Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nishukuru kupata fursa hii ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme ninaunga Mkono hoja hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa asilimia 100. Sababu ziko wazi, imesheheni karibu pande zote, mikakati yote, kutokana na utendaji wa kazi tunaouona kwa sasa wa Mheshimiwa Rais na Mawaziri wake hatuna mashaka, tusonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie upande wa hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa nane mpaka wa 10 katika eneo la siasa. Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maagizo kwenye Tume ya Uchaguzi kubaini sababu zilizopelekea wapiga kura milioni saba kutokupiga kura. Idadi hiyo ni kubwa sana, lazima na sisi tuweze kueleza baadhi ya sababu ambazo zinaweza kuwa kwa namna moja au nyingine zimechangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sababu ni umbali wa vituo vya kupigia kura. Watu walikuwa wanatembea kilometa 20 mpaka 10 kufuata kituo cha kupigia kura, sasa ni watu wachache ambao wanaweza wakamudu hali hiyo, lakini zipo sababu zingine za baadhi ya wananchi kukata tamaa zikiwemo sababu zifuatazo:-
Kwanza, wananchi kukata tamaa kutokana na baadhi ya Viongozi kutotenda haki, kuwa na upendeleo na ubinafsi uliokithiri. Hiyo ni sababu mojawapo inayowafanya wananchi wakate tamaa na ninaomba nieleze sababu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hatujaenda kwenye uchaguzi wa mwaka 2015, Tume ya Uchaguzi ilitoa vigezo vinavyoweza kuwezesha Jimbo likagawanyika. Sisi wote tunajua, vigezo tunavijua lakini cha ajabu unakuja kuona majimbo ambayo hayakufikia vigezo hivyo yaliweza kugawanywa na kuacha majimbo ambayo vigezo vimezidi hata vigezo vilivyowekwa. Unashindwa kupata majibu, wananchi wanakata tamaa, wananchi wanaelewa, wananchi wanafuatilia sana vyombo vya habari na wanachanganua na wanaona wakati mwingine kama Serikali ina upendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wanakuwa wameomba mara kadhaa, wameomba Wilaya, wameomba Halmashauri, wameomba Jimbo hawajapata na ninao ushahidi wa kutosha, katika Wilaya yangu Jimbo la Kwela Halmashauri ya Wilaya imeomba Wilaya, imeomba Jimbo, imeomba Halmshauri haijapata wakati ina vigezo vilivyopitiliza. Hii inatokana na viongozi kutokutembelea maeneo yote, hii ni moja ya sababu muhimu sana ambayo inakatisha wananchi tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu nyingine ni kuchelewa kwa utatuzi wa Migogoro ya ardhi. Kwanza napaswa nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Ardhi aliyepo sasa hivi, kwa kweli lazima tumpongeze anafanya kazi kubwa sana, tena yenye moyo na kujitoa muhanga, mimi nampongeza sana. Lakini ningeomba ajielekeze katika maeneo sugu ambayo yamelalamikiwa kwa muda mrefu kutoa ufumbuzi na utatuzi wa mara moja ili kutokukatisha wananchi tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza hivi ninaongelea suala la shamba la Malonje ambalo limekuwa ni sugu sana na kwenye uchaguzi limetupa shida sana, hasa mimi Mbunge ndiye nimepata kazi kubwa kana kwamba mimi ndiye niliyebeba mzigo huo. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri uliangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni baadhi ya maeneo kutofikiwa na viongozi wa Kitaifa. Tangu tumepata Uhuru sasa hivi tuna Rais wa Awamu ya Tano, lakini yapo maeneo hawajawahi kumuona Rais hata wa Awamu ya Kwanza, ya Pili na Awamu ya Tatu, wanamuona tu kwenye luninga, sababu za msingi hazipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine kiongozi anaenda wanasema hakupitiki barabara ni mbaya nani atengeneze? Huko ni kutenga wananchi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba viongozi mnaotumbua majipu muangalie hayo ni majipu, kama Kiongozi anakuelekeza mahali pa kwenda kuzuri huko anaficha nini? Ni majipu nayo vilevile tunaomba tabia hiyo isiwepo tena, tunaimani na Serikali hii tabia hiyo itajifuta yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kubaki nyuma kimaendeleo, kukosa huduma muhimu. Kwa mfano, nitoe mfano kwa mambo mawili, barabara na umeme. Wilaya ya Sumbawanga Vijijini pamoja na kuwa kubwa mno, ina kata zaidi ya 28, vijiji 115 hakuna hata kijiji kimoja ambacho kina umeme, na wananchi wanasikia maeneo mengine kata mbili zina umeme na hata Kata jirani zina umeme, unadhani wananchi wanatafsiri kitu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri nyepesi ya wananchi wanadhani labda Mbunge wao hana uwezo, hasemi! kitu ambacho kila wakati tunazungumza. Kwa hiyo, ningeomba Serikali ijaribu kuweka uwiano isiwe na upendeleo, iweke uwiano kwa sababu nchi hii ni yetu sote. Iweke uwiano siyo kukimbilia upande mmoja, huko ni kuumiza wananchi bila sababu, niliona na lenyewe hilo nilizungumzie. (Makofi)
Suala lingine ni miundombinu ya barabara. Katika Jimbo langu ni mibovu mno, kwanza jiografia yenyewe ya Jimbo imekaa hovyo, miundombinu ni mibaya, hata viongozi wanaokuja, mfano Dada yangu Paresso alikuja wakati wa uchaguzi, Katika vitu alivyovitumia ni uchakavu wa miundombinu katika Jimbo langu, aliuliza hii ni Tanzania au ni Tanganyika? Nikamwambia Tanzania. Tulipata taabu kweli, hebu jamani jaribuni kuangalia maeneo haya, zipo barabara zaidi ya 10 hazipitiki. Sina sababu za kuzitaja kwa sababu naona muda hautoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ninapenda kulizungumzia ni kuhusu kilimo. Katika Hotuba ya Waziri Mkuu upande wa akiba ya chakula, inaonesha kwamba wametenga kununua tani 100,000 hicho kiwango ni kidogo mno, na sijui vigezo gani mnavitumia? Sijajua vigezo gani mnavitumia hivi tani 100,000 mnapanga zinaweza kuwasaidia Watanzania kama mvua hazitapatinaka miaka miwili, mitatu? Hizo tani 100,000 zinaweza zikasaidia? Na bado miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji bado hatujafikia kiwango kizuri.
Kwa hiyo, mazoea ambayo tumekuwa nayo ya neema ambayo tunayo Tanzania tunadhani miaka yote tutakuwa tunapata mvua mfululizo ndiyo sababu ya kutenga kiwango kidogo ,tani 100,000 ni kiwango kidogo mno kwa Nchi ya Tanzania. Kwa hiyo, ningeshauri kiwango hiki kiongezwe ni kidogo sana.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Hiyo ni Rukwa peke yake kama anavyozungumza Mheshimiwa aliyepo nyuma yangu, naomba kiwango hicho kiongezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upande wa afya, tunalo tatizo la upungufu wa wataalamu, waganga, tunalo tatizo la ukosefu wa kumalizia zahanati ambazo zimeanza kujengwa na wananchi na vituo vya afya, madaktari hakuna, ukosefu wa magari ya kubeba wagonjwa.
Mfano, tatizo la Kituo cha Afya cha Milepa, maombi yamekuja huu ni mwaka wa tatu na kutokana na kuchelewa tumepoteza karibu akina mama wajawazito 10 kwa mwaka jana tu, nimetoa taarifa mara kadhaa, nimerudia kuomba mara kadhaa. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu mambo mengine kama haya uyachukulie ni mambo muhimu, yanatutia doa kwa Serikali yetu nzuri hii ya sasa. Naomba uyabebe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upande wa elimu. Tunalo tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi upande wa shule za msingi hata upande wa shule za sekondari.
Tumejenga shule nyingi za sekondari za kata, tunaomba tupate Walimu wa Sayansi na wapo walimu ambao wamepata mafunzo wamemaliza wanazagaa mitaani hatujui wataajiriwa lini? Tunaomba wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anakuja kutoa ufafanuzi atueleze wataajiriwa lini walimu wapya wa sayansi na kwa kiwango gani kinachoweza kukidhi hali tuliyonayo kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ukosefu wa hosteli hasa hosteli za wasichana. Shule za Kata zina tatizo kubwa la kukosa hosteli za wasichana, jambo ambalo linarudisha maendeleo nyuma la vijana wetu wa kike, sote tunafahamu watoto wa kike wana vikwazo vingi, kutembea kilometa 5 anapambana na vikwazo vingi, wakati mwingine tunaweza tukalaumu kumbe waharibifu ni sisi wenyewe tusioangalia matatizo kama haya. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikatilia umuhimu wa kujenga hizi hosteli kwa shule zetu za kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchukua fursa hii kuishukuru Serikali kwa haya ambayo wameandika humu, tunasubiri utekelezaji na vilevile kwa haya niliyoyasema ningeomba ufafanuzi hasa kuitenga Wilaya ya Sumbawanga kutoipa Jimbo au Wilaya au Halmashauri wakati inavigezo lukuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti naunga mkono hoja