Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuweza kuchangia.

Kwanza nianze na barabara yangu ya kutoka Magu - Kabila - Mahaha. Barabara hii ina kilometa 58, lakini mwaka huu haijatengewa fedha, matengenezo maalum au matengenezo ya mara kwa mara haina fedha. Nashukuru kwamba imetengewa fedha kwa ajili ya daraja ambalo Serikali inagharamika kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya daraja hili. Ninajua kwamba tayari upembuzi yakinifu umeshakamilika na mkandarasi ameshapatikana, tatizo ni fedha za kuendelea. Niiombe Serikali nikiamini kwamba bajeti ambayo tunayo tulitenga fedha kwa ajili ya kulijenga lile daraja angalau zitoke fedha za kuanzia lile daraja Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba tu Waziri kwa sababu sihitaji kulalamika, aiandike barabara hii ili aiwekee fedha angalau ipate fedha za matengenezo kwa mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii pia ni ahadi ya Rais kuwekewa lami alipokuwa kwenye kampeni Mheshimiwa Rais alipotembea aliona ametembea umbali mkubwa zaidi sana. Alipofika kule Kabila akasahau kwamba yuko Magu akasema yuko Kwimba, baada ya pale akasema basi barabara hii tutaijenga kwa kiwango cha lami, naomba ahadi hii nayo iheshimiwe.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara hii ya Isandula - Ngudu ni barabara muhimu iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tangu 2005, hebu tupeni fedha ili iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo barabara ambazo tuliziomba Road Board zipande kutoka Wilaya kwenda Mkoa, bahati nzuri Wizara yako Mheshimiwa Waziri ilileta wataalam wa kuzipitia, zikaonekana hizi zina qualify, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri sasa uzipandishe hizi barabara kwa sababu uwezo pekee wa Halmashauri hatuwezi kuzigharamia. Hizi ni barabara ya Kisamba - Sayaka - Salama na Simiyu kule Bariadi ni barabara muhimu sana ya kufungua uchumi. Tunayo barabara ya Ilungu kuelekea Kwimba mpaka Maswa ni barabara muhimu sana kiuchumi, tunayo barabara ya Kisesa - Kayenze - Ilemela inaweza kupunguza pia msongamano wa kuingia Jiji la Mwanza, tonayo barabara ya Nyanguge - Kwimba hizi barabara zote zime-qualify, ningetegemea kwamba bajeti hii zingeweza kupatiwa fedha, naomba zipatiwe fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara muhimu inayotoka Airport - Ilemela ambayo ikitengenezwa kwa kiwango cha lami mpaka Nyanguge inapunguza msongamano kabisa wa wananchi wote kutoka Musoma kuelekea Mwanza hawatapita Mwanza Mjini watakwenda airport itapunguza msongamano. Hebu muiweke vizuri kwa sababu tumeomba kila siku.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara ya kilometa
1.2 ya Kisesa – Bujora, barabara hii inapitiwa na viongozi wote wa kitaifa kila mwaka kwa ajili ya kwenda kwenye makumbusho, tumeiomba kama Road Board kila mwaka kiongozi wa kitaifa lazima apite, naomba na hii iingie ni kilometa 1.2.

Mheshimwa Naibu Spika, ahadi ya Rais ya kilometa tano za lami Magu Mjini, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri ulikuja Magu nikakutembeza kwenye barabara zile ukaziona zilivyo, hebu tusaidie kwenye bajeti hii angalau ahadi hii ya kilometa tano za lami ianze ili wananchi waweze kupata huduma inayokubalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi nataka nijikite kwenye taasisi hii ya marine. Taasisi hii ya Marine Services ina uhakika wa kuingiza kipato kwenye nchi hii, nina uhakika mkiijali inaweza kuchangia uchumi kwenye nchi hii pia shirika hili linaweza kujiendesha. Mheshimiwa Waziri hili shirika ni kama limetelekezwa, tunazo meli 15 katika maziwa yetu haya matatu, sekta binafsi wako ambao wana meli kule Ziwa Victoria wanafanya vizuri wana meli na kila mwaka wanaongeza meli, kwa nini Marine isihudumiwe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti iliyopita tulitenga fedha, lakini mpaka leo fedha hizi Marine hawajapewa taasisi hii. Ni kama dhahabu ambayo iko ndani hatujaipeleka sokoni, hebu tuisaidie Marine ili iweze kuchangia uchumi na iweze kujiendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya kabisa wapiga kura wetu kule ni wafanyakazi wa taasisi hii mishahara hawalipwi, bima ya afya wamefungiwa, kuna mambo kede wa kede. Ushauri wangu ni kwamba kwa sababu hii ni taasisi ambayo iki-link na bandari; ika-link na reli naamini mizigo yote ambayo inakwenda Uganda inaweza ku-support sana kupata fedha nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunacho kivuko ambacho alikiongelea hapa Mheshimiwa Mabula, Ilemala pale tumeomba kivuko cha Kayanze, Bezi na Ijinga. Wananchi walioko visiwa vile ni zaidi ya wananchi huku wako 600,000 Bezi lakini na Ijinga wapo zaidi ya 400,000. Kwa hiyo, wakipata kivuko hiki kinatasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo ambayo Serikali imefanya, makubwa sana kwa muda mfupi na wala hayawezi kuelezeka. Na mimi nilikuwa najiuliza sana, Mheshimiwa mmoja alikuwa anasema kwamba kipindi hiki tumepata Rais wa ajabu, nilishindwa kumuelewa, lakini sasa nimeanza kumuelewa kwamba kweli tumepata Rais wa ajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kitu kinaitwa Bombardier ndege mbili zimekuja, nne bado zinakuja jumla ndege sita, kwa muda mfupi, huyu ni Rais wa ajabu haijawahi kutokea! Kuna kitu kinaitwa standard gauge tukitafakari kidogo Waheshimiwa Wabunge hili ni jambo kubwa la kihistoria, nasema huyu ni Rais wa ajabu. Kupambana na ufisadi haijawahi kutokea, kupambana na dawa za kulevya haijawahi kutokea, kupambana na rushwa haijawahi kutokea, huyu ni Rais wa ajabu lazima, tumpe hongera zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yote haya yanayofanywa na Serikali kwa miradi yote ya kiuchumi na huduma za kijamii hili ni tendo la huruma, na sisi viongozi tunapaswa kuwa na huruma. Mithali ya pili maandiko matakatifu ambayo siyo ya kwako wewe sura ya 19:17 unasema, amhurumiaye maskini anamkopesha Mungu naYe atamlipa kwa tendo lake jema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa huruma hii ya Mheshimiwa Rais na Serikali yake na Waheshimiwa Mawaziri na watendaji wake wakuu wa Serikali, wanafanya kazi ya huruma wanamkopesha Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana.