Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa usimamizi wa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa kazi nzuri inayofanya kusimamia ujenzi wa miundombinu katika Taifa letu. Kazi yao ni nzuri sana. Namwomba Mungu awape nguvu na afya walipeleke Taifa la Tanzania kwenye nchi ya viwanda yenye miundombinu ya barabara za kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali, Jimbo la Igunga ni Jimbo ambalo halina barabara ya kupitika wakati wote (majira ya masika na kiangazi). Wananchi wa Jimbo la Igunga inapofika wakati wa masika (mvua) huwa hawana miundombinu ya barabara kuwawezesha kufika kwenye vijiji na hata kata za jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, wakati nachangia hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwamba eneo la Wilaya ya Igunga miaka 60,000 kabla ya Kristo lilikuwa ziwa na lilikuwa ziwa na lilikauka kwa sababu za kijiolojia na kuacha tope jeusi ambalo wakati wa mvua huwa tope ambalo hufanya barabara kutopitika kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wa Halmashauri kujenga barabara inayohitaji ujenzi wa tuta kubwa kwa urefu mkubwa ni mdogo sana; matokeo yake barabara zinazounganisha vijiji na kata hazipitiki kabisa. Pia barabara zinazounganisha Wilaya za Meatu na Igunga, Kishapu na Igunga, Uyui na Igunga, hazipitiki kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Igunga linayo barabara moja tu ya lami ambayo ni barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda Mwanza inayopita katikati ya Jimbo la Igunga. Pia Jimbo la Igunga lina kilometa zipatazo 10 tu za barabara ya changarawe inayotoka Kata ya Itunduru kwenda Kata ya Igurubi inayohudumiwa na TANROADs.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zote za Jimbo la Igunga zinahudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga yenye uwezo mdogo sana kifedha wa kujenga barabara za changarawe kwenye eneo la mbuga. Kimsingi Jimbo la Igunga halina barabara za vijijini na kwenye kata na hasa wakati wa masika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 2012 Halmashauri ya Wilaya ya Igunga iliomba kupandishwa hadhi kwa barabara itokayo Igurubi (mpakani mwa Wilaya ya Kishapu) kupitia Igunga na Itumba kuelekea Loya na kufika Tura katika Wilaya ya Uyui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha tu ya kuwa barabara hii inapitika katika maeneo makubwa ya uchumi wa Mikoa ya Shinyanga na Tabora, sehemu ambazo wananchi wa maeneo hayo wanalima pamba, mpunga na tumbaku, lakini pia wanafuga ng’ombe kwa wingi. Kufunguliwa kwa barabara hii kutakuza uchumi wa Wilaya ya Igunga na Jimbo la Igunga, lakini pia uchumi wa Mikoa ya Tabora, Shinyanga na Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kadhaa nimewahi kuuliza maswali humu Bungeni juu ya lini barabara hii inaweza kupandishwa hadhi ili kufungua Wilaya ya Igunga na kuunganisha Mikoa ya Shinyanga, Singida na Tabora?

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ikipandishwa hadhi, inaweza kujengwa kwa kiwango cha lami ikitokea Kolandoto kupitia Ukenyenge katika Jimbo la Kishapu na kupitia Igurubi hadi Mbutu - Igunga na Itumba katika Jimbo la Igunga kuelekea Miswaki - Loya hadi Turu katika Jimbo la Igalula. Barabara hii itaunganisha kwa upande wa kaskazini barabara ya lami itokayo Shinyanga kwenda Mwanza na kwa upande wa kusini barabara ya lami itokayo Manyoni kwenda Tabora. Kujengwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami kutaunganisha barabara hizi kuu za lami nchini kwetu na kufungua fursa za kiuchumi za Mikoa ya Tabora, Shinyanga na Singida. Fursa hizo ni pamoja na kilimo cha pamba, tumbaku, alizeti na mpunga, mazao yanayozalishwa kwa wingi katika mikoa hii. Pia biashara ya mifugo katika minada nayo itaimarika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ifike wakati atume wataalam wakaitathmini barabara hii muhimu kwa mikoa hii na ikiwezekana katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/2018 tupate hata fedha kidogo za kufanya upembuzi yakinifu ili bajeti ijayo iweze kupandishwa hadhi na baadaye kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, barabara ya Kininginila – Mwabakima – Mwanyagula – Mbutu hadi Igunga nayo inao umuhimu wa pekee sana kwa sababu inaunganisha Wilaya ya Meatu katika Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora. Pia barabara hii inapitia katika maeneo ya kilimo cha pamba na ufugaji wa ng’ombe. Tunaomba barabara hii nayo kupandishwa hadhi kuwa ya TANROADs ili iweze kujengwa kwa kiwango cha changarawe na kupitika wakati wote ili kuwaondolea adha ya ukosefu wa miundombinu ya barabara hasa wakati wa masika wananchi wa Kata za Kininginila, Isakamaliwa, Mwamashimba, Mbutu na Igunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa barabara za kiwango cha changarawe chini ya usimamizi wa TANROADs katika Jimbo la Igunga ni changamoto kubwa inayosumbua na kukera sana wananchi wa Jimbo la Igunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa heshima kubwa, naiomba sana Serikali ilisaidie Jimbo la Igunga kupata barabara za kutosha za kiwango cha changarawe na kiwango cha lami ili kuwaondolea adha ya usafiri wananchi wa Jimbo la Igunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.