Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii, nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijaalia nami kupata nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani, na kukiombea rehema Chama changu cha Wananchi CUF kupitia kwa Katibu Mkuu wangu Maalif Seif aendelee kuwa na subira na Mwenyezi Mungu amesema, Innallah Maa’swabiriina (kila mwenye subira yuko pamoja na Mwenyezi Mungu). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia hotuba na hoja zilizopo mezani kwangu hazihitajiki kuungwa mkono na Wabunge wa Mkoa wa Lindi na Mtwara. Nina sababu za msingi ukienda ukurasa 188, bajeti ya miradi ya Mkoa wa Lindi, ukichanganya na Mkoa wa Mtwara basi zinazidi Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa wa Lindi na Mtwara ukichanganya tunapata shilingi bilioni 1.7; wakati ukizingatia Mkoa wa Lindi ni Mkoa wa mwisho. Leo Mbunge wa Liwale hawezi kwenda Liwale hana nafasi barabara hakuna. Mbunge wa Liwale anatoka Dar es Salaam mpaka Lindi - Masasi - Nachingwea anakwenda Liwale na hawezi kufika kwa siku moja. Ameanzia Mheshimiwa Kawawa akashindwa, wamekuja Wabunge akina Hassan Chande Kigwalilo wameshindwa, halafu utasema tuna sera ya barabara, siikubali sera hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni sera ambayo inabagua, ni sera ambayo ina upendeleo, ni sera ambayo haitaki maendeleo ya watu wa Kusini. Wameitengeneza sera hii maksudi watendaji kuhakikisha Kusini inadhalilika. Nazungumzia hivi kwa sababu Mkoa mzima wa Lindi una miradi minne tu. Je, jiulizeni ukiangalia Jimbo la Lindi Vijijini la Mchinga na Mtama hawajaweka mradi hata mmoja, tujiulize kuna nini? Kujiuliza maana yake unapata maswali mengi ukijiuliza, eti kweli barabara za Mchinga hakuna hata mahali pa kufanya rehabilitation? Hakuna ndani ya kitabu hiki. Mtama kwenye Jimbo la mdogo wangu au mwanangu Nape Nnauye hakuna hata mradi mmoja, ninyi ni wabaguzi! Mnaibagua Kusini kwa maksudi kuwafanya wananchi wa Kusini waichukie nchi yao kwa ajili ya miradi yenu mibovu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani watu mikoa mingine wana lami mpaka katika kata, leo Mkoa wa Lindi hauna mawasiliano ya aina yoyote sasa hivi. Nakwambia utasikia wanakwenda mikoa mingine siyo Lindi, viongozi wakuu juzi wametembelea kwenda Lindi wameshindwa kwenda Liwale, wameshindwa kwenda Nachingwea, kwa nini wameshindwa? Hakuna njia ya kupita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ubaguzi huu ndiyo unaofanya wananchi wa kule kuichukia CCM. Na mimi naungana nao kuichukia CCM kwa vile hawataki kuwatendea haki, barabara iliyopo ni ya kitaifa ambayo ni lazima muijenge, jiulize unatoka Nanganga kwenda Nachingwea haipitiki, unatoka Nachingwea kwenda Liwale haipitiki, unatoka Liwale kwenda Nangurukuru haipitiki, unatoka Lindi - Ngongo mpaka kwenda Ruangwa hakupitiki, halafu mtasemaje sisi tuko katika Tanzania, sisi tuko Tanganyika. Ndiyo maana tunaidai Tanganyika na makao makuu ya Tanganyika yatakuwa Liwale. (Makofi/Kicheko).

Mheshimiwa Naibu Spika, kumetokea mafuriko, Jimbo linaloongoza kwa mafuriko ni Lindi Vijijini. Jiulizeni wapi wameweka bajeti ya Lindi Vijijini. Hawakuweka hata barabara moja ambayo itarekebishwa angalau wananchi wale wapate hifadhi, hakuna. Wanawake wanatembea na miguu hakuna daraja, wanawake wanataka kwenda kujifungua hospitalini hakuna daraja watapita wapi kama siyo ubaguzi mkubwa unafanyika namna hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wanaosifia wamefaidika na hili, ukimuona mtu anasifia anafaidika na hili lakini mimi nitasifia kwa lipi hapa? Hakuna cha kusifia hapa. Tunadhalilika, nitashangaa kusikia Mbunge wa kutoka Lindi anaisifia bajeti hii, hakuna kitu hapa. Huu ni udhalilishaji wa muda mrefu, mimi niko humu ndani kipindi cha tatu kila mwaka ni barabara, wakienda kutafuta kura wanawadanganya, mwaka huu kutoka Nangurukuru mpaka Liwale mpaka Nachingwea ni lami na tayari tulishatenga fungu. Tupo katika feasibility study zaidi ya miaka 40 hamna feasibility study. Ifike mahali mdanganye watoto wadogo sisi ni watu wazima sasa hivi, hata wale walioko kule ndiyo maana wamegeuka wameona kabisa maeneo ambayo yamedhalilishwa, hawapewi manufaa yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo katika mazingira haya, nani atakwenda kufanya kazi Liwale? Ndiyo maana unaambiwa Mkoa wa Lindi na Mtwara ni Mikoa ya mwisho kwa elimu. Kiwango cha elimu kimekuwa chini walimu hawataki kwenda. Sasa mnataka kutuweka mpaka lini tuwe tunadhalilika tukiwaangalia tunawabembelezeni, bajeti bajeti, sera iko wapi ya barabara?

Naomba kama kweli wale Wabunge wa Kusini wana ukereketwa tukutane Jumatatu, tufanye kikao tuikatae hii bajeti haifai kabisa. Ni bajeti ambayo haimsaidii mwananchi wa Lindi wala mwananchi wa Mtwara. Kama hutafanya vile pengine unataka Uwaziri, huwezi kupata Uwaziri katika kipindi hiki. tunachoomba tuungane, tuikatae bajeti, ili itusaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la wizi katika mitandao na hasa katika kampuni ya Airtel. Wananchi wanaibiwa vibaya sana pesa hasa kipindi cha sikukuu na kipindi cha weekend. Wizi huu unafanywa na wafanyakazi na ninao ushahidi nitakuletea. Bahati mbaya walinifanyia hata mimi mwenyewe, lakini nikawaambiwa ninyi mmechezea choo cha kike na leo mtakiona. Walifanya wizi baada ya kuletewa pesa za Mbunge mwenzangu alifiwa wakanitumia pesa katika simu yangu. Wale kule wanaona kama imeingia na ilikuwa ni kipindi cha sikukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikapigiwa simu; mama kuna pesa ilikuwa zimekatwa kimakosa tuanaomba tukuingize, wakanipeleka nikashtukia sielewi maana yake ilikuwa siku mtandao haufanyi kazi, nika- qoute agent code namba nikai-qoute, ghafla nikashtukia milioni moja laki tano wameziiba.

Walipoziiba hela zile nikakimbia nikaenda Dar es Salaam nika block, kinachosikitisha watu wa cyber crime wakishirikiano na taasisi hizi hazina mawasiliano. Sasa jiulize kama watu ambao wanaweza kujitambua wakajua wafanye nini ili waweze kurudisha hela zao, je, watu wa vijijini wanafanya nini, ni kuibiwa tu. Wizi umekuwa mkubwa sana tunataka tupate majibu hawa watu wa cyber crime wanafanya nini, mbona wizi umekuwa mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ukienda India unaambiwa utakaa kwa siku ngapi ukipewa ile card chip ya kukaa pale, unasema nakaa wiki mbili, siku unaondoka ikifika saa sita usiku jina lako limeshapotea na mawasiliano yamepotea. Tanzania acha simu yako nenda kakae Marekani miaka miwili ukirudi unakuta matandao uko online tu, mpaka leo hawajahakiki kama kweli jina lile linalotoka katika namba ndiyo kweli, wenzetu Uganda wameshaanza sasa hivi kuhakikisha yule aliyepewa namba kweli ni mwenyewe, ndiyo maana wizi wa mtandao hautaweza kuisha kutokana na uhakiki wa majina haukufanyika vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Wizara yenye dhamana ifanye kazi ya kuhakiki vizuri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali naipongeza Serikali kwa kupitia mtandao wa mwendokasi wameshinda tuzo kwa kwa kuweweza kufanya uwekezaji mzuri katika Afrika Tanzania ni nchi ya pili.