosema haya matawi ambayo yanatupeleka nchi jirani tusijenge, hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeliahidi Bunge lako Tukufu kwamba nitaleta ufafanuzi wa hoja zote tulizozipokea kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge watapata nafasi ya kuzisoma taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu nihitimishe kwa kusema yafuatayo:-
Kwanza, kulihakikishia tena Bunge lako Tukufu kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuzingatia maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge ili kuboresha utekelezaji wa Mipango yetu ya Maendeleo ili kufikia malengo ambayo tumekusudia. (Makofi)
Pia tuna dhamana ya kuleta mabadiliko makubwa kuanzia upangaji wa mipango na utekelezaji wake ili kuiwezesha nchi yetu iondoke kwenye lindi la umaskini na hasa kwa wananchi wengi ambao wanaishi vijijini, lakini hata sehemu nyingine za miji yetu. Kama nilivyosema jana asubuhi wakati nikiwasilisha hoja yangu, kila Mtanzania ni lazima atambue wajibu wake wa kufanya kazi kwa bidii, kwa uadilifu, kwa nidhamu na uzalendo wa hali ya juu ili kujenga Tanzania mpya kwa faida yetu sisi, lakini pia na vizazi vijavyo na watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kuzitaka Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, wajielekeza kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Mpango huu ili tuweze kufikia azma yetu ya kujenga uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu. Nilisema jana na narudia tena, atakayeshindwa kusimamia utekelezaji wa miradi hii tuliyoibainisha aachie ngazi. Kama hataki kuachia, tutalala naye mbele. Wananchi wetu maskini wamechoka na huu umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niwahakikishie sekta binafsi ya Tanzania kwamba tumedhamiria kuboresha mazingira yao ya kuwekeza, lakini pia kuhakikisha kwamba wawekezaji wa Kimataifa nao wanafanya biashara ambayo wao wanapata na sisi tunapata. Kwa hiyo, falsafa ya Hapa Kazi Tu itahamia vilevile kwenye kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Tunawaomba wawekezaji wote wa ndani na wa nje waweke nguvu zaidi katika sekta zote, lakini hasa katika maeneo ya kipaumbele ambayo tumeyabainisha katika Mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Watanzania wote watambue kwamba ni lazima tujinyime, lazima tujitume na kuvuja jasho ili kupata maendeleo tarajiwa. Wajibu wa kwanza wa kuiendeleza nchi yetu ni wa sisi wenyewe Watanzania. Akili za kutosha tunazo, Mungu alitujalia rasilimali nyingi na fursa tele. Hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kuwa semi-industrialize country inapofika mwaka 2025, inawezekana kabisa hata kabla ya hapo. Tutekeleze falsafa ya Hapa Kazi Tu kwa vitendo na Tanzania mpya tutaiona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kutoa hoja.