Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Newala Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, barabara ya Newala -Kitangari – Mtama inahudumiwa na TANROADs. Hii barabara inaunganisha Mkoa wa Mtwara na Lindi, lakini ni barabara ya vumbi. Wananchi wa Newala wanaomba barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami, maana pia ndiyo njia kuu wanayotumia watu wa Newala kwenda Dare es Salaam na Dodoma. Tunashukuru kwa jitihada za Serikali maana sehemu korofi kama za Kitangari na mlima Kinolombedo zimejengwa kwa kiwango cha lami. Ni vizuri kuongeza kilomita zilizojengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu Uwanja mpya wa Ndege wa Newala. Baada ya eneo la Uwanja wa Ndege wa zamani kupima viwanja, Uongozi wa Wilaya umetenga eneo jipya la Uwanja wa Ndege. Wataalam wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege walitembelea Newala na kuelekeza ukubwa unaohitajika na mwelekeo wa Uwanja. Nilipouliza swali Bungeni, Mheshimiwa Waziri alinijibu kuwa Serikali italipa fidia eneo la uwanja, wakati inafanya mipango ya Ujenzi. Wananchi wa Newala wanaomba Serikali ilipe fidia eneo la Uwanja wa Ndege ambalo halina mazao mengi ya kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami toka Newala Mjini kuelekea Masasi palitengenezwa mfereji wa kutolea maji barabarani. Mfereji huu umeleta uharibifu mkubwa kwa kutengeneza korongo kubwa zinazotishia usalama wa nyumba za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika katika Kijiji cha Mkunya, korongo kubwa lililosababishwa na mvua linahatarisha usalama wa nyumba za wananchi. Alipotembelea Wilaya ya Newala, Mheshimiwa Waziri Mbarawa alikagua eneo la korongo la Newala Mjini, akaahidi kutafuta fedha za kujenga makorongo hayo vizuri. Wananchi wa Newala tunakumbusha ahadi ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.